Kuasi kisiasa ni haki ya kidemokrasia

 

Muasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) Patrice Lumumba

Ahmed Rajab

MWAKA 1958 utakumbukwa katika historia ya ukombozi wa Afrika kwa mkutano wa All-African People’s Conference uliofanywa mjini Accra, Ghana, chini ya uenyekiti wa Kwame Nkrumah, mwanadharia wa Umajumui wa Kiafrika (Pan-Africanism). Mkutano huo ulikuwa na umuhimu zaidi kwa vile ndio uliomtoa ukumbi Patrice Lumumba na kumfanya aanze kujulikana nje ya mipaka ya nchi yake ya Congo. Wakati huo Lumumba alikuwa amekwishakuanza kupata umaarufu nchini mwake kwa harakati zake za kuupinga ukoloni Wakibelgiji lakini kimataifa, na hasa katika nchi zilizokuwa zikitawaliwa na Uingereza, alikuwa hajulikani.

Jambo moja ambalo wengi wamelisahau ni mabishano yaliyoibuka mkutanoni humo kati ya Nkrumah na wajumbe kutoka Afrika ya Kusini ambako Nelson Mandela na wenzake walikuwa wakipambana na utawala wa kikaburu.  Mabishano hayo yalihusika na mbinu gani za kutumiwa ili kuung’oa ukoloni na ubeberu barani Afrika.

Wajumbe kutoka Afrika ya Kusini walishikilia kwamba mbinu pekee ya kutumiwa ni ya mapambano ya silaha dhidi ya wakoloni.  Walihoji kwamba kufanya vinginevyo hakutoushinda kamwe ukoloni wala utawala wa wachache. Nkrumah alikuwa na rai nyingine.

Akiwa mmoja wa wahubiri wakuu wa itikadi ya Umajumui Wakiafrika, Nkrumah alikuwa pia mtetezi wa mfumo wa kidemokrasia. Nkrumah alielewa nini hasa maana ya demokrasia na akiitakidi kwamba demokrasia lazima iwe moja ya nguzo za Umajumui Wakiafrika.

Hivyo hakuwa akivutiwa na hoja za utumizi wa nguvu katika kuupiga vita ukoloni licha ya kuwa demokrasia ndiyo iliyokuwa mfumo wa utawala wa madola ya Kimagharibi yaliyozinyonya nchi za Kiafrika kwa muda wa karne sita.

Nkrumah akitambua kwamba mahusiano ya demokrasia na mapambano ya kuupinga ukoloni na ubeberu yalikuwa kama ya chanda na pete. Hivyo ni muhali mtu kuwa mpinga ukoloni au ubeberu na wakati huohuo akawa mpinzani wa demokrasia.  Hilo haliwezekani.

Kadhalika alielewa kwamba hakuna kilichokuwa kikienda kinyume cha demokrasia zaidi ya ukoloni na ubeberu. Hayo ni sawa na kusema kwamba mtu kuwa na moyo wa kidemokrasia ndiko kunakomfanya azidi kuwa na raghba ya kupambana na ubeberu na ukoloni.

Naamini kwamba moja ya makosa ya viongozi wa Kiafrika baada ya nchi zao kupata uhuru ni kuitupilia mbali dhana ya demokrasia badili ya kuifanya iwe moja ya mihimili muhimu ya mikakati ya kuleta maendeleo na ya falsafa ya Umajumui Wakiafrika.  La kusikitisha na kustaajabisha ni kuona kuwa Nkrumah alikuwa miongoni mwa viongozi wa mwanzo walioteleza walipolikanyaga ganda la demokrasia.

Ni yeye Nkrumah aliyeendelea kuitumia, kwa mfano, ile sheria  ya kikoloni ya kuwaweka watu vizuizini bila ya kwanza kuwafikisha mahakamani, sheria ambayo hata huku kwetu ikitumiwa kuwagandamiza wapinzani.  Na ni Nkrumah pia aliyeibadili Katiba ya nchi na kuifanya Ghana iwe nchi yenye chama kimoja tu kilichokuwa halali ambacho kilikuwa chake cha Convention Peoples Party (CPP).

Nkrumah akitaka kuleta mfumo mpya wa utawala usiouiga ule wa demokrasia ya Westminster unaofuatwa na Uingereza na nchi nyingi ambazo zamani zilikuwa makoloni yake.  Yeye akihoji kwamba mfumo huo wa demokrasia inayoruhusu vyama vingi ni mfumo wenye kuigawa jamii na haukuwa na tija yoyote kwa nchi changa kama Ghana.

Nkrumah hakusema kwamba mfumo wa utawala wa kidemokrasia ni mbaya ila aliukosoa ule unaoruhusu kuwako kwa vyama vingi. Naye akiamini kwa dhati yake kwamba demokrasia inaweza kumea katika mfumo wa utawala unaohalalisha kuwako kwa chama kimoja tu cha kisiasa. Akitaka demokrasia ya aina mpya, demokrasia ambayo mbegu yake itapandishwa na kumea katika ardhi ya Afrika, demokrasia itayokuwa na mizizi katika historia na mazingira ya utamaduni wa Kiafrika.

Kwa bahati mbaya fikra aina hizo zilikwenda kombo.  Tumeshuhudia kwingi Afrika, hata huku kwetu, jinsi mfumo huo wa chama kimoja ulivyoicheza shere demokrasia kwa kuzikanyaga haki za kimsingi za binadamu na kuyarudisha nyuma maendeleo.

Kuitupa demokrasia kuliidhuru mikakati ya kiuchumi ya nchi zilizokuwa na mfumo ulioruhusu kuwako kwa chama kimoja tu kilicho halali.  Hali hiyo iliwapa uwanja viongozi wasio waadilifu, madikteta, waweze kuzitumia vibaya rasilimali za nchi zao kwa vile kulikosekana njia za kidemokrasia za kuwafanya wawajibike.  Kadhalika kulikosekana uwazi katika uendeshaji na utekelezaji wa shughuli za kiuchumi.

Hakuna shaka yoyote kwamba demokrasia ni kiungo muhimu katika harakati za kuleta maendeleo barani Afrika. Wale wanenao kwamba demokrasia haijazi tumbo wanakosea. Demokrasia inaweza kuhakikisha kwamba matumbo ya Waafrika yanajaa ilimradi vigezo vingine vya maendeleo vinafuatwa kwa njia za kuwapatia wananchi wote haki sawa.

Demokrasia inaweza kuyajaza matumbo kwani inaweza sana kusaidia katika jitihada za kuufyeka umasikini katika jamii.  Sisemi kuwa hiyo ni kazi rahisi au kwamba jamii zote zenye mfumo wa demokrasia ya kweli zimeweza kuuondosha umasikini.

Nisemacho ni kwamba demokrasia inaweza kuwa ngao ya kuiwezesha jamii kujikinga na ufisadi, ubadhirifu wa fedha za umma na kutowajibika kwa viongozi. Muhimu ni kwamba demokrasia pia inawapunguzia wenye nguvu katika jamii — ziwe nguvu za kisiasa au za kiuchumi — wasiweze kuzitumia vibaya nguvu hizo bila ya kuwajibika mbele ya sheria.  Demokrasia inapokuwa inafanya kazi hiyo basi huwako uwezekano mkubwa wa kupatikana maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.

Ni rahisi kufahamu kwa nini sauti kubwa imekuwa ikivuma barani Afrika kupinga demokrasia na kuiona kuwa ni dhana ya Kimagharibi inayotumiwa kinafiki na nchi za Magharibi kulikandamiza Bara la Afrika.

Ni kweli kwamba mara kwa mara nchi za Magharibi zimekuwa zikitumia kisingizo cha demokrasia katika njama za kuwatoa madarakani viongozi wa Kiafrika wenye kwenda kinyume na maslahi ya nchi hizo, kama walivyomfanyia Nkrumah na hivi karibuni Mua’mmar Qadhafi wa Libya.

Ni kweli pia kwamba mara kwa mara nchi hizohizo za Magharibi zimekuwa zikiwavumilia na kuwalinda viongozi wa Kiafrika waliokuwa makatili na waliokuwa hawafuati demokrasia ya kweli au hata ya uongo uongo kama akina Mobutu Sese Seko.

Hadi hii leo nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zingali zikiendelea na mtindo wao wa kuwaunga mkono na kuwalinda watawala wa kimabavu madhali ni marafiki zao. Na watawala hao wanakuwa marafiki zao wanapokuwa wanayatumikia maslahi ya hizo nchi za Magharibi huku wakiwasumbua, wakiwaibia na wakiwaonea wananchi wenzao.

Tunapokuwa tunaizungumzia na kuitathmini demokrasia ni muhimu tukumbuke kwamba demokrasia si kitu kimoja pekee bali ni mchanganyiko wa mengi. La awali ni kwamba wananchi wawe na uwezo wa kujiamulia mambo yao wenyewe, kwamba mamlaka ya utawala yawe mikononi mwao. Wawe na nguvu za kisheria zinazotokana na katiba na zinazowawezesha kuwaondosha madarakani viongozi wasiowataka pale wasipowataka tena.

Miongoni mwa mengine yanayohitajika ili demokrasia halisi ishamiri ni uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kukusanyika, uhuru wa mtu kuabudu dini aitakayo pamoja na uhuru wa kutoabudu dini yoyote, uhuru wa kupata habari kutoka popote apatakapo mtu, uhuru wa kusema, kuwako kwa haki za binadamu pamoja na haki za kiraia na haki ya mtu kutoingiliwa katika mambo yake ya faragha.

Yote hayo hayatotosha kuifanya demokrasia iwe ya kweli endapo patakuwa hakuna hali ya usawa miongoni mwa wananchi, ikiwa hakuna hali ya kuheshimiana, kuvumiliana na kuwa na maridhiano katika jamii.

Wengi wanapozungumzia demokrasia huwa wanaupa kipaumbele uchaguzi.  Wanauona uchaguzi kuwa ndio msingi wa demokrasia. Kwa hakika, uchaguzi unakuwa msingi wa demokrasia pale tu unapofanywa kwa haki. Uchaguzi aina hiyo huwapa wananchi uhuru wa kumchagua wamtakaye bila ya kuingiliwa na tashwishi za aina yoyote ile kutoka vyombo vya dola.  Kwa ufupi, katika demokrasia ya kweli lazima pawepo na chaguzi zinazoendeshwa kwa uadilifu.

Haitoshi kuwa na mfumo wa kidemokrasi.  Kinachohitajika katika nyingi ya nchi za Kiafrika ni kuwa na taasisi zitazoweza kuizuia mizizi ya demokrasia isiweze kung’olewa kwa urahisi.  Iwapo taasisi aina hizo zinakosekana basi inakuwa rahisi sana kuua mfumo wa kidemokrasia.

Tunayashuhudia hayo nchini Mali ambako baada ya kuwako kwa mfumo wa kidemokrasia kwa muda wa miaka ishirini kijanajeshi kimoja tu, Kapteni Amadou Haya Sanogo, kiliiua demokrasia na kuitumbukiza nchi katika maafa.

Historia inatufunza kwamba panapokosekana demokrasia ya kweli si hasha kuona kunaibuka uhasama, misiguano ya roho na hata mapigano ya umwagaji wa damu. Panapokuwako demokrasia ya kweli kunakuwako hali ya amani, usalama na utulivu katika jamii.  Kadhalika panapotokea dhulma au manung’uniko katika jamii demokrasia huwa na njia zake za kuwafanya wanaoonewa waweze kutoa madukuduku yao na kudai haki zao.

Faida nyingine kubwa ya demokrasia ni kuwa inawawezesha watu kupanua fikra zao.  Inawakomboa wananchi kwa kuwapa uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutenda na hata wa kwenda kinyume na fikra za kikale.

Ili jamii iweze kuendelea na iwe na demokrasia iliyopevuka ni muhimu wananchi wawe na uhuru wa kuweza kuasi kisiasa na kuwa na fikra zisizofuata mkondo wa fikra za kawaida za wanajamii. Haki ya kuasi kisiasa ni haki ya kimsingi na ya kidemokrasia.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s