Polisi wanapochafua amani watu walindwe na nani?

Ahmed Rajab

Vijana wakikamatwa na kuingizwa katika gari la polisi wa FFU siku ilipotokea vurumai katika katika msikiti wa Mbuyuni Mjini Zanzibar ambapo kuliandaliwa sala na dua maalumu ya kuwaombea waliofikwa na maafa ya Mv. Skagit

KUNA simulizi mbili zenye kukinzana kuhusu vurugu zilizozuka Zanzibar Ijumaa iliyopita ya Julai 20. Siku hiyo kuanzia saa za alasiri hadi kupindukia saa sita za usiku eneo kubwa la mjini Unguja lilikuwa kama eneo la msitu uliowaka moto. Ghasia zilienea takriban mji mzima kuanzia Mbuyuni, Darajani, Michenzani, Kwa Bi Ziredi, Daraja Bovu, Mombasa, Mpendae, Amani na sehemu nyingine.
Waliokuwa wakisema kwamba Zanzibar ikiwaka moto hawakukosea. Matairi yalichomwa moto barabarani na watu waliokuwa wamepigwa mabomu ya kutoa machozi na kurushiwa maji ya kuwafanya wawashwe na kikosi cha askari wa kuzuia fujo. Waathirika hao wakaweka matofali na mawe barabarani wakizifanya barabara zisipitike.
Simulizi rasmi ya serikali ni kwamba viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) ndio walichochea vurumai hizo.
Viongozi wa Uamsho nao, kwa upande wao, wanasema kwamba walichokuwa wakifanya ni kuwaombea dua maiti na waathirika wengine wa ajali ya meli ya MV Skagit iliyozama Jumatano iliyopita. Wakati wakisoma dua zao katika Msikiti wa Mbuyuni askari wa kuzuia fujo wakaingia katika eneo la msikiti na kuanza kupiga mabomu ya kutoa machozi na ya maji ya kuwasha. Jumiki, au kwa ufupi Uamsho, ni jumuiya na si madhehebu (sect) kama gazeti moja la Kiingereza nchini lilivyoeleza.
Tukiyaangazia matukio hayo ya Ijumaa iliyopita kuna jambo moja la uhakika lisilo na ubishi. Nalo ni kwamba askari walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwashambulia watu waliokuwa wakiomba dua. Kwa ufupi, walifanya pupa kuwashambulia watu wasio na hatia na waliokuwa hawana silaha. Kwa kufanya hivyo polisi siku hiyo waliichafua hali ya amani ya Mjini Unguja.
Hii ni mara ya pili polisi kuichafua hali hiyo katika siku za hivi karibuni. Itakumbukwa kwamba fujo kama hizo zilizuka Mei 26 mwaka huu.
Siku hiyo ya Ijumaa hali ilianza kuwa mbaya kutokana na vitendo hivyo vya askari wa kuzuia fujo waliopelekwa mahali pasipokuwa na fujo na hivyo kuanzisha fujo. Walioshambuliwa hawakuwa waliokusanyika kwenye uwanja wa Msikiti wa Mbuyuni peke yao bali ilikuwa ni kisa cha ‘mpata mpatae.’ Mabomu ya kutoa machozi hayakuchagua nani na nani wa kushambuliwa.
Kwa hakika, inavyoonyesha ni kwamba ni wanaharakati wachache wa Uamsho walioathirika. Wengi waliofikwa na balaa hilo walikuwa ni wakazi wa kawaida wa Mjini Unguja waliokuwa katika maeneo ambamo amani ilichafuliwa na hao askari maalumu wa polisi.
Zanzibar inasifika kwa amani na usalama wake. Katika kanda ya Afrika ya Mashariki ni moja ya nchi chache zilizotulia kabisa ukiilinganisha hali yake na hali zilizoko katika nchi za Maziwa Makuu au Somalia, kwa mfano. Hali hiyo ya amani na usalama ya Zanzibar ndiyo inayowavutia watalii wengi kutoka nje kuja kuitembelea na wanapoondoka wanaondoka na kumbukumbu njema za Visiwa hivyo na watu wake.
Ijumaa iliyopita kikosi maalumu cha kuzuia fujo cha askari polisi wa Zanzibar hakikujuzu kuchukua hatua kilichoichukuwa. Mashambulizi hayo ya polisi yanaweza kumfanya asiyeielewa hali ya mambo ilivyo aamini kwamba kuna hali ya mapambano Visiwani humo baina ya vyombo vya usalama na wananchi wa kawaida.
Mtu aliyeingia Unguja siku hiyo angeweza kuamini kwamba mjini humo mna magenge ya wahuni watukutu yaliyofurutu ada yanayopambana na serikali kwa kuvunja sheria na amani na yasiyoweza kudhibitiwa ila kwa nguvu za kikosi maalumu cha askari wa kuzuia fujo.
Watafikiri nini watalii wa kigeni wanaozuru Zanzibar wakiyahusudu mandhari yake na wakiifurahia amani na utulivu wake na hali ya kutokuwapo vitendo vya jinai vya kutumia nguvu kama ilivyo sehemu nyingine za Afrika ya Mashariki?
Ni muhimu tujikumbushe kwamba vurugu kama hizo zinazosababishwa na hatua za mabavu za polisi huwa na matokeo mabaya kwa uchumi wa nchi, hasa kwa utalii wenye kutegemewa na serikali. Kwa bahati mbaya, uchumi wa Zanzibar unategemea kwa kiwango kikubwa sana mapato yanayotokana na utalii. Inaaminika kwamba sekta ya utalii ndiyo mwajiri mkuu wa wakazi wa Zanzibar mbali na serikali.
Jingine lililozidi kuleta sura mbaya na kuifanya idara ya polisi ilaaniwe kwa mashambulizi yake ni kwamba kadhia hiyo ya Ijumaa ilitokea mkesha wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Watu waishio kwenye sehemu zilizohusika walibidi wabakie majumbani mwao na shughuli zao za matayarisho ya mfungo wa Ramadhani ziliathirika kidogo. Wengine walilazimika kuzifunga na mapema biashara zao.
Kwa bahati mbaya tangu mwaka 1964 vyombo vya usalama vya Zanzibar vikiwa pamoja na polisi vimetiwa mwako wa kisiasa. Kama tu wa kweli basi tunapaswa tuvilaani vyombo vyetu vya usalama kwa namna vilivyokuwa vikifanya kazi zao tangu mwaka 1964 hadi 1972 hasa kwa kuwatesa na kuwaua washukiwa mbalimbali wa kisiasa.
Kwa sababu za kisiasa vyombo hivyo vya usalama kadhalika vilitumika kuzikandamiza haki za binadamu kama vile za wananchi kuwa na uhuru wa kusema, uhuru wa kutoa maoni yao, uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kuwa na rai au maoni yenye kupingana na maoni rasmi ya serikali au ya chama kinachotawala.
Hata baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, polisi na vyombo vingine vya usalama vimekuwa vikiwaona wapinzani wa kisiasa huko Zanzibar kuwa ni ‘maadui wa dola.’ Mara kwa mara kumetokea visa vya wafuasi wa vuguvugu la upinzani kudhuriwa na vyombo vya usalama au kukamatwa na kuna walioshtakiwa kwa mashtaka ya ‘uhaini.’
Katika jamii zenye kuendesha shughuli za utawala kwa njia za kistaarabu kazi ya polisi huwa ni kupambana na uhalifu na kulinda maisha ya watu na mali zao. Huku kwetu kwa muda wa miaka 48 iliyopita polisi imejitwika dhima nyingine. Imezoea kuwa na pupa ya kuilinda Serikali kwa kuwatwanga risasi wananchi au kwa ‘kuwashikisha adabu’ kwa kuwashambulia kwa silaha nyingine kama mabomu ya kutoa machozi na marungu.
Hapa tulipofika katika maendeleo ya kijamii na ya kisiasa tuna haja ya kuyachunguza upya mahitajio ya ulinzi ya Zanzibar. Na tunapoyachunguza upya mahitajio hayo itatupasa tuutie maanani ukweli wa kwamba Zanzibar ya leo ni nchi isiyokabiliwa na kitisho chochote cha maadui wala machafuko kutoka nje. Bila ya shaka uchunguzi huo unaweza ukaangalia na kupima nani hao wanaoweza kuwa maadui wake wa nje na nguvu zao zikoje.
Uchunguzi huo pia utapaswa uangalie uwezekano wa kuzuka machafuko ya ndani ya nchi kwa kuzingatia hali yake ya usalama ilivyo. Ukifanywa uchunguzi wa kina nina hakika kwamba itaonekana ya kuwa Zanzibar haistahili kuwa nchi yenye silaha nyingi na zilizo nzito nzito; sana sana itahitaji silaha kidogo, tena nyepesi kupambana na vitendo vya uhalifu wa jinai wa kutumia nguvu, vitendo ambavyo hadi sasa ni duni Zanzibar vikilinganishwa na vile vya nchi za jirani.
Kwa mintaraf ya haya, pengine inatupasa tujifunze kutokana na historia ya shughuli za kipolisi za enzi ya ukoloni. Kwa mfano, mwaka 1963 katika mkesha wa Uhuru kutoka Uingereza Zanzibar haikuwa na jeshi. Ilikuwa na kikosi kidogo tu cha polisi kilichokuwa kama pambo kwa sababu kazi yake haikuwa kupambana na waasi au wapinzani wa kuzua bali kupambana na uhalifu na kuhakikisha kwamba Zanzibar inaendelea kuwa nchi ya amani isiyo na uhalifu — hali iliyokuwa nayo miaka na dahari.
Pale askari wa kuzuia fujo walipoanza kuchanganyikiwa na kusababisha mashambulizi ya kuhuzunisha Ijumaa iliyopita wananchi waliuona utumizi huo wa nguvu kuwa ni ushahidi mwingine wa polisi kuyatumia vibaya madaraka yao. Mbali na hayo walihisi pia kwamba polisi walikuwa wanaziingilia haki za wananchi za kukusanyika kwa amani na kuutumia uhuru wao wa kukusanyika na wa kufanya ibada.
Uhuru wote huo umo katika Katiba ya Zanzibar ( na kwenye Katiba ya Muungano), hasa katika vile vifungu vya Katiba vyenye kuhusika na haki za kimsingi za binadamu. Jamii yoyote yenye kufuata mfumo wa kidemokrasia huhakikisha kwamba mahali pa kufanyia ibada, kwa mfano misikiti, makanisa na mahekalu ni mahali panapowapa wananchi hifadhi na ni haki yao wananchi kukimbilia humo.
Siku ya Ijumaa ya Julai 20 wananchi walikuwa na kila haki ya kuomba dua kwenye Msikitini wa Mbuyuni na nje ya msikiti huo. Jeshi la polisi, kwa upande wake, halikuwa na haki ya kucharuka kwa kuwavurumishia mabomu ya kuwatoa machozi au kuwarushia maji ya kuwawasha.
Katika nchi nyingi jeshi la polisi huendeshwa na kudhibitiwa na serikali za mitaa. Jukumu la jeshi aina hiyo ni kuyalinda na kuyahifadhi maisha ya wananchi na wala si kuyahatarisha. Kazi yao kubwa ni kuwahudumia wananchi na si kuwachafulia hali yao ya amani na ya utulivu.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

7 responses to “Polisi wanapochafua amani watu walindwe na nani?

 1. asante kwa makala yako ambayo ina ukweli mara hii, lakini ndugu yangu hemedi rajabu makala zako nyengine za nyuma zilionyesha ulivyokuwa na watawala ktk kujipendekeza, lakini tutazidi kukumulika tuone kama ni mkweli umetubu au unajaribu kuwachukua watu kijanja kwa makala zako, na kama umeamua kuwa mwandishi wa kuandika habari za ukweli fungu lako utaliona kwa mola utapokutana nae

 2. Asante ndugu yetu Kwa makala yako ila mie ninachouliza Mbona serikali imekaa kimya haikutoa tamko lolote kuhusu hizi vurugu?kwahiyo jambo linifanywa na wao wanakaa kimya wakifanya vijana wa uamsho inatangazwa mie namini kabisa huu ni udikteta ndani ya serikali ta Tanganyika na Zanzibar ambao unaofanywa hii ni dhulma na inshallah na ramdhan hii tukufu Allah atatulipia c mda mrefu amin

 3. Asante kwa makala yako nzuri yenye ukweli mtupu. Mwenyenzi Mungu atakujaalia malipo mema. Amin. Nashukuru sana kuliona hili na ukalieka bayana serikali yetu imezowea kufanya vurugu kama hizi kwa kutumia vyombo vya dola ili wapate kisingizio cha kuwakamata na kuwatia ndani watu wanaodai haki yao serikalini. Sisi raia tunalijuwa fika lakini Mungu atawabainisha na ataudhihirisha ubaya wao kwa ulimwengu mzima. Sisi tunategemea Nguvu za Mungu tu. HATA MUKAPIGA MIZINGA MUUNGANO HUU HATUUTAKIII.

 4. Polisi waenda kinyume na nembo Yao iliyoandikwa Usalama wa raiya-
  Polisi hao hao kukifanyika mkusanyiko bara hawathubutu kucharukwa suala linakuja nani anatowa amri hizi za kuchafuwa Amani?
  Je viongozi wetu hayakuwahusu haya au wao mazizini moshi wa mabomu haufiki?
  Hawezi kutoka hata mmoja kwenda kujuwa kumejiri nini nje mbona khasiya ?
  AMA kweli pili pili uso ila hujui iwashavyo.

 5. Mi naamin wengi wa polisi wanaotenda hayo sio waislam wametumwa na wenzao waliovunjiwa makanisa kuendeleza hujuma za waislam wa zanzibar na kwa jicho la upembuz wanaonekana kukerwa na mshikamano wa waislamu wa zanzibar.

 6. Iko siku kwa allah tutakutana halafu tutajua kama kweli wao nguvu na wana mabomu ya machozi,
  Kama wao ni askari kweli tutawaona siku hiyo watakaposimamishwa kusubiri na watawakuta askari wa kweli wakilinda lango la motoni ,
  Jee na hapo watakua na mabuti na mabomu ya kuwapiga maika wa allah ?

 7. Assalaam Alaaykum, Ramadhani Kariim
  Wazanzibari lazima tukubali hakika kwamba sisi si Waumini, hatuna sifa hata moja ya Uumini, bali hata sifa ya Uislamu hatuna. Hivyobasi, watu hutawaliwa na watu wa mfano wao; watawala wetu ni sawa na sisi watawaliwa, hawana sifa hata moja ya Uumini, bali hata sifa ya Uislamu. Haya nnayo yasema, nnayasema kwa ushahidi, Ikiwa yuko mwenye hoja dhidi ya haya nnayo yasema, nnaomba aeleze. Dini yetu inatwambia, mukiwa nyinyi waovu, Mwenyezi Mungu atakuleteeni alie muovu kuliko nyinyi akufanyieni uovu.

  Ikiwa itajengwa hoja kwamba wazee wetu waliotangulia walitenda maovu, hoja hii haijuzishi maovu ya tangu 1964 mpaka hii leo. Uovu hausahihishwi na uovu. Waliokuja madarakani tangu 1964 ilikuwa wawe mfano wa kuleta mema kwa hoja kwamba wamekuja kuondowa watenda maovu. Hapana shaka kwa kila hali waliokuja madarakani 1964 hawakuwa na sifa wala uwezo wa kutenda mema, kwa sababu msingi wa kuja kwao madarakani ni uwovu.

  Wazanzibari, wanasiasa; khasa pale baada ya kuletwa vyama vingi, 1992; badala ya kuondowa maovu, bali japo kwa uchache kuamini kwamba yaliofanywa na utawala tangu 1964 ni uwovu, hawakuwa hivyo, bali mara nyingi kufika kuona maovu ya 1964 yanao uhalali. Kuendelea na hali hii, hali ya kutokuwepo ukanyaji wa uwovu, watawala wa 1964 – Zanzibar na Tanganyika – wameendelea kuwatendea Wazanzibari kila uwovu, si kwa sababu yoyote ya msingi, lakinibasi kwa imani ya Dini yao, Uislamu. Kosa lao kubwa Wazanzibari mbele ya watawala ni kuwa ni Waislamu.

  Hali ya kuingiliwa Waislamu, kupigwa na hata kuuliwa misikitini si hali ya ajabu. Mara tu watawala wa 1964 katika kuendeleza mauwaji yao ya kiholela waliwaingilia Waumini msikitini – Kiponda na kuuwa, miongoni wa waliouliwa ni mtoto. Watawala na wapenzi wa watawala hao hawakuuona uwovu huo. Jambo lenye kusikitisha miongoni mwa waliofumbia macho na masikio uwovu ule ni wale wenyekuitwa mashehe wa dini. Kwahivyobasi, kama ilivyo ada من شاب علي شيئ شبّ عليه yaani, “mwenye kukulia kitu hukonga nacho”. Pia “mwenye kuonja asali, haonji mara moja”. Vizazi vya leo vinateseka na maovu haya kutokana na uwovu wa wanasiasa ambao wameona wasiilimishe kuondowa uwovu, kwa sababu wao wenyewe wanasiasa hawana UUMINI wala UISLAMU. Mwenyezi Mungu habadilishi yaliomo baina ya watu mpaka wao wabadilishe yaliomo katika nafsi zo.

  “……. إن الله لا يغير ما بقوم حتّى يغيروا ما بأنفسهم……..” (الرعد:11)
  “…….. Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf-sini mwao. ……………”. (Ar-raa’d : 11).

  Wa Bilahi Tawfiiq

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s