Zanzibar Yetu

soma uzinduke

ASALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH  TAALA WABAKAATUH.

Mpendwa Msomaji wa weblog hii, ninakukaribisha katika jukwaa hili la

Salma Said

mawasiliano baina yangu, kama msimamizi na mwendeshaji wa weblog hii, nawe mpendwa msomaji. Pamoja na hayo, weblog hii inatarajiwa iwe jukwaa baina ya Zanzibar na ulimwengu huu mpana ambao sasa umefanywa uwe mwembamba kutokana na njia kama hizi za mawasiliano ya mtandao.Mimi naitwa Salma Hamoud Said. Ni Mzanzibari niliyezaliwa Hurumzi Mji Mkongwe, Zanzibar, mji ambao sasa ni urithi wa kimataifa. Familia yangu inatokana na ukoo wa Al Marhuum Rashid Bin Slim Al-Ghaithiy wa Mwera Kiongoni. Nina fakhari ya kuzaliwa, kukulia na kuipenda Zanzibar. Kwangu Zanzibar sio tu kwamba ni nchi yangu ya uzawa, bali ni heshima yangu.

Mimbar ya Msikiti Mkongwe wa Kizimkazi unaoaminika kuwa wa mwanzo katika upwa wa Afrika ya Mashariki

Nchi hii ya Visiwa imekuwepo kwa karne na karne huku watu wake wakiishi pamoja kwa masikilizano na upendo hata pale inapotokea pana tafauti za kidini, kisiasa au kiuzawa. Kwa mfano, licha ya kuwa Uislam ndio dini kuu ya Zanzibar huku zaidi ya asilimia 99 wakiwa ni waumini wa dini hiyo, nimezaliwa na kukulia katika Zanzibar inayotambua uwepo wa dini nyengine kama vile Ukristo, ambao ulifika Zanzibar kabla ya nchi yoyote ya Afrika Mashariki na Kati. Ushahidi wa ukongwe wa Ukristo Zanzibar ni kanisa la Minara Miwili lililopo Mji Mkongwe, mji ambao nimezaliwa.

Nimekuwa mwandishi wa habari tangu mwaka 2000. Ninaandikia magazeti ya Mwananchi na The Citizen na pia naripoti kwa Sauti ya Ujerumani (DW)kutokea Zanzibar. Pia nimewahi kufanya kazi na Radio ya Voice Of America (VOA) na BBC Monitoring na pia hadi sasa nimekuwa mchangiaji wa makala kwa magazeti mbali mbali kama An Nuur la Dar es Salaam na Dira Zanzibar. Gazeti la Dira lilisimama kama sauti ya Wazanzibari lakini likaja kupigwa marufuku na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa madai kwamba lilikuwa likikiuka maadili ya uandishi.

Kanisa la Minara Miwili, Shangani, Zanzibar. Nalo ni katika majengo makongwe ya ibada katika Afrika Mashariki

Baada ya kufanya uandishi wa habari wa kimapokeo kwa miaka kadhaa, sasa nimeamua kuongeza ufanisi katika fani hii ya khabari kupitia kuchapisha kwenye mtandao, ambako jukwaa na hadhira itaongezeka hasa kwa wale walio nje ya Zanzibar na Tanzania.Kwa Kiswahili kibovu, njia hii ya mawasiliano huitwa gazeti tando, yaani gazeti linalochapishwa mtandaoni. Pamoja na kutokukubaliana na tafsiri hiyo, lakini dhana ipo pale pale kwamba ninatumia njia hii ya mawasiliano kuchapisha habari, makala, tafiti, na maoni mbali mbali kuhusu mada tafauti kama zinavyojitokeza katika jamii yangu ya Zanzibar.Kupitia weblog hii, msomaji ataweza kusoma khabari mbali mbali za Zanzibar kama zilivyotokea.

Jua likituwa Magharibi ya kisiwa cha Unguja. Mandhari nzuri na adimu

Kutokana na ukweli kwamba mimi mwanzilishi na muendeshaji wa weblog hii ni mwandishi wa khabari, msomaji ategemee kuzipata khabari moto moto kama zinavyotokea kwa njia zote mbili: kuzisoma kupitia magazeti ya Mwananchi na The Citizen na kuzisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle).

Saa kongwe kwenye Mjini Mkongwe

Vile vile kutakuwa na makala na taarifa za Uchambuzi kuhusu hali ya kijamii ya Zanzibar. Hali halisi ya hali za maisha ya watu wa Visiwa vya Unguja na Pemba, matarajio yao, misimamo yao, imani zao na ustaarabu zitachambuliwa katika ukurasa huo.Pamoja na hayo, kutakuwa pia na ukurasa maalum kuhusu siasa za Zanzibar.

Hii ni mada inayovutia wachambuzi wengi wa siasa za ndani na nje na weblog hii inakaribisha michango ya wachambuzi hao.Weblog hii pia ina ukurasa maalum kuhusu taarifa na makala mbali mbali zilizokuwa zimetayarishwa na kutolewa na katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani Deutshe Welle (DW) ambazo zinahusu maisha ya kila siku ikiwemo siasa, utamaduni, jamii pamoja na makala za wanawake na maendeleo, mazingira, haki za binaadamu utamaduni na sanaa na mengi zaidi kutoka Zanzibar.

Zanzibar Yetu

Lakini suala la uchumi nalo halikuwachwa nyuma katika blog hii hasa kwa kuzingatia Visiwa vya Zanzibar vinategemea sana bahari na biashara za mpito katika uchumi wake. Zao la karafuu limeporomoka na utalii bado haujakidhi haja ya kuwa muhimili wa kiuchumi kwa Wazanzibari wenyewe. Hizo ni baadhi ya mada ambazo weblog hii itazichambua.Kuna safu ya Makala na Uchambuzi ambayo baadhi ya mambo yanayojitokeza hapa Zanzibar huandikwa katika safu hii kwa urefu zaidi ikiwa ya kisiasa, kidini au kiuchumi kwa lengo la kuwapa nafasi wasomaji wa blog hii kuweza kufahamu zaidi kwa kuwa taarifa zinazoendikwa huandikwa kwa ufupi lakini makala na uchambuzi hutolewa ufafanuzi zaidi.Nina heshima kubwa kukaribisha maoni ya kila mchangiaji na naahidi kuheshimu mawazo hayo. Hata hivyo, kwa ajili ya kulinda mila na desturi adhimu za Kizanzibari, sitachapisha maandishi yoyote yanayokwenda kinyume na utamaduni wetu.Kwa mawasiliano zaidi na mwenye Blog hii tafadhali tumia barua pepe: muftiiy@yahoo.com au simu nambari +255777477101

Advertisements