Bajeti ya Afya yapita kwa tabu

Mwakilishi wa jimbo la Kitope Zanzibar, Makame Mshimba (kulia) akibadilishana mawazo na Mwakilishi wa jimbo la Dimani, Dk.Mwinyihaji Makame Mwadini nje ya umkumbi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wamepitisha bajeti ya wizara ya afya kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 baada ya kumbana waziri wa wizara hiyo Juma Duni aji kwa masaa kadhaa. Miongoni mwa hoja zilizomtoa jasho Waziri Duni ni kukithiri kwa uchafu katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, ukosefu wa wafanyakazi, upungufu wa dawa na wataalamu pamoja na utaratibu wa kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.

Wajumbe wa baraza akiwemo Makame Mshimba Mbarouk (CCM) Mbarouk Mussa Mtando (CCM) Salum Abdallah Hamad (CUF) na Ismail Jussa Ladhu (CUF) kwa nyakati tofauti walielezea kusikitishwa na hali ya uchafu uliokithiri pamoja na wagonjwa wengi kukosa nafasi ya kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu ambapo baadhi yao walisema kuna harufu ya rushwa.

Akijibu hoja hizo kabla ya kupitishwa kwa bajeti hiyo waziri wa wizara hiyo Juma Duni alijitetea na kusema kuwa hali ni afadhali kuliko siku zilizopita.

Alisema ili kuimrisha usafi katika hospitali za serikali na khasa hospitali kuu ya mnazi mmoja million 14 zinahitajika kila mwezi wakati kiasi hicho cha fedha ndicho kinachotengewa wizara yake kwa mwaka mzima.

“Nakubaliana na wajumbe kuhusu malalamiko yao juu ya uchafu lakini napenda wajue kwamba ni changamoto kubwa kutokana na uhaba wa fedha. Hata hivyo tumebahatika mwaka huu kuongezewa fungu la usafi hadi kufikia 89 milioni kwa mwaka”. alisema Duni.

Aliwataka wajumbe kufahamu hali halisi pamoja na kuomba wahisani wengine wajitokeze kusaidia kutoa misaada katika kuimarisha hospitali kuu ya mnazi mmoja.

Hata hivyo waziri huyo alilalamika kuwa pamoja na changamoto ya ukosefu wa fedha, wafanyakazi wa hospitali hiyo wanashindwa kubadilika tabia na kujenga utamaduni wa usafi.

Akizungumzia suala la kusafirisha kupelekwa nje waziri alisema hakuna rushwa yoyote inayochukuliwa na wahusika na wala hakuna upendeleo wowote kwa wagonjwa.

“Kinachotakiwa ni mtu kupeleka maombi ambayo yanaanzia kwa daktari na inapita kwa bodi ya madaktari hadi kwa mkurugenzi mkuu kabla ya kuidhinishwa na waziri” alieleza.

Alisema ngazi zote hizo ni lazima zithibitishe kwamba kuna haja ya mgonjwa kupelekwa nje lakini pia alisema changamoto iliyokuwepo ni uhaba wa fedha za kusafirishia wagonjwa.
Akijibu hoja ya ukosefu wa dawa na wataalamu Duni alisema tatizo hilo litamalizika au kupungua hivi karibuni kutokana na serikali pamoja na wafadhali kuahidi fedha zitakazosaidia.

“Serikali kupitia baraza la mapinduzi imeruhusu kuajiri wafanyakazi wa kada mbali mbali zaidi ya 500 ili kupunguza tatizo la uhaba wafanyakazi wakiwemo madaktari” aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo.

Duni aliwaahidi wajumbe hao kwamba hivi sasa kuna mpango maalumu wa kuahiza dawa kutoka nje ya nchi ili kupunguza tatizo la ukosefu wa dawa mahospitalini.

Nishati kudhibitiwa

SERIKALI ya Zanzibar inakusudia kuanzisha mamlaka yake ya kuzuwia udhibiti wa nishati na maji Zanzibar. Waziri wa maji, ardhi, makaazi na nishati, Ramadhani Abdallah Shaaban alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake ya mwaka wa fedha wa 2012/2013 ndani ya kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea mjini hapa.

Alisema tayari utayarishaji wa sheria hiyo umeanza sambamba na sheria ya usimamiaji na usambazaji wa mafuta na petrol Zanzibar (Zanzibar Petroleum Supply Act).

“Mheshimiwa Spika kwa ajili ya kutekeleza sera ya nishati Zanzibar, wizara inaendelea kujiandaa ikiwa pamoja na kuendeleza wafanyakazi katika sekta ya nishati na mafuta” alisema wakati akiwasilisha bajeti hiyo kwa wajumbe.

Aliwaambia wajumbe juhudi za kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa idara hiyo unalenga kukabiliana na upungufu wa wataalmu wa fani ya nidhati ikiwemo utafutaji na uchimbaji wa mafuta Zanzibar.

Aidha waziri alisema wizara yake kwa kushirikiana na serikali ya Norway inafanya mpango wa kufanya semina na kongamano zenye lengo la kutoa taaluma kuhusu athari za kimazingira zinazotokana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta Zanzibar.

Kuhusu tathmini ya kimazingira itokanayo na muelekeo wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, waziri alisema katika visiwa vya Unguja na Pemba ni suala muhimu na ambalo linatiliwa maanani.

Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha unaoanza, wizara yake pia imepanga malengo ya kuendelea na juhudi za kuwapatia wananchi wa Zanzibar elimu juu ya matumizi ya nishati.

Shaabani alisema kuwa uiamarishaji wa njia za kusambaza umeme, mradi wa usambazaji umeme vijijini, na mradi wa ufungaji mita 10,000 za tukuza ni miongoni mwa miradi iliyopangwa kutekelezwa mwaka huu.

                                                                                      Wahimizwa kuwa na nidhamu

WIZARA Ya Afya imeeleza kuwa wingi wa wagonjwa na ukosefu wa vitendea kazi ni miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya madaktari kuwa na hasira na kuacha maadili yao ya kazi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Dk Sirra Ubwa Mamboya wakati akijibu hoja ya baadhi ya wajumbe waliolalamikia kuendelea kuwepo kwa ukosefu wa nidhamu katika hospitali mbali mbali Zanzibar.

Dk Sirra alisema pamoja na wingi wa kazi na ukosefu wa vitendea kazi lakini wafanyakazi wa hospitali wanapaswa kuzingatia maadili ya kuwahudumia wagonjwa kwa lugha nzuri pamoja na kuwapatia msaada watu wanaokwenda hospitalini hapo.

“Madaktari na wauguzi wanafanya kazi kubwa katika hospitali za umma lakini wanapokwenda katika hospitali binafsi hubadilika tabia kwa sababu katika hospitali hizo huwahudumia wagonjwa wa chache” alisema Dk Sirra.

Aliwaeleza wajumbe kwamba asilimia kubwa ya wafanyakazi hasa madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za umma ndio hao hao wanaofanya kazi katika hospitali binafsi  ambapo wagonjwa hupata makaribisho mazuri zaidi.

“Kuanzia sasa naomba wafanyakazi wote hospitali za serikali kuzingatia maadili yao na tutafuatilia kwa karibu ili kubaini wale ambao wanakwenda kinyume na taratibu za kazi alisema” Dk Sirra.

Katika kukabiliana na tatizo hilo Dk Sirra alisema uongozi wa juu wa wizara yake utatoa namba za simu zao za mkononi ili wananchi wapate fursa za kuripoti matatizo yote yanayojitokeza likiwemo suala la utovu wa nidhamu wanaofanyiwa wagonjwa hospitalini hapo.

“Simu zetu hivi sasa zipo wazi na tunaomba mashirikiano na wananchi wote pamoja na wagonjwa kwa hivyo akiona ametendewa jambo hakuridhika basi asisite kutupigia simu” alisisitiza Naibu Waziri huyo.

Akizungumzia suala la maslahi bora kwa wafanyakazi na madaktari Dk Sirra aliahidi kuwa maslahi yao yanaendelea kushughulikiwa ikiwemo kuwalipa posho la muda wa ziara pamoja na wakati wa dharura.

Alisema mipango yote imeshakamilika ikiwemo suala suala la kuzungumza na wizara ya fedha na uchumi ili posho wanaostahiki madaktari walipwe jambo ambalo pia litasaidia kupunguza wataalamu hao kutorokea nje ya Zanzibar.

Mapema wakichangia hutuba ya makadirio ya wizara hiyo wajumbe wa baraza la wawakilishi walisikitishwa na huduma mbovu zinazotolewa katika hospitali za serikali na kutaka suala hilo kushughulikiwa kwa haraka ili kuondosha usumbufu wa wananchi.

Wajumbe wataka kuboresha maslahi ya madaktari
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali kuboresha maslahi ya madaktari nchini kuwa bora ili kuepuka wafanyakazi hao kukimbia nchini.

Hayo yameelezwa wajumbe mbali mbali katika kikao cha baraza la wawakilishi walipokuwa wakichangia hutuba ya makadirio ya wizara ya afya kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.

Miongoni mwa wajumbe waliochangia hutuba hiyo ni Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM) Asha Bakari Makame, Abdallah Juma Abdallah Mwakilishi wa jimbo la Chonga (CUF).

Wengine waliochangia hutuba hiyo ni Mwakilishi wa jimbo la Mpendae (CCM) Mohammed Said Mohammed na mwakilishi wa jimbo la ChakeChake (CUF) Omar Ali Shehe ambao kwa moja waliiomba serikali kutizama upya maslahi ya wafanyakazi wa hospitali ili kuepusha kutoroka na kutafuta maslahi zaidi.

Mohammed sababu kubwa ya madaktari wenye sifa kukimbilia nje ya Zanzibar ni kufuata maslahi bora hivyo serikali haina budi kuongeza mishahaara na posho ambazo zimekuwa zikitadawa na wafanyakazi hao wa afya.

“Mheshimiwa Spika maslahi ya watumishi wa Wizara ya Afya ikiwemo madaktari wetu bado inawavunja moyo kwa hivyo licha ya serikali kusema haina fedha za kutosha kada ya madaktari ni muhimu kuzingatiwa” alisema Mohammed.

Alisema utafiti mdogo unaonesha kwamba asilimia 50% ya madaktari pamoja na watumishi wengine wa Wizara ya Afya hukimbia nchini na kutafuta maslahi bora nchi za nje.

Mwakilishi huyo alisema hali hiyo isipodhibitiwa basi italiingiza taifa katika hasara kubwa, kutokana na gharama kubwa za kusomesha madaktari ambazo waziri ameeleza katika kitabu chake kwamba atatumia zaidi ya milioni 70.

Mwakilishi Asha Bakari Makame ameitaka serikali kuwadhibiti madaktari pamoja na wauguzi wanaopelekwa nje kwa ajili ya masomo ya juu kuepuka tatizo la kukimbia kwa kutayarisha mikataba.

Alisema baadhi ya maeneo ikiwemo kisiwa cha Pemba kinakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa madaktari kutokana na kujitokeza wimbi la madaktari kukimbilia nje wanapomaliza masomo kutokana maslahi duni.

“Ni lazima serikali itafute njia ya kuwadhibiti madaktari pamoja na wauguzi wanaomaliza masomo yao kuhakikisha kwamba wanaitumikia serikali kabla kwenda kutafuta ajira kwengine” alisema mwakilishi huyo.

Aidha Mwakilishi wa Chonga alisema wakati serikali inatumia fedha nyingi kuwasomesha madaktari haina budi pia kutafuta njia ya kuhakikisha kwamba wanatumikia wananchi kwa muda maalumu.

Pia alishauri kuwa madaktari wabaki katika taaluma zao badala ya kupewa nyadhifa za kisiasa au kiutawala ambapo badhi ya madaktari wazuri na manesi wanapewa kazi za ukurugenzi na ukatibu mkuu.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Chake Chake alliitaka serikali kuhakikisha kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) kinajengwa ili kuondosha usumbufu uliopo kwa wagonjwa ikiwemo kutafuta huduma hizo Dar es salaam.

Shehe pia alisema ICU ni muhimu kwa kisiwa cha Pemba ambako kwa miaka mingini hakujawahi kuwa na kitendo hicho na kwamba serikali ina uwezo wa kuimarisha huduma muhimu za afya Unguja na Pemba.

“Mheshimiwa Spika ni tatizo kubwa tulilonalo kwa upande wa Pemba kutokuwa na ICU kwa sababu ukiwa na mgonjwa mahututi halafu umsafirishe kwa boti umlete Unguja kwa kweli ni mtihani mkubwa” alisema mwakilishi huyo.

                                                                                       Rais ruhsa kuishi kwake

RAIS na viongozi wengine wa serikali wapo huru kuishi katika nyumba zao binafsi badala ya zile wanazopangiwa na serikali kwa kuwa hakuna sheria inayowakataza kufanya hivyo. Hayo yalielezwa na waziri wa nchi ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk Mwinyihaji Makame Mwadini wakati akijibu masuali kutoka kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi.

Alisema kimsing viongozi wa juu akiwemo rais hupangiwa nyumba za kuishi na serikali lakini kila mmoja halazimiki kuishi katika nyumba alizopangiwa.

“Hivi sasa nyumba rasmi ya rais wa Zanzibar ni migombani pia makamo wake wawili wana nyumba ambazo serikali imewatengea lakini kila mara wanakwenda katika nyumba zao binafsi jambo ambalo sio kosa kisheria” aliwaambia wajumbe hao.

Baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi walihoji serikali kutumia fedha za walipa kodi katika kutengeneza nyumba binfasi za viongozi.

Hata hivyo waziri alikanusha kuwa hakuna fedha za serikali zinazotumika kutengeneza nyumba za viongozi wa juu isipokuwa baadhi ya vifaa vya kiusalama ndivyo vinavyotumika iwapo rais atataka kuishi katika nyumba yake binafsi.

Wajumbe waliouliza suali hilo ni pamoja na Asha Bakari Makame, Jaku Hashim Ayoub na Mbarouk Wadi Mussa  ambao wote kutoka chama cha CCM ambao walionesha wasiwasi kuwa fedha za serikali zinatumika vibaya.

Waziri alisema viongozi wa serikali pamoja na mawaziri hupewa nyumba maalumu za kuishi na kuwataka wajumbe wa baraza hilo kuondokana na dhana kwamba fedha a serikali zinatumika vibaya kwa kuimarisha nyumba za viongozi wa juu.

“Sio vibaya kwa kiongozi wan chi kuishi katika nyumba yake binfsi kwa sababu ndivyo ilivyo katika nchi mbali mbali kuwa rais pia ni binaadamu na anahitaji kuwa huru baadhi ya nyakati” alisisitiza waziri.

Makame alisema viongozi mbali mbali duniani akiwemo rais wa Marekani kila mwishoni mwa wiki huenda katika nyumbani yake binafsi.

Rais wa awamu ya sita Dk Amani Karume alikataa kukaa katika nyumba ya serikali na kuamua kuishi katika nyumba yake Mbweni katika muda wake wa uarais uliomalizika mwaka wa 2010.

Wananchi wa Tumbatu wanapata maji safi

WANANCHI wa Kisiwa cha Tumbati wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama baada ya bomba la kupeleka maji katika kisiwa hicho kupasuka.

Naibu waziri wa maji, makaazi nishati na ardhi, Haji Mwadini Makame alisema kwa muda mrefu wananchi wa kisiwa hicho hawapati maji lakini juhudi za hivi karibuni zinaelekea kumaliza tatizo hilo.

“Kumekuwepo na uhaba wa maji katika kisiwa cha Tumbatu kutokana na uzalishaji wa maji kupungua lakini ilitokana na bomba linalopita chini ya bahari kupasuka” alisema Mwadini wakati akijibu suali la mwakilishi wa nafasi za wanawake, Panya Ali Abdallah.

Mwakilishi huyo alisema wananchi wa Tumbatu na baadhi ya maeneo ya Mkokotoni wamekuwa wakiishi katika maisha magumu kutokana na kipindi kirefu cha ukosefu wa maji na kuitaka serikali ichukue hatua za haraka.

Mwakilishi katika suali lake la msingi alitaka kujuwa kwa nini wananchi wa kijiji cha Mkokotoni na Tumbatu wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama huku serikali ikiwa imekawia kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Akijibu suali hilo Mwadini alikiri kwamba wananchi wa kisiwa hicho walikuwa wakikabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji safi na kuwaomba wananchi hao kuvuta subira wakati serikali yao ikijitahidi kulidhughulikia suala hilo.

“Mheshimiwa Spika nataka kumwambia mwakilishi kwamba tatizo la maji safi lililokuwa likiwakabili wananchi wa kisiwa cha Tumbatu kwa sasa limepatiwa ufumbuzi wake baada ya kufanyika kwa matengenezo muhimu”alisema Mwadini.

Mwadini alisema juhudi kubwa zilichukuliwa kwa mafundi wa mamlaka ya maji safi na salama ZAWA katika kulifanyia matengenezo bomba hilo ambalo lilikuwa likiingiza maji ya chumvi.

Mapema Mwadini alisema wizara imekuwa ikichukuwa juhudi mbali mbali kuhakikisha kwamba tatizo la maji safi na salama linapatiwa ufumbuzi wake katika vijiji hivyo viliopo mkoa wa kaskazini Unguja.

Alizitaja juhudi hizo ikiwemo kazi za kuchimba visima zaidi vitakavyokuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha kiwango kikubwa cha maji kitakachotosheleza mahitaji ya wananchi.

Alisema wizara ipo katika mikakati ya kuchimba visima zaidi vitakavyozalisha kiwango kikubwa cha maji safi na salama kwa mahitaji ya wananchi na hivyo kuwaomba wajumbe wa baraza hilo kuwa na subira na kuwapa elimu wananchi juu ya juhudi za serikali katika suala hilo.

Marufuku mifugo kuzurura ovyo

WAFUGANI na na wavuvi wametakiwa kutunza mifugo yao na kuacha tabia ya kuiacha kuzurura ovyo na kuingia katika  mashamba ya wakulima na kusababisha uharibifu mkubwa.

Waziri wa mifugo na uvuvi, Abdillahi Jihadi Hassan wakati akijibu swali lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la Kojani (CUF) Hassan Hamad Omar aliyetaka kujuwa juhudi zinazochukuliwa kuwaelimisha wafugaji kuharibu mashamba ya wakulima.

Akijibu suali hilo, Jihadi alikiri kuwpeo kwa tatizo hilo kubwa linalotokana na wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kusababisha migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji.

Alisema serikali inafahamu tatizo la wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima ambapo elimu zaidi juu ya suala hilo imeanza kutolewa ili kudhibiti tatizo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linachochea migogoro na ugomvi kati ya wakulima na wafugaji.

Waziri huyo akitoa mfano ya matatizo ya kama hayo alisema matatizo ya wafugaji kuharibu mashamba ya wakulima yanatatuliwa katika hatua za awali kupitia masheha na wakuu wa vijiji ambapo baadhi ya sehemu tayari migogoro hiyo imeana kutatuliwa.

Alisema baadhi ya migogoro imeweka kutatuliwa lakini migogoro mengine inaposhindikana kutatuliwa na masheha, basi hupelekwa katika vyombo vya sheria ikiwemo mahakamani.

Hata hivyo Jihadi alisema kwamba kuanzia sasa wizara yake imekuwa ikitoa elimu zaidi kwa wafugaji kuhakikisha kwamba wanamiliki idadi fulani ya mifugo ambayo watakuwa na uwezo wa kuiendesha.

Alisema wapo wafugaji wanashindwa kumiliki mifugo yao kutokana na idadi kubwa na hivyo kuiacha ikizurura ovyo na kuingia katika mashamba ya wakulima.

“Wizara imeanza kutoa elimu kwa wafugaji kuhakikisha kwamba wanamiliki idadi kamili ya wafugaji waliokuwa nao ili kuepuka kuzurura ovyo na kuingia katika mashamba ya wakulima lakini baadhi ya wakulima na wafugaji huwa wanaelewana na baadhi yao wanakwenda kushitakiana” alisema waziri.

Advertisements

4 responses to “Bajeti ya Afya yapita kwa tabu

 1. Hii ya Hospital kulalamikiwa ni suala lisiloepukika. Waheshimiwa mngefikiria njia bora ya kendesha sekta ya afya kwa hii ya sasa haitoshi kufanya sejta hii iwe endelevu! Watu wengi mkiwemo nyingi Waheshimiwa inabidi mbadilike muamini kuwa matibabu na kundesha sekta ya matibabu ni gharama. Kila mtu utakia akisema ” Mzee wetu Marehemu Karume alifanya matibabu kuwe bure na sasa nyinyi mnabadilisha alivyofanya”. Hii ni sawa pengine marehemu alifanya hivyo kulingana na wakkati na uwezo aliokuwa nao siku hizo. Wakati huu tukifikiria namna ya kufanya ndani ya bajeti finyu mambo haya yanawza kusaidia.

  1. Kubinafsisha Shughuli za Usafi hospital ya Mnazi moja. Hii inawezekana kwa kuanzisha Kampuni na wenye hisa wawe watumishi waliojiriwa kwa kazi hii. Watu hawa wapewe seed money kama grant au mkopo kisha waachwe wafanye kazi
  2. Zanzibar ifikirie kuanzisha Bima ya Afya kwa watu wake wote. Iwe ni mandatory kwa kila ukoo. Namna na kiwango cha kulipa kiwe kufatana na uwezo wa mlipaji. Kwa kuwa makusanyo yatakuwa mengi na si kila mwenye bima ataumwa Serikali itaweza kupunguza mzigo wa matatibabu
  3. Wizara ya Afya ipunguze Support staff na iajiri madaktari na Specialists. Hali ilivyo sasa pale Mnazi moja ni vice versa. Watu hawa watakaopunguzwa waambiwe wachague kazi waiwezayo kama kundi kisha wapewe kuifanya kwa mkataba kulingana ukubwa wa kazi.
  4. Ufatiliaji uwepo kupunguza overhead expenses. Wizarani na majengo mengine siajabu kuona feni zikiwaka na vyumbani hamna watu

 2. Huduma za afya zitalalamikiwa tu kwani hazikidhi haja ya wahudumiwa. Hili linatokana na ukosefu wa mipango madhubuti ya baadhi ya watendaji wakuu wa hospitali zetu, pamoja na idara husika katika wizara yako. Leo hii hakuna mpango wa wizara kuhusu wafanyakazi wa mahospital. Wafanyakazi wanastaafu na wengine hufariki bila ya kupatiwa replacement. Uteuzi wa watendaji wakuu wa hospital bila ya kuzingatia sifa na utendaji wa muhusika. Hivi tujiulize kuna mtendaji kapewa uongo katika hospital moja kashindwa. Kahamishiwa hospitali nyengine vivile kashindwa na aliachishwa uongozi. Sasa mtendaji huyu huyu wamrejesha katika utendaji mkuu hapo si unakaribisha maovu yatendeke. Tuwacheni mambo ya kijomba jomba katika kazi. Kupunguza hili ni vema kuondowa muhali katika watendaji wako. Vile kutowa tenda kwa watu binafsi kwa kazi maalumu kama vile shughuli za usafi. Katika kisiwa cha pemba wafanyakazi wako hawataki kufanyakazi Pemba. Nivema ukafanya motivation kwa wafanyakazi wanakubali kufanyakazi Pemba wajaalie posho iwe ni motisha. Vile vile jitahidi kufanyia ukarabati vifaa vya uchunguzi hasa mashine za x ray ambapo kwa sasa huduma ya x ray Pemba inasusuwa na hichi ni kipindi cha uchumaji karafuu. Muheshimiwa jitahidi jitahidi sana wizara ya Afya ndio uti wa mgongo wa raia. Fanya mipango mkakati wa hospital health worker plan.

 3. majambazi wa serikali wakishauriana jinsi gani ya kuwanyonya wananchi kificho ficho ( sio spika )

 4. kwa nini msiwapunguzie marupurupu na mishahara wawakilishi , mawaziri , rais na wengineo wakubwa ili fedha hizo zitumike kwenye afya? badala ya kutegemea wafadhili? si tulitaka tujitawale sasa hawa wafadhili wa nini tena? tujitegemee , tupunguze gharama kwenye mambo ya anasa au wizara za anasa kama michezo na utamaduni , tupunguze viongozi wa serikali, ktk ofisi ya rais , makamu wa rais kuna waziri wa nchi huyu ni wa nini? nchi yenyewe idadi ya watu hawazidi milioni mbili lakini viongozi ni wengi mno , hii akili ya kuwa na serikali kuuuubwaaaaa wakati nchi ( au mji vile ?) yenyewe ni ndogo. Ulaji ulaji tu SMZ ( serikali ya majambazi zanzibar)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s