Vitambulisho 112,420 havina wenyewe

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu mwenye kitabu akibadilishana mawazo na mwanasheria wa baraza la wawakilishi Mussa Kombo nje ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar

WAZIRI wa nchi ofisi ya rais Dk Mwinyihaji Makame Mwadini amesema jumla ya vitambulisho vya ukaazi wa zanzibar 112,420 havijachukuliwa na wenyewe katika wilaya mbali mbali kinyume na kauli zinazotolewa na wanasiasa kuwa wananyimwa vitambulisho.Akitoa majumuisho ya bajeti ya ofisi ya rais kabla ya wajumbe kupitisha bajeti hiyo Dk Mwinyihaji alijitetea na kusema kuwa idara ya vitambulisho zanzibar imekuwa ikifanya kazi zake kwa uangalifu mkubwa na kuwataka wananchi wafuate utaratibu.

Alisema kwa muda mrefu vitambulisho havijachukuliwa na vipo wilayani na kutaka wajumbe wa baraza la wawakilishi kuwashawishi wananchi katika maeneo yao wakachukue vitambulisho pamoja na kuacha udanganyifu hasa vyeti vya kuzaliwa wakati wanapoomba vitambulisho.

Mjadala wa bajeti ulitawaliwa zaidi katika michango yake kuhusu vitambulisho ambapo lawama zilitupiwa kwa masheha, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa pamoja na maafisa wa idara ya vitambulisho kuwa wanahusika na kufanya ubaguzi katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo pamoja na kutoa vitambulisho kwa watu wasiostahiki wakiwemo wageni.
wakichangia hutuba ya bajeti ya wizara hiyo wajumbe wa baraza la wawakilishi kutoka vyama vya CCM na CUF wamelalamika kuwepo kwa vitendo vya ubaguzi ambavyo vinawanyima haki wananchi wa Pemba kupata vitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi huku wakipewa wananchi kutoka Kenya na Msumbiji.

Mwakilishi wa jimbo la Wawi Nassor Saleh Juma alisema kwamba idara ya vitambulisho imekuwa ikiendesha vitendo vya ubaguzi kwa kuwanyima kwa makusudi wananchi wa Pemba haki yao ya msingi ya vitambulisho vya uzanzibari ukaazi.

‘Inasikitisha sana msheshimiwa spika mwananchi wa Pemba ananyimwa vitambulisho vya ukaazi na kupewa Mkenya…..ipo siku tutakuwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Kenya hapa’alisema Nassor.

Nassor ametishia kuzuwia bajeti hiyo kama hatopewa maelezo ya kina kuhusiana kwa nini hadi leo katika jimbo lake wapo watu wenye sifa ya kupewa vitambulisho hivyo lakini wanazungushwa bila ya sababu za msingi.

Mwakilishi wa viti maalumu wanawake Micheweni Pemba Bikame Yussuf Hamad aliitaka Serikali kurekebisha kasoro ziliopo ikiwemo sheria ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi kuhakikisha kwamba kila mtu mwenye sifa anapewa kitambulisho hicho kwa kuwa hivi saa kumekuwepo na malalamiko mengi ya wananchi kukosa haki yao ya kupata vitambulisho.

‘Kitambulisho cha ukaazi wa Mzanzibari ni tatizo katika jimbo langu la Micheweni……wapo watu wengi wenye sifa na umri wa kupewa kitambulisho hicho lakini hawajapewa kwa sababu mbali mbali ambazo sio za msingi’alisema.

Alisema tatizo la baadhi ya wananchi kukosa hati ya kuzaliwa isiwe kikwazo cha wananchi hao kukoseshwa kitambulisho hicho kwani wapo watu waliozaliwa wenye umri wa miaka 70 hawana hati za kuzaliwa.

Mwakilishi wa Jimbo la Kitope Makame Mshimba Mbarouk na Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu wamelalamikia kuwepo kwa vitambulisho vinavyotolewa kwa watu wasiostahiki wakiwemo watu kutoka nje ya nchi mfano Msumbiji, Kenya na nchi jirani za Uganda.

Jussa alionesha mbele ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambavyo wamepewa watu kutoka Msumbiji wenye uraia wa nchi hiyo.

‘Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi tuache kufanya siasa katika suala la vitambulisho vya Uzanzibari mkaazi……hii ni haki ya kila Mzanzibari mwenye sifa sasa kwani nini wananyimwa wazawa na kupewa wageni?’aliuliza Jussa.

Jussa aliwataka watendaji wa Idara ya Vitambulisho kuacha kucheza na siasa chafu ambazo tayari zimepitwa na wakati na kuzikwa na Wazanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi walipoamuwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Jussa alisifu utendaji kazi wa rais wa Zanzibar dk.Ali Mohd Sheni ambaye ameonesha uvumilivu wa hali ya juu katika kuendesha nchi huku akiwa mfano wa kuigwa katika Serikali ya Umoja wa kitaifa.

Mwakilishi wa jimbo la Chake Chake, Omar Ali Shehe alisema kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi ni haki ya kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 18 lakini kwa bahati mbaya hadi leo wananchi wa Pemba imekuwa kikwazo kikubwa wao kuwa na hati hiyo.

Alifafanua na kusema kitendo cha kukoseshwa kwa makusudi kitambulisho hicho kimesababisha usumbufu mkubwa kwa baadhi ya wananchi ikiwemo kushindwa kupata fursa muhimu na haki za msingi ikiwemo kupiga kura katika uchaguzi mkuu.

‘Wananchi wanakoseshwa haki zao za msingi kwa makusudi kwa kisingizio cha kukosa kitambulisho cha ukaazi wa Mzanzibari ambacho ni lazima kwa kila mwananchi……wapo wananchi wanakosa kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa kukosa kitambulisho hicho’alisema.
Mwisho.

maswali na majibu.

smz yasema uvuvi haramu haukubaliki.

SABABU za kuwepo kwa migogoro ya uvuvi katika maeneo ya hifadhi mnemba na ghuba ya minai ni zanzibar kutokana na uchoyo wa baadhi ya wanavijiji.

Hayo yameelezwa na waziri wa wa mifugo na uvuvi Abdilahi Jihad Hassan wakati akijibu wajumbe wa baraza la wawakilishi waliotaka kujua sababu za kuongezeka kwa migogoro ya uvuvi Unguja na Pemba na juhudi za serikali katika kutatua migogoro hiyo.

“Migogoro iliyojitokeza kwa sababu ya ugawaji wa mapato na kuna watu ambao hawamo katika uongozi wa kamati za vijiji ambao wanapinga kujumuisha wenzao katika ugawaji wa mapato” alisema waziri.

Waziri huyo alisema juhudi zimekuwa zikichukuliwa katika kutatua migogoro hiyo ikiwa pamoja na kutoa boti na vifaa vya kisasa vya kuvulia samaki ili wavuvi waachane na uvuvi haramu.

Aidha Serikali imesema haitaruhusu wavuvi kuendesha uvuvi haramu unaoharibu mazingira ya baharini ikiwemo matumbawe na nyavu za kukokota zenye kuvua samaki wachanga ambao hawafai kwa matumizi ya chakula.

Akitoa ufafanuzi wa masuali hayo waziri Fatma Abdullhabib Fereji wakati akijibu swali la mwakilishi wa viti maalumu wanawake kutoka CUF Kazija Khamis Kona aliyeuliza kwa nini Serikali inakataza wavuvi kutumia nyavu za kuvua samaki ambazo zinauzwa na serikali.

Fereji alisema uvuvi haramu haukubaliki kwa sababu tayari umeleta hasara kubwa ikiwemo kupunguwa kwa rasilimali za baharini na uharibu mazingira.

Aidha alisema kwa mfano uvuvi haramu unaotumia nyavu zenye macho madogo haukubaliki kwa sababu umekuwa ukivua samaki wadogo ambao hawafai kwa matumizi ya chakula na hivyo kutoa wito kwa wavuvi kuachana na uvuvi huo.

“Serikali itaendelea kupiga marufuku uvuvi haramu ambao haufai kwa mazingira ya baharini….nyavu za kukokota zenye macho madogo zimepigwa marufuku” alisema waziri huyo ambaye wizara yake inashughulika na mazingira.

Waziri wa mifugo na uvuvi Abdilahi Jihadi Hassan alisema Serikali itaendelea kutoa zana za uvuvi zinazokubalika ambazo hazina madhara ya uvuvi baharini.

Alisema kwa mfano katika Mkoa wa Kaskazini Unguja tayari jumla ya wana vikundi 22 wamepewa zana za kuvua samaki ikiwemo nyavu zinazokubalika ambazo hazina matatizo.

‘Tutaendelea kushajihisha wavuvi kuvua samaki kwa kuzingatia mazingira ya baharini ambapo pia tutaendelea kutoa zana zinazokubalika kwa ajili ya uvuvi sahihi’alisema Jihadi.

Aidha alisema katika mikoa mbali mbali kamati zimeundwa kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuvua samaii kwa kutumia uvuvi unaokubalika ili kulinda mazingira ya baharini.

Alisema nyavu zenye macho madogo,pamoja na uvuvi wa kukokota kwa kutumia nyavu na uvuvi wa kuzamia kwa kutumia bunduki haukubaliki na umepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria ya uvuvi ya mwaka 2010.

Uvuvi wa kuzamia kwa kutumia bunduki umepigwa marufuku kwa sababu ya kuharibu matumbawe kwa kuyavunja wakati mvuvi anapowinda samaki kwa kutumia bunduki.

mwisho.

smz kuendelea kuzikarabati shule kongwe.

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wamelalamikia uchavu wa baadhi ya shule za serikali na kuitaka wizara ya elimu na mafunzo ya amali kuyafanyia matengenezo majengo ya shule hizo ili kuondosha usumbufu kwa wanafunzi na walimu.

Wawakilishi Mohammed Said Mohammed wa jimbo la Mpendae, Mshimba Makame Mbarouk wa Kitope na Mbarouk Mussa Mtando. Walisema wakati wa kipindi cha baraza la wawakilishi kuwa katika majimbo yao zipo shule ambazo ni za muda mrefu na miaka mingi ambazo zinahitaji matengenezo na kuiomba serikali kufnaya kazi hiyo kwa haraka.

Akijibu hoja hiyo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad alikiri kuwepo kwa shule zenye majengo chakavu akitoa mfano shule ya migombani na kusema kwamba shule hizo zinahitaji kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara jambo ambalo wizara ilikuwa ikifanya hivyo.

Alisema baadhi ya shule za zamani majengo yake yamechakaa na juhudi za kuyafanyia ukarabati zitaendelea katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012-2013.

Akifafanua jibu hilo, Zahra alisema kazi za kuzifanyia ukarabati shule kongwe itaendelea ikiwemo kuziezeka bati na kuweka vifaa  milango na madirisha ambavyo vimeharibika kutokana na vitendo vya vijana wahuni wanaoharibu mazingira ya shule.

Zahra alisema baadhi ya matengenezo muhimu yamefanywa katika shule hiyo ikiwemo kujenga jumla ya vyoo kumi na moja,na kuondowa kabisa tatizo la ukosefu wa vyoo hapo,ambalo ilikuwa moja ya usumbufu mkubwa kwa wanafunzi wa hapo.

Mapema Zahra alisema kitengo cha majenzi cha wizara ya elimu na mafunzo ya amali kipo ambacho kazi yake kubwa ni kuzifanyia matengenezo shule zote za Unguja na Pemba.

Zahra alisema hayo wakati alipoulizwa swali la nyongeza la mwakilishi wa jimbo la Ziwani Rashid Seif aliyetaka kujuwa kama kitengo cha ujenzi cha wizara ya elimu na mafunzo ya amali kama bado kipo na kinaendelea na kazi zake.

Alisema kitengo hicho kinakabiliwa na majukumu makubwa ikiwemo kuzifanyia ukarabati shule ambazo zipo katika hali mbaya ya uchakavu ikiwemo zile zilizojengwa kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Zahra alisema kazi hiyo itafanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa bajeti 2012-2013 na kuona majengo ya shule yanakuwa na hadhi na ubora unaotakiwa.

mwisho.

smz kuimarisha vituo vya afya.

Wizara ya Afya imesema inakusudia kuimarisha huduma za afya katika vituo viliopo Unguja ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kupata matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Afya dk.Sira Umbwa Mamboya wakati akijibu swali lililoulizwa na mwakilishi wa viti maalumu Mwanaidi Kassim aliyetaka kujuwa juhudi zinazofanywa na Serikali kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja mjini hapa.

DK.Sirra alivitaja vituo hivyo ambavyo vitaongezwa hadhi yake kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wagonjwa ikiwemo Mpendae,Kwamtipura,Jangombe,pamoja na Mwanyanya,Chumbuni na Chukwani ambavyo vyote vipo mkoa wa mjini magharibi Unguja.

Akifafanua zaidi alisema lengo la kuviimarisha vituo hivyo ni kuweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kutoa huduma bora za matibabu ikiwemo akinamama wajawazito na watoto.

Alisema utekelezaji wa majukumu hayo utafanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012-2013 ikiwemo kuvipatia vifaa hospitali hizo.

Mapema Sirra aliwapongeza wananchi wa Unguja na Pemba kuwa kuhamasika na kuweza kushahihisha jamii ujenzi wa vituo vya afya mbali mbali kwa ajili ya kupata huduma bora kwa wananchi.

Alisema Serikali itahakikisha kwamba inaunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya,ambapo juhudi hizo zitaungwa mkono na Serikali kwa kuzipatia vifaa vya kisasa hospitali hizo.

‘Tutaunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya kwa ajili ya kuimarisha huduma za akinamama wajawazito na watoto kwa ujumla’alisema Sirra.

Advertisements

9 responses to “Vitambulisho 112,420 havina wenyewe

  1. Waziri acha ubabaishaiji kama kweli kuna idadi kubwa ya watu hawajaja kuchukuwa VITAMBULISHO vyao ni kwa nini hamvitangazii wakati kuna Radio ya Serikali pia na tv ya Serikali na Gazeti la Serikali mbona hamuwatangazii. Au ndio mmefanya kama sababu kwmb mwakilishi akihoji kuhusu VITAMBULISHO jawabu liwe watu hawaji kuchukuwa vitambulisho vyao. Acheni usanii dunia mapito tu mtakuwa masuul mbele ya haki.

  2. kwa kifupi sura ya visiwa hivi wanataka kuvibadilisha , lakini subiri tu hata hawa kina makame utafika wakati wataambiwa hapo si kwao tena , hao wanaowakaribisha ndio watakawafukuza kina mwadini. Nd wawakilishi acheni kutia sifa za uongo kwa dr sheni , asizostahiki, ikiwa yeye ni mwadilifu tunataka muungano uvunjike , na yeye keshasema muungano hauvunjika mnamsifu kitu gani alichofanya kizuri zaidi ya kuwa kibaraka wa tanganyika?

  3. Nyinyi mnaotoa vitambulisho kwa wasiokua wazanzibari kwa sababu za kisiasa iko siku mtakuja kujuta. Wapalestina walikua wakifanya hivihivi na leo tunaona hawana tena nchi. Yote wamempa Myahudi. Tusubiri tuone kwani sasa hao mnaowapa vitambulisho washaanza kudai nafasi za ubunge, uwakilishi na siku moja watadai uraisi. Hapo ndio mtatia akili.

  4. HAWA MADOKTA WENGINE KAMA HUYU MIMI SIAMINI KUA AMEFANYA PhD. AU SIJUI NDO PhD ZA TANZANIA MAANA NDANI YA CHAMA TAWALA KUNA PhDs NA PROFESSRIAL NYINGI MNO LAKINI HAKUNA MOJA WANALOLIFANYA ZAIDI YA WIZI NA UFISADI. HATA UKASIKIA MTU ANA PhD AU NI PROFESA AKESHAINGIA HUMO NDANI ANAKUA MJINGA KULIKO HATA ASIKWENDA SHULE. HEBU JAMANI TUAMBIENI HASA KUNA SIRI GANI HUKO MPAKA WASOMI WANAKUA HAWANA MAANA HATA KIDOGO? TUNAO AMBAO KABLA YA KUINGIA HUKO WALIKUA WATU WAZURI TU LAKINI BAADA YA KUINGIA UCHAWINI HAWAFAIIIII.

  5. Kwa hakika tuna mtaka Dr. Shein AWATAKE RADHI WAZANZIBARI Kwa kauli yake ya Kijeuri kwa wananchi anatuonesha nini
    kauli za kibabe hazina nguvu. Na huu upinzani uko wapi aulizwe kakusudiya nini kutowa kauli kama ille na imehusu nini angesema nitaulinda Muungano, lakini sio kusema mimi simuogopi mtu yoyote umemkusudiya nani kama kweli huogopi mtu mwambiye uliye mkusudia uso kwa macho

  6. ACHENI TU WAPEMBA WANA USEMI WAO UNAOSEMA “PUMBAVU LIKIPUMBAA PUMBAA NALO” KWANI NANI KASEMA KUA ANAOGOPWA NA SHENI? AU ANAOGOPA KIVULI HUYO? MTAJE HUYO AMBAE HUMUOGOPI BASI TUMJUE. MWAKA HUU DR MUUNGANO MUNGU AKIPENDA UTAKUFA NDANI YA MIKONO YAKO HATA KAMA UTALINDA KWA KUTUMIA MAJESHI NA POLISI NA DAMU YAKO.

    • Yeye ndo kiongozi lazima awe kama hivyo hata wewe usingependa watu wakutie dosari katika utawala wako.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s