Dk. Shein, lugha ya upole haitoshi?

Jabir Idrissa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akitoa Hutuba yake wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja leo,(kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis,(kulia) Bibi Tereza Olbam, Mlezi wa Jumuiya na (wa pili kulia) Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano Mohamed Ali

KAULI aliyoitoa Dk. Ali Mohamed Shein kuhusu Muungano haimsumbui mtu yeyote; si Unguja wa Pemba – Zanzibar. Anaposema Muungano hautavunjika, hakuna anayemsumbua. Anaposema yeye ndiye rais, hivyo hakuna atakayeuvunja Muungano, hakuna anayesumbuka.

Rais anaalikwa kufungua mkutano wa jumuiya ya wastaafu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema atautetea Muungano; na hakuna atakayemlaghai wala kumchezea katika uongozi wake. Waliomnukuu, wanasema Dk. Shein amesema yeye kama rais, hatomuogopa mtu wala kusita kuchukulia hatua wale watakaokwenda kinyume na matakwa ya katiba.

Hili moja ni dhahiri – Dk. Ali Mohamed Shein ndiye rais Zanzibar , na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyorekebishwa mwaka 2010; inamuongezea wadhifa wa mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Katika maelezo ya Dk. Shein kwa wastaafu, kuna maneno yanasumbua kidogo labda tu kama umma utaambiwa kuna mtu amehoji mamlaka ya rais.

Anaposema “sitomuogopa mtu yeyote” wengine wanauliza kwani kuna mtu anamtisha rais? Anayemtisha rais anastahili kuchukuliwa hatua haraka ya kushitakiwa. Kwa mantiki ya sheria, kumtisha rais ni kutishia mamlaka ya wananchi waliompa dhamana ya kuongoza nchi yao.

Hili watu wangetarajia kuliona linafanyika haraka. Nataka kuamini hakuna mtu aliyemtisha rais. Kama yupo ni wajibu wa rais kusema “nimetishwa.” Akishasema, ni jukumu la wasaidizi wake kuchukua hatua kulingana na sheria. Kama rais ametishwa, au ametishiwa, huo ni uhalifu. Mhalifu anapaswa kudhibitiwa.

Inapotokea uhalifu umetendeka, ni muhimu vyombo vya dola vikachukua hatua haraka, pasina kusita. Hakuna kuchelewa maana uhalifu huo waweza kudhuhuru mamlaka hii na hivyo kuchochea wananchi kukasirika kwa kuona kiongozi wao anadharauliwa.

Sasa inapotokea uhalifu umetendeka dhidi ya mamlaka ya rais, kasi ya ushughulikiaji wake yapasa iwe kubwa zaidi. Rais si ndiyo alama ya nchi yetu? Sasa tunazubaa nini kumshika anayemhalifu? Labda nimkumbushe rais. Katiba hiyohiyo, Ibara ya 9(2)(a) inazungumzia mamlaka waliyonayo wananchi wa Zanzibar : Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa serikali kufuatana na katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.

Sehemu (b) ya ibara inaelekeza uhakikisho wa usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndiyo lengo kubwa la serikali. Katika hali hii, baada ya rais kutaka kuyahisi mamlaka aliyopewa na katiba ya nchi, basi ni vema pia akatambua na mamlaka waliyonayo wananchi anaowaongoza kupitia katiba hiyohiyo.

Kutambua mamlaka ya wananchi kuna maana kubwa kiutawala na kiuongozi. Ni suala la kustawisha misingi ya utawala bora na kuilea pia. Kiongozi anayelea misingi ya utawala bora ni yule anayezungumza na wananchi kwa lugha fasaha siyo ya kupinda na kufumba.

Makamu wa Kwanza wa Rais, msaidizi mmoja wapo wa Dk. Shein, Maalim Seif Shariff Hamad, amezungumza na wananchi kuhusu suala muhimu linalojadiliwa sana Zanzibar – Muungano. Anasema, “Hakuna mwananchi atakayeadhibiwa kwa kutoa maoni yake kuhusu mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , iwapo atayatoa kwa utaratibu uliowekwa.

“…Njia pekee ya kuondoa kero za Muungano ni kwa wananchi kujitokeza kutoa maoni yao mbele ya Tume ya kukusanya maoni, na maoni yao yatazingatiwa, kuheshimiwa na kufanyiwa kazi kwa kadri watakavyoyatoa.”

Hizi ni lugha mbili tofauti kama mbingu na ardhi. Moja inaelekeza wananchi kutambua wajibu wao katika kile kilichopo mbele yao , huku nyingine ikiwa inayowatisha, inawatia hofu. Kwanini Dk. Shein anawaelekeza watu wamtambue kuwa ana hasira? Majibu yaweza kuwa tofauti kutegemea na yale mtu anayoyasikia au kuyajua kumhusu rais.

Watu waamini pengine rais wao anatishwa? Au anashinikizwa kutaka kile asichokipenda? Au anabanwa na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – asikilize na kutii maelekezo ambayo kwa uoni wake, ni tofauti na dhamira yake au ni tofauti na anavyoona wananchi wanafikiri?

Hebu Dk. Shein aangalie hili. Wakati akitafakari namna Wazanzibari watakavyotoa maoni yao kwa Tume ya Jaji Warioba kuhusu msimamo wao na Muungano, waziri wake, tena wa CCM, ametajwa kuwa ameandika barua moja, kuichapa nakala nyingi na kuigawa kwa wananchi ili hayo ndiyo yawe maoni yao kwa tume hiyo.

Sasa waziri huyu ametajwa hadharani na baadhi ya waliofika kwenye mkutano wa kwanza wa tume hiyo jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, walizionyesha barua hizi na kuzikabidhi kwa tume kama ushahidi.

Barua hiyo inaelekeza maoni yawe serikali mbili. Pengine kungekuwa na barua inayoelekeza wananchi kutoa maoni ya kuwepo kwa muungano wa serikali tatu, ingekuwa kashfa kubwa. Kwa kuwa mtenda hilo ni kiongozi katika CCM, natabiri haitakuwa chochote.

Jimbo la Makunduchi linalowakilishwa na Haroun Ali Suleiman, waziri wa uwezeshaji wananchi, linajulikana kuwa na wafuasi wengi wa CCM ingawa katika miaka ya karibuni limeshuhudia vuguvugu zito la vijana kupenda siasa za mageuzi.

Makunduchi pia ni nyumbani kwa viongozi wengi waandamizi serikalini na katika CCM, akiwemo Waziri wa Ulinzi wa Muungano, Shamsi Vuai Nahodha, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan.

Mbinu ya waziri kuandaa barua inaonyesha dhamira ya kulaghai wananchi hasa wale wenye mawazo tofauti na yanayoaminiwa na kiongozi huyo na chama chake, CCM.. Hiyo ni mbinu chafu ya kuwasilisha msimamo. Hakika huko ni kutisha wananchi, kuchezea uhuru wao unaotajwa na Katiba ya Zanzibar ; wa kujieleza na kutoa mawazo yao kwa masuala yanayohusu uendeshaji wa nchi yao.

Mbinu hii yaweza kuchochea vurugu kwa sababu ni kinyume na ahadi ya Jaji Warioba kwamba wananchi wapo huru kutoa maoni yao tume itakapofika kwenye maeneo yao. Pale Dk. Salim Ahmed Salim, mwanadiplomasia mahiri kitaifa na kimataifa, na mjumbe wa Tume, aliposema “tumewasikia wanaopinga Muungano sasa tuwasikie na wanaoutaka,” hakuwa na maana waziri au mawaziri na mtu yeyote yule kuandaa barua au waraka wa kuelekeza watu cha kusema.

Hebu wakubwa wafanye kama huu ni wakati wa mtihani, baada ya mtahiniwa kufanyiwa mazoezi wakati wa maandalizi, aachiwe huru kufanya kwa akili yake anapoingia kwenye chumba cha mtihani chenye ulinzi.

Nilidhani rais Dk. Shein angeshitukia wakubwa hawa wanaolazimisha watu wanayoyaamini wao, japo si lazima yawe ndiyo maoni ya wananchi husika.

Advertisements

5 responses to “Dk. Shein, lugha ya upole haitoshi?

  1. Inasikitisha kuona rais anasema hamuogopi mtu ilihali maagzo yake yote hayatekelezwi. Ningeamini nguvu zake angeweza kuondosha ufugaji wa wanyama katika mji wa Unguja, angesimamia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora isiendekeze ubinafsi katika ajira, anesimamia Serikali yake isiharibu mali za Uma hata kufikia kuleta fungu la m 40,000.000 ili litumike kununua seti ya TV, angezuia Wanachama wa CCM Kisonge, Kachorora kutoa maandishi ya kibaguzi, angewaondosha wale wote waliokataa Umoja kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa – kwa kuwa haya hakuyaweza basi siwezi anaweza kuzuia watu wanakataa Muungano wasipeleke mbele ajenda zao. Haya matamshi ya Mh. ni kujikosha tu

  2. Huu ndio mchezo wa ccm na viongozi wake. Hapa hapana haki isipokuwa wakuawa kutetea maslahi yao tu. Kama mambo yenyewe ni haya mimi naona hakuna haja ya kupoteza pesa za wanyonge walipa kodi kwa kucheza display. Kwani inavyoonesha haya sio maoni ya wananchi ila ni mchezo wa kuigiza uliotayarishwa na ccm kupitia viongozi waliopo madarakani.ili wadanganye ulimwengu. Sisi tokea zamani tulikuwa hatuna imani na hii tume sasa imedhihirika wazi wazi ubaya wake.na imetufanya moja kwa moja kuwa hatuna imani na tume. Sisi wazanzibar tunataka nchi yetu ya Zanzibar iwe na mamlaka kamili ya kidola kitaifa na kimataifa. Jamani TUACHENI TUPUWEE. Muungana hatuutaki wahishimiwa. Musitulazimishe kitu tusichokitaka. Muogopeni Mungu alieumba vyote. Hamuna nguvu mbele ya Mungu. INSHALLAH TUTASHINDA KWA UWEZO WA ALLAH. Muungano utavunjika tuu. HATUUTAKI MUUNGANO BANDIA TUSHACHOKA KUTAWALIWA. AU MUTATUUWA SOTE UWEZO MUNAO!!!?

  3. WAKATI MWENGINE HAWA VIONGOZI HUA WANAPENDA KUJITUKANISHA MBELE YA ULIMWENGU. HIVI HATA AIBU HAONI KUSEMA KUA ATAULINDA MUUNGANO? IKIWA WANANCHI WATAAMUA KWA KAULI MOJA KUA HAWAUTAKI UTAULINDA WEWE NA …………. PEKE YENU? MIMI SIFAHAMU HAYA NI MANENO YAKO BINAFSI AU NDO UNAELEZA MSIMAMO WA CCM? KAMA NDIO MSIMAMO WENU CCM HAMKUA NA HAJA YA KUWAULIZA WANANCHI WATOE MAONI YAO KUHUSU MUUNGANO TULIKUA TUMEKAA KIMYA TUMETULIA MMEYALETA WENYEWE SASA KAMA YANAANZA KUKUSHINDENI VUNJENI TUME YENU MAPEMA KABLA HAIJATUMIA MAPESA MENGI ZAIDI NA TUENDELEE NA BUSINESS AS USUAL. IKIWA MLIKUA MNATAKA KUJIKOSHA MBELE YA MACHO YA WALIMWENGU KUA NYINYI NI WANA DEMOKRASIA MWAKA HUU MTAUMBUKA MAANA MMESHAANZA KUFELI NA ULIMWENGU UNAWAJUA KUA HAMNA DEMOKRASIA NI CHUI MMEVAA NGOZI YA KONDOO. MNAWALAZIMISHA WAZANZIBARI WAUKUBALI MUUNGANO AMBAO HAWAUTAKI KWA MABOMU NA NGUVU ZA KIJESHI. TUACHENI TUPUMUEEE.

  4. Hawa watu na doctorates zao zote ni sawa na mchangiaji moja Mtende aliyesema ” tuliambiwa tukatae Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tukataa na kisha ikaundwa- naogopa isiwe na hii tume inafanya kazi kisha matokeo yatiwe kapuni”. Huyu jamaa ambaye alikuwa na dukuduku la muda mrefu lazima amshukuru Mungu kwa kutokea mahali pa kulitoa. Kama ni faida ya Kuunda Tume ya Mchakato wa Katiba basi ni huu tu wa Kuruhusu Wanachama wa vyama Kandamizi kusema dukuduku zao. Tukisikia Mjumbe wa Baraza anajiondosha kwenye shtuma za kuandika jibu kisha watu wakafanana katika kuzungumza ” Mimi fulani bin fulani, nakaa — nataka Serikali mbili ya Jamhuri na SMZ na zaidi majibu yangu ni haya.” na mwengine akija naye vile vile na mwengine vile vile ilaaakhiri L’aya inaonesha kuna jambo si la kawaida kwenye akili zao hasa wanapolingana hata uteuzi wa maneno ya kuimbia Tume. Tume hii ambayo nayo ina kasoro ingekuwa bora iwape watu anuani za barua au e-mail ili wanataka kuchangia kwa maandishi wafanye hivyo na si kwa kujitokeza kisha wakaonekana na viongozi wa vyama vyao wamesheheni kana kama wana arusi za watoto wao kwanza hii ni intimidation kwa kuwa watu wanashindwa kusema maoni yao wakiwa huru kama raia na si wanachama. Kizimkazi Dimbani kulikuwa na Gari hata RC Urban West Region – hatuji lilfata nini hapa ilihali kazi iliwahusu watu wa Kusini. Huu mwendo unaweza kuharibu na Tume ingebidi iangalie kiasi inaweza kuzuia hii isiendelee ! Hawa wanaotoa maoni pamoja na kuandkiwa majibu ni watu wazima wanahitaji pia kuachwa wafanye vile akili zao zao zinavyo watuma. Falsfa hii ya mtu na wanawe tuiache ili Zanzibar itoe watu wanaojitegemea na wanajithamini. Hii ni mentality mbaya kuendelea nayo. Ni kwa sababu ya mindset hii ndio watu wanawafata Wawakilishi wawape hata mahari ya kuolea wake wa pili, wa tatu hata wa nne Nyumbani kwetu kuwa mbunge au mwakilishi unahitaji uwe na subira kumshinda mitume ya kundi la Ulazmi. Mchakato huu wa Katiba Mpya inabidi utufundishe si tuu kuzungumza bali kuona tunayozungumza ndio na kama yanahitajika kwa sasa na baadae. Kizimkazi Dimbani mtu moja alipingana na wenzake waliodai kuwa ” baraza la mitihani ni chanzo cha kufeli watoto Zanzibar.” Kila mtu anaupeo wake wa kufahamu mambo mimi niliona hawatapingana lakini watapendekeza njia bora ilimiaka 50 ijayo watu wazungumze mahusiano yasiona utata na yaliwazi likija suala la mitihani ! Huu ni mwanzo pengine mambo yatabadilika lakini nyota njema hungaa asubuhi!

  5. Pingback: Dk. Shein, lugha ya upole haitoshi?·

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s