SMZ yakerwa na vipeperushi vinavyoleta ubaguzi

Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Ali Salum Haji kulia akibadilishana mawazo na Afisa wa Uchumi na Fedha kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi Ali Natepe huko nje ya Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mbweni nje ya Mji wa Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema haifurahishwi na tabia ya watu wanaojitokeza kuandika vipeperushi vya fitna dhidi ya wananchi wa Unguja, Pemba na Tanzania Bara. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohammed amesema hayo wakati akichangia ufafanuzi wa majumuisho ya wizara yake katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Mjini Zanzibar.

Alisema kumekuwepo na watu wanaosambaza vipeperushi vyenye maandishi ya ubaguzi na kuwagawa watu wa Unguja na Pemba pamoja na Bara ambapo alisema tabia hiyo haiwezi kujenga bali inazidi kuwagawa wananchi ambao wana udugu wa asili kwa miaka na miaka.

Kauli ya Aboud amekuja kufuatia baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kulalamika kwamba wapo watu wanasambaza vipeperushi vyenye meneno ya kuwagawa wananchi wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Wapemba warudi kwao lakini serikali imekaa kimya na kushindwa kukemea jambo hilo ambalo linaweza kuhatarisha amani nchini.

“Mimi  sina haja ya kuwakumbusha wananchi wa visiwa hivi kuhusu madhara ya ubaguzi na chuki za  kisiasa sote tunazikumbuka vizuri sana hatutaki watu waturudishe tunakotoka na napenda nisema kwamba tabia hii ni mbaya sana na serikali haipendi kabisa”alisisitiza Aboud.

Akitoa ovyo kwa watu wenye kusambaza vipeperushi hivyo Aboud alisema serikali haitawavumilia wanafanya hivyo na kuwataka wananchi kuwa macho na wenye tabia hizo kwani lengo lao ni kuwarejesha wazanziabri walipotokab katika chuki na hasama.

Alisema chuki, ubaguzi na uhasama ni vitu ambavyo vinahitaji kupigwa vita sana kwa kuwa madhara yake yanafahamika aktika jamii ambapo wananchi wa Unguja na Pemba wameshawahi kuwa katika kipindi hicho hivyo wananchi wenyewe baada ya kuchoshwa navyo waliamua kutaka mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa ili kuachana na na vitimbi hivyo amabvyo vina athari kubwa kwa taifa.

Aidha Balozi Seif aliwataka wananchi kuitumia fursa iliopo sasa ya amani na utulivu kwa ajili ya kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na nguvu za kuichumi ili kuleta maendeleo kwa wananchi wote.

Awali wakati akichangia bajeti ya ofisi ya makamo wa pili wa rais baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walisema kumekuwepo na watu wakisambaza fitna dhidi ya wananchi kwa kutaka kuwagawa na kuitaka serikali kukemea suala hilo kwani vitendo hivyo vinaweza kuwarejesha nyuma wananchi na kurudi walipotoka katiak siasa za chuki na uhasama.

Vipeperushi hivyo vinawataka watu wenye asili kutoka kisiwa cha Pemba kurudi kwao kutokana na wengi wao kuonesha msimamo wa kutaka kura ya maoni juu ya Muungano Muungano wa Tanganyika na Zanzibar huku baadhi ya watu wenye asili ya Unguja ikisema wao wenziwao ni watu wa Tanganyika kwa kuwa ndio wenye udugu wa damu.

Aboud alisema wananchi wa Unguja na Pemba ni wamoja na Muungano umefanywa kwa kuungana na Tanganyika na Zanzibar na kupelekea kuzaliwa kwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo sio vyema kwa wazanzibari kutaka kuleta fitna kama hizo wakati huu.

SMZ KUPAMBANA NA MADAWA YA KULEVYA

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema imedhamiria kwa dhati kupambana na madawa ya kulevya nchini na kuwaomba wananchi wasaidie juhudi hizo. Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Fatma Abdul-habib Ferej alipokuwa akijibu msuali ya wajumbe wa baraza la wawakilishi huko Chukwani Mjini Zanzibar.

Awali katika suali la msingi la Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM) Panya Ali Abdallah alisema miaka sita tangu washirika wa maendeleo UNDP kutoa msaada wa choo cha flashi cha madawa ya kulevya ambacho kilitegemewa kufungwa katika uwanja wa ndege na kuhoji ni sababu zipi zilizopelekea choo hicho kutofungwa hadi sasa.

Akijibu suali hilo Waziri Fatma alisema alisema sababu za kuchelewa kufungwa choo hicho ni pamoja na kutopatiwa kwa eneo muwafaka mapema kwa mamlaka husika kwa ajili ya kujenga choo hicho hasa kwa kuzingatia mazingira ya eneo husika.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba msukumo mkubwa wa hatua iliyofikiwa sasa ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na mwenyekiti wa tume kwa wakati huo. “Napenda kumjulisha mheshimiwa mjumbe kwamba choo hicho sasa kiemshafungwa, yaliobaki ni mambo madogo madogo tu ya kumalizia ili kianze kutumika” alisema Waziri huyo.

Akijibu suali la mwakilishi huyo kwamba haoni kama kuchelewa kutoa huduma kwa choo hicho kutaweza kuwavunja moyo washirika wa maendeleo, kitendo hicho cha kuchelewa kinaweza kutafsiriwa hivyo.

“Napenda kuungana na mjumbe katika hilo kuwa kitendo chetu cha kuchelewa kinaweza kutafsiriwa na washirika wa maendeoe kuwa ni kuwavunja moyo katika mapambano dhdii ya ya madawa ya kulevya” alisema.

Hata hivyo alisema nia na lengo la serikali kwa ujumla katika vita dhdi ya dawa za kulevya ni thabiti na ila lengo la kuona kwamba inatumia zahudi zake zote katika kukabiliana na janga la madawa ya kulevya.

Alisema pia urasimu kutoka kwa Jeshi la Polisi umepelekea hadi leo kushindwa kufungwa kwa choo maalumu kitakachotumiwa katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya kwa watuhumiwa wanapokamatwa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar ambapo kwa sasa hulazimika kupelekwa hospitali ya mnazi mmoja kwa uchunguzi.

“Kwa kweli naomba niseme kwamba kukosekana kwa choo hakujaathiri hata kidogo vita dhidi ya madawa ya kulevya kwa sababu wanaohusika wanawachukua watuhumiwa na kuwapeleka katika hospitali ya mnazi mmoja na kazi hizo hufanywa huko”alisema Waziri huyo.

Hata hivyo alisema Jeshi la Polisi limetakiwa kutoa makisio ya kazi za kufungwa kwa choo hicho, lakini kwa bahati mbaya hadi leo hawajakamilisha pamoja na kuleta makisio hayo. “Mheshimiwa Spika kwa upande wa Serikali kazi ya kufunga choo hicho pamoja na matayarisho yake yamekamilika lakini tatizo lipo kwa Jeshi la Polisi ambao bado hawajaleta makisio ya kukamilisha kwa kazi hiyo”alisema waziri huyo.

Waziri Fatma alisema usalama wa uwanja wa ndege ni muhimu kwa wageni na weneywe na serikali inaendelea na juhudi za kupambana na waletaji na wasafirishaji wa madawa hayo. Aidha alitoa wito kwa taasisi za dola zilizopewa majukumu ya udhibiti kuunga mkono juhudi za serikali na washirika wa maendeleo katika kukabiliana na janga hilo.

SERIKALI KUTOA HUDUMA ZA MAJI

WIZARA ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar imesema lengo la serikali ni kuwafikishia huduma za maji wananchi wote wa Unguja na Pemba. Naibu waziri wa wizara hiyo Haji Mwadini Makame aliwaambiwa wajumbe wa baraza la wawakilishi wakati akijibu masuala katika kikao cha baraza hilo kufuatia suali la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Matemwe (CCM) Abdi Mosi Kombo aliyetaka kujua serikali imejipanga vipi katika suala la kutatua kero ya upatikanaji wa maji.

Naibu waziri huyo alisema serikali imejipanga vyema katika kuhakikisha wananchi wote wanapata maji kwa wakati muafaka na kuahidi kwamba meli ya waya na vifaa hivi karibuni itawasili katika bandari ya Dar es Salaam.

Awali Kombo alisema tatizo la maji kwenye jimbo la Matemwe kutokana na kisima kidogo Matemwe ambacho hakina uwezo wa kupandisha maji na kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho na kuhoji ni lini serikali itawapatia wananchi wake mashine kubwa ili kuweza kupata huduma hiyo.

Akijibu suali hilo naibu huyo alisema uingiaji wa pampu siku zote unakwenda sambamba na uwezo wa kisima ulichonacho ambacho hutokezea dharura mafundi huweka pampu ndogo ndogo kwa muda wa kuhofia kuwakosesha wananchi huduma hiyo muhimu.

Alisema baada ya hapo hurejesha pampu ambayo inaenda sambamba na uwezo wa kisima kilichopo na kwa sasa tayari kisima cha kiachange kishawekewa pampu ambayo inakwenda sambamba na uwezo wa kisima na hivi sasa maji yanapatikana hadi kigomeni.

Akijibu ni sababu zipi zinzofanya mashine hiyo iunguwe mara kwa mara Naibu alisema “Sababu hasa zinazopelekea kuungua kwa mashine hizi ni hitilafu za umeme ikiwemo umeme mdogo ‘low voltage’ katika eneo hilo ambapo tayari ZAWA kwa kushirikiana na ZECO inafanya jitihada kulitatua tatizo hilo” alisema.

Wananchi watakiwa kushiriki katika sensa

Waziri wa Nchi Ofisi wa Mamo wa Pili wa Rais Mohammed Aboud amewataka wananchi kushiriki katika sensa ya maendeleo ili kuisaidia serikali katika mipango yake ya maendeleo. Kauli ya Aboud imekuja siku chache kufuatia kauli za viongozi wa dini ya kiislamu ambao walitoa tamko la kususia sensa nchini.

Hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari Kiongozi wa Taasisi za Kiislamu Zanzibar Sheikh Farid Hadi Ahmed alisema anaungana na waislamu wenzake wa Tanzania bara kususia sensa hadi hapo serikali itakapokubali matakwa ya waislamu nchini.

“Allah amejaalia nguvu yetu ni katika umoja wetu kivitendo lengo la azimio letu hili ni kuhakikisha tunatoa shindikizo la kutosha ili haki itendeke, kwa maana hiyo basi tunatangaza rasmi kwamba tunawaunga mkono waislamu wenzetu wa Tanganyika katika suala zima la kuikataa sensa ya taifa.

Mbali na sababu zao za msingi, kwa upande wa Zanzibar tunasababu ya msingi na ndio kipaumbele chetu, sijengine ila ni nchi yetu na tunatamka wazi kwamba, hatutashiriki sense mpaka tuipate nchi yetu kwanza” Alisema Sheikh Ahmed.

Aboud alisema wananchi wanatakapojitokeza katika kuhesabiwa kutaweza kuisadia serikali katika mipango yake ya maendeleo kwani bado serikali inahitaji kupata tamwimu za wananchi wake katika maeneo mbali mbali ili kujua namna ya kujipanga katika kuwafikishai maendeleo wananchi wa Unguja na Pemba.

“Lengo la serikali ni kuwafikishia wananchi maendelea katika maeneo yao wanayoishi sasa msipokubali kuhesabiwa serikali haitaweza kujipanga  katika hilo” alisema Aboud. Aidha alisema “Kuna baadhi ya maeneo serikali itahitaji kupeleka huduma ya maji lakini kama haijui idadi ya wakaazi wa eneo hilo itashindwa kwa sababu serikali inafahamu kuwa ina watu 300 wakati kumbe ni watu 600 kwa hivyo hapo mipango ya serikali itakwenda ovyo” aliwaambia wajumbe wao wa baraza la wawakilishi.

Katika hatua nyengine wajumbe wa baraza hilo wameombwa kuwahimiza wananchi kujitokeza katika kuhesabiwa ili kuisaidia serikali kwani jukumu la kuleta maendeleo nchini sio la serikali pake yake bali ni la kila mwananchi.

Katika hatua nyengine Aboud amefanya uungwana kwa kuwataka wazanzibari wote kuheshimiana na kurejea katika hali ya maelewano na uvumilivu na yaliotokea yawe yameshapita kutokana na purukushani na mivutano ya hapa na pale.

“Serikali haitaki kuvutana na masheikh wetu kwani …hawa ni viongozi wa dini na wao ni watu wa busara ambao tunatakiwa sisi tunapokosea waje kutushauri na kutupa maelekezo kwa hivyo naomba niseme kwamba yaliopita sio ndwele basi tugange yajaye” alisema Aboud.

SERIKALI HAINA MSIMAMO WA KATIBA

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema haina msimamo na wala haiwezi kuwashawishi wananchi wakaseme nini katika tume ya kuratibu na kukusanya maoni ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa jana Makamo wa pili wa rais, Balozi Seif Ali Iddi alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali ya katika kikao cha baraza la wawakilishi Njini Zanzibar. “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina maoni wala haina msimamo kwa wananchi wake kuhusu katiba mpya na pia hatuwezi kuwashawishi wananchi wala kuwaandaa utaratibu maalumu wa suala hilo…. maoni ya wananchi yatakuwa ndiyo ya mwisho na yataheshimiwa tunawataka wawakilishi muwaongoze wananchi wakatoe maoni yao katika tume” alisisitiza Balozi Seif.

Aidha aliwatumia lawama wajumbe wa baraza hilo katika suala zima la katiba kutokana na kushindwa kutoa elimu katika majimbo yao na badala yake kuwaachia watu wengine kuwapotosha wananchi. “Serikali haina maoni lakini sisi tuliopo hapa ndio twende kwa watu kwa sababu wajumbe wa baraza hili wamechaguliwa na watu huko majimbo kwani hivyo nyinyi muwawakilishe wananchi katika suala hili muwaelimishe wananchi wenu majimbo lakini msiwapotoshe ….” Alisema.

Na kuongewa kwamba “Tena tunawaomba sana wawakilishi muwe mnawakusanya wananchi majimboni mwenu kuwapa elimu wananchi kwa sababu naamini mpaka sasa hakuna hata mwakilishi hata mmoja aliyewaita wananchi wake jimboni na kuwaeleza suala hili la katiba” alisema.

Alisema hilo ndilo lengo na majukumu ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kutoa elimu kwa wapiga kura wao zaidi katika suala la muungano ikiwemo faida zake, matatizo yake na faida ikiwemo na madhara ya kuvunjika muungano.

“Huo ndiyo wajibu wa wajumbe wa baraza la wawakilishi katika majimbo ya uchaguzi……kutoa elimu kwa wananchi kuhusu muundo wa Muungano na faida zake na hata hasara ukivunjika lakini msiwasemee nyinyi waacheni wenyewe waseme” alisisitiza balozi Seif.

Makamo wa pili wa rais alisema serikali katika suala la katiba limetoa fursa kubwa kwa kuwapa wananchi uhuru wa kutoa maoni kwa njia za salama na kuonya kwamba serikali haitamvumilia mtu ambaye atakwenda kinyume na sheria za nchi.

Kauli ya Balozi Seif imekuja kufuatia maombi ya baadhi ya wawakilishi walipokuwa wakichangia bajeti ya wizara yake ambapo pamoja na mambo mengine waliitaka serikali kutoa muongozo na msimamo wa pamoja kuhusu katiba mpya ili wananchi wasiweze kubabaika waktai wa kutoa maoni katika tume itakapoanza kukusanya maoni mwanzoni mwa wiki ijayo.

“Sio kazi ya serikali kuwashawishi wananchi kuhusu Muungano na kutoa maelekezo yake mbele ya Tume ya marekebisho ya katiba kwani tunaamini suala hilo serikali inawaachia wenyewe wananchi kutumia fursa ya demokrasia kuamua mfumo wanaoutaka wa serikali” alisema Balozi Seif.

Akizungumzia suala la elimu kwa wananchi Balozi Seif alisema wananchi wa Zanzibar wanao ufahamu mkubwa kuhusu suala zima la katiba na kuzitambuwa kero mbali mbali ziliomo katika Muungano ambazo zimekuwa kikwazo kwa maisha yao hivyo hawahitaji kupewa muongozo na serikali.

Akionesha kukerwa na badhi ya watu wanaotumia kampeni ya kukusanya saini za watu kukataa muungano, alisema anapinga kampeni hiyo na kuwataka wananchi waache tabia hiyo na badala yake wajitayarishe kutoa maoni wakati tume itakapofika kuwahoji wananchi.

“Naomba nitoe wito kwa wale wenye kupita kila nyumba usiku na kukusanya saini za watu wakatae muungano naomba waache tabia hii mara moja na wasubiri tume wende wakatoe maoni yao” alisema Balozi.

Alisema tabia hiyo sio nzuri ya kuwasemea watu ambayo inadumaza demokrasia iliopo na kuwataka wananchi waache kufanya hivyo kwani kila mmoja atapewa fursa ya kusema mwenyewe na na hakuna sababu watu kuzungumza na niaba ya wengine.

Akifafanua mambo mengine alitaja masuala ya migogoro ya ardhi kuwa bado yanaendelea kuisumbua serikali lakini aliahidi kuendelea nayo na kamwe serikali haitasita kuchukua hatua za makusudi katika kukabiliana na matatizo hayo.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa imechangiwa na viongozi lakini utatuzi wa migogoro hiyo bado inaendelea na sio kweli kama walivyosema baadhi ya wajumbe kwamba nguvu ya soda ambapo alisema utatuzi wake unahitaji busara za hali ya juu kwani matatizo hayo yameanzia ngazi za juu hadi chini.

Alisema migogoro ya ardhi ni moja ya tatizo ambalo limekuwa likiisumbuwa Serikali akiwemo rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Sheni ambaye amelivalia njuga kulipatia ufumbuzi wake kwa kuwataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na watendaji wengine kulishungulikia katika ngazi za chini.

“Dawa ya migogoro ya ardhi ipo wala mimi sijavunjika moyo….lakini Serikali inalifanyia kazi tatizo hilo kuona kwamba ufumbuzi wake unapatikana, kwani tukumbuke tatizo hili linahitaji busara katika utatuzi wake” aliwaahidi wajumbe hao.

Hata hivyo alisema amepata moyo na matumaini makubwa kwamba baadhi ya maeneo yameanza kupata ufumbuzi wa kero hizo zinazohusiana na migogoro ya ardhi katika ukanda wa pwani ambapo baadhi ya wananchi wamepata muamko wa kwenda mahakamani kuhusiana na kesi hizo.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sauti moja jana walipitisha makadirio na mapato na matumizi ya bajeti ya ofisi ya makamo wa pili wa rais kwa mwaka wa fedha 2012-2013.

Advertisements

7 responses to “SMZ yakerwa na vipeperushi vinavyoleta ubaguzi

 1. Pingback: SMZ yakerwa na vipeperushi vinavyoleta ubaguzi·

 2. ww Aboud kama unasema kwl basi nenda KACHORORA leo kama kwl ww si mnafiki kwa yaleunayosema.Tunashangaa sana leo hii kukurupuka muda wote huo ulikuwa wapi.Basi kama kwl unayosema TUTAONA kwa vitendo si blaablaa. CHACHORORA alitukanwa makamo wa kwanza wa rais na ww upo hujasema kitu nashangaa leo.Lakin inawezekana labda umeota USINGIZINI sawa, Tunamuomba ALLAH akupe nguv insha.

 3. Hofu yangu kwa mchakato wa katiba inaonekana serikali tayari ishaandaa JIBU la mchakato huu. Kwa sababu ni kwa nini TANZANIA BARA bado tu wanaendelea na mchakato wa VITAMBULISHO VYA MTANZANIA wakati huku watu wapo kwenye mchakato wa KATIBA. Hofu yangu ni kwa nini VINATOLEWA VITAMBULISHO hivi je kama kweli Serikali hajaandaa JAWABU la mchakato wa KATIBA ni kwa nini Tanzania bara bado unaendelea wakati inawezekana watu WOTE ZANZIBAR KUKATAA MUUNGANO. Je serikali ndio kweli hasa inajiitia kwenye HASARA kwa kukubali MAONI watu watakao kataa MUUNGANO. Nauliza tena ni kwa nini Serikali ya BARA inagawa VITAMBULISHO vya MTANZANIA na vitegemewa kuja ZANZIBAR wakati bado watu hawajatoa jawabu la mnasaba wa TANZANIA.
  Hofu yangu
  Hofu yangu
  Hofu yangu.
  Naomba dada mpenzi SALMA SAID ukibahatika kuonana na VIONGOZI wetu waulize hili. Ni kwa nn au jawabu la maoni lishaandaliwa mbn hiv. Kama kweli serikali hajaandaa JAWABU bac naisubiri mchakato wa KATIBA uishe ndio tutakuwa na wakati muwafaka wa kufanya hao.
  Hofu yangu serikali imeshaandaa JAWABU ya mchakato wa maoni naomba mnisaidie jamani hofu hofu hofu yangu.

 4. SMZ kwa hili la vipeperushi si kweli mbona Kisonge na Kachochora wanaendelea kuandika. Mbona hata barazani akina Buheti wansema maneno ya kibaguzi dhidi ya Wapemba.

  • wapemba nanyi cmrudi kwenu milimani mnang’angania nn ungujja wakianza unguja kuwafukuza wapemba na cc bara mpango mzima warudi kwao pemba

   • wapemba nanyi cmrudi kwenu milimani mnang’angania nn ungujja wakianza unguja kuwafukuza wapemba na cc bara mpango mzima warudi kwao pemba maana wao ndio waanzisha vurugu eti wanajiita waarabu wapemba wao ni wakujitoa muhanga mtakiona chamoto nawashauri waunguja wazidi kusambaza vipeperushi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s