Wakati ndio unaosema na kuamua

 

Mwanahija Rajab akitoa maoni yake kuhusu katiba mpya huko katika Kijiji cha Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja

Na Juma Mohammed

Nyota njema huonekana alfajiri, ukiona alfajiri imeingia upeo wa macho yako huoni nyota ni kiwingi kitupu kimetanda kaa ukijuwa kuwa mambo kwako sio mazuri kajipange upya kimkakati. Kinyume na matarajio ya walio wengi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeanza kazi kwa wananchi wengi kujitokeza kutoa maoni yao kwa amani, utulivu na ustaarabu mkubwa kwa upande wa Zanzibar.

Nimebahatika kwenda katika mikutano kadhaa ya Tume hiyo, watu ni watulivu na kwa hili lazima niwapongeze wananchi kwa uugwana wao maana siku zote muungwana ni vitendo.

Jambo moja ambalo nimejifunza wakazi wa vijijini wamekuwa na uelewa mkubwa wa mambo, pengine kuwashinda hata wale walioko maeneo ya mijini, wanajenga hoja katika maoni yao na kutoa mifano hai.

Wakati huu wananchi wakiwajibika kwenye Tume kutoa maoni yao,hatutegemei kuzuka watu au kikundi cha watu kikawa kinaifuata Tume kila inapokwenda, hii sio sahihi, wewe kama ni mkazi wa Fujoni subiri zamu ya eneo lako itafika, ikiwa eneo lako Tume imeshapita umetoa maoni hakuna kuwabughudhi wengine.

Kama walivyoonesha uungwana watu wa Kusini Unguja, tunataraji maeneo mengine kuendelea kuiga mfano wa ukomavu wa demokrasia maana katiba inayokusudiwa kuandikwa ikiwa itaridhishwa na umma ni yetu sote sio ya viongozi wala vyama vya siasa,wasomi au matajiri.

Ilivyokuwa katiba ya nchi katika nchi yoyote ya kidemokrasia, ni mali ya wananchi wenyewe na hivyo ni wananchi pekee ndiyo wenye haki ya kubadili katiba ya nchi yao, haipendezi kutokea watu wakijigeuza mawakala wa kuwafunza watu nini cha kusema katika Tume,kila mmoja na mawazo yake.

Ni hivyo basi, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya Watanzania na si vinginevyo, ni wananchi wenyewe kwa umoja wao ndio pekee wenye haki ya kuibadili katiba ya nchi yao hivyo kutofautiana kimtazamo sio dhambi.

Yafaa kukumbuka kuwa Katiba inayokusudiwa kuandikwa Tanzania ni ya nchi kamwe si ya chama tawala cha CCM, CUF, CHADEMA,NCCR MAGEUZI,UDP,TLP, AFP nakadhalika, hivyo si sahihi suala la mabadiliko ya katiba likavaliwa njuga kwa kuifuata Tume ya Katiba kila iendako hata kama si mkazi wa eneo husika.

Vijiji ambavyo watu wake wametoa maoni, wamelitaja suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo wengine wakitaka Mabadiliko ya muundo uwe wa mkataba , wapo waliotaka muundo wa sasa wa Serikali mbili kuendelea,wapo waliotaka Serikali tatu,wapo wanaotaka Serikali moja.

Kuwepo kwa maoni na mitazamo tofauti kumetupa nguvu sisi wengine ambao awali tulidhani tuwapweke,kumbe tunawenzetu ambao imesadif mawazo yetu kama yao ingawa si kwa maeneo yote,lakini tumo tunaelea jahazi moja.

Hapa nikakumbuka kauli mbiu sio ile ya Uamsho ya “Tuachwe Tupumuwe” ni ya timu pendwa ya soka Uingereza Liverpool ambayo kauli mbiu yao ni “You will never work alone” Kamwe hutatembea peke yako.

Wakati ule nilifikiri kuwa yote yaliyo azizi au bora kwa mwanadamu ni matendo yake aliyotenda zamani nikasema sisi wengine hatujakula chumvi nyingi kwani hatukutenda lolote kwa ujana wetu,nilijihisi kuwa masikini,lakini fikra hizi sasa zimeanza kubadilika maana ubora wa mtu unaweza kuwa katika wakati ujao tutakaposhuhudia mabadiliko katika Muungano wetu.

Ilivyokuwa maisha yangu bado mapya na matumaini yakisheheni kila uchao sitaweza kubakia katika ukale ingawaje tunaaminishwa kwa msemo kwamba yakale dhahabu,lakini yafaa kutambua kuwa si kila ya zamani ni dhahabu.

Kawaida jambo la bahati mara nyingi hukawia, kwa maana yengine bahati haina miadi kama tufanyavyo binadamu, kwa miaka mingi wananchi tulingoja bahati ya kuandika katiba mpya, sasa bahati imetokea na kwa kuwa tulikuwa na shauku ya jambo lenyewe hatutazembea wala kuipoteza hidaya hii kwani kila jambo la kheri linakwenda kwa kheri.

Mara zote wakati ndio unaosema na kuamua ni kama maji kupwa na kujaa, huwezi kuyazuia wale waliotegemea kuzuka kwa makamio yasiyokuwa na tija wamebaki vinywa wazi maana kila mmoja anapewa haki ya kutoa mawazo yake na jambo la kupongeza hakuna anayebeza mawazo ya mwengine,si Wajumbe wa Tume wala watoa maoni wengine.

Katika baadhi ya mikutano hiyo wapo waliotaka katiba mpya iweke kifungu cha wananchi kuwawajibisha Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ikiwa wapigakura wataona uwakilishi wao kwenye vyombo hivyo hauna tija waweze ama kumsimamisha kazi au hata kumfukuza.

Wapo waliotaka kiwepo kifungu kinachotambua zamu za Urais katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwa na maana kama kipindi hichi Rais katoka upande mmoja wa Muungano,kipindi kinachofuata atoke upande mwengine.

Ama kweli kama kusemwa ni mauti sisi wengine tushasomewa hitima maneno hayo yamo katika wimbo wa Dua la Kuku ulioimbwa na Spice Modern Taarab ikiwa jibu la wimbo wa fimbo ya Mungu ulioimbwa na Kundi la Taarab la Zanzibar One.

Hatushindwi kushona tanga wala kuiunga heza maana unahodha ni kazi yetu hakuna moja litakalotushinda ndio maana tumekuwa tukieleza bayana misimamo yetu katika suala zima la kupata katiba mpya, hatusubiri maoni ya kupewa kwenye bahasha tukayafanya ya kwetu maana Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwahi kusema “Binadamu wote hatuwezi kufikiri sawa” basi na katika hili la muundo wa Muungano lazima kutakuwa na mawazo tofauti.

Hatutaweza kuwa kama Kinyozi aliyekuwa akilia yeye na mnyolewaji maana yule anayenyolewa yawezekana akawa anaumia,lakini huyo mnyoaji je kakumbwa na nini wakiulizwa ndio kwanza unazidisha kilio!

Hizi sio karne za ujinga au ukifuu tundu na wala sio zama za mtu kujifanya mbabe au mzalendo zaidi kupita mwenzake,kujifanya Senior Citizen, karne hii ya 21 ni ya watu kutendeana wema hisani na upendo,ni karne ya majadiliano katika kufikia maafikiano(consensus).

Kuwa kwangu muumin wa Muungano wa mkataba sio dhambi kwa Mwenyezi Mungu wala Serikali maana mamlaka ya uendeshaji nchi ipo mikononi mwa wananchi wenyewe, haijuzu kuzuka watu walikozuka kuanza kunyoosheana vidole, ushabiki wa vyama ni wa kupita tu ni sawa na wa mpira wa miguu, ziko wapi Cosmopolitan, Malindi, Taifa ya Jang’ombe, Muembe Ladu,Ujamaa, Nyota Nyekundu,Pani Africa na nyenginezo?

Vyama vya siasa ni kama ndege anayetua tawini,lazima aruke washahiri wengi wamelisema hilo nami nalirejea kwa muktadha wa mambo ya msingi katika nchi hayategemea ushabiki wa kisiasa,yanahitaji umoja na mshikamano zaidi maana tunaweza kuishi bila vyama vya siasa,lakini hatuwezi kuishi bila nchi.

Siku za hivi karibuni kulijitokeza wanasiasa waliovaa majoho ya Ujaji kwa kutoa hukumu kwa raia wenziwao wenye kutofautiana nao kimawazo. Utawasikia “huyu sio mwenzetu” Hapo tena wanabishana wenyewe kwani wewe humjui yule si fulani yule ni Hizbu tangu zamani(Hizbu ni kilichokuwa Chama cha Zanzibar Nationalist Party-ZNP kabla ya Mapinduzi).

Badala ya kujadili hoja iliyotolewa wao wanajadili watu kwa kuwanasibisha na vyama vya zamani ambayo haviwezi kuibuka juu katika bahari mpya ya siasa za kileo zenye kuhitaji umakini na weledi katika uwanja wake sio kuendesha siasa kwa mazoea ya kurithi maana waswahili wanarithi kila kitu.

Katika hili la kuwa muumini wa Muungano wa mkataba nisingelipenda kuwa mtazamaji wakati wananchi wenzangu wakijitokeza hadharani,lakini hatujawafunga mdomo waumini wa aina nyengine ya muundo wa Muungano nao kujimwaga kiwanjani kwa msingi ule ule wa ushawishi wa hoja na sio kejeli,vijembe au jazba.

Siku za nyuma niliwahi kusema kuwa kama muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ungelikuwa ni jahazi basi jahazi hilo limeshafika ufukweni ikiwa na abiria waliosafiri kwa muda wa miaka 48 je,abiria hao watabadili tanga kukabili upepo wa kusi au watakwenda na tanga bovu na foromali chakavu?

Kitandawili hicho kitaaguliwa katika kura ya maoni hapo baadaye wakati rasimu ya katiba itakapopigiwa kura na wananchi, wanaikubali au la.

Njia hii ya kura ndio sahihi kuliko zote kwani Mwenyezi Mungu ameuzidisha wepesi wa kubadili mambo kwa kumpa fikra mwanadamu kubuni kitu kura ambacho mara nyingi wapigaji kura wanatumia kijipande cha karatasi kufanya maamuzi.

Wataalam wa mambo ya siasa wanasema kwamba umuhimu wa kura unawafanya viongozi waliomo madarakani kuheshimu kazi na kuwaheshimu wananchi wenzao kwani iwapo watawatendea mabaya itapofika siku za kupiga kura bila shaka watawanyima kura hivyo madaraka yatawatoka.

Mara nyingi njia ya kura huleta heshima katika nchi baina ya watawala na watawaliwa hivyo tunategemea sana siku ya siku kura ya maoni kuamua kama tuwe na Katiba mpya au iliyopo iendelee ama inaweza kutuletea heshima au kutuvunjia heshima mbele ya walimwengu.

Jambo la muhimu ni kila mtu kuwa huru kutoa maoni yake bila jazba wala soni, ikiwa huwezi kutoa maoni yako ni bora kukaa kimya kuliko kutumiwa na wewe ukatumika maana siku zote wananchi walikuwa wakilalamika hatushirikishwi sasa mpira upo kwetu hakuna kutia kwapani wala kwa Yanga.

Advertisements

7 responses to “Wakati ndio unaosema na kuamua

 1. juma mwamedi nini ndugu yangu umelipwa kiasi gani kuandika makala hii? mbona hukutaja waliosema hawataki muungano? ni vyema kukawa na kundi la wananchi wanafatilia kwa takwimu watu waliosema hawataki muungano ktk maoni ,, waandishi wetu wote wamerubuniwa na watanganyika hawaaminiki , na kama kweli hio demokrasia ipo , kwa nini haiitishiwi kura ya maoni , mnatuletea huu upambavu wa danganya toto ya katiba , wakati katiba mnayoitaka iko mfukoni ? mnawafanya watu wapumbavu? mnawatumia watu wa vijijini kutokana na umaskini na shida zao manawarubuni kusema mnayotaka ? mwogopeni mungu akina ndugu ,

 2. Nakushukuru kutupa taarifa motomoto lakini mimi wasiwasi wangu ni matokeo ya maamuzi ya tume kujaingiliwa na dola. Wananchi tulio wengi tushachoka na mfumo huu tulionao wa muungano. Sanjari na hilo naamini kabisa kuwa upo mfumo wa uwendeshaji ulikwisha tayarishwa na uongozi ulipo madarakani ambao utapitishwa kwa nguvu zote. Mimi naomba mara nyengine ni vyema ukatupatia kwa idadi ni wangapi wanataka muungano wa mkataba na wangapi wanataka waendelee na mfumo huu tulionao, wangapi wanataka serikali moja na wangapi hawataki muungano ili tuweze kufatilia kwa umakini zaidi. Inshallah tutashinda ZANZIBAR HURU KWANZA. HATUUTAKI MUUNGANO.

 3. JE IKIWA WATU WAZANZIBAR WATAIKATAA HIYO KATIBA SI NDIVYO CCM INAVYOTAKA HIVYO ILI IENDELEE KUTAWALA KWA KUTUMIA KATIBA KONGWE. NA KAMA HIVYO NDIVYO JEE KUNA HATUA ZOZOTE ZILE AMBAZO ZIMEEKWA KISHHERIA KAMA VILE KUA NA SERIKALI YA MPITO AU ILIYOPO KUJIUZULU MPAKA IPATIKANE KATIBA MPYA? KAMA HAYO HAYAPO BASI INA MAANA CCM IENDELEE KUTAWALA TU MPAKA HUO MWAKA KATIBA ITAKAPOPATIKANA. MIMI KWA AKILI ZANGU FINYU NAHISI KUA HUU MCHAKATO NI MTEGO WA KUIFANYA CCM IENDELEE KUTAWALA MAANA WANAJUA FIKA KUA WAZANZIBARI KATIBA YAO WANAYOTAKA KUITUNGA HAWAITAKI. WANCHOTAKA NI KUA NA SERIKALI MBILI ZILIZOUNGANA KIMKATABA BILA YA HIVYO HAKUNA LIWALO.

 4. Juma tunakujua hapo nyuma ulifanyakazi kubwa ya kueneza Chuki za Uunguja na Upemba. Tunakumbuka ulipohamia Pemba ukitoa taarifa za Uongo wakati wa fujo za Pemba wakati wa Uandikishaji kwa ajili ya Uchaguzi wa 2005. Sasa kwamba Zanzibar imetengamaa tubajua huna la kuadika tena! Wakati huu ingekuwa bora utulie na kama unapesa wende shule ili elimu yako inongezeke kwa kuwa siku za kumsifu mtu upate kula zimeisha!

  • Ninachoomba mimi ni kuwa watu wapewe hoja na si JZABA nina wasi wasi sana na kusini Pemba kuwa zoezi litaenda kwa salama hasa kwa vile watu wa huko wameumizwa zaidi na huu ukoloni uitwao MUUNGANO. Nawaomba UAMSHO na kila mwenye mdomo huko PEMBA awambie tume ikja wasiseme chochote zaidi ya yale ya kutaka ZANZIBAR HURU TU. Nawaomba sana wawe na SUBRA Hapa si pahala pa kulalamika tulifanywa hivi tukafanywa vile. bali ni pahala pa kusema
   1. TUNATAKA ZANZIBAR YENYEMAMLAKA KAMILI YENYE KUTAMBULIKA NDANI NA
   NJE
   2. TUNAKA RAIS MWENYE HADHI YA KUTAMBULIKA KIMATAIFA
   3. TUNATAKA ZANZIBAR IREJESHEWE KITI CHAKE UMOJA WA MATAIFA KAMA ILVYOKUWA
   4. TUNATAKA RASILIMALI ZA ZANZIBAR ZOOOOTE ZITUMIKE KWA MANUFAA YA
   ZANZIBAR NA WALA SI KWA KUGAWANA.
   5. UHURU WA KUABUDU UHESHIMIWE KIVITENDO KWA KURUHUSIWA WATU
   KUHUBIRI NA KUTANGAZA DINI ZAO KADIRI WAWEZAVYO BILA KUINGILIA MISINGI YA DINI NYENGINE.
   6. MAMLAKA YA NCHI YAENDELEE KUWA MIKONONI MWA RAIA
   7. UTAWLA BORA UPANULIWE HADI KWENYE MIKTABA IKIWEMO KUFUTA NA KUTORUHUS MKATABA WOWOTE BAINA YA SERIKALI NA DINI FULANI KIUCHUMI NA KIJAMII. IKIWA HIYO ITALAZIMIKA KUWEPO BASI IWE NI KWA DINI ZOTE.
   8. MAHAKAMA ZA KIDINI ZIENDESHWE KWA FEDHA ZA SERIKALI.

   AU MNAONAJE HAPO KAMA KUNA WALAKINI KWENYE MAONI YANGU NAOMBA
   NIWEKWE SAWA

 5. MM NAAMIN KUA KUNA MENGI YAMESEMWA KTKA KUTOA MAONI YA MUUNGANO AMBAYO YANAASHIRIA KUUPINGA MUUNGANO HUU DHALIM LKN KUTOKANA NA UNAFIKKI WA WAANDISHI WA HABARI NA KUA VIBARAKA HAWAYATOI….LKN TUNASEMA WOOTE KWA PAMOJA HATUTAKI MUUNGANOOOO.

 6. Nsikitika kuwa juu ya jitihada zote hizi za kutowa maoni, siku ya mwisho tutakuja kusikia kuwa muungano umehalalishwa, na kura inaipa haki muungano huo kuendelea kuwepo kwakuwa wananchi wengi wanautaka!! sasa kwangu mie kazi hii yote ni ya bure!! Tutakuja shuhudia, hoja subira tu!! kilichowafanya watu hawa kuleta fikra za kubadili katiba ni kuhalalisha muungano ambao kwa miaka umekaa katika khatari ya kuwa si halali!! na kwa kukhofia kuadhirika huko twendako wakaona hakuna njia ila kukubaliwe kubadilishwa katiba!! nasi tumenasa na kuingia demani wenyewe kwa tamaa. lakini tujuwe yakuwa huu ndio mwisho wetu Wazanzibari, hatuna pa kulilia!! Hebu natutizame ule umma wa Kizanzibari ambao haulali na kuamka kwa raha kwa kushiriki katika mikutano ya UAMSHO kwa kunadi kwa sauti kuu tena kwa jazba kuukataa muungano , iwe katika takwimu hizi wawe wachache kama inavyoonyesha hii leo katika takwimu zinazotolewa? hivyo tutarajie nini baada ya kumalizika Wazanzibari kutowa maoni yao?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s