Mvuvi atamba wakiwezeshwa wataokoa abiria

Na Jabir Idrissa
MVUVI mzoefu anayeishi kijiji cha Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja anaamini shughuli za uokoaji baharini zinaweza kufanywa kwa ufanisi mkubwa pakiwepo maandalizi mazuri. Zahor Tamali, ambaye amekuwa katika maisha ya baharini kwa miaka 20, anashauri serikali ianzishe mfuko maalum wa dharura wa fedha za kutumika wakati ajali.
Katika mahojiano maalum na MwanaHALISI juzi, Tamali amesema anaona inafaa shughuli za uokoaji zikawekwa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi. Ana sababu.
“Unajua idara hii inawajua wavuvi wote. Inashughulikia kamati za wavuvi Unguja na Pemba na inatoa elimu ya uvuvi endelevu.
“Serikali itumie hazina ya mkurugenzi wa uvuvi, anajua wavuvi na viongozi wao, na anawasaidia sana . Kila wakati yuko nasi.
“Huyu amekuwa bega kwa bega kuelekeza na kukagua shughuli zetu. Hasubiri ripoti ofisini huyu. Anakwenda mwenyewe mpaka chini ya bahari pima kumi akipiga mbizi bila hofu.
“Anajua hasa oganaizesheni ya baharini. Anazijua hifadhi zote Zanzibar . Ni rahisi kuwaongoza wavuvi kwa shughuli za kuokoa watu panapotokea chombo kuzama,” anasema.
Mkurugenzi wa Uvuvi Zanzibar ni Mussa Aboud Jumbe Mwinyi, mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania kwa miaka 12 – Aprili 1972 hadi 1984.
Tamali ambaye huuza samaki wake Soko Kuu la samaki Feri, Dar es Salaam , anazitaja hifadhi hizo kuwa ni MENAI inayohudumia Mkoa wa Kusini na Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Hifadhi nyingine ni MINCA inayohudumia Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kwa upande wa kisiwa cha Pemba , kuna hifadhi ya PECO. Hifadhi hizi zinasaidia kulinda mazingira nyeti ya baharini kwa maeneo yote Zanzibar .
“Kwa kuwa hawa tunawaamini sana na wao wanatujua kwa tabia zetu, kilichobaki ni serikali kutambua kuwa mchango wetu wavuvi katika uokoaji hauna mfano,” anasema.
Anahoji, “kwani ni nani waliowahi kuokoa watu ilipozama Spice Islander kule Nungwi. Ni wavuvi pamoja na wawekezaji binafsi wa sekta ya utalii wanaomiliki boti za kasi.”
Tamali anasema uokoaji wa haraka na wenye ufanisi hufanywa na vyombo vidogo vikiwemo ngwanda, ngalawa na boti za fibre zinazofungwa mashine nje. Anasema kuna vyombo hivi vipatavyo 36,000 Zanzibar .
Fikiria, anasema, boti ya kisasa ya Police Marine, iliyotolewa msaada na Marekani, iliagizwa kwenda eneo la tukio, lakini “ilishindwa njiani (kabla ya kufika Chumbe) ikarudi.”
Hata ingefika, anasema, ingeishia kuhangaika tu. Kwanini? Anasema, “wafanyakazi wao hawana ujuzi wala uzoefu wa kuzamia kama tunavyofanya sisi. Hawajiamini.”
Anatoa mfano wa kilichotokea bandarini siku ilipozama mv Skagit . Boti kubwa ya kampuni ya Azam & Coastal Ferries ilitumwa eneo la tukio, lakini wazamiaji waliokuwa mbele na tayari kwa kazi ilikuwa ni wavuvi binafsi.
“Usidhani maskhara. Tunajuana na tunakutana kwenye kazi,” anasema Tamali, pia Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Hifadhi ya MENAI na mwenyekiti wa diko (kituo cha uvuvi) la Kigaeni, Makunduchi.
Tamali anasema tatizo kubwa jingine la serikali na taasisi zake ni kuchelewa kuratibu kazi ya uokoaji chombo kinapozama. “Udhaifu huu unaongeza maafa,” anasema.
Anasema ilipozama mv Skagit , wavuvi wadogo ndio waliowahi eneo la tukio na kuanza kuokoa watu wengi kwa kutumia vyombo vyao hivyo vidogo vya mbao.
“Sasa mkurugenzi wa uvuvi angeamuru tu ‘nyie wavuvi, tokeni mkaokoe watu kule, mambo mengine baadaye.’ Ungeona wewe. Kila mtu angetoa chombo chake na kuchukuwa mafuta yake ya akiba akakimbilia kuokoa watu.
“Tungeelekezana sote tukakimbia kuwahi kuokoa. Tunajua idara ya uvuvi itarudisha mafuta yetu na hata kutoa kifuta jasho kwa waliotoa vyombo vyao na kushiriki kuokoa,” anasema Tamali.
Anasema kwa upande mwingine, serikali ingekuwa na mafuta ya kutosha ambayo ikitokea ajali baharini, inagawa mafuta kwa vyombo vituo vya Forodhani (kwa mjini) na Fumba (Magharibi, karibu zaidi na ukanda wa bahari kutoka Dar es Salaam kufika Unguja) ambako wavuvi wangechangamkia kuokoa watu.
Anapoulizwa kama kushauri jukumu hilo lipelekwe Idara ya Uvuvi ana maana Idara ya Maafa ipunguziwe majukumu kwa kuwa hilo ni jukumu lake, Tamali anasema hata ikiwa hivyo “ni sawa.”

Advertisements

3 responses to “Mvuvi atamba wakiwezeshwa wataokoa abiria

  1. Zanzibar kwa vile ni visiwa ndivyo inavyo lazimika kuwa na usafiri wa baharini wa daima, wa abiria na mizigo. Kwa hali hii, Zanzibar inahitaji iwe na meli za kisasa nzuri na madhubuti na ziwe na wafanyakazi wazuri, wajuzi na wenye kupatiwa mafunzo muda baada ya muda; ikiwa ni pamoja na uwezo wa uwokozi; na wawe wanalipwa vyema. Zaidi ya hivi, inahitaji kiwepo kikosi maalumu cha kiraia cha uwokozi wa dharura, kiwe na nyenzo kamili za kisasa za kuaminika na za hakika kwa kilasiku, kiwe kinapatiwa mafunzo muda baada ya muda, na kiwe kinalipwa vyema. Yote haya ni wajibu na dhamana ya sirikali.

    Wa Billahi Tawfiiq

  2. WATU WAKIOKOLEWA WENGI NA MADHARA/MAAFA YAKIWA MADOGO INA MAANA HAKUTAKUA NA MICHANGO. KAMA MICHANGO HAIPO WALE WALIOZOEA KUDOKOA NA KULA HELA ZA MICHANGO YA MAAFA WAKALE WAPI POLISI? NDUGU ACHA TU HUU NI MRADI BWANA. WATU WANASAJILI MAMELI MABOVU KWA YAO. FUNIKA KOMBE.

  3. Pamoja na ushauri mzuri wa ndgu Tamali pia ingefaa tujiulize kulikoni. Nadhani suala la Tabia nchi nalo linachangia ajali miaka hii. Inabidi suala hili lifanyiwe uchunguzi wa kina kuona iwapo bahari nayo haijabadilika ukali wake unaojitokeza. Kwa sababu kasi ya mawimbi ya baharini yamekuwa makali zaidi kiasi ambacho inabidi vyombo vya baharini viundwe kufuatia mabadiliko ya bahari. Nasikia Serengeti imepunguziwa abiria na mzigo wa kubeba. Haya ni maneno tu ya kuwapatia mlo wahusika. Iwapo chombo kimepoteza uwezo wake wa kutoa huduma ni bora kikae pembeni kuliko kukipangia idadi ya abiria kumbe wakishapewa chechote wahusika husema muombe Mungu twende kazini.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s