Madawa ya kulevya bado ni changamoto

Vijana waliokuwa wameathirika na Utumiaji wa Madawa ya kulevya wakicheza mchezo wa kuigiza namna ya mtu akimia madawa ya kulevya na kuweza kujikinga na utumiaji wa madawa hayo katika Ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya kupiga vita Madawa ya Kulevya Mjini Unguja.

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wamesema serikali haijaonesha juhudi za kutosha katika kupambana na biashara ya madawa ya kulevya Zanzibar. Wakichangia hutuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya afisi ya makamo wa kwanza wa rais wajumbe wa CCM na CUF walisema bado suala la madawa ya kulevya ni kubwa na linalohitajika ni juhudi za kutosha.

“Mheshimiwa Spika ukitaka kuingia Zanzibar kuna njia mbili kuu ambazo ni bandarini na uwanja wa ndege inashangaza hadi hivi sasa bado hakuna juhudi za kutosha za upakuzi wa kutosha katika maeneo hayo” alilalamika Ashura Ali mwakilishi wa viti maalumu vya wanawake.

Mwakilishi huyo alisema kukosekana kwa uchunguzi wa kutosha katika maeneo hayo kunatoa mwanya wafanyabiashara kuingiza madawa ambayo yanaendelea kuathiri vijana wa kizanzibari. Ismail Jussa Ladhu Mwakilishi wa JImbo la Mji Mkongwe alishangazwa na kitendo cha serikali kukaa miaka sita bila ya kufunga choo kinachotumika kutazamia watu wanoasafiri na madawa ya kulevya tumboni.

“Hivi kweli ofisi ya makamo wa kwanza wa rais na makamo wa pili wa rais zitashindwa kutafuta eneo la kuweka choo hicho kwa muda wa miaka sita? Hii ni dosari katika kupambana na madawa ya kulevya” alisema.

Mwakilishi huyo pia alisema kwamba serikali haijaonesha nia ya dhati ya kuwasaidia vijana walioamua kuacha matumizi ya madawa ya kulevya. Jussa alisema watu binafsi wamefanya juhudi za kutafuta nyumba za kuwaweka vijana hao (sober houses) lakini serikali haijatoa mchango wa kutosha kusaidia nyumba hizo ambazo zina program mbali mbali.

“Sober house zinahitaji misaada ya aina mbali mbali na pia vijana wanapotoka katika kutibiwa katika nyumba hizo wanahitaji kazi za kufanya na wasipopata ndio huwa wanashawishika kurejea tena katika matumizi ya madawa hayo” alisema Jussa.

Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe Salim Abdallah Hamad pia aliishauri serikali kuunga mkono juhudi ambazo tayari zimeshaanzishwa na watu binafsi katiak kuwasaidia vijana walioachana na madawa ya kulevya.

Akiwasilisha hutuba ya bajeti ya ofisi hiyo waziri wan chi ofisi ya makamo wa kwanza wa rais, Fatma Abdulhabib Fereji alisema serikali imekuwa ikichukua juhudi mbali mbali za kuhamasisha jamii kushirikiana dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya.

Alisema katika mwaka wa fedha uliopita tume ya kuratibu na kuthibiti madawa ya kulevya ilijipanga ili kuelimisha jamii na wadau mbali mbali juu ya athari za matumizi ya madawa ya kulevya pamoja na kuziendeleza juhudi za asasi zisizo za kiserikali kuendeleza sober houses.

“Katika kuelimisha jamii mikutano mbali mbali imekuwa ikifanywa pamoja na matumizi ya vyombo vya habari hasa televisheni na radio na jumla ya shehia 17 zilifanyiwa ziara za uhamasishaji na taaluma juu ya athari ya madawa ya kulevya” alisema Fatma.

Aidha waziri huyo alisema wanafunzi wapatao 5422 katika skuli 28 walipatiwa taaluma na kuhamasishwa kushiriki kutoa elimu dhidi ya madawa ya kulevya. Waziri huyo aliomba baraza la wawakilishi limuidhinishie zaidi ya 257,091,000 millioni ili kusaidia kitengo hicho cha madawa ya kulevya.

Ofisi ya makamo wa kwanza wa rais imeomba jumla ya shilingi billion 2.7 kwa kazi za kawaida na kazi za maendeleo.

Upungufu wa mbegu za kilimo

Wajumbe wa baraza la wawakilishi wamelalamikia kuwepo kwa upungufu wa mbegu na pembejeo Zanzibar hali ambayo inakwenda kinyume na azma ya kuleta maendeleo ya kilimo nchini. Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub pamoja na wajumbe wengine wametaka kujua mipango ya serikali katika kumaliza tatizo la upatikanaji wa mbegu.

“Kwa kuwa imeamua kuleta mapinduzi ya kilimo ili kupunguza mfumko wa bei kwa nini matayarisho ya upatikanaji wa pembejeo na mbegu hayafanyiki mapema kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo?” alihoji Ayoub.

Pia Mwakilishi huyo alitaka kujua ni wakulima wangapi wamenufaika na kilimo cha matrekta Unguja na Pemba na tani ngapi za mbolea na mbegu zimeingia Zanzibar katika msimu wa kilimo. Akijibu masuali ya wajumbe katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea, waziri wa kilimo na mali ya asili, Suleiman Othman Nyanga alisema mvua za vuli zilizonyesha mfululizo kwa muda mrefu zilisababisha mabonde (mashamba) mengi kujaa maji na kusababisha matrekta kutofanya kazi.

Waziri huyo aliwaambia wajumbe hao kutokana na hali hiyo haikuwa rahisi kuwapatia wakulima mahitaji hasa matumizi ya matrekta kutokana na ardhi kujaa maji. “Kwa upande wa pembejeo za kilimo wizara ilijiandaa vya kutosha ambapo kwa mara ya kwanza tuliweza kutoa tani 322 ya mbegu mboga za mpunga mwaka huu ikilinganishwa na tani 124 mwaka jana” alisema Nyanga.

Aidha alisema maandalizi ya pembejeo za mbolea na dawa za kuulia magugu yalifanywa kwa mapema kwa kuagiza lita 20,000 za dawa ya magugu. Hata hivyo waziri alikiri kwamba pembejeo za mbolea na dawa za kuulia magugu hazikuweza kutosheleza mahitaji ya wakulima wote mwaka huu kutokana na kuwa wakulima wengi wamehamasika na kuitikia wito wa serikali wa kuendeleza kilimo cha mpunga.

“Wakulima wamehamasika hasa baada ya mpango wa ruzuku uliotolewa a serikali, wakulima wengi hivi sasa wanahitaji vifaa, dawa, na pembejeo nyenginezo ili kuimarisha kilimo” alisema waziri huyo.

Waziri Nyanga aliwaeleza wajumbe hao kwamba katika matayarisho yanayoendelea ya msimu ujao serikali itajiandaa vizuri zaidi ili kuweza kuwahudumia wakulima wote kwa sababu lengo la serikali ni kujitosheleza kwa chakula kwa kuleta mapinduzi ya kilimo.

Akitoa mfano ya wakulima wanaonufaiak na huduma za matrekta na pembejeo alisema kwa upande wa Pemba lengo la kulima kwa trekta lilikuwa ekari 2700 lakini kutokana na wakulima kuhamasika ni ekari 4430 sawa na asilimia 217 zililimwa.

MWISHO

Mayatima kujengea nyumba Pemba.

SERIKALI ya Zanzibar imo katika matayarisho ya kujenga nyumba ya mayatima ili kuwaondolea usumbufu watoto ambao wamepoteza wazazi wao. Hayo yameelezwa na waziri wa ustawi wa jamii, maendeleo ya vijana, wanawake na watoto, Zainab Omar Mohamamed wakati akijibu suali la Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM) Viwe Khamis Abdallah.

Mwakilishi huyo alitaka kujua juhudi za serikali za kujenga nyumba za watoto mayatima kisiwani Pemba baada ya rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein kuahidi kufanya hivyo wakati akiomba ridhaa ya kuingia madarakani.

“Mheshimiwa waziri tokea kutolewa kwa ahadi hiyo na rais ya kujengwa nyumba ya watoto mayatima hatua gani zilizochukuliwa hadi hivi sasa?” aliuliza Viwe. Akijibu suali hilo Waziri Zainab alisema kwamba katiak kutekeleza ahadi hiyo wizara yake tayari imeanza kulifanyia kazi jambo hilo.

“Hatua za ujenzi zitaanza wakati wowote uwezo wa fedha utakapopatikana” aliahidi waziri huyo ambaye alionesha kubabaika wakati akijibu suali hilo. Alipotakiwa kutaja kiasi cha fedha zitakazogharimu ujenzi wa nyumba hiyo na  wapi zitapatikana waziri alisema “Kwa kweli katika bajeti hii hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya jengo la nyumba hiyo lakini napenda kuahidi kuwa zitapatikana tu”.

Aidha waziri huyo alisema wizara yake imefanya mazungumzo na shirika la SOS ambalo limeonesha nia ya kuanzisha nyumba ya kuwalelea watoto kisiwani Pemba. Mradi huo alisema pia itasaidia kuwaondolea usumbufu watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika kisiwa cha Pemba.

Nyumba za kulelea watoto iliyopo Forodhani Unguja ilianzishwa na rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume ikiwa na lengo la kuwasaidia watoto waliofiwa na wazazi wao.
Watoto mahabusu

Watoto mahabusu wameanza kutenganishwa na watu wazima katika jela za Zanzibar ikiwa ni juhudi za serikali za kuheshimu haki za watoto. Kauli hiyo imetolewa na waziri wa nchi ofisi ya rais, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini alipokuwa akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua kwa nini watoto wenye umri chini ya miaka 18 wanaendelea kuhifadhiwa katika mahabusu kwa kuchanganywa na watu wazima.

Mwakilishi huyo ambaye kujitokeza kuwa ni muulizaji wa masuala mengi zaidi katika baraza hilo alisema kuwa hali hiyo inaifanya Zanzibar kwenda kinyume na haki za binaadamu na kupuuza haki za watoto ambapo Tanzania imetia saini mkataba wa azimio la kuheshimu haki za binaadamu ambapo Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.

Akijibu suali hilo Dk Mwadini alisema serikali imeipa umuhimu mkubwa suala la haki za watoto kama inavyojionesha katiak sheria mbali mbali zilizotungwa. “Hivi sasa utaratibu umewekwa katiak vituo vya mafunzo kuwatenganisha watoto na watu wazima” alisema waziri huyo.

Aidha Dk Mwadini alisema hivi sasa serikali imeanza ujenzi wa chuo kipya cha mafunzo (jela) katika eneo la hanyegwa mchana wilaya ya kati unguja, watoto watakuwa na sehemu yao maalumu na kupatiwa huduma zote wanazostahiki.

Alisema sio kweli kuwa serikali haijachukua hatua na inawapuuza watoto wanaohukumiwa kwa makosa mbali mbali na kupelekwa jela. Wajumbe mbali mbali wa baraza la wawakilishi wamekuwa wakilalamikia watoto kuchanganywa na watu wazima katika jela za Zanzibar hali ambayo inawaweka watoto katika hatari ya kunyanyaswa pamoja na kubakwa.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s