Taarifa ya serikali ya kuzama kwa Mv. Skagit

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari hawapo pichani kuhusiana na Kuzama kwa Meli ya Skagit na hatua Zilizochukuliwa na Serikali huko katika Ukumbi wa Baraza la wawakilishi la Zamani Kikwajuni Zanzibar

Mara baada ya tukio hili, Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Taifa ilikutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya hatua za kuchukua pamoja na kuandaa taarifa rasmi ya Serikali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. Aidha, Baraza la Mapinduzi lilikaa usiku wa tarehe 18.07.2012, na kutoa maagizo juu ya hatua za kuchukua ikiwemo kuwepo kwa matayarisho katika hospitali ya mnazi Mmoja ya kupokea majeruhi, kutayarisha eneo la Maisara kwa ajili ya mapokezi na utambuzi wa maiti; kutayarisha eneo la kuzika miili ya marehemu huko Kama; kuweka takwimu sahihi za majeruhi na waliofariki katika ajali hiyo; pamoja na kutolewa kwa taarifa rasmi ya hali ya uokozi iliyokuwa inaendelea

KAULI YA SERIKALI KUHUSU TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA MV. SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18.07.2012 KATIKA ENEO LA BAHARI YA CHUMBE
=======================================

Mheshimiwa Spika;
Kwa heshima naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa leo tukiwa wazima na wenye afya njema. Pili, naomba nichukue nafasi hii adhimu kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kutupatia fursa hii adhimu ili kuwasilisha mbele ya Baraza lako Tukufu taarifa ya maafa ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit iliyotokea katika bahari ya Chumbe tarehe 18.07.2012.

1.0 Utangulizi

Mheshimiwa Spika,
Meli ya MV. Skagit ilitengenezwa nchini Marekani mwaka 1989 na imesajiliwa Zanzibar tarehe 25/10/2011, na kupewa nambari ya usajili 100144. Meli hiyo ina uzito wa GRT96 ambayo inamilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Limited ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Mnamo tarehe 18.07.2012 majira ya saa saba na nusu za mchana ilipatikana taarifa ya ajali ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit katika bahari ya chumbe nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Meli hiyo ilikuwa katika safari zake za kawaida ya kutoka Dar-es-Salaam kuja Zanzibar.

Kwa mujibu wa manifest ya abiria iliyowasilishwa na wamiliki wa meli kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority-TPA) na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na Nchi Kavu Tanzania (Surface and Marine Transport Authority-SUMATRA), meli hiyo ilikuwa imechukua jumla ya watu 290 wakiwemo abiria watu wazima 250, watoto 31 na mabaharia 9.

Mheshimiwa Spika
Taarifa hii inaelezea kwa kina juu ya hali halisi ya tukio pamoja na hatua zote zilizochukuliwa kuanzia tarehe 18/07/2012 hadi hivi sasa.

Mheshimiwa Spika
Mara baada ya tukio hili, Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Taifa ilikutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya hatua za kuchukua pamoja na kuandaa taarifa rasmi ya Serikali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. Aidha, Baraza la Mapinduzi lilikaa usiku wa tarehe 18.07.2012, na kutoa maagizo juu ya hatua za kuchukua ikiwemo kuwepo kwa matayarisho katika hospitali ya mnazi Mmoja ya kupokea majeruhi, kutayarisha eneo la Maisara kwa ajili ya mapokezi na utambuzi wa maiti; kutayarisha eneo la kuzika miili ya marehemu huko Kama; kuweka takwimu sahihi za majeruhi na waliofariki katika ajali hiyo; pamoja na kutolewa kwa taarifa rasmi ya hali ya uokozi iliyokuwa inaendelea.

2.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Mheshimiwa Spika
Kufuatia maagizo hayo ya Serikali, hatua zifuatazo zilichukuliwa: –

Vituo cha mapokezi ya wahanga wa ajali hiyo vilifunguliwa katika maeneo ya Bandari ya Malindi, Hospitali ya Mnazi Mmoja na uwanja wa Maisara.
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vilipelekwa katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha huduma za ulinzi na uokozi wa haraka.
Kazi ya uchimbaji wa makaburi katika eneo la Kama ilifanyika kwa mashirikiano makubwa ya viongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi. Jumla ya makaburi 80 yalichimbwa.
Sala na dua maalum ya kuwaombea marehemu wote ilifanyika baada ya sala ya Adhuhuri jana tarehe 22.07.2012 katika misikiti yote ya Unguja na Pemba na Kitaifa ilifanyika katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Zanzibar.
Kuorodhesha majina ya wale wote ambao wanasadikiwa walikuwemo ndani ya chombo kilichopata ajali na hadi sasa hawajulikani walipo. Taarifa hizi zinakusanywa kupitia ngazi ya Shehia na Wilaya kwa Unguja na Pemba na kwa Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa Tanzania Bara.
Kutoa huduma ya kuwasafirisha majeruhi baada ya kupata matibabu kurudi makwao.
Kutoa huduma za usafiri kwa walioshiriki katika shughuli zote za operesheni.

3.0 MATOKEO YA OPERESHENI

3.1 Shughuli za uokozi

Mheshimiwa Spika;
Kutokana na operesheni iliyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa mashirikiano makubwa ya wananchi yamepelekea hadi kufika tarehe 22.07.2012 kuwa na idadi ya watu waliookolewa wakiwa hai kufikia 146 na miili ya waliofariki dunia iliyopatikana kufikia 73. Kati ya maiti hizo 68 zilipokelewa kituo cha Maisara na 5 zilipelekwa moja kwa katika eneo la makaburi la Kama kwa vile maiti hizo zilikuwa zimeshaharibika.

Kwa waliookolewa wakiwa hai waliweza kufikishwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa uchunguzi na matibabu. Hadi hii leo, majeruhi wote walishatibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani mwao.

Mheshimiwa Spika;
Katika kituo cha Maisara maiti zilipangwa ili kuwawezesha ndugu na jamaa kutambua maiti zao na kwa kurahisisha kazi hiyo, Shirika la Utangazaji kupitia kituo chake cha Televisheni kilichukua picha za sura za marehemu na kuzionyesha zikiwa tayari zimewekewa namba ili kurahisisha utambuzi na uchukuaji wa maiti hizo. Kupitia utaratibu huu, jumla ya maiti 50 zilitambuliwa na kukabidhiwa jamaa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi. Idadi ya maiti ambao hawakutambuliwa ni 23 na mazishi yao yalisimamiwa na Serikali katika eneo la Kama. Aidha, maiti mmoja aliyetambuliwa alilazimika kuzikwa Kama kwa vile mwili wake ulikuwa umeharibika sana sambamba na ndugu wa marehemu huyo kutochukuliwa na jamaa na ndugu zake. Kila maiti alizikwa katika kaburi lake chini ya usimamizi wa mashekhe kutoka Ofisi ya Mufti na Wakfu na Mali ya Amana.

Aidha, katika kituo cha Maisara huduma za uoshaji na sala ya maiti zilitolewa na pia wale wote waliochukua maiti wao walipatiwa usafiri, sanda na ubao kwa ajili ya kuzikia.

3.2 Juhudi za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana

Mheshimiwa Spika,
Katika jitihada za Serikali za kuhakikisha miili zaidi ya marehemu iliyotokana na ajali ya meli inapatikana, Serikali ilivitaka vikosi vyake ulinzi na usalama vikiongozwa na KMKM kuendesha zoezi la kuitafuta meli na miili iliyosalia. Kazi ya kuendesha operesheni ya kuitafuta meli pamoja na abiria ilianza mara tu baada ya kusikia kutokea kwa ajali hiyo. Jumla ya watu waliohai 146 waliokolewa siku hiyo na maiti 31 zilipatikana.

Asubuhi ya tarehe 19.07.2012, wazamiaji kutoka KMKM, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na makampuni binafsi walifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuanza kazi rasmi. Wazamiaji hao walifanikiwa kupata maiti 37 na hawakupata abiria aliye hai. Hata hivyo, wazamiaji hao hawakuweza kuiona meli.

Mheshimiwa Spika
Vikosi hivyo viliendelea na jitihada za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana kwa kujigawa katika makundi matatu. Makundi mawili yalihusika na kazi ya utafutaji wa watu katika maeneo ya ukanda wa eneo la tukio. Kundi jengine lilijihusisha na kazi ya uzamiaji (diving) kwa ajili ya kuitafuta meli chini ya bahari.

3.3 Kukusanya taarifa za watu waliokuwa hawajaonekana kupitia Ofisi za Masheha na Wilaya:

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliziagiza ofisi zote za Wilaya na Shehia kuorodhesha majina ya watu waliokuwa hawajaoneka na waliofariki na kuziwasilisha orodha hizo kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ili kufanyiwa uhakiki na kupata orodha sahihi kwa ajili ya matumizi na kumbukumbu za baadae. Hadi kufikia tarehe 22.07.2012 zaidi ya watu 100 wameripotiwa hawakuonekana ama wakiwa hai au maiti. Hata hivyo, kwa uhakiki wa awali imebainika kwamba baadhi ya watu wameorodheshwa zaidi ya mara moja katika maeneo tofauti.

3.4 Viongozi Wakuu wa Kitaifa kutoa mkono wa pole

Mheshimiwa Spika
Viongozi Wakuu wa Kitaifa pamoja na viongozi wengine wanatarajiwa kufanya ziara za kutoa pole na kuzifariji familia zilizofiliwa na zilizopotelewa na ndugu zao kwa maeneo yote yalizoathirika Unguja na Pemba. Kazi hiyo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

3.5 Kuratibu upokeaji wa misaada

Mheshimiwa Spika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa iliendelea kupokea misaada ya kifedha na vifaa kutoka kwa watu binafsi, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika ya Umma, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Hadi kufikia tarehe 22.07.2012 jumla ya Shilingi 320,000,000/- zimepokelewa na kuingizwa katika akaunti ya Mfuko wa Maafa Zanzibar (Zanzibar Disaster Funds) ilioko Benki ya Watu wa Zanzibar, ambayo imefunguliwa maalum kwa ajili ya michango ya aina hiyo. Aidha, vifaa na bidhaa mbalimbali zimepokelewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za operesheni ya uokozi.

4.0 GHARAMA ZA OPERESHENI

Mheshimiwa Spika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliipatia Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa jumla ya shilingi milioni ishirini (20,000,000/-) kwa ajili ya kugharamia shughuli za operesheni ambapo hadi kufikia tarehe 22.07.2012 fedha zote zilikwisha tumika.

5.0 TULICHOJIFUNZA KUTOKANA NA TUKIO HILI (LESSONS LEARNED)

Mheshimiwa Spika
Kutokana na tukio hili la kuzama kwa meli ya MV. Skagit tumeweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo ni changamoto kwetu katika kuimarisha kazi na huduma za kukabiliana na maafa nchini. Miongoni mwa mambo hayo ni haya yafuatayo: –

Umakini na maamuzi sahihi na ya haraka yaliyochukuliwa na viongozi wetu yameweza kuleta ufanisi mkubwa katika operesheni ya uokozi na hivyo kupelekea kuokoa maisha ya wananchi wetu wengi.
Muitikio wa haraka wa taasisi mbalimbali za kukabiliana na maafa, zikiwemo taasisi za Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, Sekta Binafsi na Jumuiya za Kiraia umepelekea watu wengi kuweza kuokolewa wakiwa hai pamoja na kupatikana kwa maiti hali ambayo imewezesha maiti wengi kuzikwa na familia zao.
Kutokana na wananchi wengi kutumia mtandao wa mawasiliano wa Zantel, kulisababisha ugumu wa mawasiliano kutokana na minara ya kampuni hiyo kuzidiwa na matumizi.
Udogo wa sehemu ya kuhifadhia maiti (motuary) ulipelekea maiti wasiotambuliwa na jamaa zao kuzikwa haraka na Serikali.
Uhaba wa vifaa vya kisasa vya uokozi pamoja na wataalamu wa uzamiaji (divers) umepelekea zoezi la uokozi kuwa gumu na kuchukua muda.
Kukosekana kwa taarifa za uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na maafa ikiwemo uwezo wa vifaa na wataalamu ni changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi.

6.0 SHUKRANI

Mheshimiwa Spika
Kwa mara nyengine tena kwa niaba ya Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa naomba nimshukuru Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake kubwa alizochukua ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanaokolewa. Tunamshukuru kwa maelekezo yake na miongozo aliyotupatia ambayo kwa kiasi kikubwa ilitusaidia kufanikisha kazi za uokozi. Pia, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo yao na msaada mkubwa walioutoa katika kukabiliana na maafa hayo. Aidha, tunamshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda kwa msaada mkubwa aliotupatia kupitia Ofisi yake.

Tunawashukuru pia Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kutupatia miongozo ya mara kwa mara katika jitihada za kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza athari za maafa yaliyotokea.

Vile vile tunatoa shukrani za dhati kwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Usalama la Taifa kwa maelekezo yao juu ya hatua za kuchukuliwa katika kukabiliana na janga hili na majanga yanayoweza kutokea baadae. Shukrani za dhati pia zinatolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zao za haraka zilizosaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi. Pia tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa karibu nasi na kwa michango yao ya hali na mali katika kukabiliana na tukio hili la kusikitisha.

Mheshimiwa Spika
Shukrani pia zinatolewa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, angani na nchi kavu kwa jinsi walivyoshirikiana na Serikali katika kulikabili tukio hili. Wananchi wa maeneo ya jirani hasa wavuvi na wamiliki wa hoteli na kampuni za kitalii wanapewa shukrani za pekee kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu tokea hatua za awali baada ya kupatikana taarifa za kuzama kwa meli ya Skagit. Tunashukuru washirika wa maendeleo na wawakilishi wa nchi marafiki kwa jinsi walivyolichukulia suala hili na kutuunga mkono katika msiba huu wa kitaifa. Vilevile tunazishukuru taasisi za kidini hasa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na Ofisi ya Mufti kwa kusaidia maandalizi ya mazishi ya marehemu waliotokana na ajali hiyo.

Tunawashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa namna walivyoshirikiana na Kamati. Tunawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa na wafanyakazi wa Idara ya Kukabiliana na Maafa kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kipindi chote toka kutokea kwa janga hili. Tunawashukuru wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa kupokea tokeo hili kwa masikitiko makubwa katika kukabiliana na janga hili. Aidha, tunawashukuru wale wote walioweza kuchangia kwa hali na mali katika msiba huu.

7.0 HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo nawaomba wajumbe wa Baraza lako tukufu waipokee taarifa hii na kutupatia ushauri ili uweze kutusaidia katika harakati za kukabiliana na maafa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba kuwasilisha.

Ahsanteni sana

………………………………
MOHAMED ABOUD MOHAMED [MBM]
WAZIRI WA NCHI
OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS
ZANZIBAR

Lakini pamoja na Serikali kununua Meli hizo kwa kuwa mazingira ya nchi yetu ni ya visiwa sio kama watu wote wataweza kusafiri kwa siku moja na kupanda Meli hizo la Serikali kwa hiyo bado ni lazima kutakuwa ulazima wa kuwa na vyombo binafsi , ndio maana tukasema kuwa suala kubwa hapa na la ulazima ni kuhakikisha ukaguzi wa kina wa usalama wa vyombo hivyo kwani hata hizo Meli za Serikali pia nazo zitahitajika kukaguliwa kila wakati kwani sio kama hizo Meli za Serikali hazitaweza kupata ajali zikiwa nazo hazitakuwa na ubora.

TAARIFA YA KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA JUU YA TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18.07.2012 KATIKA ENEO LA KISIWA CHA CHUMBE NJE KIDOGO YA ZANZIBAR.

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana tena mbele ya Baraza lako tukufu tukiwa wazima wa afya ili kujadili mambo mbali mbali yanayohusu mstakbali mzima wa maendeleo ya nchi yetu. Aidha tuishukuru neema hii aliyotupa M/Mungu ya kuendelea kutupa neema ya pumzi zake ili kuweza kutekeleza majukumu yetu ambayo tulikula kiapo kwa kukamata Msahafu kuwatumikia wananchi wetu kwa ukweli, uwazi na uadilifu mkubwa na tunamuomba tene atuzidishie uzima na afya njema ili tuiokoe nchi yetu kutokana na janga la umasiskini na nnaamini kwa ukweli na uadilifu tunaoendelea nao hivi sasa basi naamini si muda mrefu nchi yetu itapiga hatua kubwa za maendeleo .

Mheshimiwa Spika, Aidha kwa niaba ya kamati nakushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama mbele ya Baraza lako tukufu ili niwasilishe taarifa ya kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa juu ya tukio hilo la maafa. Pia naomba nawashukuru wananchi wangu wa jimbo la K/pura walionileta hapa kuja kuwawakilisha na nnaomba waendelee kuniamini na nnawaahidi kuwatumikia na nitajitahidi kuhakikisha kuwa nitawatumikia kwa uadilifu mkubwa na nitaishauri Serikali yetu kila ambalo nitahisi linaweza kuisaidia Serikali yetu, na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya kamati, nachukua fursa hii kumuomba Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi wale wote waliofariki kutokana na ajali hiyo, na pia kuwataka kuwa na subra wale wote waliopoteza ndugu na jamaa zao. Pia na wale walionusurika katika ajali hiyo tunawatakia afya njema na inshallah Mwenyezi Mungu atawape afueni ili tuweze kujumuika nao na kuweza kuendelea na majukumu ya kujenga Taifa letu.

Mheshimiwa Spika,Sisi Wajumbe wako wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wewe mwenyewe binafsi tulipata mshituko mkubwa baada ya kupata tarifa ya kuzama kwa meli mchana wa siku ya jumatano ya tarehe 18.07.2012 kwa masikitiko makubwa iliyokua ikitoka Dar-es-Salaam kuja Zanzibar,kwani ilitukumbusha machungu tuliyoyapata takriban ni Mwaka ukizingatia ni karibu Mwaka mmoja tu uliyopita hapa nchini kwetu tuliweza kupata msiba mkubwa unaolingana na huu.

Mheshimiwa Spika,kamati yangu inasikitika sana kwa kuona kuwa visiwa vyetu vya Unguja na Pemba vimekumbwa na msukosuko mkubwa katika usafiri wa baharini ukiacha suala la kuzama kwa meli hii kwani kwa mtu yeyote aliyekuwa makini hakupigwa na mshangao kwa kutokea ajali hii kwani kulikuwa kuna kila dalili ya kutokea ajali baharini kwani kumekuwa na mfululizo wa matukio mbali mbali yakuashiria kutokea ajali baharini kwa baadhi ya meli kuzimika injini ovyo mara kwa mara huko Baharini zikiwa katika safari zake za kila siku zikiwa na abiria wengi ndani yake.

Mheshimiwa Spika,tukio la kuzama kwa meli limetupa funzo kubwa, kwani tatizo kubwa tulilokuwa nalo hapa ZNZ ni kutokuwa waaminifu na waadilifu kwa kusimamia majukumu tunayopewa au dhamana tunayopewa na wananchi wetu aidha kwa uzembe au tamaa binafsi inayopekea kutokuwajibika ipasavyo kwa umma, kwani kuna mamlaka iliyopewa jukumu la kusimamia kuhakikisha usalama wa vyombo vya baharini laikini inaonesha kuwa mamlaka hiyo imeshindwa kazi na ndio maana uzembe mkubwa unaendelea kufanyika ikiwemo kutokukagua vizuri injini za boti hizo,upakiaji abiria kiholela na ukataji wa tiketi ovyo bila kutumia vitambulisho pamoja na uuzwaji ovyo wa tiket vichochoroni bila ya kutumia Ofisi zinazotambulikana kitu ambacho kinachopelekea kupakia abiria wengi kuliko uwezo wake. Ndio maana hata takwimu zinayotolewa wakati chombo kinapopata ajali inakuwa ni tofauti na hali halisi ya idadi ya watu wanaokuwemo. Kwa hiyo, tunaitaka Serikali kuhakikisha kwamba inasimamia watendaji wake kutekeleza yale majukumu waliyopewa ili kuepusha ajali kama hizo zisitokezee tena.

Mhe Spika, jengine tunalojifunza nia kwamba Serikali yetu kutozifanyia kazi kwa haraka ripoti mbalimbali za aidha za kamati inazoziunda wao wenyewe au zile za Baraza lako tukufu au hata za taasisi mbali mbali Srikali inazopelekea kwani ukiangalia mambo mengi yanayoshauriwa basi yanakuwa ni kwa faida ya nchi yetu na pale zinapodhararauliwa basi matokeo yake wakati mwengine yakuwa na athari kubwa kwa jamii kwa ujumla.

Mhe Spika , kwa funzo hilo Serikali yetu ililolipata kama kawaida yetu tunaishauri sasa wakati umefika kuzifanyia kazi ripoti zote ilizopelekewa ukiacha zile za Baraza bali ni kwa ripoti zote zilizopelekwa Serikalini.

Mheshimiwa Spika,jambo jengine inaonesha kuna udhaifu mkubwa katika ukaguzi na usajili wa meli kutokuangalia historia ya meli hiyo kuanzia mwaka iliyotengenezwa,kazi inazoweza kuzifanya,muda wa uhai wa kutumika kwa chombo hicho,lakini pia na udhaifu wa (modification) zinazofanywa ili kuongeza nafasi za kupakilia abiria bila ya kuzingatia uwezo wa injini ya chombo hicho kwa lengo la kutengeneza faida kubwa bila kujali maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika,imekuwa ni jambo la kawaida kwa hivi sasa mtu akitaka kusafiri kwa boti au kwa meli anawaza mara tatu tatu kwani hana uhakika wa kufika salama safari yake, hii inaonesha kuwa hakuna uhakika wa salama wa maisha yake, leo hii imekuwa hata wanafamilia wanaposafirisha jama zao huwa presa juu juu mpaka wafike safari na kuwajuilisha kuwa wamefika salama, kwa hiyo hivi sasa Serikali imeweka rehani maisha ya wanachi wake kwani hakuonekani juhudi zozote za waliokabidhiwa majukumu ya kuwasimamia usalama wa abiria wetu kama wako makini kiasi hicho, hii ni kusema kwamba wameshindwa kazi.

Lakini kwa kuwa kwa mara ya kwanza Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa imesikia kilio cha Wawakilishi na wananchi wa Zanzibar kwa kumtaka Waziri ajiuzulu ambapo suala hili tulilipendekeza tokea ilipozama meli ya Spice Islander tulimtaka ajiuzulu ili kuonesha uwajibikaji wa kisiasa, lakini kwa bahati mbaya hakufanya hivyo lakini tunamshukuru kwa hivi sasa kwa kuwa ameamua kuwajibika ili kuonesha kuwa na yeyé ameguswa katika tukio hili kubwa la kitaifa. Na hili wala asione taabu wala aibu kwani kwa mfumo huu tuliokuwa nao hivi sasa wa Serikali ya umoja wa kitaifa wa demokrasia ya ukweli na uwazi ni jambo la kawaida sana tu na tunawaomba wengine wanaposhindwa kusimamia majukumu yao basi waamue mapema kuliko kusubiri kung’olewa kwa nguvu.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha sana kwa wananchi wetu, kwani hata kuna baadhi ya wahangana waliopata ajali katika meli ya MV SPICE ISLANDER hawajapata ubani wao uliotengwa na Serikali, lakini leo hii tayari kuna msiba mwengine mkubwa ulioikumba nchi yetu, inawezekana pia miongoni mwa familia waliopata maafa hayo na katika maafa haya ikawa yamewakuta tena kama wapo watu hawa basi tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subra kwani ni mtihani mkubwa kwao na inabidi washukuru kwani kila mtihani anaokupa Mwenyezi Mungu basi ukiwa na subra kuna kheri pia inakuja baadae nawaomba Wajumbe wenzangu wa Baraza hili pamoja na Watanzania wote kwa ujumla tuwaombee kila la kheri katika kukabiliana na mitihani hii pia tumuombe Mwenyezi Mungu awaepushe na mitihani mengine.

Mheshimiwa Spika,kwa tukio hili kuna baadhi ya maneno yanayozungumzwa na baadhi ya wanasiasa kuwa kuna kundi ndani baraza lako tukufu kwamba lina chuki za ubaguzi wa kisiasa kwa baadhi ya mawaziri tunataka kuwahakikishia wananchi wote wa Zanzibar kuwa sisi sote ni kitu kimoja na tunafanya kazi kwa pamoja kuwatumikia wananchi wetu bila ya chuki wala upendeleo wowote, bali ni kwa maslahi ya umma tu. Kwani kwa hivi sasa tumeamua kuweka kando itikadi zetu za kisiasa na kuamua kujenga nchi yetu kwa pamoja kwa maslahi ya Taifa letu na wananchi wetu, kwa hiyo tunaomba kila mmoja atimize majukumu yake aliyotumwa na wananchi wake kwa upande wa Wawakilishi ya kuisimamia ipasavyo Seriakali na kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kwa mujibu wa Katiba na Sheria zote , za hapa ZNZ na Tanzania nzima. Vile vile kusimamia uwajibikaji wa watumishi wote wa umma katika majukumu waliokabidhiwa na Serikali, lakini pia na mawaziri kwa upande wao kuhakikisha wanawasimamia walio chini yao ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar.

Mhe Spika, kamati yangu inaishauri Serikali kuendelea kulitumia eneo la kama kuwa ni eneo la kudumu kwa ajili kuzikia kwani eneo hilo inaonyesha eneo hilo lilitelekezwa baada kuzikwa watu waliofariki katia ajali ilyopita, lakini pia ukizingatia kuwa hivi sasa eneo la makaburi ya mwanakwerekwe limeshajaa kwa muda mrefu lakini bado linaendelea kuzikiwa maiti hadi vivi sasa jambo ambalo halipendezi hata kidogo.

Mhe Spika. Kamati yangu kutokana na funzo la ajali hii ya tatu mfululizo ndani ya miaka mitano tumeona iko haja ya kuwashauri wananchi wetu kujikatia bima za maisha ili yanapotokea majanga kama haya waweze kulipwa Bima ya maisha au ya afya kwa wale waliojeruhiwa au kupoteza uwezo wa kufanya kazi tene katika maisha yao kuliko kutegemea ubani utakaotolewa na Serikali kama utakuwepo.

Mhe Spika, ripoti ya Serikali imeelezea kuwa wamewasaidia jamaa wa marehemu gharama za mazishi, usafirishaji wa maiti ,sanda na ubao lakini kamati yangu inaiomba Serikali pia kuwasaidia na gharama za Tahtimu kwani hali za familia zetu tunazijua kuwa nyingi zinaishi katika hali duni ya maisha na pengine hao waliofariki wengine ndio tegemeo lao katika familia, kwa hiyo kwao wao msiba unakuwa ni mara mbili. Kwa hiyo tunaamini jambo hilo litawapunguzia machungu wakati wa kuomboleza msiba.

Mhe Spika, katika ripoti ya ya Mhe Waziri ametueleza kuwa kuna baadhi ya wasamaria wema wanaendelea kufika ofisi ya Makamo wa pili wa Rais kutoa ubani wa mkono wa pole, na kwa upande fedha taslim wameziweka katika Account maalum iliyofunguliwa wakati wa ajali ya MV SPICE ISLANDER’S , lakini hadi leo Serikali yetu bado haijaanzisha mfuko wa maafa ambao utaweza kutumika au kusaidia wakati wowote maafa yatakapotokea aidha kwa upande wa Baharini ,au nchi kavu kwani ajali ziko za aina nyingi tu, kwani kuna Mafuriko, Moto, ajali za Ndege, Meli, Upepo mkali, n.k. kwa hiyo kamati yangu inaishauri Serikli kuanzisha mfuko wa maafa kwani si busara kuendelea kutumia pesa kutoka mfuko Mkuu wa Serikali, kama ilvyo hivi sasa kwani inasababisha kuwazuia wafanya biashara, Mashirika ,Makampuni au taasisi au mtu yeyote anayehitaji kuchangia mfuko huo kushindwa kufanya hivyo, lakini pia tunata kujua kuwa katia account hiyo maakum je kutakuwa na utaratibu mpya wa utoaji ubani kwa kiasi kili kile kilichotolewa katika ajali ya mwanzo?

Mhe Spika, Lakini pia tunaiuliza Serikali kupitia ahadi zilizotolewa na baadhi ya taasisi za fedha waliahidi kuwasomesha baadhi ya mayatima waliochwa na waliopoteza maisha katika ajali ya MV SPICE ISLANDER, je Serikali kupitia Ofisi yako imelifuatilia kwa kiasi gani? Na kama limetekelezwa je ni mayatima wangapi hadi sasa wanasomeshwa na taasisi hizo?.

Mhe Spika, kamati yangu inaiomba Serikali kuimarisha kikosi chetu cha KMKM pamoja na kikosi cha Zimamoto na uokozi ili kuweza kukabiliana na maafa ya ajali yoyote inayowezac kutokea aidha kwa Baharini au nchi kavu, kuwa na zana za kisasa ikwemo kuwa na Helikopta ya uokozi ambayo itakuwa na huduma za matibabu ya dharura inapokuwa angani ili kuweza kuokoa maisha ya wa wananchi wetu popote majanga yatakapokuja kutokea, vile vile tunaiomba Serikali yetu kuandaa utaratibu mzuri wa uokozi kwani tumeona udhaifu mkubwa wakati wa harakati za uokoaji pale Bandarini hapakuwa na utaratibu mzuri wa nani aliekuwa na amri ya mwisho katika kuongoza zoezi zima la uokozi, kwani tumeshuhudia hata vyombo vilivyokuwa vikitumika vilikuwa ni vikubwa kitu ambacho kilihitajika kutumika pia vyombo vidogovidogo ambavyo vingeliweza kusaidia zaidi huduma za uokozi.
Mhe Spika, katika hali iliyokuwa si ya kawaida au fadhaa tulishangaa kuona baada ya kutokea ajali chombo cha mwanzo kwenda kwenye tukio kiliwaacha wazamiaji ambao waneliweza kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi badala yake chombo hicho walipanda viongozi wakiwemo mawaziri utadhani wanakwenda kuangalia snema huko baharini wakati wao wenyewe hawajui hata kuogelea seuze kuokoa watu waliopata ajali , hili pia ni funzo kubwa tunatakiwa tujipange vizuri, vile vile kitu chengine cha kushangaa ni kule kuona hata kuna baadhi ya boti ambazo zilikwenda kuokoa watu waliozama kusikia nazo zilizimalizika mafuta huko baharini kitu ambacho ni kibaya sana kwani kinaweza kusababisha ajali nyingine huko baharini kwa hiyo inaonyesha kuwa bado hatujakuwa na mipango mizuri ya uokozi pale majanga yanapotokea,

Mhe Spika, Kamati yangu inaiomba Serikali kufanya ukaguzi wa kina kwa vyombo vyote vya Baharini, ikiwemo Engine pamoja na uwezo wa Manahodha na Mabaharia wanofanyakazi katika vyombo hivyo na wakigundulika wasiokuwa na uwezo kuachishwa kazi na ni bora kuwa na vyombo vichache vyenye uhakika kuliko kuwa na vyombo vingi visivyokuwa na ubaora au kiwango, .
Mhe Spika, kamati yangu bado inaiomba Serikali yetu kufanya kila linalowezekana kununua Meli ya kubebea abiria na mizigo kwani ni aibu kuwa sisi tunachaguliwa na wananchi hao hao na tunalipwa mishahara kupitia kodi zao lakini tunashindwa kuwahakikishia usalama wa maisha yao.

Mhe Spika, Lakini pamoja na Serikali kununua Meli hizo kwa kuwa mazingira ya nchi yetu ni ya visiwa sio kama watu wote wataweza kusafiri kwa siku moja na kupanda Meli hizo la Serikali kwa hiyo bado ni lazima kutakuwa ulazima wa kuwa na vyombo binafsi , ndio maana tukasema kuwa suala kubwa hapa na la ulazima ni kuhakikisha ukaguzi wa kina wa usalama wa vyombo hivyo kwani hata hizo Meli za Serikali pia nazo zitahitajika kukaguliwa kila wakati kwani sio kama hizo Meli za Serikali hazitaweza kupata ajali zikiwa nazo hazitakuwa na ubora .

Mhe Spika, kwa kumalizia tunaishauri Serikali yetu kuwa sasa wakati umefika wa kuyatekeleza maoni na ushauri wa kakati zote aidha ilizoziunda wenyewe Serikali ,ripoti za washauri mbali mbali wa nje na ndani na zile za Baraza la wawakilishi kwani zina faida kubwa kwa nchi yetu kaka zitatekelezwa kwa vitendo na muda muafaka, vinginevyo hata hizo idara zilizoundwa kila wizara Idara za utafiti zitakuwa hazina maana yeyote kwani nao baada ya kufanya utafiti baadae pia hutoa ripoti kwa hiyo ripoti hizo kama hazikufanyiwa kazi yatakaua ndio hayo hayo (BUSINESS AS USSUAL)
Mhe Spika kwa mara nyingine tena naomba niwashukuru wajumbe wa kakati yangu kwa kuwa wastahamilivu na kunipa mashirikiano makubwa kuandaa ripoti hii kwani tuliweza kuaa hadi saa sita za usiku na kuweza kuikamilisha asubuhi hii na kuiwakilisha hapa Barazani,
Mwaisho kabia naomba kuwashukuru wananchi wote wa ZNZ pamoja na wananchi wangu wa jimbo la Kwamtipura walionileta hapa ili ukwatumika nnawaahidi kuendelea kuwatumikia kwa uadilifu na moyo wangu wote.
Mhe Spika mwisho kabisa naomba kumkaribisha Mhe Hamad Masoud Hamad katika nyumba yetu ya Back Bancher ili kushirikiana nasi kuwatumikia wananchi wetu wa ZNZ kuwaletea maendeleo, tunakuombea kila la kheri katika kazi yako hii mpya ambayo kwa miaka mingi uliitumikia kwa uadilifu mkubwa, na tunamuomba M/Mungu akuepushe na shari nyengine naomba kuwasilisha .

Mhe Spika naomba kuwasislisha.
Ahsante sana.

Ahsante

…………………
MHE: HAMZA HASSAN JUMA
KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIOGOZI WAKUU WA KITAIFA
BARAZA LA WAWAKILISHI
ZANZIBAR.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s