Munir Zakaria afutiwa cheo chake na ZFA

Rais wa Chama Cha Soka (ZFA) Amani Ibrahim Makungu (katikati) akizungumza na Afisa Habari Munir Zakaria (kulia) na Rais aliyestaafu Ali Fereji Tamim kushoto)

CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimemuengua Munir Zakaria kuwa Ofisa Habari na msemaji wake, pamoja na kumteua Suleiman Mahmoud Jabir, kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Abdallah Juma Mohammed kuwa Mwanasheria wa chama hicho. Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano wa kamati tendaji ya chama hicho uliofanyika juzi kwenye hoteli ya Zanzibar Ocean View, chini ya Mwenyekiti Amani Ibrahim Makungu ambaye ni Rais wa ZFA Taifa.

Katibu Mkuu wa ZFA Taifa Kassim Haji Salum, ameliambia gazeti hili kuwa, kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, msemaji wa mambo mbalimbali yanayokihusu ni Rais kwa kushauriana na Katibu Mkuu.

“Kwa mujibu wa katiba yetu, Rais ana nafasi nne za kufanya uteuzi wa watu wa kumsaidia kazi, lakini pia ndani ya katiba hiyo, hakuna nafasi ya Ofisa Habari, na kazi ya kukisemea ni ya Rais kwa kushirikiana na Katibu Mkuu”, alifafanua.

Hata hivyo, alisema Zakaria anabakia kuwa mjumbe wa kawaida wa kamati tendaji, hadi hapo itakapoamuliwa vyenginevyo.

“Hivi sasa, tunafanya kazi zetu kikatiba zaidi, na kufutwa kwa nafasi ya Ofisa Habari ni miongoni mwa utekelezaji wa katiba hiyo”, alisema.

Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa ZFA ilichukizwa na kauli ya Zakaria aliyoitoa katika vyombo vya habari, kwamba iwapo klabu za Simba na Azam FC zitaingia fainali ya mashindano ya Kombe la Urafiki, mchezo huo utahamishiwa jijini Dar es Salaaam, kauli iliyozusha malalamiko kutoka kwa mashabiki wengi wa soka wa Zanzibar.

Kwa upande mwengine, alizitaja kazi zitakazomuwajibikia Mkurugenzi wa Ufundi, kuwa ni kupanga programu za maendeleo ya mchezo wa soka kwa ajili ya timu za madaraja yote, kuanzia ngazi ya watoto hadi wachezaji wakubwa.

Aidha, Mkurugenzi huyo atakuwa na wajibu wa kuandaa mipango ya mafunzo (mtaala) kwa walimu wa soka, waamuzi pamoja na viongozi wa klabu mbalimbali.

Katibu huyo ameeleza kuwa, kazi zote zinazohusiana na mambo ya kisheria, sasa zitashughulikiwa na Mwanasheria aliyeteuliwa, Abdallah Juma Mohammed.

Advertisements

3 responses to “Munir Zakaria afutiwa cheo chake na ZFA

 1. Zanzibar tunataka soka sio majungu na tunataka uwanachama wa fifa na caf ukijumlisha yote hayo inabidi kwanza tuondoe muungano.

 2. Aslaam Aleykum ndugu zangu. Katika yote yanayotokea/endelea ndani ya ZFA, jambo moja limenifurahisha sana kwa sababu ninaamini litakuwa na matokeo mazuri – Uamuzi wa kumteua SULEIMAN MAHMOUD JABIR kwa nafasi ya MKURUNGENZI wa UFUNDI. Huu ni uamuzi mzuri na muafaka kwa wakati muafaka. Why? Kwa sababu huyu ni mtaalamu wa mpira, ni mtawala na kijana mwenye hamu na dhamira njema ya kuleta mabadiliko ili mchezo huu upige hatua.
  Na uteuzi wake ni mfano mzuri wa ni vipi sisi washiriki ktk michezo, tunavyotaka mambo yaendeshwe. Mtaalamu apewe kazi ya kitaalamu, apewe nafasi ya kutumia utaalamu alionao.
  SULEIMAN nakutakia wasaa mzuri, ufanye kazi yako vizuri na ALLAH atakusaidia kushinda mitihani ktk kazi yako hiyo m uhimu kwa maendeleo ya soka.
  Napenda kugusia hili la Msemaji wa ZFA. Silaumu au kulalamikia kuondoshwa kwa MUNIR ZAKARIA, hata kidogo. Nasikitika tu kuwa waliokuwepo waliteua mtu kuwa msemaji wa chama wakati nafasi hiyo haipo kwenye KATIBA ya chama. Na nadhani ndio maana MUNIR alikuwa hatumiki ipasavyo, kumbe nafasi yake haitambuliwi na katiba ya chama kama ndivyo kweli ilivyo, maana ni bahati mbaya kwa miaka hii ya karibuni, pengine ndani ya miaka 10, sijawahi kuiona katiba ya ZFA.
  Ninachohofu ni kimoja, nilidhani katika hiyo haki ya kikatiba aliyonayo RAIS, ndipo MUNIR aliteuliwa na kwa hivyo ana mamlaka ya kikatiba ya kufanya kazi aliyopewa. Hili linahitaji ufafanuzi kwa Rais au Katibu Mkuu wa ZFA, watueleze vizuri hili.
  Sasa, mimi sikubaliani na uamuzi wa kuachia jukumu la usemaji kwa Rais au na Katibu Mkuu. Hata kama inaweza kuachwa hivyo katika KATIBA, lakini UMUHIMU na HAJA ya Chama kuwa na mwandishi wa habari, au hata asipokuwa mwandishi wa habari (journalist), panahitajika mtu mtaalamu wa kujenga uhusiano mwema/taswira njema ya Chama na UMMA ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za Chama kwa umma. Hatua hii ni muhimu sana sasa kwa sababu ndio MSISITIZO na MATAKWA ya FIFA. Shirikisho hili ambalo Zanzibar tunahitaji kuwa MEMBA wake kamili, linahimiza sana mashirikisho au vyama vya soka vya mataifa kuwa na mtaalamu wa uhusiano mwema ambaye anakuwa daraja kati ya Chama/Shirikisho la Taifa na UMMA.
  Si vizuri kuacha jukumu hili kwa hawa RAIS na KATIBU MKUU, wana majukumu mengi ya kufanya, ambayo yanawatosha. ZFA ikiwa na mtaalamu huyu, itakuwa inaionesha dunia na FIFA kuwa ipo tayari kwenda na wakati ambao kisasa hakutakiwi viongozi wenye UKIRITIMBA katika kutoa taarifa za utendani, mipango na maendeleo ya SOKA, kwa UMMA. Kukumbatia madaraka na mamlaka kwa viongozi wawili wa juu wa Chama, hakusaidii kitu, zaidi kunazidi kuonesha uongozi usiotaka uwazi.
  Uamuzi wa kumbakisha MUNIR katika Kamati ya Utendaji si mbaya, hofu yangu ni kwamba ZFA mmemchoka kijana huyu na mnatafuta namna ya kumtupa nje. Why? Nahisi mnatafuta akosee tu ili mumtupe nje. Katika hali kama hii, ninahofu kuwa mwaweza kuja kumtupa nje MUNIR kwa kumdhania tu anatoa taarifa za KAMATI YA UTENDAJI nje ya vikao. Huu ni wasiwasi wangu mkubwa na ninashangaa kwamba Rais mpya amefika hapa wakati alikuwa na MUNIR wakati wote wa kampeni za Uchaguzi ule uliopita na kuzusha mgogoro.
  Ningependa RAIS na KM muwe wazi kwelikweli ktk hatua hii.
  Mimi nimetoka kuitazama ZFA kwa muda sasa kwa sababu naona sipati cha kueleza, hakujakuwa na any tangible development agenda kwa muda mrefu sasa kwa vile uongozi uliokuwepo umejigandisha kwenye mawazo mgando badala ya kuangalia mbele na mahitaji ya mpira kuendelea mbele tena kwa kasi kubwa kama unavyoendelea kwenye mataifa mengine ndani ya Afrika.
  Wasalaam.
  JABIR IDRISSA, safarini DSM.

 3. Nawapongeza wale ambao wameshida nafasi mbali mbali katika chama cha soka cha zfa lakini wasiwasi ni kwamba chombo hichi cha kusmamaia maendeleo ya soka hapa zanzibar kinawezwa kumezwa na mtu mmoja kutokana na madaraka na nguvu za kifedha alizonazo. Rais mpya wa zfa tunamtakia kila la kheri lakini amekuwa na tabia ya kuiangilia mambo yasiyomhusu ( technical issues) katika timu alizowahi kuzifadhili. Wasiwasi wangu ni kuwa hata huko zfa anaweza kukiuka taratibu na sheria na kuingilia mambo yasimhusu. Ni vyema ikawa wazi kwamba huu si wakati wa kuendesha taasisi za public kwa kutegemea fedha za mtu binafsi. Huu niwakati wa zfa kutafuta vyanzo vya kuaminika vya mapato bila kuathiri utamaduni wa kizanzibari. Ni lazima viongozi wapya waheshimu utaratibu wa kuendesha taasisi hiyo kwa kutumia ‘ basic operational principles’ yaani haki, usawa, majadiliano na uhuru wa mawazo (mutual consultations). Kila la heri uongozi mpya zfa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s