Pemba waongoza watumikisha watoto

Wakati nchi nyingi duniani zimeanzisha kampeni maalumu ya kupiga vita utumikishwaji wa watoto wadogo ikiwemo Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa kimataifa bado hali hiyo haijaweza kudhibitiwa katika baadhi ya maeneo kadhaa Visiwani Zanzibar.

Maeneo mengi hasa vijijini watoto wadogo hufanyishwa kazi kutokana na sababu mbali mbali zinazoelezwa ikiwemo ile ya wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwaendeleza kielimu hivyo hulazimika kubakia nyumbani na kuwasaidia wazee wao katika kazi za nyumbani ambazo nyengine kubwa kuliko uwezo wao.

Hivi karibuni nilikuwa katika Kisiwa cha Pemba na kushuhudia watoto kadhaa wanaofanya kazi nzito ambazo haziendani kabisa na umri wao kutokana na kazi zenyewe ni mzito ambazo zinahitaji nguvu na uwezo mkubwa wa kiafya.

Maeneo mengi Kisiwani Pemba utawakuta watoto wakicheza mitaani nyakati za kwenda shule huku wengine wakiwa wanauza biashara mikononi , kuvunja kokoto, kuvua samaki baharini na kupara samaki kando ya bahari ambapo baadhi yao wamebuni kazi mpya wa kwenda uwandani na kufanya kazi za kukata matufali ambao ni mgumu na mzito kulingana na umri wao mdogo.

Mradi huo wa uchongaji wa matufali ya mawe uliobuniwa muda mrefu na ulikuwa ukifanywa na watu wazima pekee kutokana na ugumu wa kazi hiyo lakini hivi sasa watoto wengi wamekuwa wakishiriki katika kazi hizo ambayo ni hatari sio kwa umri wao tu lakini hata afya zao.

Watoto wadogo wamekuwa wakifanyishwa kazi kubwa kupita kiasi katika maeneo ya uchongwaji matufali ambapo wao kazi yao ni kuingia ndani ya mashimo na kukusanya matufali ya mawe yaliochongwa na kuyapandisha juu na kuyapanga kwa ajili ya kusubiri wateja wa matufali hayo.

Watoto hao huingia ndani ya mashimo ambayo ni marefu na ndani ya mashimo hutoka vumbi ambapo watoto hao huingia humo bila ya kuwa na kinga ya aina yoyote jambo ambalo ni hatari kwa afya zao za baadae.

Ndani ya mashimo hayo ya mawe utakuta watoto hao wa kike na wa kiume huonekana nyakati za asubuhi wakifika eneo la machimbo hadi jioni wakiwa eneo la kazi wakifanya kazi bila ya kupumzika ambao wengine ni wadogo sana.

Baadhi ya watoto hao ambao hufanya kazi hizo wameacha kwenda shule wakiwa darasa la saba lakini cha kusikitisha zaidi ni kuwa kati yao kuna wengine wameacha shule wakiwa darasa la tatu na la pili ambapo wapo pia waliokuwa awajawahi kusoma hata darasa moja yaani wadogo mno wameshaanza kuokota tufali moja moja na kusogea nalo juu kwa ajili ya kupata fedha za matumizi ya nyumbani.

Kitu gani kinachowafanya watoto hao kukimbilia kwenye ajira na biashara hiyo? Mtengenezaji matufali maarufu wa kisiwani Pemba, Abdallah Kheri ambaye ni Mwajiriwa wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) anasema hali duni za maisha ya wazazi wao zinachangia kwa kiasi kikubwa watoto hao kutafuta ajira mapema ili waweze kukimu mahitaji ya chakula kwa wazazi wao.

Amesema watoto wanaoingia uwandani hapo ni wadogo na wanafanya kazi kutwa nzima sawa na watu wazima na wanafanya kazi katika mazingira magumu na ya hatari kwa usalama wa maisha yao lakini kwa kuwa wazazi ni masikini na hawana uwezo wa kuwaendeleza watoto wao kielimu ndio wameamua kutafuta riziki kwa njia hiyo.

“kwa hakika watoto wadogo wanaokuja hapa wanasikitisha na siku za mwanzo tulikuwa tukiwakataza lakini naona wazazi wao wanawaruhusu maana wanaporudi kazini watoto hupeleka pesa ya mkate ..mzee kweli atakataa mwanawe asije huku” alisema Kheri.

Kheri anasema wazee wa vijijini ni watu masikini sana na hawana uwezo kwa hivyo wanategemea kazi za kuchuma karafuu, kulima na kuvua ambazo zinawaendelesha maisha yao lakini hivi sasa tokea kuingia mradi huo wa kuchonga matufali umeongeza idadi ya utumikishwaji watoto wadogo katika kazi hizo.

“wengine wadogo sana wamefika darasa la tatu tu wamekataa kuendele kwenda skuli na wengine hawajawahi kusoma hata darasa moja lakini wanakuja hapa na kufanya kazi kutwa kwa kweli inatia huruma lakini tutafanya nini ndio maisha yetu haya watanzania… “ alisisitiza kwa onyonge.

Kheri alisema kazi ya kuingia ndani ya mashimo ni mzito na ngumu hata kwa watu wazima kutokana na vumbi linalotoka ardhini linapeperuka kwa kasi kubwa hivyo unapovuta hewa hukuingia ndani ya pua na wakati mwengine huhisi kama umeziba pumzi huku ukiwa unavuta hali ya umoto puani.

“Hilo vumbi ni hatari sana kwa sababu sisi watu wazima basi wakati mwengine tunakuwa taabani kwa sababu ukivuta hewa unavuta vuke limoto na unakauka koo haraka sana lakini kibaya zaidi unahisi kama umezibwa pumzi” alisema na kuongeza kwamba

“tatizo hakuna vifaa vya kusaidia hivyo kama hao watoto wanaoingia ndani ya mashimo wanaweza kuathirika kwa siku za baadae kutokana na kazi kubwa wanayoifanya watoto hao mashimoni humo mikono yao imechubuka chubuka kwa kukwaruzwa na matufali” amesema.

Matufali yanayochongwa kwa mawe yamekuja kama mbadala kutokana na matufali ya saruji kuuzwa kwa bei ya juu ambapo tufali moja la saruji huuzwa kwa bei ya shilingi 500 na tufali la mawe huuzwa kati ya shilingi mia 200 na 300 inategemea ukubwa wa tufali lenyewe jambo ambalo wananchi wenye kipato kidogo limekuwa ndio kimbilio lao.

Licha ya ugumu wa uchongaji wa matufali ya mawe wananchi wengi wa kisiwa cha Pemba hivi sasa wanatumia matufali hayo kwa matumizi ya kujengea nyumba zao kutokana na urahisi wake.

Ingawa uchimbaji wake ni ni mgumu lakini vijana kwa wazee wamepata kazi ya kuwaingizia kipato kikubwa kama alivyoeleza Kheri ambapo amesema ni kazi kubwa mno kuchimbua hadi kupata eneo safi liitwalo mwamba ambalo ndilo lenye kukatwa matufali hayo lakini matunda yake ni mazuri kutokana na kuongezea fedha nzuri ambapo eneo la ardhi ya 50,000 huzalisha matufali ya zaidi ya lakini nane.

Mtu mwenye kutaka kufanya kazi hiyo atalazimika kununua eneo la ardhi ambalo huwa ni maalumu lenye mwamba na hununuliwa kwa bei ya 50,000 au zaidi itategemea ukubwa wa aneo hilo na maeneo ya aina hiyo mara nyingi hupatikana katika Vijiji vya Uwandani, Mwambe, Kangagani, Micheweni na Kojani Kisiwani Pemba.

Anasema uchimbaji wake ni mkubwa kwa sababu unaweza kuchukua wiki moja hadi mbili unachimba mchanga mtupu na kuupeleka juu hadi hapo utakapopata shimo na kuupata mwamba ambao ndio unaochongewa matufali hayo ya mawe.

Wakati unachimba kwa kutumia vifaa maalumu kama tindo kifaa cha chuma ambacho hutumika kwa kuvunjia sehemu ya machimbo ndani ya ardhi na sururu la kuchimbua pia jambeni nalo hutumika kama msumeno wa kukatia mwamba ambao hutumiwa na watu wawili mmoja kukaa upande wa kulia na mwengine kushoto na kuanza kukata mapande ya matufali ambayo baada ya kupatikana mawe meupe na kukatwa katwa sehemu ndogo ndogo.

Baada ya kupata mwamba ambao ndio wenye kuchongwa matufali hayo kukatwakatwa na kutengenezwa mfano wa matufali yanayotengenezwa kwa saruji na mchanga lakini tofauti yake ni kuwa matufali ya mawe huwa rangi nyeupe na hupendeza zaidi ikilinganishwa na yale yanayotengenezwa kwa safuji.

Wanawake nao huingia katika kazi hiyo lakini wao kazi yao ni kupika vyakula vya aina mbali mbali na kuwauzia wafanyakazi wanaochonga mawe na hupata matufali kwa njia kubadilishana wanawake hutoa chakula na wanaume hutoa matufali.

Wanawake hao hupika ugali, wali, maandazi, chapati na chai ambapo vikombe viwili vya chai ni sawa na kupewa tufali moja na vyakula vyengine vyote hupata kila tufali ni sawa na sahani moja ya chakula.

Wanawake hao wamebuni mradi huo wa kupika vyakula sehemu zinazochongwa mawe na kujipatia kipato ambapo hivi sasa wanawake wengi hutegemea kazi hiyo ikiwa ni mbadala wa ile ya kuchuma karafuu ambapo huja kwa msimu maalumu na faida yake ni ndogo kutokana na kuuza karafuu hizo serikalini kwa fedha ndogo.

Baada ya kukusanya matufali yao wanayopata kwa kubadilishana na wachimbaji hao wanawake huwategemea watoto kuja kubeba matufali yaliokuwa ndani ya mashimo na kupandishwa juu na watoto wadogo ambao hukaa kwenye eneo hilo la machimbo wakisubiri kutumwa na kuingia ndani ya mashimo na kuchukua matufali na kutapanga moja moja .

Wanawake wao huwapa kazi watoto kwa kuwachukulia matufali yao kuyatoa kwenye mashimo na kuyapandisha juu ambapo kila mtu huweka sehemu yake maalumu na kupanga matufali hayo na ikifika siku ya pili kazi ndio hiyo kupanga juu yake hadi kufikia matufali 50 na hatimae kuuzwa kwa mawakala wanaokuja kununua matufali hayo yam awe kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

Wakaazi wa Kisiwani Pemba hivi sasa wamekuwa wakiyapa kisogo matufali ya saruji kutokana na ughali na wamekuwa wakinunua matufali hayo ya mawe ambapo nyumba nyingi utaziona zimejengewa matufali ya kuchongwa yanayotoka maweni.

Nyumba nyingi za Mji wa Pemba mijini na vijijini hujengwa kwa matufali ya kuchonga au matufali ya mawe na wachongaji wanapopata fedha huanzia kujenga nyumba zao kwa matufali hayo licha ya umasikini uliopo lakini nyumba za Pemba hivi sasa zinapendeza kutokana na ujenzi wa mtufali ya mawe.

Leave a comment