Maandamano marufuku- polisi

JESHI la Polisi Zanzibar limepiga marufuku maandamano ya kuunga mkono msimamo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na wajumbe wa baraza la wawakilishi kuhusu suala la mafuta na gesi asilia kutolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.

Maandamano hayo yaliokuwa yameandaliwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) yalipangwa kufanyika jana katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba na kuhudhuiwa na idadi kubwa ya wazanzibari ambao kwa takriban mwezi wa pili sasa kumekuwepo na gumzo kubwa kuhusiana na sula hilo la kuungwa mkono serikali.

Kwa mujibu wa barua ya jeshi la polisi ya Aprili 24,2009 yenye kumbukumbu namba W/MJN/58/VOL.1/10 iliyosainiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mjini Unguja SP. Mkadam Khamis Mkadam imepiga marufuku maandamano hayo.

“Napenda kukujulisha kwamba ombi lenu la kufanya maandamano ya kuunga mkono serikali ya wawakilishi juu ya suala la mafuta LIMEKATALIWA. Hii ni kwa sababu suala la mafuta ni suala la kikatiba ambalo linajadiliwa na baraza la wawakilishi ili ufumbuzi wake upatikane kikatiba” Imenukuu barua hiyo ya Polisi.

Jeshi hilo limesema kwamba sio busara kwa suala hilo hivi sasa kulifanyia maandamano na kulijadili nje ya utaratibu wa kisheria kwa kuwa limo katika mchakato wa kutafutiwa ufumbuzi wa kisheria.

Jumuiya hiyo ya Uamsho mara kadhaa imekuwa ikiandaa maandamano ya kidini na yale ya kuunga mkono baadhi ya mambo ya kijamii yanayotokea katika visiwa vya Unguja na Pemba lakini yamekuwa yakikataliwa mara kwa mara na jeshi la polisi kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo suala zima la kuvuruga amani na utulivu uliopo visiwani hapa.

Kwa mujibu wa barua ya Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) yenye kumbukumbu namba JMK/OUT/VOL-8/2009 ya Aprili 22, 2009 iliyosainiwa na Amiri wa Jumuiya hiyo Azzan Khalid Hamdan imesema kwamba “Jumuiya iliandaa kufanya maandamano ya kuunga mkono msimamo wa seriakli ya SMZ kuhusu suala la mafuta siku ya Ijumaa tarehe 24/04/2009. maandamano hayo yamekataliwa na polisi” imenukuu barua hiyo.

Wananchi wa Zanzibar hivi sasa wamekuwa na shauku kubwa wa kutaka kujua hatma ya suala la mafuta na gesi asilia kuendelea kuwepo katika orodha ya muungano au kutolewa katika orodha hiyo ambapo wajumbe wa baraza la wawakilishi wa pande mbili za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF) waliungana na kutaka mafuta na gesi asilia yabaki Zanzibar na kuwanufaisha wazanzibari kwa madai kwamba suala hilo halikuwemo katika ordha ya mambo 11 ya muungano.

Katika hatua nyengine Jumuiya hiyo imeandaa kongamano la kitaifa la kujadili hatma ya Zanzibar katika Muungano leo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ambalo linatarajiwa kuwashirikisha viongozi wa serikali na vyama vya upinzani nchini.

Kongamano hilo lilipangwa kufunguliwa na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna na kufungwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Juma Duni Haji huku mada mbali mbali zimepangwa kuwasilishwa katika kongamano hilo ikiwemo Zanzibar katika Muungano, Athari za Muungano kwa uchumi wa Zanzibar, pamoja na athari za Muungano kwa utamaduni wa Zanzibar.

Wakati Jumuiya hiyo imeandaa kufanya kongamano hilo Chama Cha Wananchi (CUF) nacho kimeandaa kongamano kama hilo la wazi na kuwashirikisha wanafunzi wa elimu ya juu na jumuiya za kiraia linalotarajiwa kufanyika kesho Aprili 26,2009 katika ukumbi wa Jamat Khan Mkoa wa Mjini Unguja.

Katika kongamano hilo mada itakayowasilishwa ni ‘Miaka takriban 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wazanzibari tuna nini cha kujivunia’ itakayowasilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Juma Duni Haji.

Leave a comment