Maruhani wa Kale katika zama mpya

Mwanamke moja akiwasilisha maoni yake kwa njia ya barua mbele ya tume ya katiba huko Michamvi kusini Unguja

Na Juma Mohammed
Nami katika safu hii leo naungana na watu wote katika kutoa mkono wa pole kwa maafa yaliyotokea kufuatia kuzama kwa meli ya Mv. Skagit wiki iliyopita, “Inna lillahi wa inna ilayhi rajioon”. Baada ya salaam hizo za rambirambi, narejea katika mada yangu ya leo ambayo inayoanza kwa kuuliza swali kwamba mzimu wa Watanzania uko wapi?

Ilivyokuwa kila shetani na mbuyu wake. Mbuyu wa shetani wa muundo wa Muungano anayeinyemelea Tanzania uko wapi? Uko kwa wanaotaka mabadiliko ya muundo kuwa na Muungano wa mkataba au uko kwa muundo wa kale wa Serikali mbili chini ya muundo wa kikatiba?.

Iwe itakavyokuwa kwa mtazamo wangu na wa vijana wengi ni kuona mabadiliko ya muundo wa Muungano ikiwa kuna mtu au kundi linajidanganya kwa kujipamba kwa mauwa wanaoweza kumshika masikio na kumtuliza shetani wa mabadiliko wa muundo wa Muungano wamechelewa maana ni sawa na kufunga banda wakati Farasi keshatoka!

Wakati huu ambapo mjadala wa kutaka mabadiliko katika muundo wa Muungano ukishika kasi,umejengwa uongo mtakatifu kwa baadhi ya watu kwamba kuna watu wana dhamira ya kurudisha Usultani na Utumwa.

Kwa zaidi ya asilimia mia moja, uongo huu nao kwa mwenye akili timamu na hasa vijana wasiokuwa na ajira, wasiokuwa na uhakika wa mlo wao wapi watalala hausaidii kumtenganisha na hoja pendwa ya kutaka mabadiliko katika mfumo wa Muundo wa Muungano kutaka uwe wa mkataba.

Kwangu mimi naona wale wanaofurukuta kutaka kuwaweka mbali vijana na hata baadhi ya wazee wenye kubadilika kulingana na wakati ndio kwanza unawasogeza karibu na wanaweza kutumia kifaa kama barometa ya kujua ni kwa kiasi gani mfumo huu wa Muungano ulivyowasaidia kuondokana na dhiki,ukosefu wa ajira na nchi yao kukosa utambulisho katika medani za Kimataifa.

Kuhusu hoja ya Utumwa na Usultan, sehemu kubwa ya kizazi hichi kilichopo sasa kwao kuwaletea nyimbo hizo sawa na nchi ya kusadikika aliyoiona gwiji wa fasihi ya Kiswahili, marehemu Sheikh Shabaan Robert katika riwaya yake ya kusadikika.

Wengi tunaamini kuwa mabadiliko yoyote katika jamii ni lazima yaende sanjari na mabadiliko ya fikra,lakini ikiwa fikra zile zile, watu wale wale wananchi wanapata mashaka na watu hao wanaohubiri kutaka marekebisho ambayo yamewashinda kurekebisha miaka ya ujana wao mfano wa muundo wa Muungano kwa miaka 48 sasa maneno ni yale yale tuko mbioni kutatua kero za Muungano,lakini mbio hizo hazifikii mfundoni.

Ni vigumu kupata mabadiliko ya kweli ikiwa bado miongoni mwa watu wanaaminishwa kuwa tofauti za kifikra ni dhambi, uhalifu au usaliti jamii ya vijana na hata wazee wenye fikra mpya wasipojifunga mkaja mawazo mgando yatachukuwa nafasi,lakini ni imani yangu katika hili la mabadiliko ya muundo wa Muungano ‘Ras of good hope’ itashinda.

Mohandas Karamchandi Gandhi (Mahatma Gandhi) Baba wa Taifa la India, aliwahi kusema katika mojawapo ya hotuba zake kwamba “First they laugh at you, then they ignore you, then they fight you, then you win!”

Mwanasiasa huyu kwa tafsiri yangu ni kwamba alikuwa akijaribu kuelezea makundi mawili, wale wasiotendewa haki na wale ambao walipaswa kuwatendea wenzao mambo ya usawa na haki wanapoamka na kuanza kudai haki yao “Kwanza watakucheka, baadae watakupuuza, lakini watakupiga vita, kisha unawashinda tena kwa kishindo”(mkazo ni wangu)

Bila shaka tutawashinda maana kila uchao waumini wa Muungano wa mkataba wanaongezeka huku kambi ya muundo wa Muungano wa kikatiba ikiendelea kukimbiwa na wapiganaji wake walioko mstari wa mbele mwisho wa siku watajikuta wakibaki makamanda wachache wasiokuwa na vikosi.

Mzee Nelson Mandela katika hotuba yake ya kwanza baada ya kutoka Gerezani Februari mwaka 1990 aliwaasa watu wa Afrika Kusini kwamba ‘To relax our efforts now would be a mistake which generations to come will not be able to forgive.’

Kwa tafsiri yangu ni kwamba ikiwa tutabweteka juhudi zetu za sasa itakuwa ni makosa makubwa ambayo kizazi kijacho hakitaweza kutusamehe. Naam ikiwa nasi tutabweteka kuendelea kushikilia ukale kwa mfumo dhaifu wa Muungano, kizazi cha baadae hakitaweza kutusamehe kwa kushindwa kuweka mfumo madhubuti na wenye tija baina ya Tanganyika na Zanzibar.

Wananchi wanatamani kuwa na mfumo wa muundo wa Muungano usiosheheni kero, wanatamani Muungano kama wan chi za Ulaya, Uswis, Ubelgiji, wa Afrika Magharibi, UAE kama ambavyo Wachina baada ya kuishi katika mfumo wa Kijamaa wa kina Lenni na Karl Max na Mwenyekiti Mao.

Akitoa hotuba kwa wananchi Januari 31, aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa alisema;
“Zamani nilikuwa nafarijika nikisikia kuwa Tanzania inaitwa Bongoland? Nilidhani kuwa ilimaanisha Watanzania wameamua kutumia bongo zao kwa mambo ya ubunifu wa mikakati ya maendeleo na ujasiriamali…”

“Leo nilichodhani faraja kimegeuka karaha. Maana bongo inayozungumzwa si ya kutafuta maendeleo, au kupanua ujasiriamali, bali ni ujanja-ujanja, ubazazi, udanganyifu, ulaghai, na kutafuta mali bila kazi.

Na ugonjwa huu umezidi sana mijini ambapo ukimwamini mtu, kisha akakuingiza hasara, unaambiwa eti ?utajiju!?, au utalijua Jiji ? Ni kama vile badala ya kuionea haya hali hii ya mmomonyoko wa uaminifu, tunaitukuza”

Maneno hayo ni sawa na ya mwanafalsafa maarufu wa enzi hizo China Confucius mojawapo ya mafundisho yake kwa mwanafunzi wake, Tzu Kung, alimfunza juu ya uhusiano kati ya utajiri na umasikini.

Mwanafalsafa huyo alimwambia “ukimwona mtu tajiri , basi tamani kuwa kama yeye, lakini, ukimwona aliye masikini, basi, jitafakari wewe mwenyewe. Wazanzibari kwa miaka 48 wamejitafakari na hali ya uchumi wao ulivyo kule walikotoka mwaka 1964, walipo sasa na wanakotaka kwenda, wanadhani kuwa wakati umefika wa kutamani kuwa na uchumi bora na madhubuti kama wa EU au UAE.

Kwa kufikia uchumi imara lazima kufanya mabadiliko katika muundo wa Muungano kwa kuiwezesha Zanzibar kuwa na kiti chake katika Umoja wa Mataifa, kumiliki sera za kiuchumi mikononi mwake, kuweza kuingia mikataba ya kimataifa na msshirika na nchi mbalimbali ikiwemo OIC,FIFA, IMF, WB, FAO, UNFPA, WFP na mengineyo.

Lazima tuwaige Wachina ambao kwa miongo mingi waliaminishwa kwamba Ujamaa wa kale ndio nguzo ya uchumi wao wakivaa suruali nyeusi na shati jeupe wakidhani hakuna rangi bora na yenye maana zaidi ya hiyo, lakini baada ya kung’amua kwamba unaweza kuendelea kuwa Mjamaa,lakini ukafanya mabadiliko ya ujamaa wa kileo katika uchumi kwa kuiga mbinu

Jamhuri ya Watu wa China ilianza kuchukua mwelekeo mpya wa sera zake katika uchumi baada ya kufanya mageuzi ambayo kwa dhamira ya kuutumia upepari katika kuboresha ujamaa sahihi wa siasa na hilo inadhihirishwa na hali ya uchumi wa China ambayo sasa ni tishio kiuchumi kwa Mataifa mengine yenye uchumi mkubwa duniani kama Marekani.

Mabadiliko makubwa ya China baada ya kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, na upeo wa macho ya wageni ni tofauti na ule wa Wachina walivaa nguo sare, bidhaa katika maduka hazikuwa nyingi, na vifaa katika hoteli nzuri kabisa havikuwa vya kisasa.

Uchina ya leo sio ile ya Mwenyekiti Mao Zedong na Zhou Enlai kama angefufuka leo basi angeona mabadiliko makubwa sio yeye bali makomredi wote wa Chama cha Kikomunisti namna China ilivyobadilika,kiuchumi, kijamii, leo kuna Casino, Disko teki sio lile la Kijamaa tena, Wachina wametapakaa kila pemba ye Dunia wakifanya biashara huku na kule.

Kwanini tunashindwa kuiga wenzetu ambao siasa yao ni ya Ujamaa kama ya Tanzania? waliamua kubadilika kutoka katika mfumo dhaifu wa ujamaa wa kale na kuingia mfumo mpya wa ujamaa wa kileo chini ya soko huria ambao umewasaidia kuhimili vishindo vya kasi ya maendeleo ya dunia.

Mfumo wa muundo wa Muungano wetu sio siri tena kwamba umeshindwa kufikia matarajio ya nchi mbili hizo zilizoungana mwaka 1964 ukiacha lile la kisiasa, Umoja na mshikamano, lakini katika uchumi hakuna tulilofanikiwa maana Zanzibar ikiwa mbia katika Muungano uchumi wake unasuasua huku umaskini wa kipato ukiwa hauna jawabu.

Miaka 48 ya Muungano bado adui mkubwa wa nchi hili ni ujinga, maradhi, umasikini, ukosefu wa ajira, ugumu wa kupata matibabu, kusomesha watoto, chakula cha kila siku na mengine kadhaa je Serikali ya Jamhuri ya Muungano imesaidia vipi kuondoa matatizo hayo kwa Wazanzibari?

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine inaweka mkazo katika kushughulikia ustawi wa wananchi wa Taifa hili, kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 8 (1)(b) ya Katiba hiyo kuwa “Lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi.”

Tujiulize tumeadhimisha miaka 48 ya Muungano chini ya mfumo wa muundo wa kikatiba lengo hilo limefikiwa la kustawisha hali za wananchi hususan kwa upande wa Zanzibar ambaye ni mshirika sawa wa Muungano?

Je ni kweli kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachukuwa juhudi gani katika kutimiza wajibu huo wa kikatiba? Kero za Muungano bado kilio kikuu cha Wazanzibari wakilalamikia kutozwa kodi mara mbili bidhaa zao zinapoingia Tanzania Bara, kutopata mgao wa mafuta na gesi asilia ingawa jambo hilo ni la Muungano, ajira za watumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kodi zitokanazo na watumishi wa SMT wanaofanya kazi Zanzibar na mengineyo.

Kwa sehemu kubwa kero hizo na nyenginezo chanzo chake ni muundo mbovu wa Muungano ambao hata Wabunge 55 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Chama cha Mapinduzi wakiwa katika mfumo wa Chama kimoja walikusudia kubadili muundo wake kupendekeza Serikali tatu ambazo kwa sasa sio suluhu ya kero za Muungano.

Advertisements

3 responses to “Maruhani wa Kale katika zama mpya

  1. Muungano wa mkataba ndio suluhisho bila hivo tutabaki tunalaumu serekali lkn haina uwezo wa kiuchumi tumuondoweni huyu jini wa muungano tupate tupumue.

  2. Shukrani mwandishi kwa makala mazuri ,kwenye wakati mzuri iliyojaa hekima na mifano bora kwa wenye kutaka kuifata. Zanzibar yetu kwa sisi watu wa kale ni kishada kilo kwenda arijojo tumo mbioni kuifukuza ili tuikamate wakati matumaini yetu Uzi ukwame AMA bat ini yaani juu ya paa au kwenye mti, na arijojo hii ni ya muungano na kukwama kwake ni AMA wa katana au ujirani mwema ni mustahil kubaki tulipo.
    Kwa vijana na suala la sultani ni kuwapa habari ya sultani wa Oman au Brunei , sasa ,ukiwaambia, Hawo wasotaka muungano wanataka kuturejesha kwenye usultani nadhariya Yao wanasema bora kwani nchi zinazoendeshwa na masultani zimeendelea na kuna uadilifu na maisha bora.
    Tuwache zama zitawale zenu zimekwisha zetu zimepita zao ndio hizi.

  3. Tatizo linalotukabili watanzania ni dhana potofu. Wako baadhi ya viongozi wakuu wa serikali zetu na chama tawala wanabakia na mawazo yale yale kwamba ni wao tu wanaoweza kuokoa jahazi kwa kuidhibiti nchi hii isizame. Waasisi wa jahazi hili ni Mwalimu na Karume. Mwalimu aliweza kuidhibiti hali kwa sababu aliweza kufanya mabadiliko mengi na mengine alifikia hadi kuachia ngazi ili mabadiliko yachukue nafasi yake. Mwalimu alipendelea kuwa na chama kimoja cha siasa na alikuwa akipigiwa kura ya ndio na hapana. Alipoona muda wake umepita akaamua kurejesha vyama vingi. Alipoona Ujamaa hauna nafasi tena aliamua kuachia ngazi na kumpa Ali Hassan Mwinyi na kuanza kuregeza kampa ya Ujamaa. Kila hatua alioipiga ilichukua muda kuwachosha wananchi. Bada ya kifo chake kila mmoja alijaribu kufuata nyayo zake lakini hakuna alieweza. Liliopo sasa hivi kila anaetawala anataka aidhibiti nchi na ibakie kwenye hali ile ile ya awali uhai wa Mwalimu. Sijui wenzetu hawa hawafahamu kuwa dunia pamoja na viomo duniani vimebadilika. Ikiwa ni wabunifu wakati ndio huu wa kubuni njia za kuwafanya wananchi wakubali wanavyotaka wao sio kuwatumilia nguvu. Kuwapiga na kuwanyima uhuru sio suluhisho. Waliowengi hawataki Muungano huu na sababu zao ni nzito. ” kuna watu watasema nimejuaje” Nimejuwa kwa sababu ya maoni yanayotolewa na wananchi na pia kutokuepo uhuru wa kwa baadhi ya watu kutoa maoni maoni yao ni sababu tosha kuwa fursa ya kutoa maoni haiko huru. Vipi Nnauye atumie wadhifa wake kutishia baadhi ya kunyanganywa kadi na chama kimeshindwa kutoa kauli. Jee alilonalo Nnauye si GAMBA ?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s