Ajenda ya znz ijadiliwe sasa

Baadhi ya akina mama wa Zanzibar wakiwa katika moja ya mikutano yao ya vikundi vya maendeleo ambao wao wanahitaji sana kujadili mustakabali wa nchi yao ambayo imeanza kuonesha sura ya kuleta maendeleo ya dhati

Barazani kwa Ahmed Rajab

Wakati umefika wa kuizungumza Ajenda ya Zanzibar…

KATIKA utamaduni wetu wa Kiswahili tuna usemi usemao: ‘Ukimstahi mke ndugu huzai naye.’ Staha na kuoneana haya ni miongoni mwa sifa za uungwana wetu. Hata hivyo, kuna nyakati ambapo huwa hatuna budi ila tuziweke kando sifa hizo ili tuweze kuambizana ukweli kwa madhumuni ya kujenga, si kubomowa.

Tukiichunguza na kuidabiri historia ya Zanzibar tokea mwaka 1957 hadi 2010 jambo linalodhihiri ni kukosekana umoja miongoni mwa Wazanzibari katika muhula wote huo, hali ambayo imewagharimu pakubwa sana wao na watani wao.

Kwa muda wa zaidi ya nusu karne Zanzibar ilikuwa Taifa lililokuwa na uhasama na mfarakano. Matokeo yake hayakuwa mema — damu ilimwagika, nguvu zilitumika na nchi ikawa nyuma kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii. Zanzibar iligeuka na kuwa nyumba iliyogawika kisiasa.

Hali hiyo ya uhasama wa kisiasa miongoni mwa Wazanzibari ndiyo iliyozua Mapinduzi ya Januari 1964 na kuifanya Zanzibar ipoteze uhuru wake ilipoungana na Tanganyika miezi minne baadaye.

Katika muda wote ambao Zanzibar ilikuwa imegawika kisiasa Tanganyika haikuwa na raghba ya kuwashajiisha Wazanzibari waungane. Badala yake ilijiingiza kuupalilia huo mgawanyiko wa kisiasa miongoni mwa Wazanzibari.

Wazanzibari wengi wanaamini kwamba tokea mwanzo hiyo ndiyo iliyokuwa Ajenda ya Tanganyika. Wanahoji kwamba kwa kutowahimiza Wazanzibari waungane, Tanganyika ilikuwa na azma ya kutaka kuitawala Zanzibar chini ya mwavuli wa ‘Muungano’ lakini bila ya kuipa nyenzo za kuiwezesha ipate ustawi na maendeleo.

Kabla ya kuichunguza kwa utondoti, yaani kwa kinaganaga hiyo Ajenda ya Tangayika, lazima tukubali kwanza kwamba si jambo la ajabu au geni kwa nchi kuwa na sera kuhusu mambo yake ya ndani na pia kuhusu mahusiano yake na nchi nyingine, kwa maslahi yake.

Kwa hivyo, kama vile Tanganyika ilivyokuwa na mipango yake au sera zake kuhusu Afrika na Afrika ya Mashariki, ilikuwa pia na mipango kabambe kuhusu Zanzibar.

Tanganyika haikuwa na budi kuwa na sera zake kuhusu Zanzibar hasa kwa vile nchi hizo mbili ni jirani sana. Sasa haya tunayoyashuhudia leo ni matokeo ya mipango hiyo iliyoanza kupikwa tangu mwaka 1955 kilipoundwa chama cha Tanganyika African National Union (TANU).

Mipango hiyo ikaanza kutekelezwa kwa ukakamavu baada ya mwaka 1961 pale Tanganyika ilipounyakua uhuru wake kutoka wakoloni Waingereza.

Nini sifa bainifu za hiyo Ajenda ya Tanganyika kuhusu Zanzibar?

Kuna ushahidi wa kutosha wenye kuthibitisha kwamba lengo kuu la Tanganyika lilikuwa kuidhibiti Zanzibar. Aidha ni dhahiri kwamba hadi kufikia mwaka 1972 Tanganyika haikuwa na ubavu wa kuitekeleza itakavyo Ajenda yake ya Zanzibar.

Sababu ilikuwa moja tu: Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa kiongozi aliyekuwa akijiamini na hivyo, juu ya kuwako Muungano, Tanganyika haikuthubutu kufanya vitendo vya kuibughudhi Zanzibar. Unaweza kumshtumu Sheikh Karume kwa mengi lakini huwezi kuutia doa uzalendo wake wa Kizanzibari na msimamo wake uliokuwa huru.

Kuna ushahidi kwamba Mwalimu Julius Nyerere hakupendezwa na msimamo huo wa Sheikh Karume na tunajua kwamba katika siku za mwisho za uhai wake Sheikh Karume hakuwa akisikilizana na Nyerere. Karume akikataa katukatu yasiongezwe yale Mambo ya Muungano zaidi ya yale 11 yaliyo kwenye Hati ya Muungano.

Sheikh Karume aliikataa, kwa mfano, mipango ya Mwalimu ya kuitoa akiba iliyokuwa imenona ya sarafu za kigeni ya Zanzibar kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar na kuingizwa kwenye akaunti ya kigeni ya Tanzania na kuchanganywa na akiba za Tanzania zilizokuwa zikisimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Hali kadhalika, Sheikh Karume bado anakumbukwa kwa matamshi yake ya kwamba Azimio la Arusha likae hukohuko Bara lisivivuke visiwa vya Chumbe vilivyo baina ya Tanganyika na Zanzibar. Kwa kusema hivyo alikusudia kwamba Azimio la Arusha halitotekelezwa Zanzibar. Na hakikutekelezwa huko; hakuna kijiji cha ujamaa hata kimoja kilichokuwako Zanzibar.

Kama tujuavyo, vijiji vya ujamaa vilikuwa msingi wa Azimio la Arusha. Azimio lenyewe, ingawa lilikuwa na maadili adhimu, liliwadhuru Watanganyika na hivyo tunaweza kusema kwamba Sheikh Karume aling’amua mapema na alifanya uamuzi wa busara kulikataa lisitumike Zanzibar.

Kuna ushahidi kadhalika kwamba Sheikh Karume alikuwa na azma na mipango ya kuirejeshea Zanzibar uhuru wake na wakati huo huo kuleta upatanishi wa kitaifa. Alikuwa na nia ya kutaka papatikane suluhu na Wazanzibari wa ughaibuni ambao kwa wakati huo wakiishi uhamishoni kwa vile wakihofia maisha yao.

Siku hizo Zanzibar ikitisha kwani Serikali ikitawala kwa mabavu ikichelea isije ikapinduliwa na wale iliowapindua, yaani wafuasi wa vyama vya ZNP na ZPPP.

Tunaweza kusema kwamba wakati wote wa utawala wake Sheikh Karume alikuwa nayo Ajenda ya Zanzibar na kwamba, kama nilivyogusia, alikuwa na azma ya kuirejeshea Zanzibar uhuru wake kabla ya kufariki mwezi Aprili 1972.

Mambo yalibadilika mwaka 1977 pale wale waliorithi madaraka yake na hasa Sheikh Aboud Jumbe ambaye pamoja na Mwalimu waliviunganisha vyama vya Afro-Shirazi Party na TANU na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM).

Chama hicho cha CCM ndicho hatimaye kilichomwangusha Jumbe kutoka madarakani mwaka 1984. Ilikuwa rahisi kwa Nyerere kukitumia chama kumporomoa Jumbe kwa vile Muungano ulikuwa ukisimamiwa — na hadi sasa unasimamiwa — na CCM, kilichokuwa chama pekee cha kisiasa tokea 1977 hadi 1992.

Nikiyaandika haya leo wakati Wazanzibari wakiwa wameungana na wameitapika ile sera ya ‘wagawe, uwatale’ iliyojengwa juu ya msingi wa ukabila au wa kutafuta tofauti kati ya Unguja na Pemba sina shaka hata chembe kwamba kulifanywa jaribio la makusudi la kuwagawa Wazanzibari.

Kisingizo kilichotumiwa ni kwamba Tanganyika imewakomboa Wazanzibari wengi kutoka ‘utawala wa kidhalimu’ wa Wazanzibari wachache. Wenye kuhubiri haya wanajisahaulisha kwamba tokea mwaka 1893 hadi 1963 Zanzibar ilikuwa imebanwa na ukoloni wa Kiingereza.

Wakiichunguza historia yao ya karibuni, Wazanzibari wengi sasa wanatambua kwamba wa kulaumiwa ni wao wenyewe na viongozi wao wa kisiasa, hasa wale wanasiasa wao walio tayari kwenda kinyume na maslahi ya Wazanzibari wenzao wakiwaendekeza watawala wa kigeni.

Hata hivyo, hali halisi zilizopo leo Zanzibar zinaiwezesha nchi hiyo kuwa na Ajenda yake yenyewe itayoweza kushindana na Ajenda ya Tanganyika katika kuzidhibiti shughuli za Zanzibar.

Lakini kuna maswali ya kimsingi yanayobidi yajibiwe. Nayo ni: nini iwe Ajenda ya Zanzibar? Na nini na nini yawe madhumuni yake na njia gani itumike kuifikia Ajenda hiyo?

Ni muhimu kuyapata majibu ya hayo hasa leo ambapo Zanzibar si tena nyumba iliyogawika yenye kupigana vita ya wenyewe kwa wenyewe. Zanzibar ya leo haiyapuuzi tena yale mambo yanayoiunganisha, yaani lugha moja, utamaduni mmoja na dini moja.

Bila ya shaka nguzo kuu za Ajenda ya Zanzibar lazima ziwe za kisiasa lakini inapaswa Ajenda hiyo ishughulikie pia masuala ya kiuchumi na kijamii. Wazanzibari wanaamini kwamba hawawezi kuyajadili mambo yao ya kisiasa bila ya kulizingatia jukumu la kimkakati katika shughuli za Zanzibar la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na la chama chake kinachotawala.

Hivyo, Wazanzibari wanahitaji kuwa na msimamo mmoja kuhusu suala la Muungano, hasa kuhusu iwapo huo Muungano uendelee ama usiendelee; na kama uendelee, uselelee kuwa kama ulivyo ama ubiruliwe na uwe tofauti kabisa.

Swali lililo muhimu zaidi ni iwapo Muungano huo utapelekea Zanzibar imezwe kabisa na Tanganyika ama utaipelekea Zanzibar iwe na uhuru wake.

Wakati umefika kwa Wazanzibari kuufanya uamuzi huo. Wazanzibari wamerahisishiwa kazi ya kuukata uamuzi huo kwa zoezi la sasa lenye lengo la kuitunga katiba mpya ya Muungano.

Bila ya kuwa na Ajenda ya kitaifa itayokubaliwa na wengi wa Wazanzibari, itakuwa ni jambo la hatari kushiriki katika hili zoezi la utungaji katiba. Huenda Wazanzibari wakajiponza. Ninasema hivi kwa sababu watageuka tena kuwa watu wa nyumba iliyogawika, historia itajikariri na Wazanzibari watajikuta wanasota na shida zao kama ilivyokuwa kawaida yao miaka 47 iliyopita.

Litakuwa jambo la murua lau Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikijitwika kazi hiyo ya kufafanua kwa undani nini iwe hiyo Ajenda ya Zanzibar na halafu iyawasilishe mapendekezo yake kwa Wazanzibari kupitia Baraza la Wawakilishi.

Miongoni mwa mapendekezo hayo pawepo na Mkataba wa Kijamii wa Zanzibar utaowapa Wazanzibari wote fursa sawa, bila ya ubaguzi au upendeleo na bila ya kulifanya kundi moja tu katika jamii linufaike na mengine yadhalilike. Kinachotakiwa ni usawa ambao utahamasisha umoja na maridhiano ya kisiasa; na ni muhimu hayo yapatikane ili Zanzibar iweze kuyafikia malengo yake.

Muungano

Barua pepe: ahmed@ahmedrajab.com

One response to “Ajenda ya znz ijadiliwe sasa

Leave a comment