Taarifa usajili wa meli za nje

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad akifafanua jambo kuhusu usajili wa Meli uliofanywa na Serikali ya Zanzibar ndani ya Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi huko Mbweni nje ya Mji wa Zanzibar.

Hivyo basi Serikali inatamka wazi kwamba Usajili uliofanywa kwa meli hizi umefuata taratibu zote zilizowekwa kisheria na kwamba Serikali imekuwa ikifanya na itaendelea kufanya mazungumzo na wenye meli mbalimbali ili kuongeza idadi na ukubwa wa meli inazosajili nje ya nchi. Biashara hii ya ukubwa wa GRT 1,388,368 Tons katika kipindi cha wiki mbili na maombi mapya matano kwa meli zitakazokuwa na ukubwa wa zaidi ya GRT 500,000 imeshtua Makamuni mengine na hata nchi nyengine zisizoitakia mema Zanzibar katika juhudi zake za kukuza mapato na uchumi wake.

TAARIFA KWA BARAZA LA WAWAKILISHI JUU YA
USAJILI WA MELI ZA NJE ULIOFANYWA NA SMZ
KUPITIA MAMLAKA YA USAFIRI BAHARINI
ZANZIBAR MARITIME AUTHORITY – ZMA

Mhe. Spika,

Tarehe 27/06/2012 Vyombo vya Habari hapa Tanzania (The Citizen) na nchi za nje (International news Agency – Bloomberg) viliandika makala kuhusu usajili wa meli 10 za mafuta (Tankers). Ilidaiwa katika makala hayo kuwa Meli hizo zilisajiliwa Zanzibar na zinapeperusha Bendera ya Tanzania na kwamba zinafanya biashara na Kampuni ya Serikali ya IRAN. Gazeti la “The Citizen la tarehe 27 Juni, 2012 lilikuwa na kichwa cha habari “Iran Tankers adopt TZ Flag to avoid embargo” (meli za mafuta za Iran zinatumia bendera ya Tz kukwepa vikwazo.

TAARIFA YA ZMA

Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar Maritime Authority – ZMA ni Mamlaka iliyoundwa kwa sheria No. 3 ya mwaka 2009 ambayo pamoja na kazi nyengine inasimamia utekelezaji wa Sheria ya usafiri wa Bahari Zanzibar ya mwaka 2006 (Zanzibar Maritime Transport Act 2006).

Sheria ya Zanzibar Maritime Transport Act 2006, kifungu no. 8 cha sheria hii, kinasomeka kama ifuatavyo:

Section 8 (1). There shall be established the registers of Tanzania Zanzibar ships to be Known as:-
(a). Tanzania Zanzibar International Register of Shipping for ocean going ships; and
(b) Tanzania Zanzibar Register of Shipping for coastal Ships.
(2). A ship shall be a Tanzania Zanzibar ship for the purpose of this Act if that ship is registered under this part.
Katika kutekeleza jukumu la usajili wa meli kama ilivyoelekezwa katika kifungu 8(1)(a) hapo juu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetiliana mkataba na kampuni ya PHILTEX ya Dubai kufanya usajili wa meli za kimataifa. (Open Registry). Usajili huu umekuwa ukifanyika tangu mwaka 2009 na mpaka sasa ZMA kupitia Wakala wake imesajili meli 399 ikiwa ni pamoja na meli za mafuta, makontena, General cargo na meli za Abiria.

Kama nilivyoeleza hapo awali, vyombo vya habari vimechapisha makala ya usajili wa meli 10 ambazo zinadaiwa ni meli za IRAN kulingana na makala zao hizo.

SMZ inatoa taarifa rasmi juu ya meli za mafuta ilizosajiliwa wiki mbili zilizopita pamoja na majina ya meli, ukubwa wake, majina ya makampuni inayomiliki meli hizo na nchi zilizotoka kabla ya kupata usajili kwa ZMA, kama ifuatavyo:

Jina la meli GRT (Ukubwa) Company name Ilikotoka

1. Daisy 81479 Daisy Shipping Co. Ltd Malta
2. Justice 164241 Justice Shipping Co. Ltd Cyprus
3. Magnolia 81479 Magnolia Shipping Co. Ltd Malta
4. Lantana 81479 Lantana Shipping Co. Ltd Malta
5. Leadership 164241 Leadership Shipping Co. Ltd Cyprus
6. Companion 164241 Companion Shipping Co. Ltd Malta
7. Camellia 81479 Camellia Shipping Co. Ltd Malta
8. Clove 81479 Clove shipping Co. Ltd Malta
9. Courage 163660 Courage Shipping Co. ltd Cyprus
10. Freedom 163660 Freedom shipping Co. Ltd Cyprus
11. valor 160930 valor Shipping Co. Ltd. Cyprus

Jumla ya GRT ni 1,388,368 tons

Meli hizi ni 11 kama zinavyoonekana katika orodha hapo juu ni miongoni mwa meli nyingi zinazobadilisha usajili wao (De registration). Meli zilizosajiliwa na ZMA zinatoka nchini Cyprus na Malta. Sambamaba na meli hizi 11 zilizosajiliwa na ZMA, meli za mafuta nyengine 20 ambazo zinasemekana zilikuwa kwenye usajili wa nchi za Ulaya zimebadilisha usajili wao na kwenda usajili wa “TUVALU Islands”.

ZMA ilimtaka Wakala wake Philtex Corporation kuwaita wenye meli hizi na kuwataka kujieleza kuhusu uhusuiano wao na Serikali ya au makampuni ya mafuta ya IRAN. Philtex ilikutana na Wamiliki hao siku ya Alkhamis tarehe 28/06/2012 katika afisi za Philtex Corporation na Wamiliki hao wameeleza kwamba hawana uhusianao na Serikali au mamlaka yoyote nchini Iran na wameamua kuja kusajili meli ZMA kwa ridhaa yao na kwa kufata matangazo ya usajili wetu wa nje (Open Registry).

Pamoja na maelezo hayo, wamiliki hao wametangaza kwamba ikiwa ZMA haiko tayari kuendelea na usajili wa meli zao, wanaweza kufuta usajili wao na tayari wanafikiria kufanya mazungumzo na open Registry nyengine (PANAMA) lakini hawana nia ya kurudi walikotoka, yaani Cyprus na Malta.

Kinyume na maelezo yaliyotolewa na vyombo vya habari juu ya uraia wa wamiliki wa meli hizi, Wamiliki wa meli hizi kama walivyojieleza katika usajili wa meli zao wana uraia wa British Vergin Islands na Sychelles.

Kulingana na “United Nations Convention Law of the Sea”, Article 91, na za “Geneva convection of Registration” articles 6, 7 na 8, na kulingana na Zanzibar Maritime Transport Act of 2006, section 8, Zanzibar ikiwa ni nchi moja kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayo haki ya kusajili meli yeyote kulingana na taratibu na Sheria za Zanzibar, na sheria za Kimataifa zinazoongoza usajili huo.

Maelezo haya yanatolewa ili kutoa usahihi wa uvumi kuwa Zanzibar imesajili meli za IRAN ambazo zimewekewa vikwazo na Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya (European Union) juu ya usafirishaji na uuzaji wa mafuta kutoka Iran.

Mhe. Spika, taarifa hizi za vyombo vya habari hazina madhumuni yeyote zaidi ya kuwavunja moyo wenye Makampuni ya meli wanaotaka kusajili meli zao kwetu.

Hivyo basi Serikali inatamka wazi kwamba Usajili uliofanywa kwa meli hizi umefuata taratibu zote zilizowekwa kisheria na kwamba Serikali imekuwa ikifanya na itaendelea kufanya mazungumzo na wenye meli mbalimbali ili kuongeza idadi na ukubwa wa meli inazosajili nje ya nchi. Biashara hii ya ukubwa wa GRT 1,388,368 Tons katika kipindi cha wiki mbili na maombi mapya matano kwa meli zitakazokuwa na ukubwa wa zaidi ya GRT 500,000 imeshtua Makamuni mengine na hata nchi nyengine zisizoitakia mema Zanzibar katika juhudi zake za kukuza mapato na uchumi wake.

Hata hivyo mamlaka itafata sheria zote zilizowekwa kitaifa na kimataifa katika biashara ya usafiri baharini na itahakikisha meli zinasajiliwa chini ya mamlaka hii zinafata taratibu ilizoweka.

Mhe. Spika, kabla ya taarifa hizi za vyombo vya habari (The Citizen), Waziri wa Uchukuzi wa SMT Mhe. Harisson Mwakyembe) alipokuwa akijibu suala Bungeni hivi juzi hakuonyesha kurishika kwake katika usajili wa meli (Open Registry) inayofanywa na Zanzibar na kuahidi kufanya ziara ya kuja Zanzibar kuonana na Waziri anaehusika kuzungumzia suala hili. Taarifa za “The Citizen” zaweza kuwa ni muendelezo wa Mhe. Mwakyembe kutoridhika kwake katika usajili unaofanywa na Serikali kupitia uwakala wake huko Dubai.

Mhe. Spika, Zanzibar haifungiki kusajili meli za nchi yeyote.
Hili ni suala la kibiashara na kwamba kwa Serikali yetu ni njia moja ya kuongeza mapato yanayoendesha Serikali, alimradi tu usajili huo hauvunji sheria za Kimataifa.

Mhe. Spika,

Zanzibar ina uhusiano mkubwa na wa muda mrefu na nchi nyingi ikiwemo IRAN na hivi karibuni Zanzibar ilipata ugeni (Makamo wa Rais wa Iran) na viongozi wetu walifanya mazungumzo ya namna gani IRAN itaendelea kusaidia Zanzibar katika miradi ya Maendeleo. Zanzibar haingependa kuingizwa kwa visingizio vyovyote na kwa njama zozote katika migogoro isiyowahusu.

Hivyo, kwa taarifa hii, Serikali inakanusha rasmi uvumi wa vyombo vya habari kuhusiana na suala hili kama taarifa hii ilivyofafanua hapo juu.

Mhe. Spika, naomba kuwasilisha.

Hamad Masoud Hamad
WAZIRI WA MIUNDOMBINU NA MAWASILIANO

Advertisements

4 responses to “Taarifa usajili wa meli za nje

 1. Asaalam aleikum,
  Hiyo ndio faida ya Muungano kwani handuguzenu munaojisifia na munaowangamakona hata kuwauwa na kuwapinga mabomu raiya zenu wa Zznzibar kwaajili ya kuwarizisha watu hio ndio fadhila yao kwani kila wakiona Zanzibar inataka kujikwamuwa hufanya kila mbinu ili iangamie halafu hujifanya wao ni wema basi ujue mambo bado watazidi kuiangamiza zanzebar kwama walivyoiuwa biashara na kuipeleka kwao Tanganyika.

  Halafu museme udumu Muungano basi sio udumu sisi tunataka udumuke.

  Tunataka Zanzibar yetu huru hatuna haja ya Muungano anaeutaka mweche ende huko Tanganyika.

 2. UDUMU MUUNGANO! MIONGONI MWA FAIDA ZA MUUNGANO HUU! TOKEA TAARIFA HII ITOKE WATANGANYIKA WANAVYOTUPONDA (JAMII FORUM) JAMANI VIONGOZI WETU TUNAPOKATAA MUUNGANO HUWA HATUNA JAZBA! HII NI HAKI YETU! HAWA JAMAA WANAFITNA SANA! TUNAKOSA HAKI ZETU! HAYA NI MATATIZO. VIONGOZI WETU MUEPUKE VIBURI! SISI TUNAWAPENDA KWA NINI SISI HAMTUPENDI? SERIKALI TWAWAOMBA MULISHITAKI ILO GAZETI! TUONESHE MFANO WAZUSHI! WATAIYONA HIVI HIVI ZANZIBAR YETU! MAHASIDI WA NCHI YETU!

 3. A/alaykum!
  Kwanza baada ya kumshkuru Allah (sw), Nachkua nafasi hii KUMPONGEZA Mh. Waziri kwa ujasiri alioonesha kwa kuongea ukweli mbele ya “KADAMNASI”.

  Mh. Waziri amesema kua kuna nchi ambazo hazipendi kuona ZANZIBAR inaendelea ktk kuongeza Mapato yake ya kuendesha miradi yake,
  HAPA WAZIRI ALIMAANISHA KUA NCHI HIYO NI TANGANYIKA……….

  hatuna budi kumpongeza mh waziri kwa uzalendo alionao na tunawaomba Mawaziri wengine nao waige mfano wake mh. HAMAD.

  Mh. SHAMUHUNA AMKAAAAAAAAA! UAMSHO WAMEKUAMSHA HUKUAMKA BASI SASA UNAAMSHWA NA MAWAZIRI WENZAKO NDANI YA ZANZIBAR (Mh. HAMAD MASOUD, Mh. MANSOUR Y. HIMID NA WENGINE) WOTE HAWA WAKUAMSHENI WATU KAMA NYINYI!

  NA KAMA HIYO HAITOSHI BASI HADI WABUNGE SASA WAMESHAANZA KUAMKA.

  EWE MOLA TUNAKUOMBA UWAAMSHE WATU HAWA KINA “SHAMUHUNA” WAINGIWE NA UZALENDO WA NCHI YAO.

  HAKIKA HAKUNA KISICHO WEZEKANA JUU YA UTUKUFU WAKO.

  KAMA NYOYO ZAO “SHAMUHUNA” ZIMEJAA KUTU BASI TUNAKUOMBA ICHUKUE ROHO YAKEE ILI ASIENDELEE KUKUASI YAARRABB!

  TUNAJUA HAIFAI KUMUOMBEA MTU MAUTI ILA HATUNA BUDI KUFANYA HIVYO YARRABB!

 4. Ripoti hii ya Mheshiwa Hamad haikupaswa kuja Barazani. Hii ni kazi ya Wizara husika kw kutumia Wanasheria wao kutoa notice kwa Gazeti lililoandika kulitaka wathibitishe au walipe fidia amayo change yake ingetumika kununulia madawati kwa watoto wanaokaa chini. Kuleta ripoti hii Barazani inaonesha ni kiasi gani Wizara haijiamini kusimamia mambo yake. Baraza hili likifanywa lisikilize kila kesi mwisho litaamua kesi za watu na wake zao na naogopa hatua hii itatoa mwanya kwa wominizers walio Barazani kuongeza wake zaidi kutoka watakaoachika.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s