mnazi una faida lukuki

Mnazi kwa jina la kitaalamu unajulikana kwa jina la Cocos nucifera ambao huchukua miaka kadhaa kufikia umri wa kutoa mazao ambapo kufikia urefu baina ya mita 30-50 na mazao yake hutengenezewa vitu mbali mbali kuanzia mafuta ya kupikia sambuni, ulevi, siki, kamba, mafuta ya urembo, mafuta ya nywele, nishati, kutengenezea mshumaa, majarini ya kulia na kupikia na matumizi kadhaa yasiopungua 100.
Visiwa vya Unguja na Pemba navyo haviko nyuma katika kutengeneza vifaa vinavyotokana na mnazi ambapo Mfuko wa Kujitegemea katika mikakati ya kuwakomboa akina mama Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la SWISS CONTACTS wameweza kuwapatia mafunzo akina mama kutoka sehemu mbali mbali visiwani hapa kujifunza mambo mbali mbali ya kutengeneza bidhaa kadhaa kutokana na mnazi.

Wana historia wengi wanaona kuwa mnazi umefika katika maeneo mingi ya nchi ya joto kwa njia ya bahari, kusukumwa na kuangukia kwenye fukwe na kukuwa lakini wengine wanaamini kuwa minazi imefikishwa nchi za joto na wafanyabiashara waliotoka nchi za mashariki ya mbali.

Asili ya minazi wapi ilipotokea ni vigumu kueleweka lakini wachambuzi wengi wanafahamisha kuwa minazi asili yake ni nchi ya Malaysia na nchi ya Indonesia. Katika kumbukumbu zilizonukuliwa na Sanskrit zimefahamisha kuwa watu wa India wakitumia nazi kama chakula na matumizi mengi kwa mambo tofauti. Katika nchi ya India, Mnazi unajulikna kwa jina la kalpa vriksha, ikimaanisha kuwa “mti ambao utakupatia mahitaji yako yote yakukuwezesha kuishi”.

Wanahistoria wengi wanasema kuwa kiasili ukitoa Mashariki ya kati basi mnazi maskani yake kuu ni maeneo ya Afrika ya Mashariki, kwani kusini mwa Afrika maeneo kama Bukini minazi inaonekana kwa wingi lakini idadi yake sio kubwa kama ile minazi ambayo imeshamiri na kunawiri katika maeneo ya Afrika ya Mashariki.

Wasafiri mbali mbali katika kumbukumbu zao wametoa maelezo juu ya mnazi na kuupa sifa na namna walivyoweza kuuwona katika safari zao.

Mvumbuzi Maco Polo (1254-1324) anafahamisha kuwa alipofika katika maeneo ya Sumatra, India, na visiwa vya Nicobar aliwasikia watu wa maeneo hayo wakiita nazi kwa jina la “Tunda la Firauni”, kwani Marco Polo alikuwa akifahamu kwamba wafanyabiashara wa Kimisri katika karne ya 6 waliweza kuifikisha nazi nchini Misri baada ya kutoweka kwake ikiwa inaaminika kuwa katika nyakati za Mafirauni minazi ilikuwa ikionekana nchini Misri. Marco Polo anaelezea kuwa wafanyabiashara hao wa kimisri walizichukua nazi hadi Misri wakitokea maeneo ya Afrika Mashariki.

Wanahistoria wanazidi kueleza kuwa wafanyabiashara wa kiarabu ndio walikuwa watu wa mwanzo kuifikisha nazi Uingereza, kabla hata ya Wareno kufanya kazi hiyo kama inavyofahamika na wengi. Waarabu katika safari zao za kibiashara walifika katika maeneo ya Maldives huko waliona watu wa eneo hilo wanauenzi vya kutosha mnazi na kuanzia hapo nao wakaingiwa na hamu ya kununua vitu hivyo na kuvichukua na kurudi navyo makwao. Wakazi wa Maldives wanasifika kwa kazi ya ujenzi wa majahazi na katika karne ya 14 wafanyabiashara wa kiarabu waliwapa fedha nyingi wajenzi wa majahazi waundie jahazi kubwa ambalo litakuwa kazi yake ni kusafirisha nazi kutoka Maldives hadi nchi za mashariki ya Kati. Ilikuwa sio nazi tu ndio yenye kusafirishwa lakini makumbi, kamba copra na vyenginevyo vitokanavyo na mnazi vilisafirishwa na kupelekwa arabuni.

Antonio Pigafetta mtu mashuhuri atokaye katika mji wa Venice aliamua kufanya safari ya kuuzunguka ulimwengu akiwa kama mtalii. Aliungana na mweledi tajiri mmiliki majahazi Ferdinand Magellan katika mwaka 1519 kuanza safari yake ya kuuona ulimwengu, aliingia katika moja ya majahazi 5 ya Magellan na alikuwa katika safari hiyo akimtaka nahodha wa marekebu hiyo afike kwenye maeneo ambayo ataweza kuiona minazi.
Magellan alivunjika moyo kutokana na kutumia siku nyingi katika safari yao bila ya kukutana na mnazi, hadi alipofika katika kisiwa cha Guam ambako hapo waliteremka na kuiona minazi lakini alikuwa hajavutiwa na wakazi wa Guam kwa kuwa walijivalia majani ya mnazi na kuwa na vipande vya mifupa vya wanadamu wamejifunga kama ni mapambo. Magellan aliwaomba wakazi hao wa guam kumpatia nazi na walimgaia za shehena mzima.
Pigafetta katika kumbukumbu zake aliweza kuandika yafuatayo, “Nazi inatokana na mnazi. Ilivyokuwa sisi tunakula mkate, tunakunywa pombe aina ya wayni na kupata siki kutokana na nyezo mbali mbali, lakini hivyo vyote hupatikana kutokana na mnazi, na minazi miwili inaweza kuilisha familia ya watu kumi wakaishi kwa kipindi cha miaka 100”, alisema

Baada ya safari ya Magellan na kuwa na kumbukumbu nyingi, alifuata Muingereza Sir, Francis Drake aliyeamua kusafiri kutoka Uingereza hadi visiwa vya Cape Verde viliopo Afrika ya magharibi katika mwaka wa 1577, Drake alivutiwa mnoo na mnazi na akaandika kwamba “ Aaah mnazi haujulikani kwetu Uingereza unahitajia uelezewe na watu waujuwe”.
Ingawa wasafiri wengi na wavumbuzi waliweka kumbukumbu katika maandishi yao juu ya mnazi, lakini mnazi ukawa bado haujulikani nje ya mipaka ya maeneo ya joto. Muingereza J.W. Bannett naye aliandika waraka mrefu ambao aliuelezea mnazi kinaga ubaga, kwanza mnazi ni chakula, unatoa kamba, msuwaki unapatikana kutokana na manzi, ulevi dawa za kutibu maradhi mbali mbali.
Baadhi ya viwanda vya ulaya vilivyokuwa vinatengeneza bidhaa mbali mbali zinazotokana na nazi havikusita kutengenezwa vitu kama kashata, biskuti na tamtamu nyenginezo.
Kampuni ya kifaransa ijulikanayo kwa jina la J.H. Vavasseur ilianzisha misfara ya kubeba nazi kutoka nchi iliyokuwa ikijulikana kama Cyelone ambayo sasa inaitwa Srilanka na kuzisafirisha hadi ulaya hayo yalikuwa katika miaka ya 1890. Shehena ya nazi aliyekuwa kibeba kwa mwaka ilikuwa ni tani alfu sita katika mwaka huo nakuzidi hadi kufikia tani sitini alfu kwa mwaka.
Ikiwa watu wa bara la ulaya wameshakuwa ni watumizi wakubwa wa nazi, wakazi wa Marekani walianza kutumia nazi katika mwaka wa 1895 ambapo mfanyabiashara wa maeneo ya Philadelphia, Franklin Baker alipopokea shehena ya nazi ikiwa ni malipo aliyolipwa na mfanyabiashara wa Cuba.
Awali nazi ilikuwa haijulikani kabisa baadae ikajulikana faida zake na kuja fikra ya kuitangaza kwa matumizi ya majumbani na kwenye mabekari hapo ndipo mfanyabishara wa Cuba aliweza kufanikiwa vya kutosha na kuanza kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na mnazi.
Maandazi yaliopambwa na nazi pamoja na uji wa nazi ulikuja kuwa maarufu sana katika maeneo aya Marekani mwanzoni wa mwaka wa 1900 na baadae kusambaa duniani kote.
Nchi za Indonesia, Malaysia, India na Sri Lanka ni wazalisahaji wakubwa wa nazi na hupata mapato makubwa kutokana na mazao ya nazi, nchi ya Marekani kuanzia miaka ya 1898 ilianza kuagizia mazao ya nazi kutoka maeneo ya Philippines.
Wa-Zanzibari kwa dahari wamekuwa ni watumizi wakubwa wa nazi, tuwi la nazi hupikiwa mapishi mbali mbali, wali wa nazi, uji wa kunde, ndizi mbichi na mbivu za nazi, viazi vikuu vya nazi, kashata ya nazi. Mikeka, mazulia, kamba, na hata makumbi hutumiwa kama ni nyezo ya nishati.
Zanzibar ilikuwa ni msafirishaji mkubwa wa zao la nazi, kabla ya mwaka wa 1950 inakisiwa kuwa asilimia 60 ya nazi iliyozalishwa visiwani Zanzibar ilikuwa inasafirishwa kupelekwa nchi ya Marekani na asilimia 40 iliyobaki ndio iliyokuwa ikitumiwa kwa matumizi ya nyumbani.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na Shirika la Swiss Contacts la Nchini Sweden limeona umuhimu wa zao hilo imewakusanya wanawake 30 wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba kwa lengo la kutengeneza bidhaa hizo ili wanawake hao waweze kujikwamua na umasikini pamoja na kutumia baadhi ya bidhaa wanazotengeneza kwa matumizi ya nyumbani na nyengine kuuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akina mama hao wamejifunza njia bora na za kisasa katika kuzalisha bidhaa zinazotokana na mnazi ambao ni zao maarufu sana katika Mwambao wa Afrika Mashariki na visiwa vya Zanzibar.
Wakufunzi wa bidhaa hizo kutoka Kenya na wenyeji Zanzibar waliwafunza wenziwao kutengeneza vifaa mbali mbali ikiwemo vifaa vya kuwekea sigara, kuchonga visanamu kwa kutumia nazi yenyewe, upawa wa kuchotea mchuzi ambao unatokana na kifuu cha mnazi pamoja na cherewa
Pia wanawake hao walijifunza namna ya kutengeneza vipodozi mbali mbali ikiwemo vyakula kama kashata, cream za kila aina ambazo huchanganyishwa na parachichi, vipodozi vya kupamba ndani ya nyumba, mafuta ya nazi badala ya kuwa na maji maji yametengenezwa na kuwa ya mgando mafuta ya muarubaini ambayo husaidia katika ngozi chakavu,.
Kwa upande wa mapambo ya kike wanawake hao wameweza kujifunza namna ya kutengeneza herini, vidani, pete na bengili ambazo huchorwa majina pamoja na mikopa ya kisasa.
Pia wameweza kujifunza namna ya kusokota kamba ya kutengenezea mazulia ya kuweka mlangoni kwa njia rahisi badala ya kutumia njia ile ya asili ya kusokota kwa kutumia mguu.
Wakina mama hao pia wamepata fursa ya kutumia mashine maalumu zilizobuniwa na Mzanzibari, Ramadhan Omar ambapo wataweza kusokota kamba bila ya kutumia miguu. Jambo ambalo litarahisisha utengenezaji wa kamba hizo.
Akifunga mafunzo hayo yaliofanyika Chuo cha Utalii Zanzibar ambapo jumla ya wajasiriamali 30 walipata mafunzo, Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma, aliwataka wakina mama hao walioshiriki wayatumie mafunzo walioyapata kutoka kwa wakufunzi ili waweze kujikomboa na umasikini.
Aliwaomba akina mama hao wanaporudi katika vikundi vyao wayatumie vizuri mafunzo hao na wawafundishe wenziwao ambapo vikundi vitaweza kuzalisha zaidi bidhaa zilizo bora na viwango vinavyokubalika pamoja na kuongezeka kwa vikundi vya akina mama hao.
Bi Asha waliwataka wakina mama hao kuyatumia mafunzo vizuri na kuvitumia vifaa vipya walivyopewa katika mafunzo hayo kwani kwani ulimwengu unabadilika na ule mfumo wa zamani wa kutengeneza kamba kutumia miguu umeondoka na badala yake wanatumia mashine maalumu za kusokotea kamba.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kujitegemea, Asha Khalfan kwa kushirikiana na Meneja Miradi wa Kanda ya Afrika Mashariki Swiss Contact, Dk. Ralph Engelmann wote walionesha furaha zao jinsi wakina mama hao walivyopokea mafunzo hayo na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi wanaporudi katika vikundi vyao.
Nao akina hao ambao walivalia kanga zenye picha ya mnazi wameahidi kuyatumia mafunzo walipata kwa kutengenezea bidhaa mbali mbali na kuiomba Serikali iwasaidie katika kutafuta soko la kupeleka bidhaa hizo ambazo wamesema watatengeneza vifaa mbali mbali kwa ari na nguvu mpya ili waweze kujikimu kimaisha.

Advertisements

2 responses to “mnazi una faida lukuki

  1. Hi.
    Nimeipenda sana makala hii, kwani mie ni mmoja kati ya watu wanaofuatilia kwa karibu umuhimu wa nazi na mazao yake. kwani ulimwenguni kote sasa nazi imejipatia umaarufu na inaitwa “Tree of Life”. Natoa changamoto kwa wahandisi mitambo kufanya utafiti wa kubuni machine zinazoweza kuwasaidia wajasiliamali hao ili kuwarahisishia kazi za uzalishaji wa mazao mbalimbali ya nazi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s