Shivji na mapambano ya wanyonge

Mwenyekiti wa kigoda cha Mwalimu Nyerere, Issa Shivji

Ahmed Rajab

USTADHI Issa Shivji ni mtu mwenye sifa nyingi. Ni mwalimu, mwanasheria anayeheshimika duniani na mwanaharakati. Lakini kwa maoni yangu zaidi na hata unyenyekevu wake sifa yake iliyozipiku zote hizo ni ile ya kwamba yeye ni msomi wa umma. Tena ni msomi wa umma anayejiamini.

Katika taifa kama la Tanzania lililojaa wachochole, kaumu ya watu walio hohehahe, sifa hiyo inampa Shivji dhima kubwa katika jamii. Ni dhamana anayoibeba bila ya kuchoka, bila ya kunung’unika na bila ya woga kwani kila siku kazi yake ni kuwaelimisha na kuwatetea walio wanyonge.

Anapokuwa anawaelimisha anakuwa papohapo ‘anawawezesha’ yaani anawapa nguvu au uwezo wa kutumia hoja za kuwawezesha kuuondosha unyonge wao.

Katika sahafu au safu hii nimeamua kukizungumza kitabu chake kilichozinduliwa hivi majuzi wakati wa Tamasha la Kitaaluma la Mwalimu Nyerere lililofanywa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kitabu chenyewe — Insha za Mapambano ya Wanyonge — ni mkusanyiko wa makala mbalimbali za Shivji. Takriban insha zote hizo zimekwishachapishwa kwenye majarida na magazeti mbalimbali.

Insha hizi zinajadili mada zenya kuyagusa maisha ya wanyonge ambao ndio walio wengi katika jamii yetu. Amezigawa mada hizo katika mafungu manne. La kwanza ni insha zenye kuuchambua uchumi wa taifa na rasilimali za umma. La pili linakusanya insha zinazojadili medani ya ushirikishwaji, demokrasia, katiba na Muungano. Insha za sehemu ya tatu zinagusia ubepari, ujamaa na ufisadi na fungu la mwisho lina insha kuhusu falsafa ya Mwalimu Nyerere na usononi wa wasomi.

Kwenye tabaruki ya kitabu, Shivji anaeleza ya kuwa kitabu hicho ni kumbukumbu ya marafiki zake watatu ambao hanao tena duniani: Chachage Seithy Chachage, Haroub Miraji Othman na Henry Mapolu. Hawa wawili wa mwisho walikuwa pia marafiki zangu na makomredi wangu. Chachage, aliyekuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sikuwa nikimjuwa hivyo ingawa niliwahi kuwa naye miaka kadhaa iliyopita jijini Kampala, Uganda, kwenye kongamano moja lililokuwa limeandaliwa na Vuguvugu la Ujumuiya wa Afrika (Pan-African Movement).

Nimeandika kwamba Shivji ni msomi wa umma na nilifurahishwa kuona kwamba yeye mwenyewe katika kitabu hiki ameandika insha moja kumhusu Chachage aliyefariki dunia ghafla Julai mwaka wa 2006. Anuani ya insha hiyo ni: ‘Msomi wa Umma, Utangulizi wa Kitabu cha Maandishi ya Chachage.’

Yote aliyoyaandika Shivji kumhusu Chachage yalinidhihirikia nilipokutana naye Kampala. Kubwa lililonivutia mimi ulikuwa msimamo wake wa kitabaka na kwamba hakuwa mmoja wa wasomi wa kibwanyenye.

Katika insha inayomzungumzia Chachage Shivji ameeleza jinsi wanyonyaji wa nje wanavyoshirikiana na vibaraka vyao vya ndani ili kutimiza malengo yao. Hivyo vibaraka vinakuwa madalali wao na vilikuwako katika vipindi mbalimbali vya kihistoria. “Kwa hiyo, utumwa ulikuwa na wanyapara wake; ukoloni ulikuwa na machifu, ukoloni mamboleo ukawa na marais na makamanda wake, na uliberali mamboleo au utandawazi una makuadi wake,” ameandika Shivji. Ameendelea kuandika kwamba Chachage katika riwaya yake Makuadi wa Soko Huria “anapambanua vizuri tu silika ya hao mabwana au kwa jina lake la kitabaka, vibwanyenye uchwara.”

Shivji ameandika mengine kumhusu Chachage na msimamo wake katika insha ‘Haya ni Mahindi, sio Makana’ ambayo ni hotuba aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Makuadi wa Soko Huria Oktoba 17, 2002.

Insha zilizomo katika sehemu ya tatu ya kitabu zinaulaani ubepari na zinawapa matumaini wale wanaodhalilishwa na wakandamizaji. Lugha na msamiati unaoutumiwa ni ule ambao wale wenye mtizamo finyu wa kijamii na wenye kuigiza mitizamo ya wasomi wakibwanyenye wanaukebehi. Wao wanapenda kusema kwamba uchambuzi wa jamii unaotumia dhana za Kimarx umepitwa na wakati.

Wanachopuuza ni kwamba siku hizi maandishi ya Karl Marx yanafufuliwa na kujadialiwa tena katika vyuo vikuu na taasisi za nchi za Magharibi kuangalia jinsi yalivyotabiri hali za kiuchumi na za kijamii zilizoibuka katika enzi hii ya ubepari uliofurutu ada na utandawazi.

Mengi ya yanayojiri sasa yalikwishatabiriwa na Marx. Utabiri huo unathibitisha ule ukweli wa kwamba ubepari kama tuujuavyo sasa unakaribia mauti. Dalili tunaziona katika nchi zenye chumi za kibepari. Nchi kadhaa za Magharibi, ikiwemo Marekani, tunaziona kuwa na ishara zitazoweza kuwa sababu ya kifo hicho.

Kwanza kuna hali ya mfumo wa kifedha usio thabiti, kuna matatizo ya afya, mifumo yao ya kisiasa imepwaya na kwingine, hata imekufa ganzi na kuna uharibifu mkubwa wa mazingira.

Ndiyo maana nchini Marekani na katika nchi nyingine za Magharibi watu wanajiuliza iwapo taklifu za maisha wanazokumbana nazo kila siku zinatokana na mfumo uliopo wa ubepari wa soko na iwapo kuna mifumo mbadala ya kiuchumi inayoweza kuwapatia faraja. Kwa hakika mfumo wa uchumi wa kibepari tulio nao umo ukingoni na unastahiki uwe unajitayarisha kujizika.

Nasema hivyo kwa sababu haiwezekani kwamba ubepari wa kisasa utaweza kuendelea daima. Mfumo huo una madosari mengi na nyufa nyingi. Umezusha tofauti kubwa za kitabaka baina ya walio nacho na wasio na kitu ila utu.

Aidha, bado hatukuuona ubepari ulio muadilifu au utandawazi ulio na maadili. Wenye kunufaika katika mifumo hiyo ni wanyonyaji na wakandamizaji tu. Wanaodhalilika ni wananchi wa kawaida wasio na uwezo wa kujipatia riziki, wasiopata matibabu wanayostahiki, wasioweza kuwasomesha watoto wao na wanaosononeka kila uchao.

Katika nchi kama Tanzania tunashuhudia jinsi mfumo wa utandawazi ulivyofumka, jinsi utajiri mkubwa unavyowawezesha watu binafsi au vikundi vya watu vyenye mtandao wao kununua madaraka ya kisiasa. Wakishayapata hayo madaraka huyatumia ili kuzidi kujitajirisha. Wanachofanya ni kuila nchi.

Tatizo la Tanzania si ufisadi bali ni mfumo mzima wa kibepari na wa utandawazi ambao Tanzania, kama gombe lililotiwa shemere, inaburutwa kuufuata. Mfumo huu lazima ubadilishwe.

Shivji alianza kuichambua jamii ya Tanzania na siasa zake tangu enzi za Nyerere. Alitambua na mapema kuwa Tanzania ni taifa la matabaka, kwamba matabaka hayo yanakinzana na kwamba huo mpambano wa kitabaka, ingawa wa kimyakimya, ni wa wafanyakazi na wavujajasho dhidi ya mabepari wenye kuwanyonya. Hayo ndiyo maudhui ya kitabu chake cha kwanza — The Silent Class Struggles in Tanzania (Vita baridi vya kitabaka katika Tanzania).

Alikiandika kitabu hicho alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kitabu hicho kilimjenga na kumpatia sifa hadi nje ya mipaka ya Tanzania kwa uchanganuzi wake uliopevuka.

Shivji amejitweka jukumu la kuwatetea na kuwapigania wanyonge, wale walio dhaifu katika jamii. Inatupasa tutoe tanbihi hapa ya kutanabahisha kwamba kuna wanyonge na wanyonge.

Kuna wale waliosalimu amri na wanaojiachia, pengine bila ya kutaka, wakumbwe na jaala iliyowafika. Na kuna wale wenye mwamko na wasiokubali kunyanyaswa na kuonewa. Shivji anatambua kwamba hawa ndio wataofanya mapambano ya kujikomboa.

Shivji ni msomi mwenye kutwambia mambo tunayohitaji kuyajuwa na kuyaelewa. Haya yakiwa pamoja na mambo yaliyopita, yaliyosemwa au yaliyoandikwa katika enzi zilizopita na wasomi wa zama hizo. Kwa kufanya hivyo anatufanya tuwe kama tunaongea na magwiji wa kale. Yeye pia ni msomi aliyebobea kwa namna anavyozichambua dhana mbalimbali au kwa namna anavyotwambia tuiangalie fasihi na usanii kwa jumla na uhusiano wake na jamii.

Msomi wa aina ya Shivji ni hazina kubwa ya jamii na aghalabu huwako wachache kama hao katika kila jamii. Lengo lao kuu linakuwa si kujitakia uluwa katika kazi, kujipatia mishahara minono na kukumbatiwa na ‘wala nchi’ bali huwa ni kutafuta njia za kuwanyanyua wananchi kwa kuwaelimisha.

Kadhalika, huwa kama wanawashika masikio watawala wanaojifanya kuwa ni mamwinyi mamboleo na wanawaonyesha jinsi mambo yanavyotakiwa yawe.

Insha hizi za Shivji tunazozizungumzia zinazidi kudhihirisha jinsi uchambuzi wake wa mambo ulivyopevuka kwani anatasua na kuchanganua mambo mbalimbali kwa ustadi mkubwa sana.

Insha za Mapambano ya Wanyonge ni kitabu chenye uhondo mwingi na si dhamiri yangu kukuondoshea utamu wake kabla ya wewe kukisoma.

Nilichojaribu kufanya ni kukudodesha tu. Nina hakika kwamba kitabu hiki, ambacho si cha kusomwa kwa kikao mmoja, kitawavutia wengi wa marika tofauti na kila mzalendo anapaswa awe nacho.

Kinatufumbua macho na kuwaamsha waliopigwa na usingizi wa ulaghai wa mabepari na vishawishi vyao.

Kadri nitavyoandika juu yake sidhani kama nitaweza kukitendea haki. Lililobaki ni kwako msomaji kukitafuta na kukinunua. Bei yake ni shilingi za Tanzania 18,000. Kinapatikana kwenye maduka ya vitabu na pia katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, taasisi ambayo ndiyo iliyokichapisha.

Sikitiko langu ni kwamba ingawa kuna kiambatanisho cha Azimio la Arusha, kitabu hiki hakikuuweka Mwongozo wa TANU. Kwa mazingira ya sasa ya kisiasa nchini Tanzania na ufisadi wake uliozagaa pengine waraka huu ni mujarab zaidi kuliko Azimio la Arusha kwa vile unazungumzia aina ya viongozi wanaohitajika Tanzania hasa katika siku hizi za utandawazi.

9 responses to “Shivji na mapambano ya wanyonge

  1. kama ni mkweli na mwadilifu kama hivyo ulivyomsifu , kwa nini wazanzibari mpaka leo wanalazimishwa kwenye muungano ambao hawautaki ? na ikiwa yeye ni bingwa ktk sheria ameshindwa vipi kuwaongoza wanasiasa wa tanganyika kuwapa uhuru wazanzibari ? na badala yake akakubali kuwa mwenyekiti wa kigoda wa adui wa zanzibar ( mwl nyerere) , basi atambue professa kama walivyotangulia wenzake mbele ya Mungu na yeye hayuko mbali , aliye mbora ni yule ambaye ateleta manufaa kwa wengine kabla ya kuondoka duniani , ishauri wangu kwa profesa shivji kujiuzulu uenyekiti wa kigoda , badala yake aamke kuwapigania wazanzibari uhuru wao , hilo litakuwa bora kwake kuliko kuchapisha vitabu

    • Naungana na wewe kuhusu huyu jamaa inakuaje ushughulikie mambo ya Watanganyika wakati kwenu (Zanzibar) unatakiwa zaidi ili kuikimboa nchi yetu, achana na kigoda cha maluuni Nyerere badala yake njoo kwenye KIGODA CHA ZANZIBAR ili kijikomboe katika makucha ya Watanganyika.

  2. Asalamu Alaykum. Nina heshima kubwa kukaribisha maoni ya kila mchangiaji na naahidi kuheshimu mawazo hayo. Hata hivyo, kwa ajili ya kulinda mila na desturi adhimu za Kizanzibari, sitachapisha maandishi yoyote yanayokwenda kinyume na utamaduni wetu, matusi au dharau ya mchangiaji mmoja dhidi ya mwengine kwa hivyo nawashauri tunapochangia tuwe tunatumia lugha za kistaarabu. Ahsanteni.

  3. naomba ufafanue ni lugha gani nilyotumia hapo juu ambayo si ya kistaarabu? kumwita Nyerere adui? wakati ni kweli, kama mwizi hakuitwa mwizi ataitwaje? huu ni wakati wa uwazi na wewe kama mwandishi wa habari una majukumu yako kwako kwa Mola kwanza halafu ndio mengine , au umesahau ugonjwa ulioupata, ule ulikuwa ni ukumbusho kutoka kwa muumba usije kujisahau ,

  4. Sikiliza Bwana Ahmed Rajab huyu ndugu yetu Prof. Shivji tunamkubali kwa mengi sana kukataa wema wa mtu ni ukafiri kafanya mengi. Twaba’an, lakini kwa sasa Bwana sisi currently tunamuona kakaa mtegoni Yeye na kiyatima cha Nyerere Dr. Salim Ahmed Salim ambaye yeye kazi kusifu Muungano tuu eti anadowea uraisi 2015, sasa ili ajigomboe rehanini ni kuitetea Zanzibar kidharura na kwa haraka sana sasa hivi.

    Kama ukokaribu na yeye mwambie. Kama huwezi basi sisi tunaomba tusitolewe kwenye ajenda yetu.

    MUUNGANO HATUUKI
    ZANZIBAR KWANZA.

  5. Ndugu zangu katika kpindi hichi ambacho kila mtu anadai yu sahihi kuhusu mfumo, utawala na uendeshaji wa Muungano inabidi wakosowaji wajenge hoja ili wengine waone kwa nini Muungano haufai. Ni kweli Muungano huu kwa wengi wetu ni mchungu kama mchunga, unachoma kama mchongoma na unaunguza kama moto wa shaba. Hata hivyo, inabidi tuuchambue ili kila mtu aone haya kwa uwazi. Ubaya wa mtu yoyte kuujadili sasa haitasaidia. Tuungane katika kuonesha ukweli ili hata wasiopenda wapende hoja zetu.

    • Sikiliza kaka, sijui unataka uchambuzi wa aina gani mpaka uelewe kama huu muungano hautufai, ivo wewe, mimi au watu wengi hawajui au hawakuhudhuria ktk makongamano tofauti na kutolewa ufafanuzi na uchambuzi wa kina kuhusu huu muungano na madhara yake ???

      Muda huu sio wa kutoa elimu ya muungano tena, huu ni muda wa kutoa faida ya kuwepo kura ya maoni dhidi ya muungano huu feki, shekh upo apooo !!!

  6. Mimi nadhani ipo haja ya kuendelea kuleta mada kama hizi ambazo kwa kweli hata kwa kudokezewa tu unahisi akili yako imekwenda mbali sana kwa kufikiri.Mada hizi zinafumbua macho na zinakuza akili lakini pia zinaweza kushabihisha watu kusoma zaidi kwani wengi wetu hasa Zanzibar hatuna utamaduni wa kujisomea ambao ni muhimu sana.

  7. kwa wale wote ambao hawataki muungano , watambue kuwa watatumiwa baadhi ya watu ambao tunaona wana misimamo lakini watarubuniwa kwa fedha au kutishiwa maisha yao ili wawashawishi waznz kuukubali muungano , tuwamurike vizuri hawa akina pro shivji, pro sharif, ally saleh , awadh na wengineo ambao mnawajua , wasije kutuyumbisha na wakitugeuka , basi hakuna dhara wala dhambi kuwacharanga shaba za miguu wawe vilema maisha ,

Leave a comment