Jadilini bajeti na punguzeni shukrani na pongezi

Ibrahim Mzee Ibrahim ni Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP)

Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim amewahimiza Wajumbe wa Baraza  la Wawakilishi kuitumia ipasavyo fursa ya kujadili na kuchangia bajeti ya Serikali kwa kulenga mafanikio, matatizo na changamoto ziliopo katika uendeshaji na utekelezaji wa majukumu ya serikali badala ya kusifu serikali na kutoa pongezi pekee.
Amesema ingawa Kanuni za Baraza la Wawakilishi inatowa fursa kwa wajumbe kuchangia kwa muda wa dakika zisizozidi 30, si vyema sehemu kubwa ya muda huo zikatumika kwa pongezi na shukurani badala yake Wajumbe wajikite zaidi katika maudhui ya hoja inayojadiliwa.
“Kanuni ya 58 (6) inatowa muda usiozidi dakika thelathini kwa mjumbe anaechangia hoja ya bajeti. Ni vyema Waheshimiwa Wajumbe wakajizowesha kutumia ipasavyo muda huo wanaopewa kuchangia. Pongezi na shukurani ni muhimu sana lakini zisichukuwe muda mwingi wa mjumbe, muda mwingi utumike kujadili na kuchangia maudhui ya hoja inayojadiliwa” Alifahamisha Ndg. Ibrahim.
“Ngano, hekaya , na visaasili zinaweza kutolewa na mjumbe endapo tu kuna umuhimu na mnasaba wa moja kwa moja na maudhui ya hoja inayojadiliwa. Kinyume na hayo ni vyema kuepuke jambo hilo” Ndg. Ibrahim ameongeza kutahadharisha. Amesema mijadala ya shughuli za kila wizara wakati wa mkutano wa bajeti pia inategemewa ielekezwe kwenye uchambuzi wa sera zinazokusudiwa kutekelezwa na gharama zinazopendekezwa kwa njia ya kodi, ruzuku na mikopo.
Ndugu Ibrahim ametoa ushauri huo leo wakati akiwasilisha mada kuhusiana na mjadala wa bajeti ya serikali katika Baraza la Wawakilishi huko hoteli ya Coconut Tree Village Marumbi, Mkoa wa Kusini Unguja. Aidha wajumbe hao wameombwa majadiiano yao ya bajeti yajikite zaidi katika kuoanisha bajeti inayopendekezwa kuidhinishwa na mikakati ya kiuchumi ya kitaifa na kimataifa kama vile MKUZA , Dira ya Maendeleo ya 2020 na malengo ya Milenium kwa lengo kuangalia uwiano wa vipaumbele vya mikakati hiyo na bajeti husika.
Vile vile amefahamisha kwamba mijadala hiyo ya bajeti inategemewa ilenge katika kuainisha faida au athari za bajeti inayopendekezwa kwa makundi mbali mbali ya watu katika jamii, huku ikiwaslisha maoni, mitizamo,hofu kero na matumaini ya wananchi wanaowakilishwa.
Hata hivyo ndugu Ibrahim amewakumbusha wajumbe kwamba lazima wajiridhishwe kwanza na haja na madhumuni ya kazi inayokusudiwa kufanywa na kiwango kilichotengwa kwa kila shughuli inayokusudiwa kufanywa kabla ya kupitisha bajeti za miradi hiyo.
Ndugu Ibrahim amefahamisha kwamba matokeo halisi ya mijadala hiyo yanatarajiwa yaimarishe uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria na kuzuia udanganyifu , matumizi mabaya na upotevu wa fedha za umma.
Hata hivyo ndg. Ibarahim ametanabahisha kwamba kwa mujibu wa Katiba kazi ya kujadili bajeti ni ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao zaidi ni wanasiasa na mara nyingi si wataalamu wa masuala ya fedha na uchumi hivyo ni vyema wakajengewa uwezo ili wapate ujuzi na maarifa kwa lengo la kukabiliana vyema na dhima hiyo kubwa waliyokabidhiwa na wananchi.
Katika mafunzo hayo mada mbali mbali ziliwasilishwa na Wahadhiri mbali mbali ikiwemo Aina za bajeti, Mageuzi katika Bajeti ya SMZ , Mchakato na Changamoto za Bajeti ya Serikali na Uhusiano wa Bajeti na Ukuaji wa Uchumi.
Wakichangi mada hizo Wajumbe wa Baraza la Wawakiishi wamesema changamoto kubwa inayowakabili ni kucherewa kupata vitabu vya Bajeti jambo linalopelekea kutopata muda wa kutoshwa wa kuipitia kwa kina Bajeti ya serikali.
Wamesema hakuna ushiriki mzuri wa wananchi katika bajeti ya serikali kwani mara nyingi bajeti hiyo hupelekwa kwa Wajumbe ikiwa tayari imeshaandaliwa .
Mapema mafunzo hayo yalifunguliwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Mhe Pandu Ameir Kificho ambae ameelezea kuridhika kwake na juhudi zinazochukuliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP kwa mchango wake mkubwa wa kudhamini mafunzo mbali mbali ya kuwajengea uwezo wajumbe wa baraza hilo.
Mafunzo ho ambayo yamefungwa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe Al Abdullah Ali yamedhaminiwa na UNDP chini ya Mpango wake wa Kusaidia Mabunge yaani Legislative Support Project LSP.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s