Serikali yalifungia tena MwanaHalisi

Serikali imelifungia gazeti la MwanaHalisi kwa madai ya kuandika habari za uchochezi

SERIKALI imelifungia Gazeti la Mwanahalisi kwa kile ilichodai kuwa mwenendo wake wa kuandika habari na makala ni wa kichochezi, uhasama na uzushi.Hii ni mara ya pili kwa Serikali kulifungia gazeti hilo. Hata hivyo, safari hii imelifungia kwa muda usiojulikana kuanzia Julai 30, mwaka huu. Mara ya kwanza lilifungiwa mwaka juzi kwa kipindi cha miezi mitatu likidaiwa kumchonganisha Rais na familia yake.

Akitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam kwa niaba ya Msajili wa Magazeti, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Habari – Maelezo, Fabian Rugaimukamu alisema jana kwamba makala hizo zimesababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Alisema hivi karibuni gazeti hilo katika toleo lake namba 302, la Julai 11 hadi 18, mwaka huu na toleo la Julai 25 hadi Agosti Mosi, lilichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

“Tumeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana Gazeti la MwanaHalisi. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, Kifungu namba (25) (1), adhabu hiyo itaanza Julai 30 (jana), 2012 kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba 258 lililochapishwa Julai 27,” alisema Rugaimukamu.
Alisema Mhariri wa gazeti hilo ameitwa na kuonywa mara nyingi lakini, hakutaka kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Alisema mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu Kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kusema kwa makusudi amekuwa akiacha kukinukuu Kifungu cha 30 cha Katiba, kinachoweka ukomo wa uhuru wa habari.

Kufutia matukio hayo, alisema Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.

Alisema kama ilivyoelezwa bungeni wakati wakuwasilisha bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni, waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya taifa na uzalendo.

Alisema kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini.

MwanaHalisi wasikitika
Akizungumzia uamuzi huo wa Serikali, Mhariri wa Mwanahalisi, Jabir Idrissa alisema umemsikitisha kwani umechukuliwa kwa kutumia sheria ambayo ni moja kati ya zile ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwamba ni kandamizi.

Idrissa alisema hadi jana mchana kampuni yao haikuwa imepata taarifa rasmi za uamuzi huo wa Serikali lakini, aliupinga akisema unalenga kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Kama unavyojua, Waziri ametumia sheria ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwamba ni kandamizi, hii (Sheria ya Magazeti) ni moja ya sheria 43 ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwamba ni kandamizi tangu miaka ya 1990. Kwa hiyo, siwezi kusema tutachukua hatua gani kwani tunahitaji kukaa na kujadili kwanza uamuzi huo,” alisema.

Jukwaa la Wahariri
Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alisema hatua hiyo ya Serikali ni kitisho dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Alisema wakati dunia inaendelea kufungua milango ya uhuru wa vyombo vya habari, demokrasi na uhuru wa uhariri, inashangaza kuona nchini hali ni tofauti na Serikali inataka kurudisha mambo nyuma.
Alisema malalamiko juu ya sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari yalitolewa mbele ya Rais Jakaya Kikwete katika sherehe ya kutoa Tuzo kwa Waandishi bora wa habari, lakini inasikitisha kuona ukandamizaji, vitisho na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari unazidi kushika kasi.

Kibanda alisema hadhani kama uamuzi huo wa Serikali unatokana na MwanaHalisi kufanya kazi zake bila kuzingatia weledi wa kitaaluma, bali pengine ni kutokana na msukumo wa hofu ya mambo yanayoandikwa na gazeti hilo kwamba yanaiweka pabaya Serikali.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

8 responses to “Serikali yalifungia tena MwanaHalisi

 1. Nchi hii kusema ukweli ndio kosa, poleni sana mwanahalisi kwa hasara mlioipata, fungueni blog au website muendelee kutupasha habari hawana uwezo wa kuihack, kuifunga, iko nje ya uwezo wao, wala haihitaji kibali

 2. ¤An-Nuur hawajaliona Ehee…. Gazeti linalotukana Hadi Viongozi wa Nchi.

  ¤Gazeti linalogomea Sensa ya Kitaifa..

  HAWAJAONA HAYA????

 3. Hiyo ndio faida ya kuandika ukweli kwenye magazeti ukiandika ukweli hatua zinchukuliwa ukiandika uongo poa tu

 4. inashangaza tupo katika karne za uwazi lakini bado udikteta unachukua nafasi, vyombo vya habari viwe huru kuandika ukweli, waswahili wamesema ukweli unauma …… ndio maana mmelifungia gazeti lakini ukweli utadumu hata mkifanya nini

 5. Hivi ndivo walivyo viongozi wa afrika. Wanataka kusifiwa tu. Japokuwa wananuka mavi. Ukiwaeleza ukweli wanakasirika, na wanakuona mkorofi. Viongozi wetu inafaa mubadilike wakati wa kufagiliana umepitwa na wakati huu ni ulimwengu wa ukweli na uwazi likitangazwa baya lako likubali na ujirekebishe kulifungia gazeti haitosaidia kitu kwani kuna njia nyingi za kupashana habari. Viongozi inafaa mukubali mabadiliko. Ukweli ni nzuri lakini ni mgumu na unauma vumilieni machungu hii ndio democracy.

 6. POLENI GAZETI LA MWANAHALISI HII NDI TANZANIA. INAJIFANYA NI NCHI YA KIDEMOKRASIA USONI ILA NI NCHI YA KIDIKTETA NDANI YA ROHO NA NAFSI ZA VIONGOZI WAKE. TABIA YA MADIKTETA SIKU ZOTE HUWA WANAPENDELEA WASIFIWE TU HATA KAMA WANAHARIBU. HUJIUNDIA VYOMBO VYA HABARI VYA SERIKALI ILI WASIFIWE TU. HUU SIO TENA WAKATI ULE NI WAKATI WA UWAZI NA UKWELI WAKATI HUU HAMUWEZI KUWADANGANYA WANANCHI SIKU ZOTE NA MASAA YOTE KAMA NI WEZI HAKUNA JINA JENGINE LA KUWAITA ZAIDI YA HILO. KAMA NI MAFISADI AU MADIKTETA HALI NDIO HIYOHIYO. KIONGOZI BORA NI YULE ANAEKUBALI KUKOSOLEWA NA AKAJIREKEBISHA NA SIE ANAETUMIA UBABE NA SHERIA KANDAMIZI KUWANYAMAZISHA WANAHABARI. UNAWEZA KUMCHUKUA PUNDA HADI MTONI LAKINI HUWEZI KUMLAZIMISHA KUNYWA MAJI. MWANA HALISI SASA NI WAKATI WA KUTUMIA NJIA MBADALA AMBAYO ITAWAUMIZA ZAIDI MADIKTETA.

 7. Hii ya kufungia Magazeti haishangazi. Kwenye nchi ambayo hata watunga Sheria wanachukua Rushwa haya lazima yatokee. MwanaHalisi tafuta njia nyengine ya kupasha watu habari. Mbona akina Kisonge ambao wanaandika maandishi ya kichochezi hawapigwi marufuku kufanya hivyo! Kuvumiliwa kwa Kisonge kuandika maandishi ya Kichochezi kunatushangza. Wengi wetu hatujui hawa ni akina nani. Sijui wanatumia Sheria ipi kufanya watakavyo! Lakini maandishi ya Kisonge si tu yanahatarisha amani lakini yanavunja haki za Watu za Kikatiba.

 8. Ni kweli inasikitisha kuona Serikali zetu zinataka kuturudisha tunakotoka, uhuru wa habari ni kitu muhimu katika kukuza ustawi wa taifa lolote lile hasa katika zama hizi za demokrasia na uwazi.
  Wanaweza kufungia gazeti lakini hawawezi kutuzuia kufikiri.
  @okey. ANNUUR, Haliwezi kufungiwa maana haliandiki porojo, wanayoyaandika yote yana ukweli ndio maana serikali haijaibuka kujibu hoja hata moja iliyoandikwa na gazeti hili. Ninachokiona kwako Okey ni chuki tu dhidi ya gazeti hili kwa vile linaibua mambo ya msingi na kuwasemea wasio na sauti katika nchi hii “WAISLAMU NA WATANZANIA WOTE”
  Sasa kama wewe hoja ni kugomea SENSA gazeti hili halijaandika udaku kuhusu kitu kinachoitwa SENSA, labda nikumbushe tu. Kabla ya mchakato wa SENSA kuanza serikali iliwaita viongozi wa dini zote na kuwataka kutoa maoni yao katika kufanikisha mcahakato huo. Miongoni mwa hoja iliyoibuliwa na viongozi wa dini ya kiislamu ni uwepo wa kipengele cha dini katika dodoso la sensa. Na hayo hayakusemwa bure au kw akujifurahisha.

  Miongoni mwa hoja za Masheikh kutaka kipengele cha dini kuwepo katika sena ni:-

  Kwanza, kutokuwepo kwa takwimu rasmi zinazohusu dini za Watanzani jambo ambalo limepelekea baadhi ya makundi kupotosha idadi halisi ya wanadini. Mfano ni juzi tu, TBC TAIFA walitoa takwimu kuhusu idadi ya waumini wa dini na wale wasiofuata dini yoyote hapa Tanzania. Matokeo yake gazetui hilo unalodai lifungiwe likahoji chanzo cha takwimu zilizotolewa na TBC, lakini walishindwa kutoa chanzo walichotumia kupata takwimu hizo. Mwishowe TBC walilazimika kuomba radhi. Je kwa kuhoji mamabo ya msingi Annur nalo lifungiwe?

  Kwa taarifa yako, Annur wanahaki ya kusimamaia msimamo wa WAISLAMU TANZANIA wa kutokushiriki SENSA mpaka hoja zao za msingi zisikilizwe. Na kwa vile wao wanasimama kama chombo cha habari na SAUTI YA WAISLAMU basi wanahaki ya kufanya hivyo.

  Labda mimi niulize tu Serikali, kuna magazeti haya yanayoitwa ya UDAKU, kazi yake kubwa ni kuandika habari za uchokonozi na baya zaidi magazeti hayo ni vinara wa kuandika picha za uchi, makala zake nazo hazina zaidi isipokuwa kushabikia ngono tu. Jambo ambalo ni kinyume cha utamaduni wetu. Je nao WADAKU wataendelea kudakua, huku wakichafua utamaduni wetu?

  Nawasilisha….

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s