Ubakaji wa watoto Zanzibar, tatizo sugu linaloisumbua jamii

Dk Marijali Msafiri Daktari wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar

Na Salma Said

KATIKA utafiti wa hivi karibuni wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) imebainika kuwa tatizo la ubakaji limeonekana kuwa sugu visiwani Zanzibar. Wengi waliohojiwa wanasema kuwa ni rahisi kulimaliza iwapo jamii, serikali, na vyombo vya sheria kwa pamoja wataamuwa kulishughulikia kwa dhati.

Ofisa Wanawake na Watoto, Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Watoto na Wanawake katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mjini Magharibi, Hidaya Mohammed Ramadhani anathibitisha kuwa kesi za kubaka na kulawiti watoto katika wilaya yake zipo, lakini nyingi zinaishia mitaani baada ya maelewano katika familia.

“Utafiti unaonyesha kuwa wabakaji wengi ni wanaume wakiwamo wanaoishi katika familia. Wapo babu, baba, kaka, mjomba, binamu, ndugu wa karibu, mwalimu au jirani. Hali hii inafanya kampeni dhidi ya udhalilishaji kuwa ngumu sana kwa sababu watuhumiwa wanakwepa mikono ya sheria kwa kuelewana katika familia,” anasema Hidaya.

Anaongeza kwa mfano kuwa katika mwaka wa 2011 kesi za ubakaji zilikuwa nane ikiwemo mbili za kulawiti na mwaka mwa huu, 2012, kati ya Januari na Mei, kesi sita ikiwemo na moja ya kulawiti zilifunguliwa.

Lakini, uchache wa kesi katika ofisi yake ya Wilaya ya Mjini Magharibi haina maana kuwa vitendo vya udhalilishaji wanawake na watoto vimepunguwa kwani vitendo hivyo hufanywa kwa siri na baadhi ya wanaofanyiwa hawajitokezi kwenda katika vyombo vya sheria wala polisi kuripoti.

Maria Obel Malila wa kitengo cha uhifadhi mtoto (Child Protection Unit), pia anathibitisha kuwa vitendo vya ubakaji vinaendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo wilaya hiyo na kwamba tangu kitengo cha uhifadhi wa mtoto kizinduliwe mwaka 2010 ni kesi 141 zikiwamo 30 za kulawiti watoto zilizofikishwa katika kitengo hicho.

Maofisa hao wanasema kesi za ubakaji na kulawiti haziripotiwi kutokana na usiri wake pamoja aibu, mtizamo finyu, woga, muhali, na kulindana katika familia, kwani kesi nyingi za ubakaji na kulawiti zinawahusu wana familia.

“Kilio cha wengi ni kuwa haki haitendeki katika ngazi zote, kuanzia wazee, sheha, polisi, na mahakama ili kuweza kukabiliana na tatizo la ubakaji. Bado tatizo lipo katika jamii na vyombo vya kusimamia sheria hali ambayo itafanya kazi ya kupambana na ubakaji kuwa ngumu,” anasema Hidaya.

Naye Ofisa Wanawake anasema kwamba kesi nyingi hazipatiwi ufumbuzi na kwamba itakuwa vigumu kupambana na udhalilishaji wa wanawake na watoto katika Wilaya ya Mjini bila jamii kubadilika pamoja na polisi na mahakama kuonesha kutenda haki.

Hidaya anasema kuwa, kwa bahati mbaya, baadhi ya walimu wa dini au ‘watu wanaojitokeza sana kuhubiri dini’ ndio wanaoongoza katika udhalilishaji wanawake na watoto, na kufanya kazi ya kupiga vita udhalilishaji kuwa ngumu.

Maria Obel Malila anasema kuwa japo dhamana katika mahakama ni haki ya mtuhumiwa, lakini haki hiyo inatumika vibaya kwani watuhumiwa wengi wanapewa dhamana bila kujali watoto wanaoathirika.

Kwa upande wake, Rahma Ali Khamis, Mkurugenzi wa Wanawake- Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Watoto, na Wanawake anasema, “Ubakaji upo, japo ni vigumu kujuwa ni kwa kiwango gani kutokana na kutokuwepo mfumo maalum ukusanyaji takwimu. Mfano takwimu za polisi, kitengo cha uhifadhi wa watoto, hospitali na zinaweza kuwa ni hizo hizo.”

Anasema tatizo la ubakaji katika jamii lipo, lakini halijapewa uzito na jamii yenyewe katika kulishughulikia na kulimaliza. Serikali inajitahidi kuweka mikakati ya kusaidia kupunguza au kumaliza kabisa, lakini bila mashirikiano ya dhati katika ngazi zote kuanzia familia, shehia, wadau (hasa viongozi wa dini), polisi, mahakama, na serikali haitokuwa rahisi.

“Ipo kesi moja iliyokuwa maarufu sana mwaka jana ambapo mwalimu wa chuo (madrasa) alibaka na kulawiti wanafunzi wake zaidi ya 20, lakini pamoja na ushahidi ulijitosheleza, hakimu akamwachia huru mtuhumiwa kwa sababu tu ya tofauti kati ya kuvaa shuka na kuvaa seruni!” anasema Maria.

Maria anaongeza kuwa pamoja na kwamba kesi karibu zote zilifikishwa mahakamani, ni chache sana ambazo zilipatiwa ufumbuzi. “Nyingi bado zinasuasua, na nyingine kutupwa kutokana na kinachodaiwa kukosa ushahidi,” anasema.

Ofisa Mwandamizi wa Polisi, Kamishna Mussa Ali Mussa anasema hali si nzuri katika kesi za kulawiti na kubaka.
“Nakubali baadhi ya askari polisi inawezekana wanashirikishwa katika vitendo vya rushwa na kupoteza kesi, lakini tatizo kubwa lipo katika jamii.

Uelewa mdogo, ambapo unasababisha kupotea ushahidi. Pia, mara nyingi wanafamilia wanaamua kumaliza kesi katika ngazi ya familia,” anasema Kamishna Ali.

Pamoja na kwamba Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma kutoweza kutoa ushirikiano, takwimu za polisi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka jana (2011) kesi za kutorosha, kulawiti, na mtoto wa kike kuingiliwa kinyume na maumbile ziliongoza, ambapo kesi kati ya kesi zote 268 za udhalilishaji katika mkoa huo ni 55 tu ambazo zilifikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa polisi, kesi 213 hazikufikishwa mahakamani kutokana na kukosekana ushahidi wa kutosha, watuhumiwa wa taarifa hizo kutoroka na wahanga wa taarifa kutokuwa tayari kuendelea na kesi zao mahakamani.

Watafitiwa 21 wakiwamo Khamis Ali Mohamed wa Shehia ya Malindi, Mabruk Salum Khamis wa Amani, Ishaku Hassan Machano wa Mwembe-Tanga, Salama Abdulrahaman Machano wa Bububu na Zahrani Machano Abubakar wa Mwembe-Shauri, wanaeleza kuwepo kwa ubakaji na kulawiti wa kiwango kikubwa katika maeneo wanaoishi.

Chanzo cha ubakaji katika Wilaya ya Mjini

Katika utafiti huo kulijitokeza mtizamo tofauti kuhusu chanjo cha watoto kubakwa katika wilaya ya mjini, lakini Hidaya alisema tatizo la ubakaji limechangiwa na upungufu wa maadili miongoni mwa wanajamii, ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa wanajamii, uwezo mdogo wa wanawake wa kujitetea, rushwa, sheria dhaifu, na chuki.

Baadhi ya watu waliohojiwa (watafitiwa), pia walitaja kuporomoka kwa maadili, tamaa (kuendeleza matamanio), ulipizaji kisasi, ugumu wa maisha (umasikini), ukosefu wa uadilifu katika vyombo vya sheria, kuvunjika kwa ndoa, na kuongezeka kwa vishawishi vinavyotokana na utandawazi, kuwa ni miongoni mwa sababu kubwa za ubakaji na kulawiti.

Wanasema tamaa za kimwili kwa watu wazima kiumei na hata vijana zinazosababishwa na kuporomoka kwa maadili (mfano, watu kuacha mazingatio ya dini, na kukosa aibu), na watoto-vijana kuanza mapema kujiingiza katika starehe.

Mwanadada Maria anasema kwamba ukosefu wa utulivu katika familia likiwemo kuvunjika ndoa na ugomvi pia imekuwa ikichangia vitendo vya ubakaji kwa sababu watoto wanakuwa katika hatari ya kubakwa.
Mkuu wa wilaya ya Mjini, Kanali Mstaafu Abdi Mahmoud Mzee anasema kwamba pamoja na kuporomoka kwa maadili, lakini pia matumizi ya pombe na dawa za kulevya (mfano bangi) inachangia vitendo vya ubakaji katika wilaya yake.

Athari za ubakaji

Watafitiwa walielezea athari nyingi za kubakwa watoto, zaidi ikiwa ni athari za kiakili (saikolojia), kuharibika sehemu za siri, kupata ugonjwa (ikiwemo virusi vya Ukimwi), kupata ulemavu kwa baadhi ya matukio, watoto kushindwa kusoma vizuri, kunyanyapaliwa, mimba, kuzoea ngono mapema wakati wa umri mdogo, na pia uhasama miongoni mwa familia/jamii na wabakaji.

Dk Msafiri Marijani wa One-Stop-Centre (kituo katika hospitali kuu ya Mnazimmoja cha kuwahudumia waliobakwa) anasema watoto wengi wanaobakwa wanapata athari kubwa katika maisha yao yote,
“Pia kuna zaidi athari za kiafya ambapo watoto wanaharibika sehemu zao za siri, na akili.”

Nini kifanyike kuzuia ubakaji?
Mfano, baadhi ya watu waliohojiwa walipendekeza kuimarishwa sheria, wabakaji wahasiwe, wabakaji wafungwe maisha, sheria za Kiislamu – wabakaji kupigwa mawe zitumike, na sheria kali ya kunyongwa.
Ushirikiano wa pamoja

Katika hilo, Rahma na Maria wanasema ili kushinda vita dhidi ya ubakaji, ni lazima wadau wote wafanye kazi kwa mashirikino, na pia ni muhimu kuanzishwa kitengo maalum cha takwimu ili kiwe chombo pekee cha kutoa takwimu za kuaminika na zinazowakilisha Zanzibar.

Vita dhidi ya ubakaji iwe ni ajenda:

Hidaya anasema kwamba ikiwa suala la ubakaji litafanywa kuwa ni ajenda na makundi mbalimbali, litakwisha.
Mfano mzuri ni kwamba viongozi wa kidini kupitia jumuia zao, mfano Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki) walichukuwe kwa uzito kama walivyonyanyuwa sauti zao juu ya katiba na suala la muungano, ubakaji utakwisha.

Advertisements

7 responses to “Ubakaji wa watoto Zanzibar, tatizo sugu linaloisumbua jamii

 1. Ndugu yangu Salma Said tuseme Tanganyika haya hayapo au vipi?

  Mbona kimya hawaja report au wanataka kutwambia Wazanzibari ni mabasha na Watanganyika ni Wastaarabu?

  Siamini hata kidogo kuwa Tanganyika ubakaji ni mdogo, ya gujuu!.

  Haina maana hawa wabakaji wa Zanzibar waachwe no wakomeshwe. Lakini hatutaki wayashikie bango/kidedea matatizo yetu, kama kweli watendaji waanze na yao kwanza huko kwao Tanganyika.

  Nilimsikia Geoge Njogopa kwenye DW juu ya ushoga na mashoga kudai kutambuliwa kikatiba eti alikosa wasenge woote wa Kitanganyika wa kuwahoji badala yake mwandishi yule alimtafuta kwa vumba na udi kijana mmoja msenge wa Kizanzibari anayeishi Dar-es-Salaam akamhoji na kumrusha hewani kupitia DW ilikuwa ni wakati cha Rasimu ya mabadiliko ya Katiba mpya ya Tanzania.

  Lengo lao ni ile propaganda ya kuwa Wazanzibari (WAISLAMU) ni mabasha na wasenge na ni founders wa jambo hili.

  Salma Said ndugu yangu kesi hii iliniuma sana na ndio maana Geoge Njogopa huwa sipendi the way anavyo undermine Uislamu na Wazanzibari katika fani yake yuko after Utanganyika na Ukristo zaidi.

  MUUNGANO HUU HATUUTAKI.

  JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR KWANZA.

  “When peace fails apply force”

  Nawasilisha.

  SERELLY.

 2. Ubakaji hawishi kwasababu nchi yetu inatawaliwa na dhulma na rushwa. Mbakaji anajuwa kuwa nikibaka hata nikikapatwa basi nitazima tu kwa rushuwa. Hii ni sababu kubwa inayowafanya wanafamilia kumaliza kesi za ubakaji kimya kimya. Kwani wanajuwa fika kuwa hakuna haki mbele ya pesa, isipokuwa ni kutangaza aibu tu. Mfano nzuri hivi karibuni kama miezi sita iliyopita askari mmoja jina nalihifadhi alimbaka mwanafunzi wa shule huko wilaya ya Mkoani Pemba na kesi mpaka hii leo inasusua. Hatujuwi kama inaenda au ndio tayari ishazimwa. Sisi Wananchi tushakata tamaa na mambo haya tumepoteza imani zetu. TUJIREKEBISHENI KWENYE DHULMA NA RUSHWA KWANZA MENGINE YATAFUATA WENYEWE. TUSITAFUTE MCHAWI TUNAMJUWA. Ni RUSHWA DHULMA ULAJI ULAJI NGWAFUWA BWAGIA. Mnyonge hana haki.

  • Mtu sheria kichwani mwako akilawiti wa kwako au akibaka k atoto kako we fanya unavyo jua, mahakamani kukasomwe kesi nyingine lkn si ubakaji wala liwatwi. Ivi ivi ahkha.

 3. Niwajibu wa jeshi la polisi kuhakikisha Usalama wa raiya sio kuwa mbele kwenda kudhulumu watu kwa mabomu ya machozi na maji ya muwasho.
  Leo vipi kisiwa kidogo Kama Zanzibar uhalifu uzidi ? FFU wako wapi, Usalama wapo au hawajuwi kazi zao . ?
  Wakati umefika kuwa na polisi yetu iliyo na mchanganyiko wa jamaii za kizanzibari sio Kama unaasili ya kiarabu,kihindi au kingazija huandikwi lazima ule na asili ya baadhi ya mashamba ya kiunguja.
  Zanzibar kwanza vyama baadaye.

 4. Asalamu Alaykum, Ndugu Sellely naomba chukulia kila jambo kwa upana wake wake na tuwache mawazo ya kuwa tunahujumiwa kwa kuwa waislamu au tunakuza mambo bali ndio ukweli ulivyo, sipendi niseme kama matatizo kama hayo yapo kwa wenzetu au hakuna lakini mimi nazungumzia hali ilivyo zanzibar na wala sitaki kumjibiwa Njogopa kwa nini kafanya hivyo kwa kuwa yeye ni mwandishi ana anajua mwenyewe watu wa kuwatafuta lakini kama kampeata mtu kutoka zanzibar na mwenyewe amekubali kurikodiwa na ndio ukweli hakumzulia nadhani sio tatizo, lakini tukirudi katika suala la wingi wa matendo haya ukweli haupingiki kwamba jamii yetu imeharibika kwa kiasi kikubwa katika uvunjifu wa maadili na uharibifu wa watoto wa kike na kiume na mambo haya hufanyika mpaka kwa walezi kwa maana ya walimu ambao wanapewa jukumu la kuwalea na kukaa na wanafunzi, na imefika pahala hujui nani umuamini kwa kuwa ikiwa wajomba ndio wanaowabaka watoto, ikiwa kaka ndio wanaowabaka ndugu zao ikiwa walimu ndio wenye kuwabaka wanafunzi wao ujue jamo hilo sio siri tena na wala sio la kulionea aibu kwa kuwa limevuka mipaka na wala hakuna saabu ya kumtafuta mchawi ni sisi wenyewe kwa sababu utafiti umeonesha ni kuwa wafamilia ndio wanaohusika na maendo haya. Na ningekuwa sijashiriki katika huo utafiti ningesema sio kweli lakini ni kuwa mimi mwenyewe nimeshiriki na hii ni mara ya pili kufanya utafiti kama huu tena mara hii naona mambo yameharibika zaidi. Hatupaswi kubadilsha sauti kwa kuwa jambo hilo linafanywa na jamii yetu bali tunatakiwa kunyanyua sauti na hakuna kufica kwa sababu huko kufica na kuna aibu na kujitia tunalinda mila ndio limetufikisha hapa lilipotufikisha na hivyo ni wakati wa kupaza sauti ili kutafuta namna ya kuliondoa kwa kulizika kabisa na sio wakati wa kuanza kutafuta vizingizio ambavyo havina maana na wala haviwezi kutusaidia kusema kwani tanganyika wao hawabaki hakuwezi hata siku moja kutusaidia kwani wao wakiwa wanabaka au wakiwa ndio wanaongoza jee kwetu litaondoka kwa kusema hivyo? na kwa nini tutafute visingizio wakati kweli tatizo lipo? Naamini yapo baadhi ya mambo yanatokana na mfumo ulionayo au kero za muungano lakini katika hili halitokani na hilo kwa sababu wenye kuathirika zaidi ni maeneo ambayo hata hayajaathirika na huo utalii wala hayajaahirika na wageni kiasi hicho, mfano suala la ubakaji linaongoza zaidi katika mkoa wa kaskazini Pemba kwa mujibu wa takwimu sasa jee kaskazini kuna utalii? kuna wageni ukilinganisha ni maeneo mengine? sasa hapo ndio pa kujiuliza ni kiu gani? halafu kwa upande wa Unguja ni mkoa wa kaskazini pia maeneo ya kuanzia Mahonda na kwenda mbele kabla hujafika Nungwi ndiko kwenye matukio mengi ya ubakaji na halafu yanafuatiwa na maeneo ya mijini Saateni, Jangombe, Miembeni na maeneo mengine yakiwemo Mwera na Makunduchi jee kuna nini huko? Nakuachia suali hilo. Salma Said

 5. Mi nawaulizeni nyie mlio fanya tafiti, hawa wabakaji waliofikishwa mahakamani ni wangapi ambao wamechukuliwa sheria kali za kukomeshwa? Na niwangapi wame tolewa kwa rushwa? SIRIKALI inachukua hatua gani za kukomesha?
  Mimi wito wangu kwa jami
  Kwanza, nawambia wenye tabia hizi waache haraka mno.
  Pili, atakaye fanyiwa uchafu huu, WAA-ALLAH TUMIA UPANGA kutakaza dhambi hii, SIRIKALI lazima watapata taarifa na itakua hapo haujaficha, kwani SIRIKALI wanajifanya hawaskii. Samahanini sana, mtuafikiri kua km kafanyiwa yeye binafsi inakuaje? Ina uma sana.

 6. Wabakaji wanalindwa na dola hutowa rushwa wakadunda mitaani hawafanywi kitu kutokana na dhuluma. Ole wenu wabakaji sasa tunachukuwa sharia mikoni mwetu. Tukikumata tutakuweka kilema. Tunakuchoma kwa moto au tunakata kichwa au tunakufanyia unyama wowote. Mahakamani zitasomeka kesi nyengine lakini sasa hivi tumeshajiandaa kupambana na wabakaji sisi wenyewe. Serikalini rushwa juu ushahidi haupatikani.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s