Kwa hili, viongozi wa SUK wafuta ujinga

Hamad Masoud Hamad aliyekuwa waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar

HATA kama wapo wanaojaribu kujenga imani kuwa waziri wa miundombinu na mawasiliano aliyejiuzulu, Hamad Masoud Hamad afaa kushitakiwa, uamuzi aliouchukua ni muafaka. Mjumbe huyu wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Ole, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, hajatenda kosa bali ameonesha uwajibikaji.

Yeye kama waziri lazima atangulie kutoka kitini. Ingeshangaza kama angeshikilia pale. Atakaaje huku mamia ya wananchi wametokomea katika matukio mawili ya kuzama meli chini ya mwaka?
Asingetenda haki kwa nafsi yake, asingetendea haki wananchi na serikali yao.

Tena heko kwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein kukubali ombi la Hamad Masoud Hamad la kujiuzulu uwaziri aliomteua tangu alipounda serikali ya umoja wa kitaifa Novemba 2010. Naye rais asingekuwa ametenda haki kwa nafsi yake kama kiongozi wala kwa wananchi na serikali. Angekuwa amejipalia makaa ya moto.

Ile ni hatua ya kwanza nzuri. Kuachia wadhifa ambao kiongozi amepewa kuongoza watu pale panapotokea matatizo yaliyosababisha hasara kwa taifa – hata iwe ndogo kiasi gani, ni jambo la lazima katika dhana ya uwajibikaji.

Ndiyo gharama ya siasa – kuwajibika kiuongozi kunapotokea mkasa kwa wale wanaoamini katika dhana ya uongozi bora. Sasa je, kupotea roho za mamia ya wananchi kwa sababu ya uzembe katika kushika majukumu si mkasa? Ni nini?

Ndio msimamo wangu kwamba kuna uzembe wa kusimamia sheria na kanuni katika nyanja ya usafiri na usafirishaji. Sheria zipo hazilindwi. Kibaya kwamba siyo hazilindwi kwa vipi – rushwa na ufsadi.
Sitaki kuamini kuwa wale maofisa usalama waliopo bandarini Malindi na Dar es Salaam , wanaruhusu bure vyombo vibovu au vizima lakini visivyo na wafanyakazi wabobezi, vizima ila havina vifaa vya usalama vya kutosha na vya kisasa.

Wanalipwa, tena fedha nyingi. Viwango na namna wanavyolipwa wanajua wenyewe, mawakala na washirika wao. Na kama wanaruhusu bure, ni watumishi wajinga wa aina yake. Nataka kusema Hamad Masoud Hamad ameanza tu kuwajibika. Bado wakurugenzi, wachunguzi na wakaguzi ndani ya Zanzibar Marine Authority (ZMA) na Surface and Marine and Transport Authority (SUMATRA). Nao waende sasa halafu!

Malindi mv Skagit ilianzia safari; bali Dar es Salaam bandarini chombo hiki kilipakia na kuondoka kuanza safari ya kurudi nyumbani. Kilipakia pomoni. Hii ni hatua ya pili. Tume ya uchunguzi ni hatua ya tatu, hatua nzuri kabisa. Itafute nahodha ana sifa? Alikuwa na wafanyakazi wajuzi wa nafasi zao? Alikuwa na zana za uokoaji? Chombo kizima? Kimejengwa kwa kiwango stahili?

Napata moyo kwamba kumechukuliwa hatua ambayo ni sehemu muhimu ya ufumbuzi wa mashaka makuu katika usafiri wa baharini – kununua meli ya abiria wengi. Rais Dk. Shein anapomuagiza waziri wake wa fedha, Omar Yussuf Mzee, atafute fedha popote kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kupatikana meli kubwa ya kubeba abiria wafikao 1,000 ni jambo kubwa.

Kinachowasukuma wananchi wa Unguja na Pemba , na ndugu zao walioko Tanzania Bara na wasafiri wengine kimaisha, kupanda vyombo duni ni umasikini. Wangekuwa na kipato cha maana wangepanda boti za kasi ambazo kwa saa mbili na kdigo hivi wamefika waendako. Vyombo vya kasi, na nauli zake ni za kasi pia. Hawa wananchi pangumakavu, hawavimudu.

Heko nyingine serikali kuzuia meli chakavu kufanya kazi. Uamuzi huu ulitakiwa uwe wa kawaida kila pale inapoonekana chombo fulani kina mushkeli kiufundi. Muhali si muhali. Basi nini? Rushwa. Muhali unaendana na malipo haramu. Maofisa waliopo bandarini wanaachia vyombo vichakavu visafiri. Hawa si wataalamu, ni majununi. Huwezi kuachia chombo kibovu kibebe watu; wakifa, unakwepa kuwajibika! Haikubaliki.

Kelele zimepigwa kwa muda mrefu tangu zilizokuwa meli za serikali, mv Maendeleo na mv Mapinduzi zilipochakaa na kutoka mikononi mwa serikali. Liliibuka tatizo kubwa la wananchi kukosa chombo muafaka cha kusafiria, hasahasa kati ya Unguja na Pemba hadi Tanga, ambako watu wake wana maingiliano sana .

Serikali ilikuwa haijaona umuhimu wa kupata meli mpya. Kwa lugha mbaya, mtu aweza kusema misiba ndio imewazindua. Sina maana hiyo. Walijisahau mno. Ila sasa natoa indhari. Tupo macho kufuatilia utaratibu wa kununua meli mpya. Twenye kazi zetu tutasema tukinusa tu kuwa maofisa wa serikali wanapanga ufisadi katika hili.

Serikali isikae kitako. Hatua za kujipanga zingalipo. Hata ukiwa na meli na vyombo vipya, ajali ni jambo la kawaida si baharini tu hata barabarani. Nyingine hazitokani na uzembe. Hizi ndizo zile unaweza kusema “kwa rehema tu ya muumba.”

Anapoleta dhoruba kali, hakuna chombo chema. Hapa ndipo pale meli kubwa huzama, vidau vikapona. Janga halichagui akitaba Rabbana. Sasa ikitokea ajali tumejipanga kusaidia wasafiri? Ni jambo kubwa linalohitaji ufumbuzi wa kudumu. Tunahitaji wazamiaji, zana zao, vifaa vya kustiri waliozama mara tu wakishaokolewa au wakishaopolewa.

Panahitajika mochwari ya kisasa pale Mnazimmoja Hospitali, tunapojinasibu ndio hospitali yetu kubwa kabisa – ya rufaa. Hatuwezi kuendelea kuanika miili viwanjani. Haiwezekani na haikubaliki. Maiti ni jambo kubwa kiutu, yapasa kutunzwa vizuri kwa ajili ya utambuzi, kabla ya kuchukuliwa kuzikwa.
Watu wasiangalie tu ajali za barabarani walizozizowea, na za majini zinazoanza kuzoeleka; kuna ajali za angani ambazo nazo zinahusisha watu wengi. Na yetu ni nchi ya visiwa inayotegemea utalii na watalii wanatoka mabara yote duniani.

Kwa kweli, mita 30 chini ya bahari kwa mafundi si mbali hivyo. Wakiwepo wazamiaji mahiri na wakiwa na zana nzuri, wanaweza kufika mbali chini ya bahari hata kuzidi mita 50.

Nilipozungumza na Mzee Ahmed Khamis kwa umaarufu Kipande, mtaalamu wa uzamiaji aliyepata mafunzo ya juu nchini Uingereza, alisema:

“Tuseme ndege ya watalii 500 imeangukia baharini, tutafanyaje kusaidia abiria na wafanyakazi wa ndege hiyo?” Siku hizi ndege kubwa za watalii zinatua Zanzibar kutoka miji mbalimbali ya Ulaya.

Hili linataka viongozi kutafakari. Pamoja na mawaziri wa sekta nyingine, haya ni majukumu muhimu ya waziri mpya, maalim Rashid Seif Suleiman.

Baada ya kuzuia meli chakavu kusafiri, serikali ifute usajili wa meli hizo. Wenyewe waziondoe bandarini. Watafute nyingine. Na kuanzia sasa, mleta meli alete kwanza nyaraka, zikaguliwe na kuthibitishwa. Tusiruhusu chombo chakavu.

Mwenyezi Mungu ana sifa nyingi, moja ni kumpa mwanadamu maarifa. Sasa viongozi wa SUK wanakataa kumsingizia muumba; wanatumia maarifa aliyowapa. Alhamdulillah.

Advertisements

One response to “Kwa hili, viongozi wa SUK wafuta ujinga

  1. Ripoti ya Omar Ali Shehe, which implicated top officials of this Ministry with scandals also needs to be considered.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s