Chunga unaposikia CCM inalia rafu

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza kwa makini Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja alipozungumza nao kuhusiana na Kikundi cha Watu kinachotaka kuharibu mchakato mzima wa kukusanya maoni ya katiba mpya unaoendea hivi sasa katika Mkoa huo

Jabir Idrissa.

LEO nimeguswa na mambo mawili – malalamiko ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba kinahujumiwa katika utoaji wa maoni ya Katiba mpya ya Jamhuri, na kauli ya SMZ kuhusu vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi. Mawazoni mwangu, suala la vitambulisho ndio nilikusudia litawale mada wiki hii. Malalamiko ya CCM yaliibuka katikati na ni vema nikayashughulikia kabla ya kupoa.

Kwa umuhimu wake, nitaanza na malalamiko haya. Nikitumia uzoefu wa utendaji katika siasa za Zanzibar , nina kila sababu ya kusema ukiona chama hiki kinalalamika hadharani kuhujumiwa, ujue kimezidiwa kete.

Wakati mwingine unaposikia kelele za viongozi wake, hwenda ni dalili za mkakati wake chenyewe kugonga mwamba. Hebu sikiliza anachosema Katibu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Zainab Khamis Shomari: “Kuna jina la Said Mwema limejitokeza katika barua na baada ya barua hizo, Tume ilitaka kumjua huyo mtu mwenye jina hilo la Said Mwema lakini matokeo yake hakuna aliyejitokeza.

“Kwa hivyo sisi tuna shaka na hao watu wanaokwenda kupeleka maoni kwa njia ya barua tukiamini kuwa zinaandaliwa na baadhi ya wanasiasa.”

Zainab aliyewahi kuwa naibu waziri wakati wa serikali ya Amani Abeid Karume (2000-2010), anasema vitendo vingine “vibaya” ni watu kuzomea watoa maoni pamoja na kutumia wanafunzi kutoa maoni baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa walimu.

Kwa namna nilivyokuwa nikisikia chama hiki kinajiandaa kwa ajili ya utoaji maoni ya katiba, malalamiko haya ni mzaha. Kwani wakuu wa tume wako wapi wasiyaone?

Huyu hakutaja kamwe tukio la kuhusishwa waziri kutoka CCM, na kuandika barua na kuigawa kwa wanachama wengi wa CCM ili yaliyomo ndiyo yawe maoni yao kwa tume.
Ilikuwa bahati tu, baadhi ya waliopewa barua hiyo, waliifichua kwa kumtaja waziri aliyewapa na hatimaye wakaikabidhi Tume.

Mwaka 1995, Ali Ameir Mohamed, akiwa naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar , alijitokeza mbele kulalamikia matokeo ya uchaguzi hata kabla hayajatangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya mwenyekiti Zubeir Juma Mzee.

Ameir ambaye pia alikuwa mbunge wa Donge na waziri wa mambo ya ndani, baada ya kutuhumu watendaji wa tume kuwa walishirikiana na upinzani, alihitimisha lawama zake kwa kusema hawakubaliani na matokeo yatakayotangazwa.

Wakati huo, sisi waandishi wachokonozi tulikuwa na taarifa imara kuwa mawakala wa ulinzi na usalama walikuwa wanavuruga kura, ili kuhakikisha mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma, anatangazwa mshindi.

Ndivyo ilivyokuwa. Mzee wa watu, Zubeir, aliingia kwenye ukumbi mdogo wa tume, akiwa ‘amebanwa’ kila pembe na mabunduki katika mbinu ya kumlazimisha kusoma matokeo anayoamini hasa ni haramu.

Waandishi tulisukumwasukumwa na wanausalama waliojaza silaha za dhahiri na walizozificha viunoni, na wengi wao ndio wakapata nafasi ya kuingia ukumbini.

Kweli, mzee yule akatangaza matokeo haramu yaliyompa Dk. Salmin ushindi mwembamba ambao mwenyewe alikiri na kuuita, “ushindi ni ushindi tu hata ukiwa wa goli moja,” alipokutana na waandishi wa habari pale Bosnia , Kikwajuni.

Mara tu matokeo hayo yalipotangazwa, CCM ikiwa imepata asilimia 50.2 dhidi ya asilimia 49 za Maalim Seif Shariff Hamad, Ali Ameir Mohamed alitimka mbio mpaka ofisini kwake Kisiwandui. Tulipomfuata, kumuuliza kama amebadili kauli, alisema, “Mngekuwa nyinyi mngefanyaje.”

Maana yake alitaka tufahamu ushindi katika uchaguzi kwenye nchi za Afrika, si lazima upatikane kwa njia za haki. Hata maguvu yakitumika si tatizo. Bado serikali zote mbili zinahaki ya kujinasibu zinafuata misingi ya utawala bora na utawala wa sheria.

Mara zote CCM walipolalamika kuhujumiwa, matokeo ya mwisho yalionyesha walipata walichokitaka, hata kama ni kwa kujeruhi wananchi na kuvuruga taratibu za uendeshaji mambo kisheria.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, 2010, mambo yalikuwa hivyohivyo – uvurugaji taratibu na mwisho, CCM ikatangazwa mshindi wa kila kitu, urais na viti vingi katika Baraza la Wawakilishi.

Hiyo ndiyo CCM – Unachukua, Unaweka, Waaa (UUWA). Kwa Zanzibar, mbali na kaulimbiu hiyo wananchi wamezoea kusikia “Mapinduziiii Daima.”

Wala viongozi wake hawajali kama wanayoyafanya ni aibu mbele ya umma na ulimwengu. Hawajali chochote maana wao “ndio” mamlaka ya nchi.

Nyakati za uandikishaji wapiga kura na upigaji kura, viongozi wa CCM walipolalamika, basi maji yalikuwa yamewafika shingoni katika kusimamia mikakati ya kuhujumu taratibu. Lakini pia walikuwa wakizuga tu umma uamini eti hawatendewi haki.

Angalieni, kipindi chote hiki ambapo wananchi wamekuwa wakilalamika kubaguliwa katika taratibu za kupata kitambulisho cha Mzanzibari, siyo tu kwamba hakuna kiongozi yeyote wa CCM anayewasikiliza, bali wanawapinga na kuwabeza eti wanatumiwa na wanasiasa.

Viongozi kadhaa wa chama hiki wanasema hakuna tatizo lolote katika upatikanaji wa kitambulisho, labda kwa yule mwananchi ambaye hana sifa za kupewa kitambulisho.

Ule mtandao imara wa kubagua watu wanaohisiwa si wapenzi wa CCM, wanaujua vizuri viongozi hawa; na vile ulivyonyonga haki ya kuchagua 2005 na 2010.

Masheha wote ni watiifu wakuu kwa viongozi wa CCM wa ngazi zote, chini mpaka juu mwisho. Wakielekezwa chochote wanatekeleza hata bila ya kuuliza kama wanachotenda ni haki kisheria na kiutu.

Hata pale Maalim Seif, ambaye tangu Novemba 2010 amekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, alipolalamikia ukorofi wa masheha wa kuzuia wananchi kupata kitambulisho, alionekana kinyago. Viongozi wa CCM hawakujali.

Ni desturi kwa viongozi wa CCM kutojali kitu kwa malalamiko ya watu ambayo kwao, yanachojaribu kufanya, ni kuwasumbua tu. Wanaamini hata watu wakilalamika vipi, hakuna kitakachobadilika.

Ni bahati mbaya sana wakati viongozi wa chama cha siasa wakipuuza na kuchekelea malalamiko ya wananchi kunyimwa haki za kiraia, ikiwemo hii ya kupata kitambulisho, watendaji wa taasisi za serikali, wanaopaswa kuwasaidia kupata haki hiyo, nao hawajali.

Ndio maana wakati malalamiko ya wananchi yanaongezeka kila siku ipitayo kuwa wanakwamishwa kupata idhini ya masheha ya kupata kitambulisho, kunatoka takwimu za kulaghai ulimwengu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, analiambia Baraza la Wawakilishi vitambulisho 112,420 vipo ofisini havijachukuliwa na wenyewe.

Takwimu hizi amepewa na Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambayo, pamoja na jitihada zote za kujieleza kama taasisi inayotii sheria na katiba, haijajivua na lawama za kuchangia sana kunyonga haki za raia katika suala hilo .

Takwimu hizi zinatolewa huku mkuu wa idara hii, Mohamed Juma Ame, akijua fika kuwa mpaka leo hajakubali rai tuliyompa baadhi yetu, ya kutangaza majina ya wenye vitambulisho hivyo ili kuangalia kama wapo kweli. Hapana shaka, anajua yeye kwanini hili ni gumu mno kwake kutekeleza.

Advertisements

11 responses to “Chunga unaposikia CCM inalia rafu

 1. hawa CCM hawafahamiki wana lala mika nin kwani haya maoni ya vyama vya siasa or ya WAZANZIBARIA kutaka mungano wa mustakabal upi? me ninavyojua tume ya maoni ni ya sirikali na sirikali ni watu si chama,sasa hawa ccm wameingiangiaje na malala miko? kama kuna matatizo tume ndo ya kulalamika na sio ccm.CCM wameshazoea kuburuza buruza watu ,lakini watu wamesha choka sasa kuburuzwa,nyinyi CCM kaeni pembeni muangalie hilipira litaishiaje kwani hu siouchaguzi wa vyama vya siasa, yachieni tume ipumue na kazi zake kwa uhuru.CCM acheni kimbelembele hi nchi si ya ccm bali ni ya WAZANZIBAR.

 2. Nimetishika na makala hii imenifanya niuchukie mchakato wa katiba mpya kuwa hautakuwa wa haki na wala hauna nia ya kuipa zanzibar inachokitaka katika muungano, lo!

 3. KATIKA SUALA HILI LA KATIBA BADO MIMI NAONA KUNA NAMNA FULANI YA USANII UNAOFANYWA NA CCM NA SERIKALI ZAKE ZOTE MBILI. NASEMA HIVI KWA SABABU KWANZA HIYO SHERIA YA KATIBA YENYEWE INA UTATA KWA KUKOSA MAMBO YA MSINGI SANA. INAVYOONEKANA NI KUA CCM TAYARI IMEJIPANGA KUPITISHA KATIBA WANAYOITAKA WAO KWA HALI YOYOTE ILE AU HAWATAKI KUPITISHA HIYO KATIBA KABISA.IKIWA KATIBA WANANCHI WATAIKATAA KATIKA KURA YA MAONI JEE KWA WAKATI HUO AMBAO ITAKUA NI KARIBU YA UCHAGUZI WA 2015 JEE UCHAGUZI HUO UTAAGHIRISHWA AU TUTAINGIA KATIKA UCHAGUZI KWA KUTUMIA KATIBA KONGWE? HAPA CCM NA SERIKALI YAKE ITUPE JIBU KWANI INAONYESHA WAZI KUA HAWANA NIA NJEMA ILA NI USANII TU ULIMWENGU UONE KAMA VILE CCM WANA NIA YA KATIBA MPYA LAKINI WANANCHI HAWAITAKI.MAMBO YOTE HAYA YANAWEZA TU KUKAA SAWA IWAPO KUNA NIA NJEMA KATIKA MCHAKATO HUU WA KATIBA AMBAYO KWA SASA HAIPO. HII INGEWEZEKANA KWA KUWAULIZA WANANCHI KAMA MUUNGANO WANAUTAKA AU LA? NA BAADA YA HAPO IKAUNDWA TUME YA WATAALAMU KUKUSANYA MAONI NA KUANDIKA KATIBA MPYA. MCHAKATO HUU UNAOENDELEA NI WA WIZI MTUPU NA HAUNA NIA YA KULETA KATIBA MPYA TANZANIA KWA SABABU CCM IMEKOSA NIA THABIT KATIKA HILI NA NDIO MAANA MPAKA LEO WATU WANANYIMWA VITAMBULISHO, MARA WANADAI KUA WANACHEZEWA RAFU NA MAMBO MENGINE. CCM WANA HAKIKA KUA WAZANZIBARI HAWAUTAKI MUUNGANO NA BAADAE WATAIKATAA HIYO KATIBA KWENYE KURA YA MAONI AMBAPO WAO WATAENDELEA NA KUTAWALA KWA NJIA ZA KUIBA KURA NA MATOKEO YA UCHAGUZI KWA KATIBA KONGWE AMBAYO INAHALALISHA MAMBO HAYO YA WIZI WA KURA NA MATOKEO YA UCHAGUZI KWA KUTUMIA VYOMBO VYA DOLA. BAADA YA KUTANGAZWA RAIS ATAKAA MADARAKANI NA KATIBA HAIRUHUSU KUHOJI NA AJIDAI NA YEYE KUTAKA KUANDIKA HIYO KATIBA ILIYOMSHINDA KIKWETE.
  WAZANZIBARI TUWE MAKINI TULIANGALIE HILI KWA MAKINI HAPA KUNA MCHEZO AMBAO UNATAKA KUCHEZWA NA VIONGOZI AMBAO WAO WANAJIONA KUA NA AKILI KULIKO WATANZANIA WOTE.

 4. me nawaomba waz’bari wenzangu tucwe na khofu, njia ya muongo fupi, inshallh dhamira yao haitafanikiwa.

 5. Pingback: Chunga unaposikia CCM inalia rafu·

 6. HATA VIOGOZI WALIOCHAGULIWA NA WANANCHI TUNAWASIKIA WAKITAMKA WAZIZI KAULI ZA KULINDA NA KUTETEA MUUNGANO HALI YA KUWA SS WANANCHI HATUUTAKI MUUNGANO HII NI DHAHIRI WAO WAPO KWA AJILI YA MUUNGANO NA SI WANANCHI. Lakini sisi tunasema fanyeni mufanyavyo muungano utavunjika ilivyokuwa sisi raia zenu hatuutaki. TUACHENI TUPUMUWE HATUUTAKI MUUNGANO.

 7. Jabir asishutumiwe kuwa “anaandika fitna na uchochezi” hii ndio hali haslisi. Yeye ansema yanayotokea na halazimishi mtu kukubali au kukataa maoni yake. Wanaodai “anaandika fitna” pengine hawajaona yanayotokea kwenye mikutano ya utoaji maoni kuhusu Katiba. Kule Ukongoroni kwa mfano, mtu anaesemekana kuwa ni Katibu wa CCM Tawi la Ukongoroni alisimamia utoaji wa maoni kwa wanaunga mkono Muungano huu ambao Rais na Mwenyekiti wa Chama Chake wa Taifa anaona unahitaji kufanyiwa marekebisho!

  Kijana huyu ambaye siku hiyo alivaa shati la rangi ya ndimu, rangi inayofanana na vazi la Chama Chake bila kujali kuwa kushawishi ni sehemu ya corruption aliwavuta kina mama kutoka majumbani na kisha akawasimamia waseme anayataka! Kijana huyu akiwa kama mwenye kupagawa alienda kuwatoa watoto katika madrasa na ingekuwa si kikwazo cha wakati minors hawa wangefumbiwa macho waseme meneo waliyotiliwa kwenye vichwa vyao! Hatujui kuwa Commissioners wangejifanya vipofu wasione hili ! Huu ni ukweli na ndio ulioambatana na utoaji wa maoni katika kijiji cha Ukongoroni. Jabir anavyoeleza haya na kaonaekana ni mkosa basi sijui kosa lake lipo wapi!

  Katika maeneo mengine tunaskia kuwa magari yalitumika kuwaleta watu kwenye mikutano ya kutoa maoni huku viongozi wa Chama wakisimia operation hii. Hadi leo sijafahamu ni kwa nini suala hili ambalo ni la Serikali linasimimiwa na vyama tena kwa nguvu zote! Ivo Sheha ambaye anatambulika hata na sheria hii ya Mchakato wa Katiba hatoshi kufanya kazi hii. Mwenyekiti wa CCM Mkoa na Katibu wake kuwa waangalizi na wasindikizaji wa Tume inatia mashaka mno!

  Jabir akieleza kuwa Chama kinafanya yasiostaki si fitna wala uchochezi ni ukweli ambao hata Makamishna wa TUME wanaukubali. Mara nyingi Kamisha moja kambla ya Mkutano husema ” Sisi hatufungamani na cHama chochote na kwamba Tume yetu ni huru.” Yanayoendelea katika utoaji wa maoni ni ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa utawala Bora kwa kuwa mipaka ya kiutendaji inakiukwa!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s