Jussa ang’ara mbele ya Marando, Nape

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) Ismail Jussa Ladhu

Jussa ang’ara mbele ya Marando, Nape
Monday, 29 August 2011 09:36

Elias Msuya na Aidan Mhando

MVUTANO mkali wa hoja uliibuka katika mdahalo uliopewa jina la Itikadi za vyama vya siasa na Tanzania tunayoitaka, ambao mwakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), Jussa Ismail Ladhu aling’ara kutokana na hoja zake kuonekana kuwazidi nguvu wenzake, Mabere Marando wa Chadema na Nape Nnauye wa CCM.

Jussa aling’ara katika mdahalo huo uliofanyika juzi jioni Dar es Salaam ambao uliandaliwa na Taasisi ya Vox Media huku ukiwa umetawaliwa na vijembe vya hapa na pale vya watoa hoja hao kwa upande mmoja na wafuasi wao nao wakikosoana kwa malumbano kwenye ukumbi huo wa mkutano kwa upande mwingine.

Kung’ara kwa Jussa kulionekana dhahiri wakati wa swali kuhusu itikadi za vyama hivyo baada ya kueleza vyema itikadi ya CUF, huku washiriki wenzake Marando na Nape, wakizungumza kadri walivyoweza lakini wakishindwa kufafanua kikamilifu itikadi zinazofuatwa na vyama vyao.

Cuf na uliberali wa kati

Jussa alisema itikadi ya CUF ilibadilika kutoka kwenye sera ya utajirisho na kuwa ya uliberali wa kati na kuongeza: “Tulipoanzisha chama tulisema hivyo, lakini tulibadilisha katika Mkutano Mkuu wa mwaka 2009. Tulisema hatutaki ujamaa wala ubepari, bali uliberali wa kati.”

“Binadamu mwenyewe ana haki ya kusimamia misingi yake, kuheshimu haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria uliberali wa CUF siyo wa kulia wala kushoto.”

Alikiponda CCM kwa kutumia sera ya ujamaa na kujitegemea huku kikiwa kimeuza mashirika yote na kutegemea wafadhili kwa asilimia 40.

Pia alikirushia kombora Chadema akisema kimeshindwa kupambanua sera yake na kuwaonya Watanzania kutokishabikia:
“Nawaonya Watanzania kutoshabikia vyama visivyokuwa na mwelekeo wa kiitikadi. Kule Zambia MMD iliingia kwa nguvu ya umma, ikapoteza mwekeleo kwa muda mfupi.”

Nape na ujamaa CCM

Nape ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alisema chama chake bado kinaamini katika sera ya Ujamaa na Kujitegemea. “CCM bado tunaamini na tunataka kujenga Tanzania katika misingi ya ujamaa, kuishi kama ndugu na kuheshimiana,” alisema Nape na kuongeza. “Tunaamini katika kujitegemea, tujiamulie mambo yetu wenyewe. Kama kuna msaada basi uje pale ambako kuna kitu tumeshakifanya.”

Hata hivyo, Nape alizua minong’ono alipokazia kauli yake kuwa bado CCM kinafuata ujamaa uleule ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere na kuongeza: “Kuna mikakati ya kutekeleza ambayo imekuwa ikibadilika kisiasa, kiuchumi na kijamii. Lakini lengo letu bado liko palepale.”

Kauli hiyo ya Nape iliibua malumbano makali wakati wa kipindi cha maswali. Wachangiaji wengi walimwuliza Nape, “Mwaka 1990 viongozi wa CCM walikutana Zanzibar na kuvunja Azimio la Arusha. Ni ujamaa gani unaouzungumzia?” Aliuliza mchangiaji aliyejitambulisha kwa jina la Bura.

Mchangiaji mwingine aliuliza kama ujamaa huo wa CCM ndiyo unaoruhusu watoto wa viongozi kurithi madaraka; “Ujamaa huu ndiyo unawaruhusu watoto wa viongozi, kurithi madaraka? Adam Malima kuwa Waziri kama baba yake, Nape kuwa kiongozi wa CCM kama baba yake, Vita Kawawa na Zainabu Kawawa kuwa mbunge kama baba yake?”

Akijibu maswali hayo, Nape alisema Azimio la Arusha siyo sera ya ujamaa, bali ni mkakati wa kutekeleza na kuongeza kwamba, hakurithi nafasi ya baba yake huku akiwataka watu wapime uwezo wa watoto hao huku akisisitiza, “Watanzania tusimhukumu mtu kwa wazazi wake, tupime uwezo.”

Itikadi ya Chadema yamtesa Marando

Kwa upande wake, mambo yalimwendea kombo Marando baada ya kushindwa kubainisha kwa ufasaha itikadi ya chama chake na kubakia kutetea falsafa ya nguvu ya umma. “Katiba ya Chadema inasema, falsafa ya nguvu ya umma… umma ndiyo mwanzo na mwisho katika kuamua mambo yao. Umma ndiyo wenye mamlaka ya kujiamulia mambo yao kupitia uchaguzi ulio huru na wa haki,” alisema Marando kabla ya kulimwa swali na mwendeshaji wa kipindi hicho, Rosemary Mwakitwange kuhusu itikadi yao hasa kati ya ujamaa, ubepari na uliberali.

Marando alijibu kuwa Chadema inafanya mambo yake kimatendo: “Chadema hatufikirii tu, tunafanya kiutendaji, tukipata Serikali tutaweka viongozi imara. Nguvu ya umma itaondoa viongozi wabovu, mfano wabunge wetu wanafanya kazi na Watanzania wanaiona.”

Marando, Jussa wapigana vijembe

Swali la Mwakitwange kuwa Chadema na CUF vina itikadi ya pamoja lilisababisha vyama hivyo kupigana vijembe. Jussa alisema Chadema kinafuata itikadi za kibepari na ndiyo maana kiko kwenye muungano wa vyama vya kibepari duniani. Lakini, Marando alisema Chadema hakiwezi kufananishwa na CUF ambayo imeungana na CCM huko Zanzibar na hivyo kina michanganyo.

Akijibu hoja hiyo, Jussa alisema Serikali ya umoja wa kitaifa imeundwa ili kumaliza mgogoro uliojikita kwa zaidi ya miaka 50 visiwani Zanzibar, huku akitoa mfano wa Chadema ilivyoshirikiana na CCM kwenye Halmashauri za Kigoma na Arusha. “Zanzibar ilikuwa na mgogoro wa miaka 50, mkikubaliana kuendesha Serikali, mnakubaliana pia mambo ya kushirikiana. Ukisoma Hotuba ya Rais wa Zanzibar Dk Shein (Ali Mohammed)alipokuwa akizindua Baraza la Wawakilishi alizungumzia mikakati iliyohusisha Ilani za CCM na CUF,” alisema Jussa.

Kuhusu kuunganishwa kwa vyama vya CUF na Chadema ili kupata nguvu zaidi, Marando alipinga akitoa mfano wa suala la posho za wabunge ambalo alisema wakati wabunge wa Chadema wakizipinga, CUF na CCM walikuwa wakiunga mkono. “Katika Ilani ya Uchaguzi ya Chadema ya mwaka 2010, Chadema kilikataa posho. Kikawaelekeza wabunge wake wazipinge Bungeni. Hatuwezi kuungana na wenzetu wanaoziunga mkono” alisema Marando.

Hata hivyo, taarifa kutoka ofisi ya Bunge hadi jana zinasema ni Zitto Kabwe pekee ndiye mbunge wa Chadema ambaye aliacha kusaini posho huku wengine wote wakitia kibindoni. Baada ya kuona mdahalo unakwenda nje ya mada, Jussa aliwataka washiriki kutojadili mambo yasiyo na maslahi kwa taifa kama ya posho na badala yake yale mambo ya msingi ambayo yataifanya Tanzania ipige hatua katika maendeleo na ustawi wa watu wake.

Jussa alisema CCM kimechoka na kinapaswa kuondoka madarakani kwa kuwa kimekuwa kikiongoza dola kwa miaka mingi bila ya kuleta mafanikio yaliyokusudiwa. Nape alijibu mapigo akisema CCM ni kati ya vyama vinne vikongwe duniani hivyo vyama vingine nchini vinapaswa kujifunza kutoka kwake.

“Sijui umri wa chama unapimwaje, lakini kwa nchi zilizoendelea kama Marekani na Uingereza, kuna vyama vikongwe. Kwa uzoefu, CCM ni kati ya vyama vya kijamaa vinne duniani vilivyobaki, vingine viko China, Korea na Cuba. Watanzania wanatuamini, tumevuka mawimbi ya bahari,” alisema Nape.

Nape alirusha kijembe kwa Chadema aliposema kimeshindwa kumfukuza uanachama Mbunge wa Maswa, John Shibuda licha ya kutofautiana nao kimsimamo. Marando alikataa kuzungumzia suala hilo la Shibuda ambaye ameonyesha msimamo tofauti na chama chake hasa katika suala la posho za wabunge.

“Siwezi kumzungumzia Shibuda, kwani yeye siyo chama,” alisema Marando na kuufanya ukumbi mzima ugune, kisha akaendelea, “Shibuda ni Mbunge wa Chadema, lakini siyo chama” na kufanya ukumbi mzima kuimba… “Shibuda, Shibuda, Shibuda…”

Suala la mgogoro wa Arusha

Nape aliwataka baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini kuachana na dhana kwamba CCM inawakumbatia madiwani wa Chadema Arusha akisema mgogoro huo siyo wa CCM. “Kumekuwapo na maneno kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kwamba mawaziri wamewakumbatia madiwani wa Chadema na kuwaruhusu kuingia katika vikao vya halmashauri huku wakiwa wamesimamishwa kufanya hivyo na chama chao ,” alisema Nape.

Alisema, CCM haiwezi kuingilia mgogoro huo na kwamba watu wanaosambaza taarifa za mawaziri kuwakumbatia madiwani hao wanatumia njia hiyo kujisafisha.

“Tunatambua ya kwamba kuna baadhi ya viongozi wa Chadema wanakabiliwa na kesi huko Arusha sasa wanaanza kutumia chanzo cha mgogoro wa madiwani hili kujisafisha na kwamba watambue hata siku moja CCM haiwezi kuingilia masuala ambayo haihusiki nayo.”

MWANANCHI

2 responses to “Jussa ang’ara mbele ya Marando, Nape

  1. kweli Jussa ameshiba maarifa, anawagawia na wasio nayo. Tunatamani mjadala mwingine tena Jussa awepo. Tumeelimika mengi sana. Alilyoyasema wengi wamenufaika nayo. Naomba kuwasilisha hoja.

  2. ni muhimu nd Jussa , kwa sasa uwaongoze wananchi katika kuvunja muungano , wananchi tayari wameshachukua hatua kubwa lakini naona wanasiasa mmekaa kimya kama vile hamtambui unyonywaji unaofanywa na madhalimu wa tanganyika , huu si muda wa kukaa kimya , wewe ni mwanasheria na nategemea ni mtu mwenye msimamo , huenda ukatishiwa maisha yako na mashushu , lakini kama utakamatana na ukweli na kuwa na msimamo huo huo, utakuwa ni mbora kwa mola kuliko kuogopa binadamu hata ikibidi kupoteza maisha yako au cheo chako.

Leave a reply to Ayoub Cancel reply