Tusipoujadili Muungano kwa makini, utavunjika

Makamishna wa tume ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania wakisikiliza na kuandika maoni yanayotolewa na baadhi ya wananchi huko mkoa wa kusini Unguja

Tumeshuhudia na kujionea jinsi muungano wa siku nyingi, kati ya Uingereza na Ireland ya Kaskazini ulivyogubikwa na mitafaruku, ikiwa ni pamoja na hoja tata juu ya uhalali wa Wabunge wa Bunge la Muungano kutoka Ireland ya Kaskazini kupigia kura bungeni mambo yasiyoihusu Ireland Kaskazini. Ni sawa tu na hapa kwetu juu ya uhalali wa Wabunge kutoka Zanzibar kupigia kura mambo yanayohusu Tanzania Bara au Tanganyika. Kuna hoja pia juu ya Wazanzibari kuruhusiwa kumiliki ardhi Tanzania Bara; au Wazanzibari kushika nafasi za uongozi katika Serikali ya Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, wakati Watanzania Bara hawaruhusiwi kugusa mambo hayo Visiwani. Kwa nini tunaendelea kuwa na Wazanzibari na Watanzania Bara, wakati wote hao ni Watanzania ndani ya nchi moja? Je, Zanzibar ni nchi au Taifa kiasi cha kuwa na watu wenye utaifa wa Zanzibar – Wazanzibari; au Watanzania Bara nao wana Taifa lao, Taifa la Watanzania Bara?

Tusipoujadili Muungano kwa makini, utavunjika
Sehemu ya kwanza:
Joseph Mihangwa

SASA ni ruksa kujadili hatima ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa miaka 48 iliyopita, Aprili 26, 1964. Hili limewekwa wazi na Mwenyekiti wa Tume ya kuratibu Maoni juu ya Katiba mpya, Jaji Joseph Sinde Warioba hivi karibuni.
Awali na mwanzoni kabisa mwa mchakato huu, na kusema kweli tangu kuasisiwa kwake; wananchi hawakuruhusiwa kujadili Muungano. Kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na mtu kujaribu kukanyaga mahali patakatifu umevaa viatu. Wengi iliwagharimu nafasi zao za kisiasa na hata kiuchumi.
Ruksa hii imefungua mafuriko tele ya mawazo mbalimbali juu ya Muungano. Wapo wanaotaka Muungano upitiwe upya kwa kuzingatia madhumuni sahihi ya kuanzishwa kwake na kwa mazingira ya sasa; wapo pia wanaotaka muundo wa serikali tatu badala ya muundo wa serikali mbili wa sasa; na wapo pia wahafidhina wa siasa za utengano wanaotaka uvunjwe.
Yote haya ni sehemu ya demokrasia chini ya dhana ya uhuru wa mawazo. Ingekuwa enzi za demokrasia ya chama kimoja, wote hao wangeishia Keko.
Kuzuka kwa mawazo kinzani juu ya Muungano ni uthibitisho wa kutosha kwamba Muungano wetu si shwari tangu mwanzo; na kwamba ukimya wa wananchi juu yake ulibeba hofu, ghadhabu na kiu ya haki ya maoni iliyopokwa, na ambayo sasa imezaa kishindo chenye mwangwi mkubwa.
Muungano wowote wa kisiasa unaofikiwa bila ridhaa ya wananchi siku zote ni wenye mitafaruku, kero na uhasama, na hivyo hauwezi kudumu mara waasisi wake wanapoondoka madarakani; ila unaweza kuokolewa tu kwa kusikiliza hoja za wananchi na kwa kurekebisha kasoro zilizokithiri.
Tumeshuhudia na kujionea jinsi muungano wa siku nyingi, kati ya Uingereza na Ireland ya Kaskazini ulivyogubikwa na mitafaruku, ikiwa ni pamoja na hoja tata juu ya uhalali wa Wabunge wa Bunge la Muungano kutoka Ireland ya Kaskazini kupigia kura bungeni mambo yasiyoihusu Ireland Kaskazini. Ni sawa tu na hapa kwetu juu ya uhalali wa Wabunge kutoka Zanzibar kupigia kura mambo yanayohusu Tanzania Bara au Tanganyika.
Kuna hoja pia juu ya Wazanzibari kuruhusiwa kumiliki ardhi Tanzania Bara; au Wazanzibari kushika nafasi za uongozi katika Serikali ya Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, wakati Watanzania Bara hawaruhusiwi kugusa mambo hayo Visiwani.
Kwa nini tunaendelea kuwa na Wazanzibari na Watanzania Bara, wakati wote hao ni Watanzania ndani ya nchi moja? Je, Zanzibar ni nchi au Taifa kiasi cha kuwa na watu wenye utaifa wa Zanzibar – Wazanzibari; au Watanzania Bara nao wana Taifa lao, Taifa la Watanzania Bara?
Nimesema, muungano unaopatikana kwa shuruti na shinikizo kwa wanachama una hatari ya kukataliwa na kuvunjika siku zote, tena kwa aibu.
Kushindwa kwa Shirikisho la Afrika ya Kati (CAF) miaka ya 1960, Muungano wa Nchi za Kiarabu (UAR) na Muungano wa Ethiopia – Eritrea ulioanzishwa mwaka 1952, ni mifano hai ya Muungano iliyokufa kwa kukosa ridhaa ya wananchi, kama ambavyo kujitenga kwa Sudan Kusini na Sudan Kaskazini kunavyothibitisha jinsi muungano unaosimamiwa kidikteta unavyoweza kuvunjika hima.
Kitendawili cha uhiari wa Muungano
Mengi yameandikwa juu ya chimbuko la Muungano wetu; lakini kwa sehemu kubwa kwa kupotoshwa. Wapotoshaji wakubwa ni wale wanaodai ulifikiwa kwa hiari, wakati ukweli ulipatikana kwa shinikizo la mataifa makubwa ya Magharibi katika jitihada za kuzima kuenea kwa Ukomunisti Afrika Mashariki, wakati huo Zanzibar kilikuwa kitovu cha kuenea kwa itikadi hiyo.
Zaidi ya hilo, hofu ya Karume ya kupinduliwa na wanaharakati wa siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx Visiwani, ilimfanya aombe msaada wa Askari 300 kutoka Tanganyika kumlinda na kuimarisha utawala wake na hivyo akawa tayari mateka wa Tanganyika kwa maamuzi yaliyofuata.
Na pale juhudi za Mwalimu Nyerere za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki (likihusisha Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar) – EAF, zilipogonga mwamba (kama ambavyo juhudi za kuunda Shirikisho la Afrika ya Kati, likihusisha, Nyasaland, Rhodesia Kaskazini na Rhodesia Kusini zilivyogonga mwamba kwa sababu zile zile za EAF), aligeukia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa msaada mkubwa wa nchi za Magharibi, siku nne tu tangu kugonga mwamba; na Muungano ukazaliwa siku 100 tu baadaye, katikati ya malumbano makali kati ya Mataifa ya Magharibi na Mataifa ya nchi za Kikomunisti za Mashariki, zikiwamo Urusi, China na Ujerumani Magharibi.
Wanaobisha hili, waeleze kwa nini Zanzibar ilibatizwa jina la “Cuba ya Afrika” enzi hizo za vita baridi? Kwa nini Marekani na Uingereza ziliandaa majeshi kuivamia Zanzibar kama Muungano usingefikiwa?
Si hivyo tu; inafahamika pia kwamba pale Karume alipoonyesha kutokuwa na hiari ya haraka kuunda Muungano na Tanganyika, Nyerere alitishia kuondoa askari wake Visiwani kumwacha Karume bila ulinzi ili apinduliwe na mahasimu wake wa kisiasa Visiwani, wakiwamo viongozi wenzake wa Baraza la Mapinduzi.
Hakuna ushahidi kuonyesha kwamba Watanganyika na Wazanzibari walihusishwa kufikia Muungano wa Tanzania. Wala hakuna ushahidi kuonyesha kwamba Bunge la Zanzibar, maarufu kama Baraza la Mapinduzi, liliridhia Mkataba wa Muungano wala kutunga sheria kuhalalisha kutumika kwa mkataba huo kwenye ardhi ya Zanzibar.
Sisemi kwamba kwa mapungufu hayo ya kikatiba na kisheria, Muungano ubatilishwe; la hasha; hilo litakuwa ni jambo la kijinga kubatilisha taasisi iliyodumu kwa miaka 48 kwa mema na mabaya.
Ninachosema hapa ni kuwa Muungano ujadiliwe kwa kuendeleza na kuimarisha yale mema yote ya Muungano, na kwa kuzingatia muundo wa Muungano uliokusudiwa ili kukomesha kero zisizo za lazima.
Na katika kufanya hivyo, tuzingatie na tuishi kwa matakwa ya Mkataba wa Muungano kwa yaliyokusudiwa kwenye Mkataba huo wa Kimataifa. Tunajua, ni mambo 11 tu yaliyokusudiwa kuwa kwenye Serikali na Katiba ya Muungano; lakini hadi Katiba ya kudumu ikitungwa mwaka 1977, mambo ya Muungano yalikuwa yemefika 17, ambapo sita yaliongezwa kinyemela na kinyume cha Mkataba wa Muungano.
Mambo hayo 11 yaliyotajwa kwenye ibara ya nne ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) na kuridhiwa kwa Sheria ya Bunge Namba 22 ya 1964 (Acts of Union) chini ya kifungu cha tano cha Sheria hiyo hayabadiliki (unalterable) na hivyo kwamba marekebisho yenye kuongeza mambo ya Muungano chini ya kifungu hicho ni haramu na batili.
Vivyo hivyo, kitendo cha Bunge cha kujitanua na kujitwalia mamlaka ya kurekebisha Mambo ya Muungano kwa kuvuka uwezo wake, kinadhalilisha msingi mzima wa Muungano. Hiki ndicho kinachoitwa “ubabe” wa kisiasa unaotibua na kuchefua Muungano. Huo ndio mwanzo wa kuchezea Muungano. Hili ndilo chimbuko la hasira, kero na uhasama wa kisiasa ndani ya Muungano ambalo Mchakato wa Katiba wa sasa lazima ulijadili ili kuokoa Muungano.
Hapa nisisitize tu kwamba, Mkataba wa Muungano ndiyo Katiba ya Muungano; kwa maana ikitokea kwamba kuna mgongano kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Mkataba wa Muungano au kati ya Mkataba wa Muungano na Katiba ya Zanzibar, Mkataba wa Muungano utashinda (shall prevail) kwa turufu yake.
Maoni yangu ni kuwa wote wanaodhani kwamba kujadili Muungano ni dhambi au kwamba kutojadili Muungano ni kuusalimisha, ni wapofu wa kisiasa, kidemokrasia na kikatiba. Hao ndio wafichao ugonjwa alivyosema Mwalimu Nyerere, kwamba kilio ndicho pekee kitakachowaumbua.
Hatari ya Muungano kuvunjika
Kuna kila dalili kuonyesha kwamba Muungano uko hatarini kusambaratika kama hatutachukua hatua za haraka na za makusudi. Hatari hiyo inatokana na sababu kuu mbili: kwanza, ni kukosekana kwa nahodha au manahodha wa kuongoza Muungano kwa utamaduni (wa kidikteta) na kwa mtizamo wa madhumuni ya kuanzishwa kwake.
Kuondoka kwa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume, kama manahodha wa meli ya Muungano kwa muundo waliofikiria wao na kutumika kwa nguvu na udikteta mkubwa, kumefanya meli ya Muungano kuyumba.
Yaliyoupata Muungano wa Ethiopia – Eritrea hadi kuvunjika kufuatia kung’olewa madarakani kwa Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia, yanaweza kuukumba pia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu Zanzibar kwa Tanganyika ni sawa na ilivyokuwa Eritrea kwa Ethiopia, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.
Pili, kuna usiri mpya na mkubwa zaidi miongoni mwa Wazanzibari (dhidi ya) kwa Muungano unaoashiria chuki, uhasama na kuchoshwa na Muungano.
Tunachofahamu, Muungano kwa Wazanzibari umeweza kushinikizwa na kudumu kutokana tu na siasa zao za chuki miongoni mwao wenyewe (divide and rule) tangu enzi za harakati za Uhuru mwaka 1957 hadi kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) miaka miwili iliyopita.
Lakini sasa Wazanzibari wanaweza wakahoji na kujadili Muungano kwa umoja na kwa sauti moja kwa kulindwa na Katiba ya nchi yao na Bunge (Baraza la Wawakilishi) lao lisiloweza kuingiliwa na chombo chochote au taasisi yoyote ya Muungano.
Wakati huo huo, wananchi nao wanadai na kutaka kuonyeshwa Mkataba wa Muungano; wanataka kujua ni aina gani ya Muungano uliokusudiwa, na kwa nini kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa misingi na matakwa ya Muungano?
Majibu tuliyozoea kuwapa wananchi, kwamba nakala za Mkataba huo zilipotea na kuwashauri wakaulizie Umoja wa Mataifa ambao una nakala, ni ya kihayawani na yatazidi kuongeza kero za Muungano.
Tatu, misingi yote mitatu iliyofanya Muungano ufanye kazi imeporomoka; hivi sasa kunatakiwa tathmini mpya. Msingi wa kwanza ulikuwa ni Vita Baridi kati ya Mataifa ya Magharibi na Mataifa ya Mashariki vilivyokamiana kumalizana kwa kugombea nchi za dunia ya tatu.
Msingi wa pili ni mfumo wa demokrasia ya chama kimoja cha siasa uliozaa rais dikteta, maarufu kama “rais beberu” (imperial presidency) asiyeambilika.
Rais aliweza kurekebisha na kuchezea matakwa ya Muungano kwa amri yake (decree) na Bunge la chama kimoja likaridhia bila kuhoji.
Yeyote aliyehoji Muungano aliwajibishwa kwa viwango mbalimbali. Mfano ni Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, aliyevuliwa nyadhifa zote za uongozi wa Serikali na chama mwaka 1984, alipotumia haki yake ya Kikatiba, kutaka kujua Muundo sahihi wa Muungano uliokusudiwa chini ya Mkataba wa Muungano.
Jumbe, kwa kutumia ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, aliandaa Hati kupeleka Shauri kwenye Mahakama Maalumu ya Kikatiba kutaka itoe ufafanuzi ni aina gani ya Muungano uliofikiwa kati ya Tanganyika na Zanzibar na mgawanyo wa madaraka kati ya nchi hizo mbili ndani ya Muungano.
Kazi pekee ya Mahakama hiyo ni kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake, na kutoa uamuzi wa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Msingi wa tatu ulioporomoka ni Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea lililosimamiwa na Serikali ya chama kimoja na ambalo lilipigwa dhoruba na Azimio la Zanzibar mwaka 1992. Na ingawa Azimio na Siasa hii haikuwa na nguvu sana Zanzibar, lakini kikatiba ilijenga Umoja wa Kitaifa na kuondoa dhana ya watu kuhoji hoji mambo mengi ya kiserikali na kiuongozi, lakini leo mambo ni tofauti ambapo matakwa ya Haki za Binadamu, Haki za Kisiasa na za kiraia na kuwapo kwa Asasi huru za Kiraia [Civil Society], kunafanya mfumo wowote unaobana jamii uhojike na kuzua changamoto na vuguvugu za mabadiliko.

Sehemu ya Pili:

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya toleo lililopita, tuliona jinsi Muungano wowote wa nchi uliofikiwa bila ridhaa ya wananchi unavyoweza kuvunjika kwa urahisi, ukiwamo Muungano kati ya Uingereza na Ireland Kaskazini ambao Muungano wa Tanzania umenakili na kuiga mengi, ulivyoanza kuyumba.
Tuliona pia dalili zinazoashiria kuvunjika kwa Muungano wetu, zikiwamo, kukosekana nahodha makini wa kuendesha meli ya Muungano iweze kuvuka salama bahari iliyochafuka; kuanzishwa kwa Muungano wa kitaifa wa Wazanzibari ambao umefufua umoja wao wa kitaifa na kudai kurejeshewa hadhi yao kama nchi; na kuvunjika kwa mihimili mitatu iliyoshikilia Muungano, ambayo ni Rais dikteta asiyeambilika (imperial presidency), mfumo wa Chama kimoja, Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Kabla hatujaichambua kwa kina athari ya kuvunjika kwa mihimili hii mitatu, tuangalie kifananisho cha Muungano wa Ethiopia – Eritrea ulivyovunjika kwa sababu, kama ilivyokuwa Eritrea kwa Ethiopia, ndivyo ilivyo Zanzibar kwa Tanzania. Eritrea ilijitoa kwenye Muungano kati yake na Ethiopia na kuwa nchi huru mwaka 1993.
Harakati za Zanzibar kujitoa kwenye Muungano, kama zilivyokuwa harakati za Eritrea kujitoa kwenye Muungano kati yake na Ethiopia kunatishia na kujenga hofu kwa Watanzania juu ya hatima ya Muungano, hasa baada ya kuundwa kwa Serikali ya Kitaifa (SUK) kwamba sasa hofu hiyo na yenye kuogofya ni dhahiri na yenye kuzua hofu.
Kwa mfano, nani alitarajia kabla ya hapo, kwamba siku moja Zanzibar itakuwa na bendera yake ya Taifa, Wimbo wake wa Taifa, Ngao ya Taifa, “Jeshi” la Taifa, Katiba yake yenye kulinda ukuu wa nchi na maslahi ya Wazanzibari bila kuingiliwa na Katiba wala taasisi yoyote ya Muungano?
Nani alitarajia siku moja Zanzibar itazuia rasilimali zake kutumika kwenye Serikali ya Muungano kama mafuta, ardhi na bahari, ila kwa matumizi na maslahi ya Wazanzibari pekee?
Nani alitarajia kwamba Zanzibar ingeweza kujiunga na Shirikisho la Mpira la Bara la Afrika (CAF) kama nchi nje ya Muungano wa Tanzania na sasa inataka ijiunge na Shirikisho/Jumuiya ya Afrika Mashariki kama nchi?
Yote haya yanatia hofu na kuogofya juu ya hatima ya Muungano, kama tu hatutarejea upya Mkataba wa Muungano kuona wapi unavunjwa na yapi wanayofanya ni sahihi tuwaachie waendelee, badala ya kuendeleza udikteta wa kizamani kuzima hoja sahihi. Kuna dhambi gani wananchi kupewa Mkataba wa Muungano wakasoma na kujiridhisha na yaliyokusudiwa kwenye Muungano huo?
Hofu hii juu ya SUK inaweza kufananishwa na hofu kama iliyozua Eritrea kwa Serikali ya Muungano wa Ethiopia – Eritrea, pale Eritrea alipoanzisha harakati halali kutaka kujinasua kutoka kwenye Muungano huo, uliodumu tu kwa udikteta wa Mfalme Haile Selassie kama nahodha wa Muungano, na alipoondolewa madarakani, meli ya Muungano iliyumba na kuzama kwa nguvu ya tufani.
Na ndivyo ulivyo Muungano wetu, baada ya kuondoka madarakani kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyeshika hatamu zote za Muungano na kuuendesha kwa staili ya mpanda Farasi.
Zanzibar kama Eritrea kwenye Muungano
Eritrea ilitawaliwa na Wataliano kwa miaka 50 hadi 1941 waliposhindwa vita na Waingereza. Baada ya ushindi huo, Uingereza iliruhusu nchi hiyo kujitawala kama nchi huru chini ya usimamizi wake. Hapo vyama vya siasa na vya Wafanyakazi vikaanzishwa, pamoja na vyombo vya habari huru kwa ajili ya elimu kwa umma.
Mwaka 1952, wakati hatima ya Eritrea ilipojadiliwa kwenye Umoja wa Mataifa, Ethiopia ilitaka ipewe nchi hiyo kwa madai kwamba, kihistoria ilikuwa ni sehemu ya ufalme wa Ethiopia. Hapo kukatokea mzozo.
Wakati nchi jirani za Kiarabu zilitaka Eritrea iwe Taifa huru, Waeritrea wenyewe, ambao idadi yao wakati huo ilifikia 3,000,000, waligawanyika; nusu yao ambao ni wa madhehebu ya Kikristo, na wa kabila la Tigraya waishio maeneo ya milimani karibu na Mji Mkuu, Asmara, waliunga mkono Muungano na Ethiopia.
Kwa upande wa pili, nusu ya Waeritrea ambao ni Waislamu, wanaoishi sehemu za jangwa karibu na Bahari ya Sham na bonde la Magharibi, walitaka Eritrea ipewe uhuru.
Mwafaka ukafikiwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, wa kuunda Shirikisho la Ethiopia na Eritrea ambapo Serikali ya Ethiopia ilipewa kusimamia mambo ya Nje, Ulinzi, Fedha, Biashara, Bandari na Forodha.
Chini ya Muungano huu, ambao muundo wake unafanana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Eritrea, kama ilivyo kwa Zanzibar, iliruhusiwa kuwa na Serikali yake na Bunge huru kusimamia mambo yake. Tena, kama ilivyo Zanzibar ndani ya Muungano, iliruhusiwa kuwa na bendera yake, lugha zake za Taifa, ambazo ni Kitigrinya na Kiarabu.
Tangu mwanzo, Mtawala wa Ethiopia, Mfalme Haile Selasie, aliuona Muungano huo, kama ambavyo Rais Julius K. Nyerere alivyouona Muungano wa Tanzania, kuwa ni hatua ya mwanzo tu kuelekea Muungano kamili kwa kuunda nchi moja.
Kero na kelele juu ya Muungano zilianza kusikika pale Watawala wa Ki-ethiopia, kwa ubaguzi na kujuana, wakisaidiwa na wanasiasa Wakristo wa Kitigraya, walipoanza kuvuka mipaka ya mambo yaliyokubaliwa chini ya Mkataba wa Muungano, kwa kuongeza mambo kwa njia ya shinikizo, vitisho na udhibiti kwa Waeritrea.
Kwa njia hii, uhuru ambao Waeritrea walifurahia kwa muda baada ya ukoloni wa Kitaliano (na kabla ya Muungano), kama vile haki za kisiasa, vyama vya wafanyakazi na uhuru wa vyombo vya habari, vilidhibitiwa. Hapo tena, kelele juu ya Ethiopia kutaka kuimeza Eritrea, kama ambavyo Wazanzibari wanalalamikia kutaka kumezwa na Tanganyika, ikazua moja ya kero za Muungano.
Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa Aprili 26, 1964, ulibainisha mambo kumi na moja tu ya Muungano, baadhi yakiwa ni yale yale yaliyokuwa chini ya Muungano wa Ethiopia na Eritrea, tuliyoyaeleza hapo mwanzo.
Na kama ilivyokuwa kwa Ethiopia/Eritrea, Serikali ya Zanzibar iliachwa kusimamia mambo yote yasiyo ya Muungano, na vivyo hivyo kwa Serikali ya Tanganyika.
Lakini kama ilivyokuwa kwa Ethiopia/Eritrea, kadri Muungano wa Tanzania ulivyopiga hatua mbele, mambo ya Muungano yalizidi kuongezwa kwa njia ya Amri za Rais (Decrees) kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano, na kufikia 23.
Katiba ya muda ya 1965 (ibara ya 12), ilimpa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya utendaji kwa mambo yote (11) ya Muungano na kwa Tanganyika; kwa maana kwamba, Rais wa Muungano alikuwa sasa ndiye Rais wa Muungano na hapo hapo Rais wa Tanganyika.
Vivyo hivyo, ibara ya 49 ya Katiba hiyo, ilitoa mamlaka ya kutunga sheria kuhusu mambo ya Muungano na kwa ajili ya Tanganyika, kwa Bunge la Muungano. Ndiyo kusema kwamba, Bunge hilo la Muungano sasa lilikuwa ndilo Bunge la Tanganyika pia.
Mwaka 1967, Bunge lilitunga Sheria Na 24 ya 1967, iliyompa Rais wa Muungano na Rais wa Tanganyika uwezo wa kupachika jina “Tanzania” katika sheria zote popote pale jina “Tanganyika” liliposomeka hivyo.
Hii ilimaanisha kwamba, “Tanganyika” sasa ndiyo iliyogeuka kuwa “Tanzania”, na “Tanzania” ndiyo Tanganyika, lakini Zanzibar ikabakia kama Zanzibar.
Ni kwa misingi hii kwamba, Sheria ya Tafsiri za Vifungu vya Sheria (Interpretation of Laws and General Cluses Act), Namba 30 ya 1972 (kifungu cha 3), iliweza kutafsiri neno “Jamhuri” kumaanisha “Jamhuri ya Tanganyika, inayojumuisha Jamhuri ya Muungano”.
Tanganyika ndiyo Tanzania?
Sheria Namba 24 ya 1967, iliyofuta jina “Tanganyika” kwenye vitabu vya Sheria; na Sheria Namba 30 ya 1972 iliyotafsiri “Jamhuri ya Tanganyika” kujumuisha “Jamhuri ya Muungano” zilitoa tafsiri mbaya na mitazamo potofu kuwafanya Watanganyika kuamini kwamba nchi yao Tanganyika ilipandishwa hadhi kuwa Tanzania, kama mshirika mwandamizi kwa Zanzibar katika Muungano; wakati ukweli Tanganyika na Zanzibar zina hadhi sawa ndani ya Muungano.
Katiba ya kudumu ya 1977 inayotumika sasa ilitibua mambo zaidi na kuongeza utata na mtafaruku kwa Muungano.
Tunafahamu kwamba, Mkataba wa Muungano (ibara ya 5, 6 na 7) kwa Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964 (kifungu 5, 7 na 8) zinatamka bayana kuendelea kuwapo kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar baada ya nchi hizo kuungana kuunda ubia wa mambo kumi na moja ya “Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”, kwa maana ya kuwapo Serikali tatu: Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Kwa mfano, ibara ya tano ya Mkataba huo inasema: “Sheria za sasa za Tanganyika na zile za Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika maeneo (territories) ya nchi hizo”.
Na kifungu cha 8 (1) cha Sheria ya Muungano kinasema:
“….. Kuanzia siku ya Muungano na baada ya hapo na kuendelea, Sheria za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kuwa Sheria za nchi za Tanganyika na Zanzibar ….. na hazitaathirika au kuathiriwa kwa namna yoyote ile kwa kukoma kutumika kwa Katiba ya Tanganyika kwa Serikali ya Tanganyika kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano inayojiongoza na kujitawala…..”.
Tofauti na Mkataba wa Muungano; pia tofauti na Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya 1965, iliyotambua kuwapo kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 inayoendelea kutumika sasa haiundi au kutambua kuwepo kwa Tanganyika; wala haimpi mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano, au mtu au watu wowote wale, kuitawala Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano.
Hapa, upungufu huu unazua dhana potofu kuwa, Tanzania ndiyo Tanganyika, na Tanganyika ndiyo Tanzania; na kwa sababu hiyo kwamba hapana haja ya kuwa na Serikali zaidi ya moja kwa Tanzania nzima!.
Vivyo hivyo, kama ambavyo uhuru na uwapo wa vyama vya siasa na vya wafanyakazi ulipigwa marufuku kwa AMRI ya Mtawala wa Ethiopia nchini Eritrea (1959), na bendera ya nchi hiyo kufutwa (1958); ndivyo vivyo hivyo mwaka 1977 hapa kwetu, Chama cha ASP kiliunganishwa na Chama cha Tanganyika National Union (TANU), kuunda “Chama cha Mapinduzi” – CCM, kama moja ya mikakati ya kuimarisha Muungano, wakati ukweli mambo ya Vyama vya siasa si moja au sehemu ya mambo chini Mkataba wa Muungano, wala sehemu ya Sheria za Muungano (Acts of Union) kwa utekelezaji.
Kelele za Wazanzibari kama za Waeritrea
Ni kwamba, kelele za Eritrea, kama zilivyo kelele za Zanzibar juu ya kero za Muungano, hazikuwa za uongo, kwani ubabe wa Ethiopia (kaka mkuu ndani ya Muungano, kama ilivyo Tanganyika) ulianza kujionyesha dhahiri kwa kushinikiza mambo yasiyo ya Muungano.
Kwa mfano, mwaka 1958, bendera ya Eritrea ilifutwa; ambapo mwaka 1959, Sheria za Ethiopia zilishinikizwa pia kutumika Eritrea; vyama vya siasa na vya Wafanyakazi navyo vikapigwa marufuku.
Ubabe huu ulikwenda mbali zaidi kwa kudhibiti habari na vyombo vya habari, lugha za Taifa za Kitigranya na Kiarabu zikapigwa marufuku, na nafasi yake kuchukuliwa na lugha ya Kiethiopia ya “Amhari”, kama lugha ya Taifa.
Kana kwamba hayo yalikuwa hayatoshi, mwaka 1962, Bunge la Eritrea lilishinikizwa kukubali kufutwa kwa Shirikisho, na Bunge hilo kulazimishwa kujifuta lenyewe ili Eritrea imezwe na Ethiopia. Kuanzia hapo, Eritrea ilihesabiwa na kupewa hadhi duni kama moja tu ya majimbo 13 ya Ethiopia.
Kwa miaka yote ya 1960, Serikali ya Haile Selasie ilikabaliwa na maasi pande zote. Kwa mfano, maasi ya Wa-Oromo katika Jimbo la Bale upande wa Kusini, yalidumu kwa miaka sita; nao Wasomali waasi wa Ogaden, waliunda Chama chao cha Ukombozi – “The West Somali Liberation Front” (WSLF) kuwafukuza Waethiopia Ogaden ili kurudisha Serikali ya Kisomali.
Huko Eritrea, vikundi vya wapiganaji wa msituni vilianzisha vita ya ukombozi ambapo Serikali ya Selasie ilitumia silaha nzito na ukatili mkubwa kujaribu kuizima. Ukatili huu ulidhalilisha utaifa wa Waeritrea, wakaapa kutorudi nyuma hadi uhuru upatikane.
Septemba 12, 1974, Mfalme Haile Selasie, alipinduliwa na Kanali Mengistu Haile Mariam, ambaye naye hakuweza kuzima vita ya ukombozi ya Wa-eritrea. Si hivyo tu, itikadi na sera zake za Ki-karl Marx/Ki-Lenin, zilimletea maasi mengine ya ndani na juu ya vita ya Eritrea, kufuatia zoezi lake la utaifishaji wa njia kuu za uchumi kwa kasi ya kutisha; kuanzia na Makampuni ya Bima na Mabenki (Januari 1975), Viwanda vikubwa na Makampuni ya biashara (Februari 1975), ambapo Machi 1975, alitaifisha ardhi yote na hivyo kuharibu kabisa nguvu za kiuchumi za utawala uliopita na masalia yake.
Kwa mfano, katika jimbo la Tigray, waasi waliunda Jeshi la ukombozi la “Tigray People’s Liberation Front” (TPLF) kwa msaada wa Wa-eritria.
Na huko Ethiopia ya Kusini, Wa-Oromo walikuwa na Jeshi la “Oromo Liberation Front” (OLF) likiungwa mkono na Wasomali, ambao nao walifufua Jeshi lao la ukombozi – “The Western Somali Liberation Front” (WSLF) ili kurejesha “ardhi yao iliyopotea”.
Hatimaye, Mei 1991, Kanali Mengistu Haile Mariam alizidiwa nguvu na muungano wa Majeshi ya waasi wa Eritrea na Tigray na kukimbilia uhamishoni.
Matokeo ya kura ya maoni iliyoitishwa Julai 1991 chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kujadili hatima ya Eritrea, yaliwezesha Eritrea kurejeshewa uhuru kamili mwaka 1993, na hivyo kufunga ukurasa wa miaka 30 ya Vita kwa nchi hiyo.
Hatuwezi kuyapuuza malalamiko ya Wazanzibari juu ya uendeshaji wa Muungano wetu wenye kuzua kero. Kama ambavyo Serikali ya Ethiopia ilivyoutumia utengano wa Waeritrea milioni tatu kushinikiza mambo yake yasiyo ya Muungano, na hatimaye Eritrea kumezwa ndani ya Ethiopia; ndivyo nasi tulivyo na kila sababu ya kuhofu juu ya SUK, iwapo Wazanzibari wataungana na baadaye kutaka tafsiri sahihi ya Muundo wa Muungano wetu, ambao kwa muda mrefu, kero zake zimekosa utashi wa kuzitafutia ufumbuzi.
Na ingawa SUK haiwezi kuzua mtafaruku mkubwa kwa sasa kwa Muungano wetu kama ilivyokuwa kwa Ethiopia na Eritrea, lakini lazima tujiandae kwa mazingira mapya Visiwani chini ya SUK, ambayo kwa vyovyote vile, yatagusa mustakabali wa Muungano.
Itaendelea.

CHANZO: RAIA MWEMA

Advertisements

4 responses to “Tusipoujadili Muungano kwa makini, utavunjika

 1. sema weeeee , muungano hautakiwi znz ktk njia yoyote ile na kabla hatufakia hali ya kuingia msituni na kuuana kama huko ethiopia au sudan kama ulivyotoa mifano yako , chachandu mpopo haipati kitu

 2. Hakuna haja ya kujadili hoja alizotoa Bwana Mihangwa ambae kiukweli ni mshiriki tu kati ya waandishi mahiri wa makala za kisiasa na kijamii hapa Tanzania. Nasema mshiriki kwasababu makala zake nyingi hazilengi kuwapap watu mwanga kwa kupitia umahiri wa ujenzi wa hoja kama waandishi wengine wanavyofanya. Badala yake Joseph Mihangwa anaingia katika orodha ya waandishi ambao hutumia propaganda chafu kwa kudhani kuwa njia hiyo itaweza kuficha au kusahaulisha watu mabo yaliyopita husussan suala la muungano.

  Katika hoja nyingi alizotoa Mihangwa katika makala yake hii lengo sio kueleimisha lakini ni kutia propaganda chafu katika akili za watu. Mfano katika makala yake hii napenda nimnukulu akisema.
  “…Wazanzibari kuruhusiwa kumiliki ardhi Tanzania Bara; au Wazanzibari kushika nafasi za uongozi katika Serikali ya Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, wakati Watanzania Bara hawaruhusiwi kugusa mambo hayo Visiwani”

  Kama utaisoma vizuri sehemu hii ya makala ya Mihangwa na kuangalia hali halisi ya mambo yanavyoendeshwa utagundua kuwa. Tanganyika ilijivisha koti la Tanzania kuendesha mambo ya muungano, na wizara zote za Tanganyika hata zile zisizo za muungano zimebandikwa jina la muungano. Na kama hilo halitoshi Wazanzibari walio katika wizara hizo hawakuajiriwa kwa kigezo chochote ambacho kiko wazi na kueleweka. Wengi wao wamepewa nafasi hizo ili kufumbwa midomo tu. Sasa unapomsikia mtu kama Mihangwa anadai kuna Wazanzibari walioajiriwa katika seraikali ya Muungano na kudai ati wao Wabara hawagusi kitu hili ni kweli. Kwa vile Zanzibar haijajivika koti la muungano haiwezi kuwakosesha haki rai zake na kuwaajiri Watanzani nkutoka bara. Mihangwa anaingia katika sampuli ya wale wapotoshaji wanaojidai kuwa ati Tanzania Baba (TANGANYIKA) inawasaidia Wazanzibari. Kitu amabcho hata mgonja wa akili wahezi nkukikubali.

  Iweje TANGANYIKA ipokee miokopo pamoja na ruzuku halafu iinyime Zanzibar ambae ni mdau na mshiriki mkuu katika kile kitu kinachoitwa muungano? Isitoshe mamlaka ya mapato TRA= TANGANYIKA REVENUE AUTHORITY inachukua mapato ya Wazanzibari hata katika sekta ambazo sio za muungano, mfano hata muuza maandazi na muuza kiduka cha bizari utaona ameekewa karatasi limeandikwa leseni ya biashara yenye nembo ya TRA . Je haya akina Mihangwa hawayaoni?

  Ati kwa kujifanya anampenda Nyerere Mihangwa amechomeka hoja katika makala yake kuufananaisha Muunagano huu na ule wa Ethiopia na Eritrea, kwa kutaja mamabo kama ya ubaguzi kitu ambacho anafanya huyu jamaa ni kupotosha ummah kwa kufananisha “unrelated things” vitu visivyohusika.

  Tunakwambia Mihangwa na wenzio akina Lula wa Ndali Mwananzela, Muungano umedumu kwa kutumia vitisho, usiri katika kuuendesha , hadaa pamoja na upotoshaji wa viongozi waliojali maslahi yao. Na hawa akina Mihangwa na wenziwe nao wanafauta mkondo huo huo. Hawaoni hata aibu.

  Kibaya zaidi hawa wenzetu ni malimbukeni, ukigusa Muungano utawsikia mara Wapemba wapo Karaikoo, mara wanamilki ardhi, mara wameowana na wabara, yaani hawa wenzetu hawana hoja ni upuuzi tu na kutandaza pumba.
  Badala ya kuwashukuru Wazanzibari kwa kuwajengea uchumi wanaanza kuwatusi na kuwatisha. Lakini wasichofahamu ni kuwa sisi Wzanzibari sio malimbukeni, kila pahali duniani tupo, tunatafauta maisha na hakuna aliyelalamika kwa sisi kufanya hivyo.

  Namalizia kwa kusema kuwa Muungano huu hautalindwa kwa kuwapotosha wananchi na kutumia vitisho. Muda huo umepita, mabadiliko ni suala la lazima.

  “ZANZIBAR HURU KWANZA “

 3. Muungano huu unamapungufu mengi na kama alivyosema muandishi ulidumu kwasababu ya khofu!
  Ikiwa sote tunakiri kuwa vita baridi na sindikizo za mataifa ya nje zilichangia kumezwa kwa zanzibar hatuna budi kuirejeshea zanzibar uhuru wake ili iweze kujiendeleza na kuishi maisha karima.
  Hapana shaka kilichokusudiwa sio muungano bali nikuiondoa zanzibar katika ramani ya dunia.
  Ikiwa Tanganyika inajigamba kuzisaidia nchi nyingi afrika kupata uhuru wake!
  Nasisi tunawaomba wafanye bidii na busara ya kuturejeshea uhuru wetu.
  Huika zanzibar,huika uhuru wetu na visiwa vinavyotuzunguka.

 4. Du hizi makala nyengine zinazinguwa na kwa kweli kwa muda huu ndugu zanguni musipige debe kuhami muungano huu wa kidhalim ambao sisi wazanzibari hatuutaki. Sisi kwa muda huu hatusikii lolote isipokuwa ni kuvunja jinamizi la muungano tu. Nyinyi tayari mushatunyonya vya kutosha kwa miaka 48 takriban sasa mutuachie tupumue kwa hali ya maelewano. Mukijifanya wajanja na ikiwa munahila za kijanja na munataka kutuchezea ule mchezo wa katafunuwa kwa muda huu sisi hatutakubali na mutakuja juta baadae kaeni mukifahamu umma ukishaamuwa hamuna uwezo wa kuwazuwia. Muungano huu hatuutaki na utavunjika tu. Mukitaka musitake na wala hamuna ubavu na hilo wacheni kutuletea makala potofu mara Ethiopia, Eritria, Scotland, Uingereza sisi si watoto wadogo wacheni kutuletea pumba wewe, tunasema kwa sauti kubwa ZANZIBAR BILA YA MUUNGANO INAWEZEKANA. HATUUTAKI MUUNGANO. ZANZIBAR HURU KWANZA. MENGINE BAADAE.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s