Sensa ina matatizo Zanzibar

Maafisa wa Sensa ya mwaka 2012 wakitoa mada kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakiwataka wawahamasishe wananchi kushiriki katika sensa

Salim Said Salim

ZOEZI la kuhesabu watu nchini (sensa), Bara na Visiwani, linatarajiwa kufanyika mwezi ujao, lakini kwa kiasi kikubwa hali inaonesha limekumbwa na dhoruba kali katika hivi visiwa vya Bahari ya Hindi vya Unguja na Pemba. Wengi hawakutarajia hilo kutokea, lakini kwa jinsi Zanzibar ya leo ilivyo, ni taabu kutabiri nini kitatokea kesho au kesho kutwa, kama ilivyo hali ya hewa katika Bahari ya Hindi, asubuhi shwari, jioni dhoruba.

Hapana ubishi juu ya umuhimu wa nchi kuwa na sensa baada ya kila kipindi, kwa kawaida huwa ni miaka 10.

Sensa inasaidia sana kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya kiuchumi, kijamiii na mengine kutokana na kujua idadi ya watu katika sehemu mbalimbali na takwimu nyingine zinazopatikana katika zoezi la sensa.

Kwa mfano, takwimu za sensa ni muhimu sana katika kupanga mipango ya huduma muhimu za kijamii kama za afya, elimu na maji safi na salama.

Sensa si kitu kigeni Zanzibar na wakati wote ilipofanyika hapakuwepo na mtafaruku wa aina yoyote ile.

Sensa ya kwanza ninayoikumbuka kufanyika Visiwani ni katika mwaka 1958, nikiwa na miaka 11. Matokeo yake yalionesha visiwa vya Unguja na Pemba kuwa na jumla ya watu 223,533 .

Wengi wao (79,702) walikuwa watu wenye umri wa miaka 25-34 na kidogo kabisa ni watu wenye umri wa miaka 65 kuelekea mbele (21,289).

Baada ya hapo, palifanyika sensa nyinginge tano na hapakuwepo matatizo yoyote yale na watu waliiridhia na kushiriki vizuri.

Sasa umefika wakati mwingine wa kufanya sense katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Bara na Visiwani), lakini hali ni tofauti na ilivyokuwa wakati zilipofanyika sensa zilizopita.

Hivi sasa zinasikika kelele nyingi Unguja na Pemba kutoka kwa vikundi na watu binafsi kutaka kususia sensa na kuwataka wananchi wasishiriki.

Mengi yanasemwa juu ya suala hili, lakini ukitafakari utaona ni refu na pana na lililojaa hisia za kila aina zinazowasababisha baadhi ya watu kuwa na mawazo ya kila aina na ambayo hatimaye wanataka watu wa Zanzibar waisusie sensa.

Wapo ambao hesabu zao zinawafanya wawe na hisia kuwa siasa imo ndani, wengine wanaona viongozi wa dini, hasa wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho kuwa na ajenda ya kuvuruga sensa na wapo ambao wanahisi lipo kundi la watu lililoamua kupinga kila linalofanywa na serikali na wengine wanaona sensa haiwasaidii chochote na haiwahusu na kujihusisha nayo ni kupoteza muda.

Ninachoweza kusema yote haya ndiyo yaliyoleta mkorogo na wahusika wakuu, hasa kutoka Bara, inaonekana hawakuyaona licha ya juhudi kubwa za kuelimisha na kutafuta maoni kwa miezi kadha iliyopita.

Baadhi ya viongozi wa dini hawasemi hadharani, lakini hudokeza pembeni kuwa wanahisi kuna ajenda ya kutengeneza takwimu za kuonesha Waislamu ni kidogo Tanzania na hatimaye kutumia hizo takwimu kuwanyima haki mbalimbali, kama za elimu na nafasi za kazi katika serikali na taasisi za umma.

Lakini, lingine linalofaa kukumbukwa ni kwamba baadhi ya hawa viongozi wa dini wana joto la roho kwa namna walivyotendewa miaka michache iliyopita, kwa baadhi yao kudai kupigwa na kuteswa katika msitu wa Paje, kusini Unguja na hata kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu.

Hii ilitokana na kauli zao za kupinga na kulaani mwenendo wa vikosi vya ulinzi kukong’ota watu mijeledi mitaani na hata majumbani wakati wa utawala uliopita na ule wa komandoo Salmin Amour.

Sina hakika, lakini dalili zinaonesha kuwa, sasa wamepata nafasi ya kulipiza kisasi kwa kuiwekea ngumu serikali kwa wananchi wasusie sensa.

Kuna kundi la watu ambao hawataki kuhesabiwa kwa sababu wanadai kuwepo kwao kama Wazanzibari au Watanzania, japokuwa wao na wazee wao wamezaliwa nchini na wanaishi ndani ya nchi hawatambuliwi kuwepo kwao, hivyo hapana haja ya kuhesabiwa.

Maelezo wanayotoa ni kwamba wamenyimwa vitambulisho vya Mzanzibari na haki ya kushiriki katika chaguzi zote mbili zilizopita, ule wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano.

Kwa maana hiyo, wapo tu na kwa hivyo kwa nini hivi sasa wajumuishwe katika kuhesabiwa katika zoezi la sensa?

Wapo ambao wanasema hawana imani na hatua yoyote ile ambayo Serikali ya Muungano inahusisha Zanzibar kwa sababu wamekuwa wakidanganywa sana na kwa hivyo hawaamini kwamba sensa ina nia njema kwa Wazanzibari.

Mifano wanayoitoa ni namna walivyodanganywa juu ya Zanzibar kulazimishwa kujitoa katika Jumuiya ya Kiislamu ya IOC na kuambiwa Tanzania ingejiunga, na hivyo Zanzibar pia kufaidika, lakini hakuna lililofanyika na sasa miaka zaidi ya 15 imepita.

Pia, wanasema mara kadha Serikali ya Muungano imeahidi katika miaka mitatu iliyopita kuwa mwenendo wa kuwatoza wafanyabiashara wa Zanzibar kodi mara ya pili unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika bandari ya Dar es Salaam utasimamishwa, lakini hakuna lililofanyika.

Kwa kifupi, suala la sensa limegubikwa na mazonge mengi Zanzibar na si vyema hata kidogo kulitafutia jawabu la mkato, jazba au za kisiasa.

Ni vizuri kwa wahusika kukaa na viongozi wa dini na wanasiasa kukaa pamoja na kutafuta njia ambazo zitarudisha imani ya wananchi ili washiriki kikamilifu katika sensa.

Kinyume chake, huenda zoezi la sensa lisipate mafanikio yanayotarajiwa na nchi kupoteza nafasi muhimu ya kupata takwimu za kupanga mipango yake ya mendeleo ya siku zijazo.

Tusichoke wala tusikate tamaa katika kujadiliana masuala yenye matatizo kwani siku zote hatima ya mijadala yenye nia njema huzaa muafaka na kutoa nafasi ya watu kusonga mbele.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

Advertisements

19 responses to “Sensa ina matatizo Zanzibar

  • Kwa kweli hili la kususiwa kwa sensa ya 2012 limefanikishwa na Serikali, viongozi wa Makanisa na Mashekhe wachumia tumbo, Mashekhe ambao wako tayari kuisaliti dini ya Allah kwa maslahi ya kidunia.
   Madai yao ni kwamba kipengele cha dini hakina maana kwenye sensa. Pia
   wanasema kama waislamu wanataka kujua idadi yao wajihesabu wenyewe. Mimi najiuliza zile takwimu zinazotolewa na kudai wakristo ni wengi kuliko waislamu zimetoka wapi, waislamu walihesabiwa na nani na ni mwaka gani?
   Kama hakuna kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa waislamu wenye kumuamini mwenyezi mungu na siku ya mwisho hatoshiriki sensa. Lakini kwa wale waislamu wachumia tumbo sina ushauri kwao zaidi ya kuwataka wamuogope muumba ambaye watakutananaye hata kama wanadhani hapa duniani ndiyo makao yao yamwisho hataondoka tena hii ni kwa wale wa Bara na Visiwani.

 1. demokrasia ya kweli ni ile inayoendana na matakwa ya watu , watanganyika imefika sasa muda kuwapa uhuru waznz , mlikuwa mstari wa mbele kuwapatia uhuru nchi za kusini mwa afrika , kumbe mnaitawala znz kwa mabavu , .ukweli ukidhihiri uongo hujitenga, ili kuepusha maafa , ni vyema kuvunjwa kwa muungano haraka sana kabla watu hawakumbana na kumwaga damu,

 2. nd salim nimeona makala yako inayohusiana na vipeperushi , inaonyesha unataka vurugu ifanyike hapo znz kwa kutaka polisi kuingilia , au unataka kujipendekeza , usisahu ktk nchi yenye demokrasia kuna uhuru wa kutoa mawazo bila uoga , hapa kwetu hakuna demokrasia ndio maana wanatumia vipeperushi , sasa kama wewe ni miongoni mwa wale waandishi wanaolipwa au kujipendekeza kwa serikali madhalimu zanzibar ( SMZ) basi usisahau kuna siku utakutana na mola wako , mwenzenu halima amerudisha namba na nyinyi mko njiani hakuna ataeishi milele kumbuka hilo , makala yako inachochea vurugu baina ya polisi na wananchi . Nampongeza kamanda wa polisi znz kwa kuwa mwenye mtazamo wa kidemokrasia ambao unatakiwa ni vyema kwa polisi na majeshi kukaa chonzo bila kupata shinikizo kutoka kwa wanasiasa madhalimu wenye kunuka rushwa kuliko maiti anavyonuka

  • Salim Said Salim ni mwandishi mkongwe, mzoefu, mahiri, mkweli na mwadilifu. Naamini sifa zote hizo anazo.
   Kweli demokrasia ni uhuru wa kutoa mawazo yako, kusikilizwa na wewe kusikiliza ya wengine pia, lakini sio uhuru wa kutukana wengine au kuchochea uvunjifu wa amani. (mfano; huwezi kutoa vipeperushi umeandika “wapemba si watu au wapemba warudi kwao”) hili halikubaliki ni uvunjifu wa sheria za nchi.
   Mwisho, Salim bila shaka yoyote story yake ililenga KISONGE na yanayoendelea kila leo.
   Ushauri: kabla hujacoment, soma story kwa kina, uifahamu khasa @msema

   • hakuna lolote nd kassim , makala ya nd salim inachochea polisi kuleta vurugu na karaha kwa raia , waznz hawataki muungano huo ndio ukweli kwa hio waandishi waandike yaliyo kweli sio kwenda na sera za kichama au kiserikali , sema kweli hata kama itakudhuru……..na kama story ililenga kisonge awe wazi asiandike habari kwa woga au lugha za kificho ( sio spika )

 3. bwana said nadhani hukumfahamu dasalma hana nia hiyo na wala da salma hajawahi kujipendekeza na naamini hatowahi kujipendekeza alichoeleza yeye ni hali halisi ilivyo na kutaka sheria ichukue nafasi yake ili kuepusha kuivuruga amani iliypo na mwisho naomba ujue kuwa siku zote da salma huwa anaeleza ukweli tu

 4. nd khalfan usiwe kama kipofu kuna sheria hapa nchini kwetu? kila mtu amelaaniwa kwa rushwa , vyombo vyote vya sheria na usalama ni vyombo vyenye kuendeleza rushwa hakuna lolote, kama mimi mwongo fanya kosa halafu uende mahakamani ukaone mapaka yanvyotaka kukuvamia kama samaki. Waandishi wa habari asilimia zaidi ya 99 ni mamluki wa serikali na vyama kama hujui ndugu yangu

 5. Kwa kuwa kuna Waheshimiwa wanaohusisha kila kitu na Sera za vyama vyao ni bora watu wakatae kuhesabiwa mpaka hawa waweke wazi ni yepi ya kitaifa na yepi ya Chama. Utaona kwa mfano, Mheshimiwa anakataa watu kujadili matatizo au mfumo wa Muungano eti kwa kufanya ni kinyume na Sera za Chama. Mtu huyu pia husema Barazani na akijua Baraza ni la Watu wote akasema kwa sauti pana kuwa yeye ni muumini wa Sera za Chama- Sawa lakini ni kwa nini haya hayasemi kwenye Tawi lake la Chama. Ni kweli yeye alikuja pale Barazani kupitia Chama sawa – lakini ajue kuwa Zanzibar kuna watu pia ambao hawana hata vyama lakini ni sehemu ya Zanzibar. Mheshmiwa huyu sijui anajiamini kiasi lakini nadhani anawalakini! Tunajua kuwa Chama chake anakiheshimu lakini asitumie baraza kupeleka mbele ajenda yake kwa hapa ni pa kila mtu.

  Watu leo wakizungumza kuhusu kehesabiwa au kutohesabiwa ni kwa sababu wanaona wametengwa kisiasa na Watu ambao hawajui mipaka ya taifa na vyama. Katika hali ya kuchanganya maslahi ya chama na yale kitaifa watu lazima watagoma kutoa mchango wao kuendesha nchi kwa kuona kuwa michango yao itatumika kufaidisha watu kisiasa.

  Wanasiasa wa Zanzibar ni wakulaumiwa kwa haya yote pamoja na mengine- Wao wakiamka hawafikiri zaidi ya vyama vyao – Hili la Sensa pamoja na uhimu wake hawalizungumzi wao ni sera za vyama tuu – inabidi waamke la sivyo sensa hii itafeli!

 6. Kwa kila anayependelea wema znz na uislaam asishiriki kwenye sensa ili kuipa vikwanzo serekeli dhalimu ya muungano, tumemsikia jana mufti wa znz akiwataka viongozi kuwahamasisha waislamu kushiriki sensa ila sidhani kama alisema yaliyoo kwenye moyo wake just kapangiwa tu, yeye mwenyewe haitaki na hao walohudhuria wote ni uamsho hawaitaki pia so waislamu musiwe na wasi ZANZIBAR KWANZA sensa baadae.

 7. Aslaam Aleykum ndugu zanguni. Wala silalamiki kwa yanayoisibu SENSA mwaka huu. Upinzani dhidi ya Sensa ni uthibitisho kuwa watu wana maamuzi na ndio wenye dhamana ya uendeshaji nchi yao. Wazanzibari wamekuwa wakikataliwa mangapi, hata yale ya haki kabisa kwao? Mbona maelfu kwa maelfu hawajapewa ID ya Zbar ilhali wana sifa zote? Viongozi wa SMS utawasikia mara kwa mara inapokuja hoja ya wananchi kunyimwa ID wakisema “tutafuatilia.. tutaangalia, tutajitahidi kuchunguza…” Inakera sana kwamba Sheria inasema wazi mwananchi lazima awe na ID na asipokuwa nayo bila sababu akishitakiwa ataadhibiwa kifungo au faini au yote mawili. Bado maofisa wa vitambulisho na viongozi wa Serikali wanajitia hamnazo. Huku Bara wananchi Waislamu wanaojitambua, wameshajiishwa wasishiriki sensa kwa sababu Serikali imekataa kuingiza kipengele cha kuuliza dini ya mtu. Waislamu wanataka kufuta takwimu za uongo zinazokubaliwa na SMT, maana zimetangazwa na TBC kuwa Wakristo ni 65% na serikali haijazikana takwimu hizi. Sasa ukiuliza watu si unaondoa utata? Labda serikali imebanwa na wakubwa zao wapi sijui wasiweke kipengele hichi. Mbona nchi kadhaa Ulaya, ikiwemo Uingereza, sensa watu wanaulizwa dini zao? Kinachofichwa Tz ni kitu gani?
  Sasa kwa kuwa Waislamu hawajaridhika na jambo hili, wameweka ngumu. Viongozi wa Kiislamu Zbar, hasa taasisi za kijamii, wanaunga mkono msimamo wa Baraza Kuu la taasisi za Kiislamu Tz kupinga Waislamu kushiriki sensa, na watu wanakataa kwelikweli kushiriki.
  Leo asubuhi Bungeni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema wazi serikali haioni hilo kama ni jambo la kusikilizwa na serikali, hawataingiza dini, eti maendeleo ya wananchi hayapangwi kwa misingi ya dini za watu. Kwa kuwa wamelikoroga, waweza kulinywa wenyewe I suppose.
  Wasalaam.

  • @Brother Jabir Idrisa

   Unaposema “Viongozi wa SMS” unakusudia kina nani? au
   SMS zipi? za Zantel, tiGO, Airtel au Vodacom. Tuekee wazi.

 8. wanaogopa kwa sababu wanajua ukweli kuwa waisilamu ni wengi tz kwa asilimia kubwa tu , lakini ktk maeneo yote ya serikali na mashirika yake hakuna uwiano , angalia mfano bodi ya wakurugenzi muhimbili au BOT , na nyenginezo , mbali polisi na majeshi , mahakamani , sheria, vyombo vya habari , elimu na vyuo vikuu , na ndio maana wakaweka NACTE , NECTA na TUC hivi ni vyombo vya kuendeleza madhila amkeni mliolala , ktk nchi zenye demokrasi ya kweli kama uingereza ugawaji wa nafasi zozote zinazingatia asili za watu , rangi zao , dini zao , jinsia yao , ulemavu nk ,

 9. AMA KWELI TANGANYIKA NI NCHI INAYOISHI KWA DHULMA. WAMEIBA MALI ZOTE ZA ZANZIBAR SASA WAMEANZA KUIIBIA MALAWI. Ni bora vita vitokee kati ya tanganyika na malawi ili wazanzibar tupate UHURU.

 10. Aslaam Aleykum Wanaukumbi. Nimepitishwa tena kwenye nilichokiandika jana. Nilikosea. Ila SERELLY lazma umefahamu, umefanya tu inda. Ni rahisi kujua nimekusudia kusema Viongozi wa SMZ, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Ungesahihisha tu yakesha kuliko kuongeza utata kama vile hukujua kilichokusudiwa. Sikulaumu tafadhal. Kosa ni kosa tu hata akilifanya nani au vipi. Jamani ni viongozi wa SMZ.

  Haya mjadala uendelee, mzuri.

  Wakatabahu.

 11. Leo nilisali Ijumaa Msikiti wa Mtambani, Kinondoni. Imam alihimiza kwa mara nyingine Waislamu wasishiriki SENSA kwa sababu hawaheshimiwi na Serikali bali serikali inazingatia na kusikiliza sana KANISA. Bado viongozi wa Kiislamu wanasisitiza ipo haja ya kipengele cha DINI kujumuishwa katika dodoso za SENSA. Nimewasikia vionngozi wa taasisi za Kiislamu Zanzibar wakiendelea kutia shindo Waislamu wa Zanzibar waungane na wenzao wa Tanganyika kususia sensa. Haya, kumbe jambo hili si lelemama. Ni kipimo na serikali inatakiwa kupima kwelikweli. Njia wanayoichukua na kutisha wananchi kuwa watafungwa wanaosusia sensa ni kuwadanganya. Maelezo ya serikali, yakiwemo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda bungeni jana, hayayaridhisha hoja ya Waislamu. Nchi ngapi bwana zinahesabu kila sect ya kijamii wakati wa sensa, yanini kudanganya wananchi mchana kweupe?
  Wakatabahu.

 12. wajua m2 ukimbana sn matokeo yake unaadhirika ww ss hawa jamaa watapatapa me nasema km wataka wawahisabu huko Tanganyika cc huku mwisho chumbe Hatuisabiwi Muhudi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s