Uzalendo wawakimbiza Wataalamu

Baadhi ya maofisa mbali mbali na wananchi wakiwa katika baraza la wawakilishi wakisikiliza hotuba na michango ya wajumbe inayotolewa na wajumbe wa baraza wa baraza la wawakilishi huko Chukwani Mjini Zanzibar

Serikali ya Zanzibar imesema ukosefu wa uzalendo na tamaa ndio unapopelekea wataalamu wa fani mbali mbali kukimbia Zanzibar. Hayo yameelezwa na waziri wa nchi ofisi ya rais utumishi wa umma na utawala bora, Haji Omar Kheri wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma aliyetaka kujua sababu za wataalamu kuendelea kukimbia nchini.

Mwakilishi huyo apamoja na Mwakilishi wa Salum Abdallah Hamad (CUF) wa Matambwe, Rashid Seif Suleiman (CUF) wa Ziwani na Jaku Hashim Ayoub wa Jimbo la Muyuni (CCM) wote walilalamika kuwa serikali inachangia kuwatorosha wataalamu kwa kuwawekea mazingira mabaya ya utendaji kazi na malipo duni.

“Naomba nikubaliane na wajumbe wa baraza la wawakilishi kuwa nchi nyingi zilizopo kwa janga la sahara hukimbiwa sana na wataalamu wake hususan madaktari wakiwemo pia maprofesa na wahadhiri licha ya kulipwa stahiki mbali mbali” alisema waziri Kheri.

Waziri alisema Zanzibar pia imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kukimbiwa na wataalamu wake hasa kada ya udaktari hospitali ambao wanakwenda nchi nyengine kupata maslahi mazuri zaidi. Hata hivyo waziri huyo alisema miongoni mwa sababu zinazosababisha wataalamu kukimbia ni ukosefu wa maslahi bora na vitendea kazi lakini kubwa zaidi ni kukosa uzalendo.

“Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuimarisha maslahi ya watumishi wake na kuanzia mwaka jana wataalamu mbali mbali walirekebishiwa mishahara pamoja na posho wakiwemo madaktari lakini licha ya hilo kutokana na kukosekana uzalendo baadhi ya madaktari wanaondoka” alilalamika waziri huyo.

Waziri Kheri aliwataka wajumbe wa baraza la wawakilishi kusaidia katika juhudi za kuwashawishi wataalamu waliokuwepo nchini kupenda nchi yao na kuwatumikia wananchi huku serikali ikifanya juhudi za kuimarisha maslahi na mazingira bora ya kazi.

UBOVU WA BARABARA

BANKI ya Dunia inatarajia kutoa fedha zaidi ya billion 1.8 kwa ajili ya mradi wa kuendeleza barabara zinazoingia na kutoka mji wa Zanzibar. Naibu waziri wa miundombinu na mawasiliano, Issa Haji Ussi alisema kazi ya upembuzi yakinifu tayari imefanywa kwa ajili ya barabara hizo zeney jumla ya kilomita 77.9 kwa ufadhili wa benki hiyo.

Akijibu suali kutoka kwa mwakilishi wa nafasi za wanawake (CUF) Kazija Khamis Kona aliyetaka kujua maendeleo ya mradi huo wa barabara pamoja na ujenzi wa daraja ambazo zimechakaa waziri alijibu kwamba serikali imefikia hatua nzuri za kutekeleza mradi huo.

“Mheshimiwa Spika madaraja ya barabara kutoka mjini Zanzibar kwenda kaskazini Unguja mfano Mahonda, Kinyasini na Kitope ni chakavu na inahatarisha usafiri ni lini serikali itaifanyia marekebisho?” alihoji mwakilishi huyo.

Naibu waziri alisema kuwa tayari mandalizi ya michoro na nyaraka za zabuni zimefanywa kwa ushauri wa kampuni ya Intercontinental  Consultants and Technocrats kutoka India na kwamba wakati wowote fedha zitakazoingizwa kazi itaanza.

Alitaja barabara ambazo zitajengwa kuwa ni kutoka mjini Zanzibar, mwembeladu- amani, kariakoo- mwanakwerekwe- tunguu, amani -kiembe samaki na mnazi mmoja –uwanja wa ndege. Alisema serikali itaendelea na juhudi zake za kutafuta wafadhili ili kuimarisha miundombinu ya barabara katika mji wa Zanzibar katika kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano wa magari.

VIKUNDI VYA USHIRIKA

WAZIRI wa kazi, uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika Haroun Ali Suleiman jana ameliambiwa baraza la wawakilishi kuwa serikali serikali ina nia ya dhati ya kuviendeleza vikundi vya uzalishaji mali ikiwa ni juhudi za kupunguza umasikini nchini.

Akijibu suali la msingi kutoka kwa mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM) Salma Mussa Bilal aliyehoji kuhamahama ofisi ya ushirika na juhdi ya serikali ya kuviendeleza vikundi vya ushirika, waziri alisema serikali inachukua juhudi za kuleta mabadiliko katika vyama vya ushirika.

“Mheshimiwa Spika wizara ya kazi, uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika bado haijajipanga vizuri kukabiliana na kutoa huduma kwa vikundi vya ushirika. Kumekuwepo na tatizo hata la kuhamahama ofisi kutokana na kukosa jengo la kudumu” alisema Mwakilishi huyo.

Waziri Haroun baada ya kukiri kuwa ni kweli ofisi ya idara ya ushirika imekuwa ikihama kutoka eneo moja hadi jengine alisema tayari idara ya ushirika imeshapatiwa eneo la kudumu eneo la amani viwanda vidogo vidogo.

“Hii kuhama imesababishwa na mabadiliko ya kiwizara. Aidha wizara inachukua juhudi za makusudi za kutaka kuliendeleza jengo la wizara iliyopo mwanakwerekwe ili idara ya ushirika ipate kuhamia jengo hilo” alisema Waziri.

Aidha alikaa kwamba sio kweli kuwa serikali ya Zanzibar kupuuza idara ya ushirika ni dalili za kushindwa kuviendeleza vikundi vya ushirika na kusisitiza kuwa  vikundi vya ushirika vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi” alisema.

WALEMAVU
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeziagiza  wizara zote na taasisi zake ikiwemo baraza la wawakilishi kuzingatia haki za walemavu katika ujenzi wa majengo yake. Waziri wa nchi ofisi ya makamo wa kwanza wa rais Fatma Abdulhabib Fereji alisema wakati akijibu suali la msingi kutoka kwa mwakilishi wa nafasi za wanawake Salma Mussa Bilal (CCM) kuwa ofisi yake itaendelea kusimamia haki za walamavu visiwani hapa.

Mwakilishi huyo alitaka kujua kwa nini wizara na taasisi nyingi za serikali hazina miundombinu maalumu iliyojengwa kwa kuzingatia haki za watu wenye ulemavu. “Mheshimiwa naomba nikubaliane na wajumbe kuwa taasisi na wizara nyingi hazina miundombinu ya watu wenye ulemavu ambapo hupelekea tatizo kubwa wanapofuata mahitaji yao” alisema waziri.

Fatma alisema taasisi na wizara nyingi zina uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa haki za walemavu na mara kwa mara inazungumzwa suala hilo lakini bado majengo yanajengwa bila ya kuzingatiwa haki za watu wenye ulemavu.

“Ofisi ya makamo wa kwanza wa raia itaendelea kuwakumbusha wizara na taasisi hizo zizingatie suala hilo ikiwemo baraza la wawakilishi ili majengo yote yawe rafiki kwa watu wenye ulemavu” alisema waziri Fatma.

Alisema wakati umefika kwa Zanzibar uwe mfano katika Tanzania na Afrika Mashariki kwa kuzingatia mahitaji na kutoa haki na fursa sawa kwa watu wenye ulemavu ili kuwa na jamii jumuishi.

MWISHO.

WAKATI wajumbe wa baraza la wawakilishi na baadhi ya wananchi wanalalamikia urasimu katika utoaji wa vitambulisho vya ukaazi Zanzibar (ZAN-ID) ofisi ya msajili ya vitambulisho hivyo inasema kuna vitambulisho kadhaa ambavyo havijachukuliwa na wenyewe kwa muda mrefu.

Kamati ya kudumu ya baraza la wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa imesema katika taarifa yake wakati wa kujadili mapato na matumizi ya fedha ya ofisi ya rais kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 kuwa inaambiwa vitambulisho vya ukaazi havijenda kuchukuliwa.

Akisoma taarifa hiyo mjumbe wa kamati hiyo Ali Salim Ali alisema kamati yake iliambiwa kuwa kuna idadi kubwa ya wananchi ambao hawajenda kuchukua vitambulisho vyao kwa muda mrefu. “Tunaiomba ofisi ya vitambulisho kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wende wakachukue vitambulisho vyao ili kuepusha malalamiko yasiokuwa yalazima” alisema Salim.

Aidha alisema kamati yake imeishauri serikali kufanyia marekebisho ya sheria ya usajili wa vitambulisho vya mwaka wa 2005 ili kutoa nafasi wageni wanaoishi nchini Zanzibar kupewa vitambulisho maalumu.

Hata hivyo wakati serikali na kamati inazungumzia kuhusu kurindikana kwa vitambulisho katika ofisi za wilaya za vitambulisho, wajumbe wa baraza la wawakilishi wamesema taarifa hizo sio za kweli na kwamba bado wananchi wengi wananyimwa fursa ya kupata vitambulisho.

Kamati hiyo ilisema zaidi kuhusu matumizi bora ya vitambulisho ya mzanzibari mkaazi kupitia vyombo vya habari yatolewe hususan vyombo vya habari vya serikali. Suala la vitambulisho limekuwa likibuka mara kwa mara katika vikao vya baraza la wawakilishi na katika mikutano ya hadhara ya kisiasa na pia katiak ripoti ya haki za binaadamu ya mwaka huu imeeleza urasimu unaolalamikiwa katika tasisi za serikali.

MWISHO

WAFUNGWA WAONGEZEKA

KUMEKUWEPO kwa ongezeko la wafungwa katika jela za Zanzibar mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita hali ambayo inaashiria kujitokeza kwa uhalifu nchini. Hayo yamebainika katika hutuba ya bajeti ya waziri wa nchi ofisi ya rais iliyosomwa na Dk Mwinyihaji Makame Mwadini katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea mjini hapa.

Alisema kwa mwaka huu uliomalizika 2011/2012 vyuo vya mafunzo (jela) vilipokea wanafunzi 479 ambao kati ya hao wanawake ni 17 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 17 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Waziri alisema pia kuwa mahabusu kwa mwaka huu walikuwa ni 2,620 wakiwemo wanawake 110 katika jela mwaka huu unaomalizika. Hata hivyo waziri alisema kwa bahati nzuri wafungwa pamoja na mahabusu hakuna aliyewekwa kizuizini kutokana na mashtaka ya kisiasa.

“Mahabusu wapatao 2,110 waliruhusiwa kwa dhamana na wengine kuachiliwa kutokana na kuonekana hawana hatia na hakuna mfungwa wa kisiasa” alisema waziri. Waziri huyo alitaja makosa makubwa ya wanafunzi wanaoletwa chuoni (jela) ni kuuwa, wizi wa kutumia silaha, wizi wa mazao, shambulio, kubaka na kuvunja nyumba na kuiba.

Waziri alisema serikali inaendelea na mpango wake wa kuimarisha vyuo vya mafunzo ikiwemo kuhakikisha kuwa wafungwa wanavaa vizuri na wanakula chakula kizuri pamoja na kulala. Hivi sasa katika kuimarisha vyuo vya mafunzo, serikali imepanga kujenga chuo kipya katiak eneo la hanyegwa mchana Unguja ambapo pia kitakuwa na sehemu maalumu kwa ajili ya wafungwa watoto.

Waziri huyo alisema mradi wa ujenzi wa chuo hicho kipya cha mafunzo umeshaanza kwa kusafisha eneo, kununua vifaa vya ujenzi, na kuimarisha miundombinu ya maji na umeme. Pia waziri huyo alisema wanafunzi (wafungwa) wanalima mazao mbali mbali ambayo yatawasaidia kuimarisha afya zao kwa kuwa wameanza kupata milo mitatu kwa siku.

Advertisements

10 responses to “Uzalendo wawakimbiza Wataalamu

 1. kwa kawaida wataalamu wa fani mbalimbali sio sawa na wabunge au wawakilishi , wao ni watu ambao wametumia muda mwingi ktk kutafuta elimu na ujuzi , kwa hio wanahitaji kupewa mafao yanayofanana na kuhangaika kwao ktk wakati wakitafuta elimu , wao si wanasiasa kwa hio kama hawana uzalendo si kitu cha ajabu , nyinyi wawakilishi na wabunge ambao hamna lolote lile zaidi ya utalaamu wa kupiga domo kaya , mbona hamna uzalendo wakati nyinyin ndio mnategemewa kuwa kigezo wa uzalendo , huwa mnataka mambo mazuri mazuri yote mpewe nyinyi kwa kutumia kodi na mapato ya walalahoi wakati kazi mnayofanya haijulikani, Muungano mpaka leo mnashindwa kuuvunjwa kwa kuangalia matumbo yenu na ya watoto wenu , mtawaambia nini wananchi wa kawaida , hebu jipangieni mishahara na marupurupu madogo kabisa kabisa ili mutoe mfano kwa wengine , na hizo pesa zielekezwe kwenye kuwalipa zaidi walimu, madaktari , manesi , mainjiia na wataalamu wengine ambao wamepoteza ujana wao kwa kujifunza taaluma mbalimbali wakati nyinyi mnaenda kuangalia taarabu , wenzenu walipinda migongo kusoma , kwa nini hamuwaenzi? wasikimbie wafanye nini? leo miaka zaidi ya hamsini tangu kufanya mapinduzi haramu yaliyowaua watu na kuwakimbiza wataalamu hata maji yamekushindeni kusambaza ktk visiwa hivi , sina haja kusema umeme uliokuwa haushi kero , mnakaa na matumbo yenu juu hapo barazani kupiga porojo hamna lengine lolote , laana ya mungu itakuwa juu yenu kwa kusimamia haki za watu ambazo hamuwezi kuzilinda .

  • Wataalamu wawe na uzalendo wa nchi gani wakati Wazanzibari hawana nchi yao wala hawana taifa lao. Unataka watu wawe na uzalendo wa mkoa wa Zanzibar chini ya nchi inayojulikana kama Tanzania. Wananchi wengi wa Zanzibar vichwa vinawauma wanapoitwa Watanzania. Ulimwenguni hakuna taifa linaloitwa
   Zanzibar. Rudisheni Taifa la Zanzibar na sote tutakuwa wazalendo na kuijenga hiyo nchi yetu, kwani mtu ni chake.

 2. Wawakilishi tuelezeni nyie binafsi uzalendo mmeutolea wapi ? Kila kukicha wananchi wanadai kura ya maoni, badala yake mnakaa barazani kupongezana.Leo mwaibuka ati watalaamu wanakimbia kwasababu hawana uzalendo wa nchi yao….haya tuu mkuki kwa nguruwe 😀

 3. Mh. Haji Omari Kheri: Nimefurahi sana kwa jawabu lako kuwa wasomim wengi sio wazalendo. Na mimi naomba kuchangia kidogo maana nyie mukisha kuwa kwenuye uongozi huwa hamuonai sabau zinazo wakabili wafanya kazi Zanzibar. Kwanza, heshima ya elimu na watu walio elimika haipo. pili, serikali haitambui wala haithamini wasomi wakizanzibari hata uwe na PHD kwao wao ni upuuzi tu. Seerikali haithamini mchango unao tolewa na wasomi wakizanzibari. Uzalendo ni mbali kabisa na uwajibikaji. Tunakuomba kupitia ofisi yako mubadilike muone kama wazanzibari wasomi hawatarudi makwao kuja kujenga nchi yao. Matatizo ni nyinyi viongozi wetu.
  Mfano mwengine, muna uhafidhina wa hali ya juu katika uongozi wenu. Sasa hivi tukiangaliakutoka juu kwenda chini, tuanze katika wakurugenzi. Sitawataja majina lakini ukisoma majina yao utaona lazima uwe ni ndugu yake fulani, mwanawe fulani, shemegi yake fulani n.k.
  Kama munataka kuzungumzia uzalendo, sis ndio wazalendo natunajuwa kila kitu lakini hatusemi sabau na sisi tunalengo letu na lengo letu sio kukupurushana. Tunaheshimu sana na tunataka tuheshimiana. Hivi siasa za pesa nane acheni.

 4. Hii ya kuwa Zanzibar inakimbiwa na Wataalamu inachangiwa na mambo mengi. Sijui tunafahamu kuwa Zanzibar sasa haikimbiwi tu na Wataalamu bali na Wasio wa Taaalamu pia. Watu sasa wengi wanakimbilia kufanya kazi za majumbani katika nchi za Ghuba. Sijui hawa wakimbizwa na mahitaji au kukosa uzalendo

 5. Kuna watu wamekimbia kwa dhulma, kuuliwa kwa wazee wao pasi na hatia, kunyanywa kwa Mali zao, kufelishwa kwa watoto wao,hawa si wataalamu ni watu wa kawaida tu,
  Lawama ni kwa serekali na mipango mibovu,
  Ajira hakuna,kufelishwa kwa watoto na mishahara midogo ukifananisha na upande wa pili wa muungano,kodi sawa sawa au pengine Zanzibar zaidi, pesa yetu moja vipi tutaweza kupanga uchumi wetu kwenye muungano wa mwenye kondoo 99 alo changanya na wetu mmoja?

 6. Mh. Haji Omar Kheri

  Mimi nachukuwa fursa hii ya kukuweka sawa maana naona umeteleza kwa kutwambia kuwa Wataalamu wamekimbia nchi kutokana na kukosa uzalendo.

  Kwa kweli Wataalamu wengi walioondoka Zanzibar basi utakuta wana Uzalendo ndani ya damu zao nikiwemo mimi kuliko hao waliobaki maana wengi waliobaki wanajitia uzalendo lakini baadhi yao wamejitajirisha katika kipindi cha muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani. Pili, hao unaowaona wewe wana uzalendo ndio waliokuwa wakishika bendera ya kuwatilia fitna wenziwao wafukuzwe makazini kwa kisingizio cha imani yao ya kisiasa nikiwamo mimi.

  Mh. Haji, kubaki kufanya kazi Zanzibar sio kujiveka jokho la uzalendo bali uzalendo ni moyo wa kuitumikia nchi yako na wananchi kwa moyo safi na sio kujilimkikizia mali wakati wengine wako hoi

 7. hata mimi nikipata elimu ckai katika koloni la tanganyika, kazi unafiki tu. raia kila cku marungu na mabomu unafikiri mtaalam gani atakaa?

 8. Hoja ya Mh. Omar Kheiry kuwa kuondoka kwa Wazanzibari Wataalam kwenda nchi nyengine kwa ajili ya kupata kazi imechangiwa na ukosefu wa uzaledo ilizingatia zaidi mitazamo pengine ya kisiasa au kijamii, na kusahau haki za kisheria za kila mzanzibari ya kwenda anakopenda. Haifurahishi kuona mtu anatumia haki yake kwa mujibu wa sheria za nchi halafu mmoja akamlaumu kwa misingi ambayo inamfanya adharaulike kwa jamii. Hii si haki na haitoi sura njema katika kuheshimu haki za watu kwa mujibu wa sheria. Lakini ni kweli kuwa ni vyema Wazanzibari waoneshe uzalendo na huu ni wajibu wa kila raia kwa nchi yake. Lakini cha kutazama hapa ni nini kinawafanya wazanzibari wataalamu wakimbia nchi yao na hususan kwa kuwa ukimbiaji huu ulianza tokea zamani. Jibu la haraka haraka ni kuwa walikosa kuthaminiwa kisaikolijia, kiutawala na hata kimaslahi. Na kuna sababu nyingi za hali hiyo ikiwemo ulegelege wa kufuata mfumo wa utumishi Serikali, hali ambayo ilichangia kutolewa vyeo vya kazi kwa udugu au misimamo ya kisiasa. Hali hii ilifanya baadhi ya wataalamu kujiona hawathaminiwi na kwa hivyo kutafuta sehemu nyengine za kazi ili kupata mahitaji ya kutunza familia zao. Mfano mdogo – katika utumishi wa Serikali ya Zanzibar watumishi wamekosa haki ya kupandishwa vyeo vya kitaaluma kwa muda mrefu.Hii ilifanya hata watumishi wapya na vijana kutokujua kuwa katika kazi kuna haki ya kupandshwa vyeo vya kitaalamu. Kwa maana nyengine utumishi ulikosa dira ya kuwahamasisha watendaji ili waongeze ufanisi.

  Lakini labda sasa SUK inataliona hili na kuandaa mazingira bora ya utumishi ili ufanisi uongezeke. Na labda ndio Mhe. Kheiry akatamka kuwa hakuna uzalendo baada ya kuona kuna uboreshaji wa kiutumishi. Cha kuzingatia sasa sio kuwalaumu hao walioondoka ila ni kuandaa mtandao wa kuwaunganisha hao walioko nje na kuona ni kiasi gani watachangia maendeleo ya Zanzibar. Naamini hili likifanyiwa kazi msaada wa wazanzibari kwa nchi yao utapatikana hususan kwa kuwa kila mzanzibari aliko huwa anaona fahari kubwa kujilabu kwa uzanzibari wake.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s