Wajumbe watishia kuzuwia bajeti ya Ardhi

Waziri wa Maji Ujenzi Nishati Ardhi na Mazingira, Ramadhan Abdalla Shaaban akiwasilisha kwenye Baraza la wawakilishi Zanzibar Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wametishia kutopitisha makadirio ya bajeti ya wizara ya ardhi, makaazi, maji na nishati kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi Unguja na Pemba. Wakichangia bajeti ya wizara hiyo wawakilishi wa CM na CUF waliungana kulaumu serikali kwa kutochukua hatua madhubuti ili kupunguza au kuondosha kabisa migogoro ya ardhi inayozorotesha maendeleo nchini.

Walisema  licha ya malalamiko ya wananchi pamoja na rais mwenyewe lakini hakuna dalili za kumaliza tatizo hilo ambapo wameshauri kuundwa kwa kamati teule ili kuchunguza matatizo ya ardhi.

“Rais amelalamika na hali katika vijiji kadhaa sio nzuri baina ya wananchi na viongozi na wawekezaji. Tatizo lipo wapi mbona ni muda mrefu?” alihoji Mwakilishi wa Jimbo la ChakeChake (CUF) Omar Ali Shehe. Alisema ili kupata jibu sahihi kutokana na kilio cha kila mtu na rais wa Zanzibar ni kuundwa kwa kamati teule ili kufuatilia tatizo la ardhi ambalo pia linaipa jina baya Zanzibar.

“Mheshimiwa Spika tuna orodha ndefu ya madudu katika utoaji wa, ukodoshaji, na uuzaji wa ardhi ni lazima tuchunguze. wapo wawekezaji ambao wamenyanganywa haki zao kutokana na makampuni feki wanaoshirikiana na baadhi ya viongozi kujitajirisha” alilalamika Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura (CCM) Hamza Hassan Juma.
Mwakilishi huyo alimkabidhi Spika nyaraka za ushahidi mbali mbali zinazotuhumu ukodishaji ardhi usizingatia sheria na utaratibu na nchi na kuwataka wajumbe waunge mkono kuundwa kwa kamati teule. Naye Makame Mshimba Mbarouk ni Mwakilishi wa jimbo la Kitope (CCM) alisema makampuni feki kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo wamekuwa wakifuta mikataba halali na kutengeneza mikataba feki inayokosesha serikali mapato.
Akitoa mfano mwakilishi huyo alitaja kampuni moja ambayo ilikuwa ikilipa kodi ya dola za kimarekani 13,000 ambapo mkataba wake ulifutwa na ardhi hiyo kupewa kampuni hiyo inayolipa kodi ya dola za kimarekani 3,000.

“Kuna baadhi ya mazingira mengi ya kutatanisha katika mikataba na tumefuatilia kwa wanasheria ambao wametueleza kuwa lazima utaratibu wa kufuta mkataba ufuatwe kwa kutoa indhari ‘notice’ kwa mwekezaji lakini kinachotokea mikataba inafutwa bila ya kuzingatia sheria. I we serious na huu ndio utawala bora” alihoji mwakilishi huyo.

Mwakilishi wa jimbo la Mkwajuni (CCM) Mbarouk Wadi Mussa alisema baadhi ya viongozi wasiokuwa waaminifu wanavimba matumbo kutokana na kukithiri kudhulumu katika biashara ya kuuza ardhi.

Alisema serikali ikubali kutoa nafasi kwa wajumbe kuangalia chanzo na sababu ya migogoro ya ardhi katika kila wilaya na mikoa ili kuisaidia serikali kupata ufumbuzi na wenye haki warejeshewe ardhi zao.

Mwakilishi wa Kikwajuni (CCM) Mahmoud Mohammed Mussa alisema tatizo la ardhi pia limewakumba baadhi ya waasisi na wana mapinduzi wa Zanzibar akiwemo marehemu Said Iddi Bavuai ambaye shamba lake limechukuliwa katika mazingira ya kutatanisha na hadi leo halijarejeshwa kwa familia yake.

Wajumbe wengine ambao ni miongoni mwa wasemaji katika baraza hilo Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu, Mwakilishi wa Kiwani (CUF) Hijja Hassan Hijja waliwatupia lawama viongozi wa serikali za mitaa wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na maafisa wa wizara ya ardhi kuwa ni chanzo cha migogoro ya ardhi.

Suala la ardhi limekuwa likitawala mijadala katika bajeti kila mwaka ambapo rais Dk Shein alitoa agizo kuwa migogoro ya ardhi iweze kutatuliwa na waliosababisha migogoro hiyo jambo ambalo linaonekana na vikwazo.

                                                                                       Maji bado ni tatizo Zanzibar

WAKATI serikali imetangaza kuimarisha upatikanaji wa maji katika vijiji na miji ya Zanzibar wajumbe wa baraza la wawakilishi wamesema hali ya maji bado ni mbaya. Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara ya ardhi, makaazi, maji na nishati kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, Waziri wa wizara hiyo, Ramadhan Abdallah Shaaban alisema maji ni miongoni mwa vipaumbele vya wizara yake.

Alisema miongoni mwa mikakati ni kuhifadhi mazingira hasa katika vyanzo vya maji pamoja na kupata ufadhili wa nchi rafiki kusaidia miradi ya mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) ili kufikia malengo yake.

“Mheshimiwa Spika tatizo la maji lipo lakini serikali inachukua juhudi kubwa kwa kushirikiana na washirika ili kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hilo sambamba na hilo wizara kwa kupitia ZAWA inatoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuchangia huduma ya maji na uhifadhi wa miundombinu ya maji” alisema waziri.

Waziri Shaaban aliwaomba wajumbe wa baraza hilo kusaidia kuvilinda vianzio vya maji ambavyo vinaonekana kuvamiwa na wananchi kwa kujenga nyuma za kuishi.

Mamlaka ya maji imekuwa ikifuatilia kwa karibu katika maeneo yote ambao wananchi wamevamia mfano kijito upele, kwarara, dimani, mwanyanya na maeneo mengine kwa kuweka uzio lakini muhimu ni ushirikiano wa kuhifadhi maeneo hayo.

Shaaban alisema ili kuijengea uwezo mamlaka ya maji pia paipu na matangi ya kuhifadhia maji yalichakaa yatabadilishwa na kuwekwa mapya katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba jambo ambalo litasaidia kuimarisha usambazaji maji safi na salama.

Aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kwamba maji mengi yamekuwa yakipotea kutokana na miundombinu chakavu pamoja na matumizi mabaya ya maji huku mahitaji ya huduma hiyo kwa wananchi yakiongezeka kila mwaka.

“Kutokana na uchakavu wa miundo mbinu wa usambazaji wa maji katika maeneo mengi ya mjini wizara inatarajia kuendeleza kutanua huduma ya maji katika maeneo yasio na huduma nzuri ulazaji wa mabomba mapya, uchimbaji wa visima na ununuzi wa pampu mpya” aliahidi waziri.

Alisema miradi yote hiyo inayosaidiwa na China, Japan na Banki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) pamoja na washirika wengine unalenga kupunguza matatizo ya maji katika kipindi cha muda mfupi ujao.

3 responses to “Wajumbe watishia kuzuwia bajeti ya Ardhi

  1. Wawakilishi mbona hamukuliongelea suala la mafuta? Au mmeridhika na uandikaji wa katiba ya tanganyika?

  2. Waheshimiwa hamuwezi kushughuliki mafuta chini ya muungano. Vunjeni muungano musiulinde. Sisi wananchi wenu hatuutaki muungano. Mwaogopa nini? Kuhusu migogoro ya ardhi haiwezi kuisha sababu hao wakubwa ndio chanzo. Rushuwa na kujinufaisha ndio sera iliopo. Sisi wadogo na wanyonge hatuna haki. Matajiri wametubana. Semenii lakini hili haliondoki sababu migogoro ya ardhi inachangiwa na vigogo wa nchi.

  3. alia: Hawa kina Hamza ni mahodari kuzungumzia migogoro ya ardhi, lakini nasikia yeye amevamia ardhi ya wazi(open space) ambayo alikabidhiwa mwananchi mmoja na municipal tangu miaka ya 90 kwenye area ya mbweni. Hakuna tume itayoweza kulichungua hili, maana dhulma hizo zinaendelea mpaka kwenye awamu hii. Mungu awasaidie viongozi wetu safi kama Balozi, Maalim na Dk. lakini kusema kweli wana kazi kubwa, viongozi wengi bado wana tamaa na wanaendelea kuvamia ardhi. Suluhisho ni kuzuwia viwanja vyote vyenye mgogoro, wajulikane wote waliovitoa na wawajibishwe, signature zao si zipo? Serikali ioneshe nguvu zake haiwezi kuchezewa na watu inaowaajiri. Hiyo ndio njia pekee ya ku-win confidence ya wananchi.

Leave a comment