Jinamizi la mfumo kristo

Rais Mstaafu wa Zanzibar,Amani Karuma na Maalim Seif Shariff

Karume, Seif waupiga Chenga Mfumo Kristo, *CCM Bara haikutaka, ikapinga maridhiano *Kwa nini miafaka ya nyuma ilikufa? Jiulize

Wazanzibari wametakiwa kujiuliza ni kwa nini miafaka ya awali ya CCM na CUF ilifeli, lakini Maalim na Rais Mstaafu Mheshimiwa Amani Abeid Karume walipokutana kwa siri wakafanikiwa.Walifanikiwa kwa sababu waliupiga chenga Mfumo Kristo, “ukistuka Wazanzibari washapatana, ukakasirika, ukapinga na bado unaungulia kwa hasira.”

Katika hali hiyo imesemwa kuwa, Wazanzibari wakitafakari vyema, wataiona nguvu ya Mfumo Kristo na kutambua kwamba bila ya kuufyeka kwanza hakuna salama.

Hayo yameelezwa katika kongamano juu ya hatari ya Mfumo Kristo lililofanyika katika uwanja wa Mnazi Mmoja Wete, Pemba mara baada swalat Aswri Jumatatu Oktoba 3.

Katika kufafanua jambo hilo ilikumbushwa kuwa mara baada ya uchaguzi wa mwanzo wa vyama vingi mwaka 1995, uliibuka mgogoro wa kisiasa ambapo ilibidi pawe na mazungumzo yaliyohusisha wapatanishi kutoka nje ya nchi akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyauko.

Mwisho wa mazungumzoa ikafahamishwa kuwa umefikiwa muafaka. Huo ukawa muafaka wa kwanza.

Mtoa mada Sheikh Ilunga Hassan Kapungu akasema kuwa, hata hivyo, hadi unafikia uchaguzi mkuu mwingine hakuna kilichokuwa kimefanyika katika muafaka huo.

Kipigo kikawa kikali zaidi kilichowahusisha mpaka Janjaweed. Wananchi wakapigwa na kuteseka sana katika uchaguzi mkuu wa 2000 hadi kuuliwa mamia ya watu.

Kwa nini kilitembea kipigo? Sheikh Ilunga aliuliza na kufafanua kuwa kwa kupoteza nguvu ya kisiasa, Rais waliyemtaka Wazanzibari siye aliyetakiwa na Dodoma, hivyo kikapita kisago ili lile wasilolitaka Wazanzibari liwe.

Hali hiyo ilipelekea kufanyika mazungumzo mengine, yakiwahusisha tena makatibu wakuu wa CCM, Yusuf Rajab Makamba na wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.

Baada ya muda ikatangazwa kwa mbwembwe kubwa kuwa umepatikana muafaka.

Ukasifiwa sana kwamba ulitokana na sisi wenyewe bila kuhusisha mtu wa nje na kwa hiyo kutajwa kuwa wa maana na wa kupigiwa mfano.

Wengine wenye migogoro wakatakiwa kuiga Watanzania wanaoweza kutatua migogoro yao ya kisiasa wenyewe na kwa amani.

“Hata hivyo ilipofika wakati wa uchaguzi mkuu 2005 kipigo kikawa pale pale.”

“Muafaka haukufanya kazi, chuki na farka ikazidi kujengeka miongoni mwa Wazanzibari.” Alisema Sheikh Ilunga katika kongamano hilo.

Akasema kuwa hali hiyo ilimfanya Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwanzo Bungeni baada ya kuingia madarakani kuahidi kwamba katika jumla ya mambo atakayoyashughulikia mwanzo ni pamoja na hili la mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

Ilunga akasema kuwa, pamoja na jitihada za kisiasa zilizofanyika baada ya kauli na ahadi hiyo, suala hilo lilipelekwa katika kikao cha CCM Butiama na kujadiliwa juu ya uwezekano wa kuwa na serikali ya Mseto.

Hata hivyo akasema, hakuna maafikiano yaliyofikiwa Butiama, kikao kikavunjika watu wakaachana kila mtu akishika njia yake, Wazanzibari wakarudi Unguja na Pemba wakiwa na chuki zao na siasa za visasi. Ile agenda ya kuwa na serikali ya ‘mseto’ ikafa.

Baada ya hapo, Ilunga akasema kuwa kilipiga kimya, mpaka siku isiyotarajiwa kukapambazuka watu wakitangaziwa kuwa tayari CUF na CCM, Rais Karume na Maalim Seif, walishafanya mazungumzo na kufikia maridhiano ya kuzika tofauti zao na kufungua ukurasa mpya wa amani na utulivu Zanzibar.

Ilunga katika mawaidha yake kwa watu wa Wete akasema kuwa ajabu ya mambo ni kuwa wa kwanza kupinga maridhiano hayo ilikuwa CCM ambapo Katibu Mwenezi wake alisema kuwa maridhiano hayo hayana ridhaa ya CCM.

“Katibu Mwenezi huyo alipinga kwa sababu maridhiano hayo hayakuwa na ridhaa ya Mfumo Kristo, miafaka ya mwanzo ilikufa kwa sababu Mfumo Kristo ulikuwa hautaki Wazanzibari muelewane, Rais Mstaafu na Maalim Seif, waliupiga chenga Mfumo Kristo ndio maana walifanikiwa na sasa mpo katika amani.”

Alisema Sheikh Ilunga na kusisitiza kuwa Wazanzibari wanatakiwa kuwaunga mkono viongozi wao na kuhakikisha kuwa wanayalinda maridhiano yaliyofikiwa.

“(Kadinali) Pengo halali toka mmeridhiana, Mfumo Kristo unagugumiya, umekasirika, unachukia mkaridhiano haya”.

Aliongeza akihimiza kuwa ni lazima Wazanzibari wawe macho asijekutokea kidudu mtu wa kuwarejesha tena katika shimo la moto walilotaka kutumbukia.

“Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu. (Zamani) mlikuwa maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo, kwa neema yake, mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto (wa Jahannam), naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kuongoka.” (3: 103)

Alinukuu aya hizo zinazopatikana katika sura Al Imran akihimiza kuwa kilichotokea ni nusra ya Allah na hivyo inapasa kushukuriwa na kuithamini, lakini pia kuwa macho adui asiihujumu.

MWISHO

Taasisi nyeti zisiwe miliki ya wachache

 

*Baraza la Mitihani lifumuliwe kujenga imani *Serikali haina Sabato, wala siku ya Mungu jua

Baraza la Mitihani la Taifa pamoja na taasisi nyingine  nyeti zinatakiwa kuwa na muundo ambao utawafanya wananchi kuwa na imani nazo kutokana na kazi zake  muhimu kwa taifa.Haitakuwa jambo lenye masilahi na taifa iwapo taasisi hiyo itaonekana kuwa miliki ya watu wa dini fulani kutokana na wingi wao na kushikilia nafasi zote muhimu za uongozi katika Baraza.

Hayo yameelezwa katika kongamano la Waislamu lililofanyika Ole Kianga katika viwanja vya Ijitamai Jumapili iliyopita.

Kwa upande mwingine imeelezwa kuwa serikali haina Sabato wala siku ya mungu jua (Sunday) kwani yenyewe inajinadi kuwa haina dini.

Kwa sababu hiyo imetakiwa isiwe na mapumziko ya Sabato (Jumamosi) wala mapumziko ya Jumapili, kwani hizo ni siku za Wasabato na Wakristo.

La kama inataka kuzienzi siku hizo kwa vile Watanzania wana dini zao, basi ijumlishe pia na Ijumaa.

“Baraza la Mitihani la Taifa litoe ushirikisho ulio sawa kwa Waislamu na wafuasi wa dini nyingine.” Limesema tamko la Waislamu katika kongamano hilo.

“Kwa sababu serikali haina dini, siku za mapumziko ya kazi (za wiki) zisizingatie dini yoyote ile,…(la sivyo) Ijumaa nayo ifanywe siku ya mapumziko.”

Limeongeza tamko hilo kama lililovosomwa kabla ya kufungwa kongamano.

Tamko hilo lililopewa anuwani ya “Tamko la Waislamu wa Pemba juu ya madhara ya mfumo kristo kwa Waislamu wa Pemba”, limetoa mapendekezo kadhaa kuhusiana na mabadiliko ya katiba yanayosubiriwa.

“Katiba izingatie kwamba zilizoungana ni nchi mbili kwa hivyo kila nchi iwe na haki sawa na mwenzake.”

Hilo ni pendekezo la mwanzo ambalo lilifuatiwa na kauli kwamba iwe marufuku kwa katiba kuifuta nchi yoyote katika hizi zilizoungana.

Na katika kuliwezesha hilo, mfumo mzuri wa muungano unaopendekezwa ni ule wa serikali tatu.

Kwa upande mwingine tamko la Waislamu wa Pemba limesema kuwa, haitakuwa jambo la busara kwa Wazanzibari kuacha maadili yao ya Kiislamu yakavurugwa kupitia mlango wa muungano.

Kwa hiyo watizame historia yao, maadili yao, dini yao, utamaduni wao, na sio kuparamia yanayoitwa maadili ya ki-Tanzania.

Aidha, limetaka kuwe na udhibiti wa utoaji wa ardhi kinyume na ilivyo hivi sasa ambapo, hata wale wasio Wazanzibari wamerahisishiwa kununua na kumiliki ardhi Zanzibar.

“Sheria ya ardhi Zanzibar itoe kipaumbele kwa wananchi wake ambao wanaendelea kuburuzwa kwa spidi (kasi) kubwa, siyo kila anayetaka anapewa ardhi hata kama si Mzanzibari.” Limesema tamko.

“Bali pia ujenzi wa majengo ya ibada utilie maanani uwepo wa waumini wake siyo kujenga majengo ya ibada hata kama uwepo wa waumini wake ni mdogo. Mfano mzuri ni ujenzi wa makanisa katika kambi ya jeshi ya Vitongoji ambapo hivi sasa kuna makanisa yasiyopungua (matatu) 3.”

Limeongeza tamko hilo likieleza jinsi Wakristo wanavyohodhi ardhi kwa kisingizio cha kujenga makanisa ambayo mengi hayahitajiki kwa vile hakuna waumini wa kuyajaza.

TAARIFA HIZI NI KWA HISANI YA GAZETI LA ANNNUR 

Leave a comment