Madai ya Wawakilishi ni kilio cha samaki?

Wajumbe wa baraza la wawakilishi wakiwa katika kikao cha kujadili bajeti ya serikali mwaka 2012/2013 huko Chukwani Mjini Zanzibar

Na Juma Mohammed, Zanzibar
Si katika Baraza la Wawakilishi wala nje ya Baraza,katika viunga vya Zanzibar hakuna jambo linalozungumzwa katika kila pemba ya viunga hivyo ni Muungano, Muungano,kama atatembelea mgeni hii leo ataweza kujiuliza Muungano ni kitu gani,nyumba,mtu,shamba au nini hasa?

Kwa kila makadirio ya Wizara yatakapowasilishwa, Wawakilishi wa wananchi hawakusita kutoa maoni yao kuhusu kero za Muungano, wiki iliyomalizika tulishuhudia mjadala mkali ukijitokeza ndani ya Baraza hilo kwa wajumbe kuelezea hisia zao na bila shaka za wananchi katika majimbo wanaoyoyaongoza.

Lakini mbali ya Wawakilishi hao, watu wengine katika majukwaa yaliyorasmi na yasiyo rasmi wameendelea kzungumzia suala zima la Muungano na mustakabali wake watakiitazama zaidi ujio la Katiba mpya ya Tanzania.

Yamejitokeza makundi karibu matatu makubwa, kundi la kwanza ni la wale wanaotaka kubakia na mfumo wa muundo wa Muungano wa sasa kama ulivyo,lakini ukifanyiwa marekebisho kidogo, kundi la pili wanataka Serikali tatu,lakini kundi la tatu linawakilisha kizazi kipya wenye fikra mpya kwamba umefika wakati mfumo wa muundo wa Muungano wetu uwe wa mkataba wenye Serikali mbili zenye Mamlaka kamili.

Hapa ndipo nilipowakumbuka ‘Majini Bahari’ Bendi ya Muziki wa Dansi ya Dar es Salaam Jazz( Dar Jazz) katika wimbo wao maarufu wa “mtoto acha kupiga mayowe, waache watu waone wenyewe” naam tuache watu waone wenyewe katika mchakato wa katiba mpya nini wananchi wataamua.

Dar Jazz walikuwa wakiwakoga mahasimu wao Bendi ya Western au kama walivyokuwa wakijulikana Wana Saboso.lakini kwa maana ya makala haya,hakuna kundi linalowakilisha Bendi hizo zaidi ya kupendezwa na utunzi wa wimbo wao wa mtoto ache kupiga mayowe.

Wakati naandika makala haya, moyoni nimejawa na furaha isiyokifani iliyochanganyika na matumaini ya kuona naishi katika karne ya ishirini na moja nikitarajia mabadiliko katika muundo wa Muungano na hasa nikiwasikiliza Wawakilishi wale wa wananchi katika chombo cha kutunga sheria namna walivyochoshwa kwenye masikio yao kusikio kero za Muungano.

Maoni ya Wawakilishi wengi waliozungumzia Muungano nayatafsri kama wanaiambia Serikali kwamba ichukuwe maamuzi magumu na sahihi katika kuona Muungano unadumu bila ya kero.

Sauti za Wawakilishi ni sauti za umma maana wao ndio waliopewa dhamana kupitia uchaguzi kuwawakilishi wananchi katika majimbo hamsini ya uchaguzi ya hapa Zanzibar, hivyo hatutegemei maoni yao kupuuzwa kwa kutiwa kapuni.

Mabadiliko ya kisiasa,kiuchumi na kijamii  hayataweza kuzuilika,ni kama mvua utaamua mwenyewe kujificha uipishe mvua ipite au kuingia ikunyee ndio, uchaguzi  ni wako maana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kupanga ni kuchagua.

Sisi wengine tunachagua muundo wa Muungano kama ule wa Muungano wa Ulaya ambao utatuhakikishia tutadumisha Muungano bila manung’uniko kuwa huyu kapunjwa hiki au kile,mambo yatakuwa sawa sawa.

Kilio cha Wawakilishi tumekisikia kupitia  maoni ya Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa kama yalivyosomwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani(CCM) Ali Salum Haji ambaye alielezea kero katika ushirikiano wa kimataifa ambapo Zanzibar inashiriki kutumia mwamvuli mmoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Baya zaidi katika vikao hivyo kuna mambo yanayojadiliwa na kupitishwa si ya Muungano lakini bado Zanzibar inashiriki kwa mwa mvuli huo ambao kwa muda mrefu sasa umeonekana kuwa ni kero kwa wananchi wa Zanzibar” Alisema Mwakilishi huyo kupitia maoni ya Kamati yao.

Kwa sababu hiyo nini Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa ilipendekeza wakati wa kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi?

“Mheshimiwa spika, kwa kuwa kuna mchakato wa utoaji wa maoni ya uundwaji wa Katiba mpya, kuna umuhimu kwa Wazanzibari kuhakikisha kuwa masuala ya Mambo ya Nje yanakuwa si ya Muungano ili Zanzibar iwe na uwezo wa kushiriki katika vikao mbali mbali ikiwa nchi kamili” Alisema Mwakilishi Ali.

Wawakilishi wanataja kasoro za mfumo wa muundo wa Muungano katika maoni yao kupitia Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa walipokuwa wakijadili makadirio ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ambaye mambo ya Muungano yanaratibiwa katika Ofisi hii kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mojawapo ya kasoro hizo wametaja Mawaziri walioko Tanzania Bara ambao si Mawaziri wanaoongoza Wizara za Muungano kuonekana kuwa ni wanaongoza Wizara za Muungano.

“Mheshimiwa Spika, kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano,  Wizara za Muungano wa Jamhuri ya Tanzania ni chache mno,  lakini  kiuhalisia Mawaziri wote waliopo Tanzania Bara wanafanya kazi zao kama ni Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Sasa, je! tujiulize, hii ndiyo sahihi? Waliohoji Wajumbe kupitia kamati yao ya kudumu kusimamia viongozi wakuu wa kitaifa.

Nini dawa ya kero hizo za Muungano? Mwakilishi wa Kwahani (CCM) ambaye alisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa alisema muarubaini wa matatizo au Kero za Muungano wetu ni kuwa na katiba ambayo itakayobainisha na kuzitambua haki za kila upande wa Muungano huu na kutofautisha zipi zitashughulikiwa na kila nchi katika Muungano huu na zipi zitashughulikiwa na chombo cha Muungano.

Katika kipindi hichi  tumeona harakati mbalimbali ambazo zimechangia ari na nguvu mpya kwa watu kutaka kuona Zanzibar mpya ikizaliwa chini ya Muungano wa mkataba ambao utawakonga nyoyo Wazanzibari .
Chama cha Mapinduzi kimeshatoa fatwa kwa wanachama wake kwamba kinaendelea na msimamo wa muundo wa Muungano wa Serikali mbili, Chama cha Wananchi(CUF) sera yake katika muundo wa Muungano ni Serikali tatu, vyama vyote hivyo vitakabiliwa na changamoto ya mageuzi ya umma kupitia kura ya maoni kuamua katiba mpya baada ya kuandikwa kwa rasimu na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapo baadaye.

Idadi za Serikali hazitaweza kuondoa kero za Muungano, muarubaini wa kero hizo ni kuwa na mfumo mpya wa muundo wa Muungano ambao ni ule wa kuzifanya nchi mbili zilizoungana kuweza kujiamua mambo yake wenyewe, kuwa na kiti katika Umoja wa Mataifa ambapo Tanzania itakuwa na viti viwili UN hii ni faida mojawapo ya mfumo wa muundo wa Muungano wa mkataba.

Zanzibar na Tanganyika zote zikiwa wanachama wa UN zitaweza kupata nguvu za kiuchumi kwa haraka zaidi kuliko ilivyo sasa, yale malalamiko ya Wizara zisizo za Muungano kujigeuza za Muungano hayatakuwepo, wakati huo huo Muungano wetu utazidi kuwa madhubuti  na unaweza kuwavutia wengine kujiunga.

Kwa muda mrefu kumekuwa na jitihada za kutatua kero za Muungano,lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda,ni kama mtu wa mvumo ambao unaota jangwani kwani baadhi ya matatizo katika Muungano utatuzi wake hauchukui hata nusu siku seuze miaka 48.

Tanzania imebahatika kuongozwa na watawala wenye majigambo, hakuna anayewashinda ni wajuzi wa nahau na semi utasikia wakisema ‘kero za Muungano zitakuwa mwisho, wengine nitatatua matatizo ya Muungano kwa siku mia moja, shabash,miaka kumi hakuna lililotendeka wimbo ndio ule ule tuko mbioni,hivi jamani mbio hizo mbio gani zisizofikia ukingoni,  hata hizo za cross country zinafikia mwisho.

Hivi kweli kero ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili kuna ugumu gani kuiondosha kero hii, kodi ya watumishi wa SMT waliopo Zanzibar kwanini iende hazina ya Dar es Salaam nalo linaugumu gani hadi likachukua miaka nenda miaka rudi?

Kwa sababu hiyo basi, sisi wengine ndio tumeanza kuchukua maamuzi magumu na sahihi kufikiria muundo wa Muungano uwe wa mkataba ambao utabaishani maeneo ya ushirikiano katika Muungano.

Waumini wa Muungano wa mkataba wanaamini katika kulinda na kutetea Muungano udumu,lakini ili kudumisha na kuufanya usiwe wenye kero zinazowakera wananchi wa pande mbili za Muungano twendeni kwenye mfumo mpya ambao wenzetu wa Ulaya wanatumia na umewalatea mafanikio.

Tabaan. Makundi yote yana hoja, na kwa kuwa nchi hii inafuata misingi ya kidemokrasia ambayo mamlaka ya uendeshaji nchi yapo mikononi mwa wananchi wenyewe tunatarajia kura ya maoni itakayofanyika baada ya kumalizika kwa Bunge la Katiba itaagua kitendawili cha siku nyingi cha mfumo upi muafaka,ule wa kale wa Serikali mbili,Serikali tatu au wa mkataba.

Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliwahi kunukuliwa katika hafla ya kuaga wananchi akistaafu madaraka ya Urais mwaka 1995 alisema anadhani umefika wakati wa kuwa na muundo wa mfumo wa  Muungano wa Serikali moja.

Ingawaje wapo watu wachache Zanzibar wanafikiri hivyo, lakini pamoja na kutawaliwa na ushabiki huo hawataki kufutwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kwa misingi ile ile iliyositizwa katika adidu rejea za Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba mambo matatu ni lazima yawepo, kuwepo kwa Muungano, kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuwepo kwa mihimili ya Dola.

Advertisements

2 responses to “Madai ya Wawakilishi ni kilio cha samaki?

  1. Pingback: Madai ya Wawakilishini kilio cha samaki?·

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s