Serikali yakamilisha sheria ya rushwa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheri akiwasilisha Hotuba ya Makadirio na Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2012/2013 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema imo katika kukamilisha utaratibu wa kuanzisha rasmi taasisi ya kuzuwia na kupambana na rushwa Zanzibar. Hayo yameelezwa na waziri wa nchi ofisi ya utumishi wa umma na utawala bora, Haji Omar Kheri wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/2013 katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea.

Alisema kufuatia kutungwa kwa sheria ya rushwa na uhujumu uchumi mapema mwaka huu wizara yake inategemea kufungua ofisi ambayo itakuwa na majukumu ya kuchunguza mambo na vitendo vya kuwepo au kuruhusu rushwa.

“Tumefikia pahala pazuri na taasisi hii muhimu ya kuzuwia na kupambana na rushwa pamoja na uhujumu uchumi, itaanza kazi zake sio muda mrefu baada ya taratibu kukamilika” alisema waziri huyo.

Alisema katika kuimarisha utawala bora Zanzibar mamlaka ya kuzuwia na kupambana na rushwa na uhujumu uchumi ni muhimu na itaweza kusaidia kuimarisha utendaji kazi pamoja na nidhamu serikalini.

Kwa muda mrefu wajumbe wa baraza la wawakilishi na wananchi kwa ujumla wakitaka Zanzibar iwe na sheria ya rushwa lakini serikali haikuwa tayari kutunga sheria hiyo wakati huo hadi kuingia madarakani kwa Dk Ali Mohammed Shein.

Waziri Kheri pia alisema katika bajeti yake kuwa serikali imo katika kumalisha kuanzisha kwa taasisi ya serikali ya mtandao na manejementi ya taarifa (e-goverment and central data-base).

Alisema mfumo huo unategemewa kuongeza ufanisi katika utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia mipango mikuu ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni Dira 2020 na mpango ya kupunguza umasikini (MKUZA) na malengo ya milenia.

Waziri huyo aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba mfumo wa mtandoa huo sio tu utanufaisha serikali bali pia wadau wengine mbali mbali kama wafanyabiashara, makampuni ya simu, utalii na vyombo vya habari vitanufaika.

Waziri alisema serikali imekuwa ikitekeleza hatua za kufikia malengo ya utawala bora ili kuongeza uzalishaji na kufikia malengo yaliopangwa ambapo amewaomba wajumbe wa baraza hilo kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 7.6 kwa ajili ya kazi za maendeleo na kazi za kawaida za wizara hiyo.

AFYA

Wananchi wa vijiji vya ukongoroni katika mkoa wa kusini Unguja wanakabiliwa na ukosefu wa huduma za afya kutokana na ukosefu wa madaktari na wakunga.

Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM) Panya Ali Abdallah na Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma walilalamika kuwa akina mama wajawazito ni miongoni mwa watu wanaoathirika zaidi na ukofuwa wa huduma hizo.

Akijibu malalamiko hayo Naibu Waziri wa Afya Dk Sira Ubwa Mamboya alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema hivi sasa hakuna daktari wala wakunga ambao wanafanya kazi katika kijiji hicho.

“Kituo cha afya cha Ukongoroni kilikuwa na daktari mstaafu wa jeshi ambaye aliajiriwa kwa mkataba na alikuwa akiishi hapo hapo lakini sasa ameondoka kutokana na mkataba wake kumalizika” alieleza Dk Sirra.

Kuhusu wakunga Dk Sirra alisema walikuwa wawili wanaotoa huduma katika kijiji hicho lakini mmoja amepata dharura ya kuumwa na mwengine ameolewa katika kijiji cha Bwejuu na hivyo amehama na hivi karibuni amejifungua.

Hata hivyo alisema mkunga mmoja ambaye amemaliza likizo ya kujifungua tayari amerudi kazini japo anaishi mbali na kituo hicho kutokana na kuwa na mume Bwejuu ambapo ni kijiji chengine kabisa.

Naibu waziri alisema wizara yake kwa hivi sasa haijapata daktari wa kufanya kazi katika kituo hicho kutokana na upungufu wa madaktari katika wizara na kwamba huduma zinaweza kutolewa kwa njia ya madaktari kuwafuata wagonjwa wanaohitaji matibabu (Mobile clinics).

ELIMU YA JUU

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad ameliambia baraza la wawakilishi kwamba hivi sasa wizara yake ina fedha za kutosha za kuwakopesha wanafunzi wanaotaka kujiunga na elimu ya juu.

Alitoa kauli hiyo wakati akijibu masuali ya Mwakilishiwa Jimbo la Mpendae (CCM) Mohammed Said Mohammed na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu waliotaka kujua juhudi za serikali za kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi kujiunga na vyuo vikuu.

“Hivi sasa fedha zipo za kutosha na tunawashauri wanafunzi wenye sifa kuleta maombi yao ili yafanyiwe kazi badala ya kupeleka maombi katika bodi ya mikopo ya elimu ya juu ya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania” alisema Zahra.

Miongoni mwa wasiwasi wa wajumbe wa baraza la wawakilishi ni kuwa wanafunzi wengi wa Zanzibar wamekuwa hawapati mkopo kutoka bodi ya mkopo wa muungano kutokana na vyuo vikuu vya Zanzibar kutopitia mfumo wa udahili (Central Admission System -CAS).

Mwakilishi wa Mpendae alisema vyuo vya elimu ya juu vya Zanzibar kutotumia mfumo huo wa CAS unapelekea wanafunzi kukosa mikopo kwa sababu tume ya vyuo vikuu vya Tanzania inaidhinisha majina kutoka vyuo ambavyo vinatumia mfumo huo.

Hata hivyo Naibu waziri licha ya kukiri kuwa vyuo vya elimu ya juu Zanzibar havitumii udahili wa CAS alisema sio sababu ya wanafunzi kutopata mikopo kutoka bodi ya elimu ya muungano.

“Wanafunzi wetu wana haki sawa kufaidika na mikopo ya elimu kutoka bodi ya mikopo ya muungano lakini nawashauri hivi sasa wanafunzi waombe kwani tunazo fedha za kutosha wizarani baada ya serikali kutupatia fedha zaidi.”. Alisema Zahra.

KILIMO

LICHA ya juhudi za kuimarisha kilimo cha mpunga Zanzibar wakulima wamepata mavuno hafifu mwaka huu wa kilimo kutokana na sababu ambazo baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi wameeleza kuwa kutoimarika kwa mbegu za mpunga.

Wajumbe wa baraza la wawakilishi Abdi Mosi Kombo kutoka Jimbo la Matemwe (CCM) na Salim Abdallah Hamad wa Jimbo la Matambwe (CUF) walihoji wakati wa kipindi cha masuali na majibu kwamba kwa nini serikali inahimiza matumizi ya mbegu za mpunga za NERICA.

“Mheshimiwa Spika wakulima katika kisiwa cha Pemba wamesikitishwa sana na mavuno hafifu baada ya kilimo cha NERICA kwa nini serikali imewapelekea mbegu ambazo matokeo yake haikuwa na uhakika” alihoji Hamad.

Akijibu masuala hayo waziri wa kilimo na mali ya asili Suleiman Othman Nyanga alikiri kwamba hivi karibuni walifanya ziara yeye pamoja na rais wa zanzibar Dk Ali Mohammed Shein na kuona kuwa baadhi ya maeneo mavuno yalikuwa sio ya kuridhisha.

Hata hivyo alisema wizara yake imejipanga vizuri zaidi katika msimu ujao wa kilimo ili kuwasaidia wakulima kupata mavuno mazuri na kwamba wizara yake imanzisha vishamba vya maonesho katiak shehia 230 Unguja na Pemba ili kutoa mafunzo kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mbegu za NERICA.

Alisema katika msimu uliopita ambapo baadhi ya wakulima hawakupata mavuno mazuri wizara yake ilizalisha tani 21 za mbegu za aina ya mpunga huo na kusambaza kwa wakulima ili ipandwe katika maeneo ya juu ya Unguja na Pemba.

Waziri huyo aliwataka wakulima kutovunjika moyo kutokana na mavuno hayo hafifu na kuwaahidi kupewa mbegu za kutosha ili kuendeleza kilimo hicho cha mpunga.

UMEME

VIJIJI kadhaa vya Unguja na Pemba bado havina umeme kutokana na huduma hiyo kutowafikia wananchi wenye kuishi katika maeneo ya vijijini.

Hayo yamebainika jana baada ya Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM) Viwe Khamis Abdallah kusema kwamba baadhi ya vijiji havina umeme na kutaka kujua mipango ya serikali katika kuwapatia wananchi huduma hiyo muhimu kwa ajili ya maendeleo.

Akijibu suali la mwakilishi huyo pamoja na Mwakilishi wa Mfenesini (CCM) Ali Abdallah Ali, Naibu waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame alisema wizara yake itafikisha umeme katika vijiji vyote ambavyo havina umeme hivi sasa.

“Wizara yangu itakapopata uwezo zaidi itahakikisha usambazaji wa huduma ya umeme katika vijiji vyote vilivyobakia na kuondosha usumbufu kwa wananchi” alisema naibu huyo.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kuwa hivi sasa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linaendelea kupokea maombi ya kuunganishiwa umeme wakati serikali inatafuta fedha za mradi huo.

Akifafanua zaidi waziri wa wizara hiyo, Ramadhani Abdallah Shaaban alisema tatizo jengine limejitokeza ni kuwa na mahitaji mengi ya umeme kutokana na wananchi kuwa na muamko wa kutumia huduma hiyo.

“Hivi sasa mahitaji ni makubwa katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba hadi kupelekea uwezo wa transfoma kupungua. Tuna mradi wa kuimarisha transfoma zote ili kuondosha tatizo la upungufu wa umeme” alisema waziri.

Advertisements

4 responses to “Serikali yakamilisha sheria ya rushwa

  1. Pingback: Serikali yakamilisha sheria ya rushwa·

  2. nakubaliana na wewe ni kudanganya wananchi , na hio taasisi itaongozwa na watanganyika kama kawaida aidha kwa uwazi au kwa nyuma ya pazia ,

  3. Hawa Bwana ni Watu wanafanya Genocide kama ya Rwanda katika mgongo wa Siasa. Ni nani asiyejua kuwa ajira zinatolewa kwa misiingi ya udugu na na ya uanachama. Hawa wanawadanganya watu waonekane ni wema kumbe ni chui waliovaa ngozi ya kondoo. Tunasikia matangazo ya kazi yakitolewa kupitia majimbo huku eti wakidai kuwa Zanzibar inakimbiwa na Wataalamu. Hawa jamaa tuwakee kumbukumbu ili siku moja tudai mahakama ziwashitaki kwa kuikuka haki za watu za Kikatiba. Kuna jamaa aliniiambia kuwa Idara ya Uhamiaji hapa Unguja inaongoza kwa ubaguzi katika ajira. Yeye huyu jamaa na wenzake waliitwa kwenye interview mara mbili na wakagundua majina yalioitwamara ya tatu ni mapya yote. Tumewasikia Wawakilishi wakilalamikia ajira za upendeleo na kwa kuwa hakuna aliyekanusha basi ukweli upo. Waziri anadai kuunda Mamlaka ya kuzuia rushwa ilihali wao ndani ya Wizara wanafanya ajira kwa rushwa ya itikadi, jamaa au ngono. Wanadai wasaidiwe kuimarisha utawala bora huku wakivulimia matumizi ya serikali kwa mfumo wa vouchers kisha TV ya 1,000.000. inawekea fungu la 40,000,000. Katika kipindi hiki cha kutoa maoni ya Katiba mpya ya Tanzania tulidhani watu watachangia pia mahitaji ya Zanzibar kupata Katiba mpya. Watu ambao wengi wao huja na majbu ya kuandikiwa wanazungumza vitu vya ajabu. Kwa mfano, jana Kizimkazi Dimbani mtu Moja alimsifu Dr. Salim kwa sifa zote kisha akatoa mambo ya kichekesho. Tunasikia kuwa huyu jamaa ni Kiongozi wa Chama hapo. Ikiwa Chama kinachoongoza nchi kinaongozwa na kilaza kama yule basi sijui vyama vyegine rafiki vikoje. !

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s