Nitautetea Muungano -Dkt Shein

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesema ataendelea kuutetea Muungano na hakuna atakaemlaghai wala kumchezea katika uongozi wake. Kauli hiyo ameitowa jana katika mkutano wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika Bwawani mjini Unguja.

Dk Shein amesema kwamba yeye ndie rais wa Zanzibar na ndie mwenye mamlaka na hatomuogopa mtu wala kusita kuwachukulia hatua kwa wale wote ambao watakwenda kinyume na matakwa ya kikatiba.

Alisema kuwa dhamana ya nchi hii pamoja na ile ya Jamhuri ya Muungano imo mikononi mwao kati yake na Rais Jakaya Kikwete na ndio maana wakawa wanashirikiana na kushauriana kwa yale yote ambayo yana maslahi na nchi.

“katika kuiongoza Zanzibar mimi ndie rais simuogopi mtu yeyote”, alisema kwa kujiamini Dk Shein.

Dk Shein alisema Zanzibar ni nchi ya kidemokrasia inayotoa uhuru wa maoni kwa kila mtu, lakini kwa upande wake pia  yeyé ndio mwenye dhamana kubwa ya  kuendesha nchi kwa mujibu wa katiba iliyopo. “Mimi  ndio rais siogopi mtu katika kuendesha nchi, siko tayari kuirudisha nchi katika misukosuko na kuirejesha Zanzibar kule ilipotoka wakati iko katika hali ya amani hivi sasa,” alisema katika mkutano huo.

Hata hivyo alisema kuwa Muungano upo na utaendelea kuwepo na kwani yeye ndiye rais ambaye anatokana na chama cha mapinduzi na pia ameingia madarakani chini ya ilani ya chama chake hivyo lazima afuate ilani ya chama chake ambapo alisema changamoto zilizomo zinahitaji kujadiliwa ili kuweza kuziondoa na sio kuvunja muungano.

“Hakuna mtu asiyejua kuwa kuna kero za Muungano hivyo ni vizuri tukajitokeza kwa wingi katika kutoa maoni yetu juu ya katiba na sio kukaa pembeni yanazungumzwa mengi kuhusu mimi lakini yote nimeyapokea kwa kuwa ukubwa ni jaa”, alisema Dk Shein bila ya kutaja jina lakini alikuwa akijibu hoja zilizokuwa zimeibuka kuwa hana uwezo wa kuchukua maamuzi magumu katika suala la uongozi.

Aliwaeleza wastaafu hao kwamba Muungano una kero, zinazojadiliwa na ndio maana njia nyingi, ikiwemo ya mawasiliano baina ya Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeanzishwa ili kuzitafutia ufumbuzi ambapo alisema njia hizo zitaendelea kutatua mambo ya muungano.

Aidha Dk Shein alisema kazi hiyo anaifanya kwa umakini ili kuhakikisha kuwa Muungano upo na unazidi kuwepo na kwamba wasioutaka wasubiri tume ikija  ndio watoe maoni yao na sio kuanza kutoa maoni hivi sasa kabla ya wakati hufika.

“Hakuna asiyejua katika Muungano kuna kero,…wananchi wazijadili kupitia tume ya mabadiliko ya katiba, na kwa nini tunaanza kusema sema… subirini tume mkatoe maoni yenu” alisema.

Katika hatua nyengine Dk Shein alisema kwa sababu hiyo anaagiza kutokufanyika kwa maandamano ya aina yoyote kuhusiana na suala hilo na  kuwataka wazanzibari  kutoshiriki hadi pale wanaotaka kufanya hivyo wanaporuhusiwa kuandamana na jeshi la polisi kwa kufuata taratibu za kisheria.

“Naagiza maandamano  yasifanyike,…wakiruhusiwa kufanya basi msiende kushiriki,” alisisitiza Dk Dk Shein alikuwa akizungumza na zaidi ya watu 500, waliohudhuria katika mkutano huo,  ambao ni wastaafu wa taasisi za Muungano waliopo Zanzibar.

Katika waliohudhuria katika mkutano huo ni taasisi mbali mbali pamoja na Bunge, Ulinzi na Uslama,  Mambo ya Nje, Mamlaka ya hali ya hewa (TMA), Mamlaka ya Kodi na mapato (TRA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Idara ya Uhamiaji, Shirika la Posta na Simu, na taasisi za masuala ya elimu na ufundi.

Sambamba na hayo aliwataka vijana kuthami ni jitihada, michango na maelekezo ya wastaafu kwa kutambua kuwa uzoefu wao katika maisha ni sehemu muhimu kwa maendeleo yao.

“Sote hatuna budi kuelewa kuwa iko siku tutakuwa wastaafu hivyo ni muhimu kujitayarisha hasa kwa kujenga tabia ya kujiwekea akiba na matayarisho mengine ya lazima kwa maisha ya wastaafu”, alisema.

Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa jumuiya hiyo , Mohamed  Ali Maalim, alisema miongoni mwa majukumu ya jumuiya hiyo ni kudumisha Muungano kwa sababhu unalinda maslahi ya wastaafu wote nchini.

Katika risala yao wastaafu hao wamesema kwamba wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ndani ya Jumuiya yao ikiwemo uwezo mdogo wa uendeshaji na usimamizi wa ofisi ikiwemo ukosefu wa ofisi ya kutosheleza mahitaji.

Katibu mkuu wa Jumuiya hiyo Rashid Ali alitaja changamoto nyengine ni kukosekana kwa wataalamu na waratibu wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya Jumuiya, ukosefu wa vitendea kazi, ukkatika kutekeleza malengo yao.

Jumuiya ya wastaafu Zanzibar imeanzishwa mwaka 2009 ina wanachama 537 ambapo 486 kati ya hao ni wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

 

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI  MOHAMED SHEIN, KATIKA  MKUTANO WA JUMUIYA YA WASTAAFU WA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA- ZANZIBAR, HOTELI YA BWAWANI, ALHAMISI, TAREHE 28 JUNI, 2012.

Mheshimiwa Waziri wa  Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto,

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa  Mjini Magharibi

Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Serikali,

Ndugu Wafanyakazi Wastafu,

Mabibi na Mabwana,

Assalam Alaykum

 

Awali ya yote, natanguliza shukurani zangu kwa Mwenyezi Mungu aliyeumba Mbingu na Ardhi na kila kiliopo kati yake kwa kutujaaliya uhai na afya njema tukaweza kuhudhuria mkutano wetu huu muhimu. Aidha, natoa pongezi kwa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Zanzibar (JUWASEJMUTAZA) na waandaaji wote wa hafla hii kwa kunialika kuwa mgeni rasmi.

Mtu yoyote akisikia leo kuna mkutano wa wastaafu anajenga picha akilini ya kuwa, hapo zipo mada nzito nzito zinazohitaji busara na ufumbuzi wa haraka ndiyo maana wakaamua kukutana. Ni sawa na enzi za zamani kuona wazee wa mtaa wapo jamvini. Mategemeo yangu ni kuwa mkutano huu utakuwa ni muhimu katika kujadili na kupanga mambo mbali mbali yenye mnasaba na maendeleo yenu na ya nchi kwa jumla. Napenda kuelezea furaha yangu ya kuwa pamoja nanyi katika mkutao huu. Ahsanteni sana kwa kunialika.

Ndugu Wastaafu na Wazee Wenzangu,

Ni faraja kubwa kwetu kuona wastaafu wa fani mbali mbali wana jumuiya zao zilizo madhubuti na wanakutana mara kwa mara kwa ajili ya kupanga na kujadili mambo mbali mbali muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Mikutano hii inatufahamisha kuwa ingawaje nyinyi mmeshastaafu lakini mko pamoja nasi kama ni wataalamu waangalizi wa shughuli mbali mbali mlizotuachia kutekeleza na kuziendeleza. Wahenga walisema ‘Mkeka mkuukuu dawa’.

Napenda kukuhakikishieni kuwa Serikali na wananchi wake wote inathamini jitihada zenu na kila saa tupo tayari kupokea rai na maelekezo yenu. Ni wazi kuwa katika mkusanyiko huu wapo wataalamu wa fani mbali mbali. Wapo kati yenu waliokuwa viongozi wakubwa, mashujaa, wakulima wazuri, wavuvi mashuhuri, wahandisi maarufu, wahadhiri waliobobea, na si hasha katika wanachama wenu wapo waliokuwa marubani wa ndege na kadhalika.

Napenda kutanabahisha kuwa katika vichwa vyenu mna hazina mbili kubwa ambazo jamii inazihitaji; nazo ni elimu na uzoefu. Tumefika wakati ambapo unaweza kununua elimu, lakini ni dhahiri hautofika wakati pesa ikatumika kununua uzoefu. Ukitaka uzoefu lazima uende  kwa wazoefu, ambao kwetu sisi ni nyinyi. Hivyo, naomba mtambue kuwa Serikali na wananchi bado wanahitaji uzoefu na ushauri wenu katika mambo mbali mbali.  Jambo zuri kuhusu elimu yenu ni kuwa ‘nguvu zinaondoka mwilini lakini elimu inapenda kubaki kichwani’. Ni wazi kuwa hizi hazina mbili – elimu na uzoefu bado mnazo na zote tunazihitaji. Tunaweza kuwasamehe kwa hili la nguvu lakini kwa hayo mawili niliyobainisha hatuwezi. Kwa kujuwa umuhimu wa watu kama nyinyi katika  jamii yoyote Waingereza  wao walisema ‘Old is Gold’.

Natoa wito kwa wastaafu wote kuelewa kuwa utaalamu na uzoefu katika  fani zenu havimaliziki pale mnapostaafu. Ukweli ni kuwa bado vitu hivyo vinabaki kama ni hazina ambayo taifa inazihitaji wakati wote wa maisha yenu na muwe tayari kuvitoa pale vinapohitajika.

 

Ndugu Wastafu na Wazee Wenzangu,

Mwezi Januari mwaka huu tuliadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964. Tukitafakari na tukikumbuka nyuma tulikotokea, itabainika kuwa wengi wetu, ikiwa siyo sote hapa, ilikuwa ni ile nguvu kazi ya vijana ambayo nchi yetu iliihitaji mara tu baada ya Mapinduzi katika harakati mbali mbali za maendeleo. Baada ya mwaka 1964, zilihitajika jitihada za ziada za kuinua hali za maisha za wanyonge waliokandamizwa na utawala uliokuwepo kabla. Jiitihada hizo ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa nyumba za maendeleo, hospitali na skuli. Aidha, jitihada zilihitajika katika kukuza elimu ili kukidhi mahitaji ya wataalmu katika njanja mbali mbali. Kadhalika, nguvu kazi ilihitajika katika kusambaza huduma nyengine za jamiii ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.

 

Ni nyinyi wastaafu wa hivi sasa ndio mliyokuwa nguvu kazi ya vijana wa nchi yetu waliohitajika ili iweze kubadilisha kwa haraka sana hali duni za maisha ya wananchi wake waliyokuwa nayo wakati huo. Si mwengine ila ni nyinyi vijana wa wakati huo mliotekeleza miradi mingi kwa njia ya kujitolea au kwa maneneo mengine Ujenzi wa Taifa.

 

Mliweza kubadilisha taswira za miji na vijiji vyetu kwa kipindi kifupi na tukaweza kuwa na nyumba za kisasa katika sehemu mbali mbali Unguja na Pemba. Ni nguvu zenu nyinyi mlipokuwa vijana wa wakati huo, mlioijenga hoteli hii ya Bwawani ambayo ilikuwa ni miongoni mwa hoteli bora katika ukanda wa Afirka ya Mashariki na Kati. Ni nyinyi mliojitolea kuwa maaskari wa mwanzo wa nchi yetu na wengine mlishiriki katika vita wakati taifa letu lilipovamiwa na Iddi Amini kwenye mwaka wa 1978. Pia, ni nyinyi mliojitolea katika kutafuta elimu ndani na nje ya nchi ili tuwe na wataalamu wetu katika fani mbali mbali. 

 

Bila ya shaka hii ni mifano michache tu ya jitihada zenu, lakini ni ithibati kamili ya kuwa mliutumia ujana wenu ipasavyo katika kulitafutia maendeleo ya haraka taifa letu. Kwa dhati kabisa, tunawashukuru nyote kwa  uzalendo na michango yenu mikubwa iliyoijengea Zanzibar ya leo misingi imara na bila ya shaka itabaki kuwa ni misingi madhubuti kwa vizazi vyetu vijavyo. Hakuna mja anayeweza kuzilipa jitihada zenu, lakini kwa kuwa mlijitolea kwa nia njema na kwa ajili ya maendeleo ya taifa lenu, sisi daima tunathamni jitihada zenu. Ahsanteni Sana. Wazee walitwambia kuwa ‘Mtenda wema huitendea nafsi yake’. Tunamuomba Mwenyezi Mungu akulipeni malipo mema duniani na akhera kwa michango yenu mikubwa mliyotowa na mnayoendelea kutoa katika ujenzi wa nchi yetu. Amin.

 

Ndugu Wastafu na Wazee Wenzangu,

Tokea mliponikabidhi madaraka ya Urais, nimekuwa nikiwakumbusha  wananchi kitu kimoja muhimu sana kuwa tuwe na utamaduni wa  kujifunza kutoka kwa wazee Ari ya Kujitolea. Vijana wa miaka ya zamani, ambao wengi wao ni wastaafu sasa, walishajiika sana katika suala la kujitolea kwa ajili ya kutafuta maendeleo ya nchi hii. Hii ilikuwa ni siri kubwa ya maendeleo ya haraka tuliyoyapata wakati wa uhai wa Mzee wetu Marehemu Abeid Amani Karume na miaka michache iliyofuata baada ya kuaga dunia.  Ingawaje bado imani na ari hii ipo kwa baadhi ya vijana wetu wa leo na inatupa matumaini kuona kuwa inazidi kufufuka, hata hivyo, lazima tukiri kuwa bado mmetushinda sana juu ya suala hili. Natoa wito kwa wastaafu wote kushirikiana na Serikali katika jitihada zetu za kuhamasisha vijana wetu juu ya kufufua ari ya kujitolea. Pia, nawanasihi vijana kupokea miongozo kutoka kwa wastaafu  na kuendelea  kufanya mambo yetu. Zaidi ya hayo, vijana waendeleze juhudi zao za kudumisha mshikamano na kulinda amani na utulivu kwa manufaa ya nchi yetu.

 

Ndugu Wastafu na Wazee Wenzangu

Nilifurahi sana kupokea ujumbe wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania – Zanzibar (JUWASEJMUTAZA) ulionitembelea Ofisini kwangu Ikulu, tarehe 16 Februari mwaka huu. Mambo tuliyojadiliana na ujumbe wa Jumuiya hii yamenizidisha matumaini yangu kwa wastaafu wetu wote na kuamini kuwa  bado mna ari na hamu kubwa ya kuleta maendeleo kwa manufaa ya nchi yetu.

 

Kwa vile wengine hamkuwepo kwenye mazungumzo hayo, nachukua fursa hii kuwajuilisha kuwa miongoni mwa mada zilizojitokeza katika mazungumzo yangu na ujumbe huo ilikuwa ni kujadili changamoto zinazokukabilini katika  kilimo cha mpunga kwenye Bonde la Cheju, mahitaji ya nyenzo za uvuvi na haja ya kuimarisha umoja wenu kwa kutizama uwezekano wa kuwa na ofisi ya kisasa katika sehemu moja kati ya zile mlizozipendekeza, iwapo nafasi itapatikana.

 

Mada hizi kutoka kwa wastaafu zinaashiria nia yenu thabiti ya kwenda sambamba na malengo makubwa ya Serikali yenu katika kuwatafutia maendeleo wananchi wake.  Miongoni mwa mambo ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Awamu ya Saba, inayoyatilia mkazo ni pamoja na Kilimo, Uvuvi na Ufugaji. Ni faraja kwangu kuona kuwa hata wastaafu nao hawataki kingine ila kwenda sambamba na utekelezaji wa sera na mipango mikuu ya Serikali yao. Hongereni sana.

Ndugu Wastaafu na Wazee Wenzangu,

Michango yenu katika kulinda rasilimali na usalama wa nchi hii nayo pia iko dhahiri na bado ni muhimu kwa maendeleo yetu. Tunaishukuru na tunaipongeza michango mikubwa iliotolewa na askari wastaafu kupitia Umoja wa Maaskari Wastaafu (UMAWA) wakati wa uchumaji wa karafuu. Juhudi kubwa walizifanya kwa kushirikiana na vikundi mbali mbali vya ulinzi shirikishi juu ya kuzuwiya biashara haramu ya magendo ya karufuu hasa Kisiwani Pemba.

 

Matokeo yake ni kuwa tumeweza kupindukia malengo yetu ya awali tuliyojipangia ya ununuaji wa karafuu. Nachukua fursa hii kutoa shukurani zangu kwa  Umoja wa Askari Wastaafu kwa jitihada zao hizi na mategemeo yangu ni kuwa  jitihada kama hizi za pamoja zitafanyika katika misimu myengine ijayo kwa manufaa na ustawi wa uchumi wetu na wananchi wote kwa jumla.

 

Ndugu Wastafu na Wazee Wenzangu,

Umuhimu wa wastaafu katika jamii yetu hauna mipaka, na ndiyo maana wahenga walisema ‘Isiyo kongwe haivushi’.  Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaendeleza jitihada katika kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho ya maslahi ya wastaafu kila hali inapowezekana. Aidha, Serikali  zote mbili zinafanya kila jitihada katika kuharakisha mafao ya Wastaafu wote.

 

Kwa waliokuwa watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nilibainisha jitihada zetu katika hotuba yangu niliyoitoa Uwanja wa Amaan wakati tukiadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar tulizofanya mwezi wa Januari mwaka huu. Wakati tukiwa katika sherehe hizo,  wastafu wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi  Novemba, 2011 walikuwa wameshapatiwa mafao yao, na jitihada kama hizi zinaendelezwa hivi sasa na Serikali zote mbili.

 

Ndugu Wastafu na Wazee Wenzangu,

Nimefurahi kuona kuwa jumuiya za wastaafu zinafanya jitihada mbali mbali za kuimarisha ustawi wa wazee wetu katika makaazi yao ,Sebleni na Welezo kwa Zanzibar na Gombani kwa upande wa Pemba. Nimearifiwa kuwa Jumuiya ya Wastaafu Zanzibar ( JUWAZA) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Walimu Wastaafu na taasisi nyengine wamekuwa wakiwapatia misaada mbali mbali wazee wetu  wanaoishi Sebleni na Welezo. Miongoni mwa mambo ya kuwafariji ni pamoja na kuwawezesha kusherehekea kwa pamoja Siku ya Wazee Duniani inayosherehekewa Oktoba Mosi kila mwaka. Kwa hakika hili ni jambo zuri ambalo linafaa liendelezwe kwani huwaongezea faraja zaidi wazee wetu.

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, nayo imepania katika kuwatunza wazee wetu. Wakati nikiwa katika ziara zangu za Mikoa nilizozifanya kuanzia mwezi wa Machi, mwaka huu, nilipata fursa ya kuwatembelea wazee wa Sebleni na nilipata kujua changamoto mbali mbali zinazowakabili katika kukabiliana na maisha yao  ya kila siku. Tayari tumeshayapatia ufumbuzi baadhi ya matatizo yao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, chakula cha uhakika, usafiri, matibabu na kufanya ukarabati wa baadhi ya majengo na kuimarisha ulinzi katika eneo hilo na kabla ya hapo tulijenga ukuta unaozunguka eneo hilo na kuwawekea askari ili kuwakinga  wao na mali zao  na vitendo vya wizi.

Naamini kuwa tukitekeleza wajibu wetu wa kuwatunza wazee itakuwa tunatekeleza yale malengo mahsusi ya Mapinduzi yetu kama yalivyoelezwa katika Manifesto ya ASP chini ya uongozi wa Jemadari wa Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Natoa wito kwa jumuia mbali mbali za wastaafu na wananchi wote kushirikiana kwa pamoja katika kuwalinda na kuwahifadhi wazee wetu wote tulionao katika jamii yetu kwa kukumbuka kuwa bila ya jitihada zao nchi yetu isingefikia hapa ilipo hivi sasa.

 

Ndugu Wastafu na Wazee Wenzangu,

Tukumbuke kuwa  nyinyi wastaafu mna nafasi kubwa ya kuufanya wakati wa kustaafu kuwa ni wakati  bora wa maisha yenu. Wengi tutafikiri kuwa wakati bora ulikuwa ni wakati wa ujana wetu. Kwa sabubu ya hili na lile au huyu na yule.  Lazima tukumbuke, wakati wa ujana ni wakati wa maguvu  na wakati wa kustaafu ni wakati wa busara. Haiwezekani  nguvu zikashinda busara. Hivi sasa mmevua majukumu mazito na mmewakabidhi vijana. Huu ni wakati wa kukaa na kutafakari maisha yetu na raha zetu bila ya masuala mazito kichwani zaidi ya ibada na michango yetu ya kitaalamu na ya kibusara kwa watoto wetu na jamii kwa jumla. Tujishughulishe na harakati ndogo ndogo zitakazosaidia katika kuimarisha afya zetu, yakiwemo mazoezi na kufanya yale mengi mazuri tuliyokuwa tukiyakosa kwa sababu ya majukumu mazito na ufinyu wa muda tuliokuwa nao.

 

Huu ni wakati wa kukaa na familia, watoto, wajukuu  na virembwe vyetu tukila vizuri huku tukiwaelezea maadili mema na hadithi nzuri nzuri za kusisimua ambazo kila siku vijana wenyewe wanazihusudu na hutamani kila saa kuzisikia. Raha za namna hizi huwezi kuzipata ukiwa kijana.  Ninafuraha kuwaona  nyote hapa mko katika hali nzuri kiafya, bila ya shaka hali hii inatokana na jinsi mnavyojitunza-Mashaallah,  Mwenyezi Mungu akuzidishieni.

 

Ndugu Wastafu na Wazee Wenzangu,

Nafahamu kuwa kwa upande mwengine, maisha baada ya kustaafu yana changamoto zake ikiwa ni pamoja upekwe baada ya kuachana na marafiki tuliozoweana nao tukiwa kazini, mahusiano katika kazi nayo pia huwa na mazowea yake ambayo wakati mwengine huwa taabu kuyasahau. Waimbaji walisema mazowea yana tabu. Najua pia, tunakabiliwa na changamoto ya kupunguwa kwa kipato baada ya kuondoka kwa mishahara au kupunguwa nguvu katika harakati za uzalishaji mali.

 

Katika kukabiliana na changamoto hizo natoa wito kwa wastaafu  kuendeleza mawasiliano na baadhi ya marafiki muhimu mliokuwa nao kazini kwa njia ya kutembeleana mara kwa mara. Aidha, ni muhimu kila siku  kuushughulisha mwili ili kujijengea afya bora. Tabia ya kusoma vitabu vya ibada na vya taaluma nyengine ni muhimu kwa afya ya akili zetu. Aidha, huu ni wakati wa kuwa makini zaidi katika matumizi yetu na tuamini kuwa furaha inaweza kuja bila ya kuwa tajiri. Kadhalika, tuzidi kuziimarisha Jumuiya zetu za Wastaafu ili ziwe na nguvu na ziwe ni sehemu muhimu kwa harakati zetu za kijamii na za kimaendeleo.

Natoa wito kwa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania – Zanzibar (JUWASEJMUTAZA)  kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Jumuiya ya Wastaafu Zanzibar (JUWAZA) pamoja na Jumuiya nyengine za wastaafu kwa lengo la ustawi wa wanachama wao na ufanisi wa kiutendaji wa jumuiya hizi. Aidha, nawasihi wafanyakazi wa Serikali na wasio wa Serikali kujiunga na jumuiya hizi mara tu umri wa kustaafu unapokaribia ili waweze kufaidika na juhudi zao katika kutafuta maslahi na ustawi wa wastaafu.

 

Vile vile, natoa wito kwa vijana  na wananchi wote kuwa tuthamini jitihada, michango na maelekezo yanayotolewa na wastaafu wetu kwa kutambua kuwa uzoefu wao katika maisha  ni sehemu muhimu kwa maendeleo yetu. Kadhalika, sote hatuna budi kuelewa kuwa iko siku tutakuwa wastaafu hivyo ni muhimu kujitayarisha hasa kwa kujenga tabia ya kujiwekea akiba  na matayarisho mengine ya lazima kwa maisha ya wastaafu.

 

Kabla ya kumaliza, napenda kukuhakikishieni kwa mara nyengine tena kuwa Serikali itashirikiana na jumuiya hii katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mlizozibainisha katika risala yenu na nyengine zinazozoretesha shughuli za kila siku za utendaji wa jumuiya hii ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ofisi unaosababisha usumbufu katika kufuatilia haki zenu. Tatizo la ukosefu wa sera rasmi kwa ajili ya wastaafu hili ni suala muhimu linalotaka tulitizame upya kwa haraka hasa tukijuwa kwamba hata sera zilizopo kama za afya, MKUKUTA, MKUZA  hazikumtamka mstaafu.

 

Kwa kumalizia, naitakia jumuiya yenu maendeleo zaidi na napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inathamini sana jitihada zenu kwa maendeleo ya nchi yetu na itaendelea kushirikiana nanyi kila panapohitajika. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kutekeleza mipango yetu kwa ustawi wa nchi yetu na atuzidishie afya njema na baraka katika maisha yetu.

 

Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kwamba Mkutano wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-Zanzibar umefunguliwa.

 

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Advertisements

18 responses to “Nitautetea Muungano -Dkt Shein

 1. inasikitisha kuona raisi mzima anazungumza kama vile amelewa madaraka, nafikiri amelewa kweli , vipi utazungumza kitu kinachotofautiana na wananchi waliokuchagua? samahani nilisahau kuwa uliwekwa na watanganyika, kwa hio kauli yako si ngeni , lakini utaingiza nchi ktk matatizo kama wewe humuogopi mtu kwa sababu una jeshi la watanganyika linakulinda , basi muogope mungu aliyekuumba , asije kukurejesha ktk hali duni, haki za wazanzibari lazima zipatikane ukipenda usipende nd rais , kama wewe kweli humuogopi mtu mbona ukipita na gari lako unakwenda mtutu kama umefukuzwa nchini mwako mwenyewe? na kulindwa mbele na nyuma? mungu akitaka hata ulindwe vipi hakuna kitachozuia kukufika , wakati umefika uunganike na waznz wenzako kujitoa ktk muungano feki kabla hujapoteza heshima ya urais, usisahau kulikuwepo na wafalme na watawala wakafikiri hawana mwisho , lakini umauti ulipowajia wakawa miongoni mwa waliodhalilishwa mbele ya mungu, MUUNGANO HAUTAKIWI UKITUMIA NGUVU BASI UJUE HUNA TOFAUTI NA DIKTETA YOYOTE YULE DUNIANI , UMESAHU KUWA KUNA KIFO UNAKUMBUKA KUNA KUSTAAFU EWE RAISI USIJE KUSEMA HUKUKUMBUSHWA, KAMA UNAVYOKUMBUKA KUSTAAFU BASI UKUMBUKE KUNA UMAUTI BAADA YA KUSTAAFU NA HAYO YANAHITAJI MATAYARISHO MAKUBWA ZAIDI KULIKO YA KUSTAAFU, KUMBUKA KIGEZO CHA MTAWALA MWADILIFU NI MTUME ALIPOFARIKI NYUMBANI KWAKE HATA MAFUTA YA KUWASHIA TAA YALIKUWA HAMNA NA HALI ALIKUWA ANAMILIKI HAZINA YOTE YA UTAWALA WAKE , HAKUFIKIRIA KUCHUKUA CHOCHOTE KTK HAZINA YA BARA ALILOLITAWALA , ALIKUWA HANA MAFAO YOYOTE YALE , LAKINI ALIJITAYARISHA NA MAFAO BAADA YA UMAUTI, , HUYU NDIE MTAWALA AMBAE ANATAKIWA KILA MTAWALA AWE KIGEZO KWAKE , UKUBUMBUSHO UTAWAFAA WENYE KUKUMBUKA.

 2. Asalamu Alaykum. Nina heshima kubwa kukaribisha maoni ya kila mchangiaji na naahidi kuheshimu mawazo hayo. Hata hivyo, kwa ajili ya kulinda mila na desturi adhimu za Kizanzibari, sitachapisha maandishi yoyote yanayokwenda kinyume na utamaduni wetu. Naomba toa maoni yako bila ya kukejeli wala kutukana tafadhali kwani maoni yako ni muhimu sana katika jamii yetu. Na kwa mawasiliano zaidi na mwenye Blog hii tafadhali tumia barua pepe: muftiiy@yahoo.com au simu nambari +255777477101. Shukran. Salma Said

  • Asante sana kwa muongozo huo, inahitaji busara ya hali ya juu kutoa such a balanced caution. Mimi ni Mtanganyika lakini napenda kufuatilia hii blog ili nijielimishe zaidi juu ya Muungano from Zanzibaris’ perspective.
   Wasalaam.

 3. asante nd salma , kama kuna maneno ambayo unahisi si sahihi ktk makala hapo juu , nakuruhusu uifanyie marekebisho

 4. Its so sad, we still have a long way to go and so much to go through for us to get the kind of zanzibar that we want. it hurts like a hell to see zanzibar is being betrayed by its own leaders. they are so pathetic,caring nothing but their walfare, i cant wait to see them dead.
  oh god plz help us,we are going through hell. it has reached a point now that we are ashamed to say we are from zanzibar.

 5. Maoni ya Dr Shein ni sawa na tungetarajia aseme nini hivi sasa. alipopewa dhamana ya kuiongoza Zanzibar kama Rais alikula kiapo cha kuutetea muungano. Hawezi kusema vynginevyo wakati huu. Iwapo kweli maoni ya wananchi yatazingatiwa na kufanyiwa kazi basi Dr Shein na wengineo watajionea wenyewe namna wazanzibari wanavyotaka mabadiliko. Tatizo kubwa ni kuwa Tanzania kama nchi hakuna democrasia ya namna hiyo wanavyosema. Sera ya Tanzania katika siasa ni kuwa siasa ni mbinu za kuwafanya wananchi wakubali wanavyotaka viongozi waliokueko madarakani. Hakuna njia mbadala ya kusikiliza mawazo kutoka chini kwenda juu. Siku zote mawazo mazuri kwao wao ni yale yanayotoka juu ( kwao wao } kuja chani. Tungewaomba wabadilike wenzetu hawa waone kuwa siasa si ujanja ila ni utaratibu. Siasa bila demecrasia ni fujo.

 6. huyu rais naona shibe inamsumbua au anajisahau kuwa hapo alipo ameekwa kuepusha maafa kauli kama hizo si leo keshazitoa nyingi ntuu inawezekana hasomi yaliowafika waliomtangulia mtu mwenye busara na hekima katu hatoi kauli hizo kama kaamua kufata amri za waliomsimika bai pale i tusiseme mengi nafikiri pale maustadh wanapo msifu hujisahau sijui anakusudia nini pale aliposema musiandamane hao polisi wana kesi na rais ndio anawakingia kwenye democracy aliye toa amri kuvamia msikiti walipolipiga kanisa ilikuwa adha mjini leo msikiti umevamiwa wamekaa kimya lakini haya yana mwishoooo

 7. Usiseme mbabe ukweli tunaujua WEWE ni moga kabambe, tena kijiwaziri kisichokuwa na wizara maalum chini ya Ufalme wa Mizengo Pinda. Aibu gani hii!. Eti “mimi simuogopi mtu”

  Wewe umechukua uamumuzi huo because you have no way out ni yatima wa kisiasa Zanzibar, kwa sababu wewe una madaraka lakini huna raia wafuasi ndani za ZNZ wanakupenda au kukutaka ukae hapo kwenye huo URAISI, hata CCM hatukukutaka WEWE usijipendekeze tuliyemtaka anajulikana, “eti mie si mugopi mtu” mfano: Pinda alisema ZANZIBAR SIO NCHI mchana kweupe na kukariri Je! Kama kweli humuogopi mtu babu weye uliitetea Zanzibar kama Raisi?, ndio maana unazungumza kwa kutaka huruma za Dodoma 2015 bila kujali Kisiwa Ndui kwa kuogopa asije kupewa Moh’d Aboud 2015 ambaye anaonekana kupanda cheo huko ginyingi kwa kuwatoa kikowa Wazanzibari walio wengi. Lakini one day yes.

  Tukereeeni lakini mara hii upepo huu ni mwingine kabisa.

  MUUNGANO HUU HATUUTAKI.

  JAMHURI YA WATU ZANZIBAR KWANZA.

  “When peace fails apply force”

  Nawasilisha.

  SERELLY.

 8. kama humuogopi mtu kwa nini alipokutuma ujekusema simuogopi mtu hukukataa?, hukukataa kwa sababu unamuogopa na asieogopa hasemi mimi siogopi

 9. A/Alykum!
  @Mohammed juma/////
  Shekh nakubaliana na ww ni kweli Rais na viongozi wote wamekula kiapo kuilinda na kuitetea katiba ikiwa ni pamoja na kuulinda MUUNGANO.

  HAPA CHA MSINGI NI KWAMBA TUMESHAELEWA KUA HAWA VIONGOZI HAWAWEZI KUIREJESHA ZANZIBAR YETU,
  NA NDIO MAANA TUKAWA TUNASISITIZA KWAMBA ZANZIBAR ITALETWA NA WAZAJNZIBARI WA KAWAIDA!

  Mh. RAIS AMEWAAJMBIA WASTAAFU WASISHIRIKI KTKA MAANDAMANO. HILI MIMI SIONI KUA TATIZO KWANI HAO WASTAAFU WENYEWE NI 500 TU NA HUMOHUMO NDANI YAKE KUNA KUNDI KUBWA TU HALITOKUBALIANA NAE!

  HAPA LA MSINGI NI KUENDELEZA HARAKATI HADI KIELEWEKEEEEEEEEEEEeeeeeeeeee………

  TUJITAHIDI KUWALINDA MASHEKH WETU MUDA WOTE! KWANI TUMEONA YALIYOTOKEA DAR!

  SERIKALI IMEFANYA NJAMA YA KUMVAMIA MWENYEKITI WA UMOJA WA MADAKTARI Tz, NA AMEJERUHIWA VIBAYA SANA, SO Dr. SHEIN ANASEMA KUA ANASHAURIANA NA KIKWETE HIVYO TUWENI MAKINI ASIJE AKASHAURI JUU KUFANYA HIVYO KWA MASHEKH WETU WA JUMUIYA!

  ZANZIBAR KWANZA MPAKA KIELEWEKEEEEE…
  TUACHIWE TUPUMUEEEEEEEEEEEEEE!!!!!!!!!!

 10. KWELI UONGOZI MTAMU, RAISI ANADIRIKI KUSEMA ATAULINDA NA KUUTETETA MUUNGANO KWA JITIHADA ZAKE ZOTE! HE!!! WAZANZIBARI TUMEKWISHA TUSIPO TANNABAHI KULITATUA HILI HATA KWA KUMUUOMBEA DUA YOYOTE ILE TUIYONAYO INAFAA KUMUOMBEA DR. SHEIN, LAKINI HEBU TUMTIZAME SALMINI YUKOJE KWA SASA. TUOMBE KWA MUNGU KWANI MUNGU ANANGUVU KULIKO DR. SHEIN, TUKUSANYIKE TUMUOMBE MUUNGU ATUTEULIE KIONGOZI MWENGINE BAADA YA KUMUONDOA HUYU KWA NJIA AITAKAYO ILE. SAWA!!!!

 11. Kabarikiwa RAİS DKT Ali Mohamed Shein kwasababu anaijua historia ZANZIBAr sio visiwa viwili tu unguja na pemba historia hakuna taifa TANGANYİKA. İtabidi tubadilishe jina la TANZANİA badala yake tuite ZANZİBAR kutokana zanzibar mipaka yake ni kutoka unguja mpaka ziwa victoria unajua hayo ,, kutoka ISTANBU TURKEY ,,

   • wewe unaniambia ninyamaze mimi nimekuja kuhukumu duniya unasia sasahivi unayasikia mabom huko PALESTİNA na ISRAIL wenzio niliwambia kama nyinyi msiponisikia SHARIA YA MUNGU ITAKUA kamawenzenu niliwambia msitege mabom kuauwa wenzenu wakanitukana mpaka matusi yanguoni

 12. Hawa hawapendi kuagizw waishirki kwenye Muungano. Serikali ingewapenda ingewapatia nyezo ili wasiishi kwa kuomba.

 13. PUMBAAAAAAAAAAF. HUU NI UPUMBAVU WA MWISHO. IKIWA WANANCHI WALIOKUPA KURA ZAO HAWAUTAKI HUO MUUNGANO WEWE BADO UTAULINDA KWA NGUVU ZOTE TU ? TUNAKUSUBIRI 2015 WEWE NA KILA MWENYE KAULI ZA KIPUMBAAAAF KAMA HIZI. MTAULINDA MUUNGANO MUKIWA NJE YA HIZO OFISI ZETU TULIZOKUPENI. MUUNGANO UNATUUMIZA WAZANZIBARI KILA KONA NYINYI KWA KUA MNASHIBA NA WATOTO WENU MNAUNGANGANIA TU. HEBU TUACHENI TUPUMUEEEEEEEEEEEEEEEE !

 14. assalaamu aleikum; Wala musiwe na wasiwasi. khatma ya muungano haipo mikononi mwa Rais. Hii ni haki ya wananchi. Wao CCM zanzibar hawana walicho nacho ni kishindo cha “COCA COLA”> Wakati ukifika muungano utavunjika tu. Ishara zote zipo.

 15. jugdment testmone…I will sing of loyalty and of justice,to thee o Lord, I will sing.2 I will give heed toway that is blameless oh when wilt thou come to me? I will walk with integritly of heart within my house. 3 I will not set before my eyes anything that is base hate the work of thos who fall away, it shall not cleave to me 4 perverseness of heart shall be far Iwill know nothing of evil 5 Hem who slander his neighbor secretly I will destroy, the man of noughty heart I will not endure .6 I will look with favor on the faithful in the land. that they dwell with me he who walks in way that blameless shall minister to me 7no man who practices deceit shall dwell in my house no man who utter lies shall continual in my presence.. 8 morning by morning I will destroy all the wicked in the land cutting off all evildoes from the city of THE …LORD ,,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s