Wawakilishi wataka uwiano sawa wa ajira

Baadhi ya maofisa mbalimbali na wananchi wakiwa katika Baraza la Wawakilishi wakisikiliza Hotuba na Michango mbalimbali inayotolewa na Wajumbe wa Baraza hilo

Wajumbe wa baraza la wawakilishi wamepitisha makadirio ya mapato ya matumizi ya wizara ya nchi ofisi ya rais utumishi wa umma na utawala bora kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 huku wajumbe hao wakitaka nafasi zaidi za ajira kwa wazanzibari katika serikali ya jamhuri ya muungano.

Pamoja na mambo mengine wajumbe hao walizungumzia kwamba wanahiotaji mgawanyo sawa au angalau asilimia 40 ya nafasi za kazi ndani ya seikali ya muungano. Wajumbe kadhaa walisema nafasi za ajira ndani ya serikali ya muungano ni muhimu ziwe sawa ili kuondosha manunguniko kwa upande mmoja wa muungano.

Wajumbe wa baraza la wawakilishi pia walitaka serikali ya Zanzibar kuondosha michango ambayo inachangishwa kwa vikosi vya ulinzi na polisi michango ya aina mbali mbali na kwamba ni kinyume na sheria za utumishi wa umma kuhusu mishahara.

Aidha wajumbe wa baraza hilo walitaka serikali kufanya mabadiliko ya mishahara na maslahi kwa watumishi wa muda mrefu serikalini ambapo hupokea mishahara midogo kwa kisingizio cha kiwango kidogo cha elimu.

Pia wajumbe wameiomba serikali kuwepo na ajira nyingi ya waalimu ili kuondosha ufumbufu kwa wanafunzi hasa katika masomo ya sayansi. Suala la ulazima wa kuitumikia serikali pia liliubuka kabla ya wajumbe kupitisha bajaeti hiyo ambapo walisema watumishi wa serikali wawe na mkataba maalumu ambao utawafunga wasitoroke nchini.

Akijibu hoja za wajumbe wakati akifanya majumuisho ya wizara yake, waziri Haji Omar Kheri aliwataka wajumbe wan baraza hilo kuridhika na mgawanyo wa sasa wa nafasi za kazi ndani ya muungano ambao ni asilimia 21 kwa Zanzibar na 79 kwa Tanzania bara.

“Naomba wajumbe kwa sasa tukubaliane na mgawanyo huu kwani haikuwa rahisi kufikia hapa tulipo wenzetu walitaka tupange kwa kulingana na idadi ya watu ambapo tungepeta nafasi kidogo sana lakini tukaamua tutazame utawala ndio tukafika hapa tulipo” alisema Kheri.

Hata hivyo waziri alishauri wajumbe wa baraza la wawakilishi pamoja na wananchi kutumia fursa ya kutoa maoni ya katiba ili kupendekeza mgawanyo ambao utakaozingatia maslahi ya wazanzibari. Waziri Kheri aliahidi kuyafanyia kazi maoni yote yaliotolewa na wajumbe wa baraza hilo ikiwemo suala la kutazama upya mishahara ya watumishi wa muda mrefu ambao elimu yao ni ndogo.

Alisema bado serikali ina nafasi nyingi za ajira hasa kwa waalimu wa sayansi ambapo kati ya nafasi 500 zinazohitajika kujazwa ni walimu 240 tu waliopatikana. “Wajumbe nafasi bado zipo nyingi kama mnao vijana walimu wenye sifa nileteeni tutawaajiri sasa hivi ili kuwasaidia watoto wetu kufanya vizuri maskulini” alisema waziri huyo.

Marufuku ya uchimbaji kokoto

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imepiga marufuku uchimbaji wa kokoto na kuchonga matufali katika visiwa vya Unguja na Pemba huku wajumbe wa baraza la wawakilishi wakilalamikia kitendo hicho kitawakosesha ajira wananchi.

Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub alisema maamuzi ya serikali kupiga marufuku shughuli hizo kabla ya kuwatafutia wananchi kazi mbadala ni kuwakosesha kazi za kufanya na kuwaendelea katika umasikini.

“Jee serikali ilifanya utafiti gani kabla ya kuzuia kazi hizo na wananchi wangapi wanaathirika tangu kuzuwiwa uchongaji wa matufali na uchimbaji wa kokoto” alihoji mwakilishi huyo. Akijibu suali hilo waziri wa kazi uwezeshaji wananchi kuchumi na ushirika, Haroun Ali Suleiman alisema lengo la serikali sio kuendeleza  umasikini bali ni kupunguza uharibifu wa mazingira.

“Serikali imepiga marufuku ili kuona kwamba shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wananchi haziharibu mazingira na kwa faida ya wananchi wenyewe na vizazi vijavyo. Tunahitaji kushirikiana kuhifadhi mazingira” alisema Haroun.

Waziri huyo aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba wizara yake imekuwa ikichukua juhudi ya kuwahamasisha na kuwaunganisha kuanzisha miradi mengine kama upandaji wa mwani, upandaji wa miti na kilimo cha migomba.

“Kwa kushirikiana na benki ya CRDB wizara imetoa mafunzo kwa wananchi hao kwa lengo la kubuni miradi mbadala na kuachana na uharibifu wa mazingira” alisisitiza. Aidha waziri huyo alisema wizara yake imekuwa ikifanya juhudi kuwashajiisha wananchi kuanzisha ushirika wa akiba na mikopo na kwamba idara inatoa mikopo kwa wale wanaoomba kuendeleza miradi ambayo haina athari kubwa kwa mazingira.

Kuhusu ni watu wangapi ambao wameathirika katika vijiji vya majimbo ya Kiwani, Tumbe,  Micheweni na maeneo mengine ya Zanzibar walioathirika kwa kupiga marufuku uchongaji wa mawe na kokoto, waziri alisema bado wizara yake haijafanya utafiti wowote.

Ukosefu wa fedha za kilimo

BAADHI ya wakulima visiwani Zanzibar wameshindwa kupata matrekta ya kuwalimia katika mashamba yao ya mpunga kutokana na ukisefu wa fedha za kukodi matrekta hayo kwa muda mrefu. Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa nafasi maalumu za wanawake (CUF) Mwanajuma Faki mdachi ambapo alitaka kujua serikali itawasaidia vipi wakulima ambao hawana uwezo wa kukodi matrekta.

Alisema katika suali lake miongoni mwa ahadi za mheshimiwa rais wa zanzibar ni kuwasaidia wakulima lakini baadhi yao wameshindwa kupata matrekta hayo kutokana na uwezo mdogo na ardhi yao imekauka kutokana na uhaba wa mvua.

Akijibu suali hilo waziri wa kilimo na mali asili, Suleiman Othman Nyanga amekiri kuwa baadhi ya mabonde yamekauka sana kutokana na kipindi kirefu cha jua na upepo mkali na wakulima wanahitaji msaada.

Alisema kuwa baada ya kuanza kwa msimu wa mvua ndogo ndogo, wizara yake itatoa matrekta ili kusaidia wakulima hao ambao hawana uwezo wa kukodi na sehemu kubwa ya mabonde hayo yatapatiwa huduma hiyo.

“Nakiri kuwa wapo wakulima kidogo sana ambao hawakuwahi kulimiwa na tayari maafisa wa kilimo wamegizwa kuwaorodhesha wakulima hao ambao pia waliwahi kutoa fedha kidogo ili wakalimiwe” alisema Nyanga.

Nyanga aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kuwa wakulima wote amabo wanatoa fedha kwa ajili ya kulimiwa huwa hazipotei na kwmaba fedha hizo hukusanywa na kutolewa risiti.

Waziri Nyanga alisema kwamba kilimo ni miongoni mwa vipaumbele vya serikali ya awamu ya saba na kwamba juhudi zote zimeelekezwa katika kuimarisha kilimo ili kuwa na akiba ya kutosha ya chakula.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s