Wananchi watakiwa kuwa makini

Waziri wa Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Mwinyihaji Makame akiwa pamoja na Waziri wa Katiba na sheria wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya Baraza la Wawakilishi huko Mbweni nje ya Mji wa Zanzibar.

KAMATI ya kudumu ya baraza la wawakilishi ya kusimamia viongozi wakuu wa kitaifa imewashauri wananchi  kuwa makini na kusoma katiba za nchi wakati wakisubiri mchakato wa kutoa maoni yao katika tume ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Salum Haji aliyasema hayo wakati akiwasilisha maoni ya kamati yake mbele ya wajumbe wa baraza la wawakilishi ambapo alisema wakati huu wa kutoa maoni ya katiba mpya ni muhimu kwa wananchi wote kwani katiba ndio msingi wa Taifa.

“Tunawashauri wananchi wetu kuzisoma katiba zetu zote mbili na kujua mapungufu yaliopo ili kujua kile wanachokifanya wakati wa kutoa maoni yetu, lakini kamati yangu imegundua kuwa Wazanzibari wengi  hawaijui   Katiba zote ikiwemo hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa hali hiyo sijui tutegemee ni kipi watakachokuja kukichangia kwenye Tume ya Kukusanya Maoni Kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano”. Alisema Haji.

Alisema licha ya kuwa serikali imechelewa kujipanga na kukaa pamoja na kuwauliza wananchi wote wa Zanzibar nini tatizo na wanahitaji nini nini wakati wa kutoa maoni lakini ipo haja na kujipanga hivi sasa.

“Naamini tutaweza kuondoka na jawabu moja na tukiwaelekeza wananchi wetu naamini watatuelewa na watajua wanachokifanya, kwa hiyo kazi hiyo sio ya kuiachia Serikali peke yake, zaidi ni kazi yetu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi sote kwani wao ndio waliotuleta hapa ili kulinda na kutetea maslahi yao” Alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema kwa kuwa kwa muda mrefu watanzania na wazanzibari wamekuwa wakitumia katiba ikiwa ndio nyundo na majembe yao katika kutekeleza majukumu yao basi ni lazima ni muhimu serikali isaidie kutoa elimu majimboni kwa wananchi.

Mwenyekiti huyo amesema licha ya kuwa kumekuwepo na vikao mbali mbali vya kutatua mambo ya muungano lakini bado tatizo lipo pale pale hivyo kuja kwa tue ya kukusanya maoni ya katiba mpya iwapo wananchi wataitumia fursa hiyo inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha matatizo ya wananchi wa pande mbili hizo za Muungano.

“Vikao mbali mbali vya Makatibu  Wakuu ,Mawaziri na vikao  kati ya  Waziri Mkuu, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar lakini bado matatizo yapo pale pale na yanaendelea kuwepo na yanaonekana hayatamalizika” Alisema.

Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema “Muarubaini wa matatizo au Kero za Muungano wetu ni kuwa na katiba ambayo itakayobainisha na kuzitambua haki za kila upande wa Muungano” Aliwaambia wajumbe wa baraza hilo.

Aidha alisema ipo haja ya kutofautisha kero zitashughulikiwa na kila nchi katika Muungano huo na zipi zitashughulikiwa na chombo cha Muungano ili kurejesha imani kwa wananchi kwani wananchi wengi wamepoteza imani na utatuzi wa kero za muungano.

“Nchi itakayo mlaumu mwenzie kama aidha ni mzigo au anaonewa na mwenziwe. Sio kama ilivyo hivi sasa kuwa kuna Mamlaka moja imebeba mambo ya kwake na ya Muungano ambapo mwingine anahisi kuwa kuna haki zake za msingi ananyimwa na mwenzake, na hii ndio inayopelekea kuwepo kwa manung’uniko ya kila siku kwa upande mmoja ambapo yamefikia kupachikwa jina na kuitwa kero za Muungano” alisema Haji.

suala la ker za muungano limechukua nafasi kubwa katika vikao vya baraza la wawakilishi tokea lilipoanza wiki mbili zilizopita ambapo Mwenyekiti wa kamati huyo alisema “Katiba ya Jamhuri ya Muungano,  Wizara za Muungano wa Jamhuri ya Tanzania ni chache mno,  lakini kiuhalisia Mawaziri wote waliopo Tanzania Bara wanafanya kazi zao kama ni Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Sasa, je! tujiulize, hii ndiyo sahihi?” alihoji Mwneyekiti huyo.

Alisema katiba ya Jamhuri ya Muungano, kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa kifungu cha 64 cha katiba ya Muungano, mamlaka yake yanaishia hapa Zanzibar tu basi, tafsiri hiyo inabaki kuwa ni sahihi na wajumbe wenyewe wamekubali kwani wameshiriki katika kupitisha hayo mambo ya Muungano kupitia wabunge wa Zanzibar ambao tangu mwaka 1964, wanashiriki katika maamuzi makubwa ndani ya Muungano.

Kwa hiyo kama wananchi na viongozi tunahisi mambo yalivyo kwa wakati huu sio sahihi basi ni lazima tuirekebishe katiba yetu hii na hivi sasa wananchi wako huru kuzungumza wanachokitaka lakini kwa kufuata utaratibu na Sheria za Nchi zilizopo na hakuna wakati mwengine isipokuwa ni wakati huu wa kutoa maoni kuhusu katiba tunayoitaka itutawale hapa Nchini petu, katiba ambayo kila Mtanzania atajivunia popote Duniani atapokwenda na kuiga mfano wetu.

“Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa liliopo hapa kwetu ni kuwa wananchi wengi wanaisoma katiba ya Zanzibar pekee bila ya kuiangalia Katiba ya Jamhuri ya Muungano na hufanya maamuzi yao kwa kutumia katiba moja tu, wakati hivi sasa tunasubiri kutoa maoni ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Ni lazima watu wetu hasa vijana  tuwaelimishe vya kutosha” aliwaambia wajumbe wenzake.

MWISHO
HALI YA UCHAFU ZANZIBAR

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wamelalamikia hali ya usafi katika mji wa Zanzibar wakati ambapo baraza la Manispaa linakusanya ada ya usafi kila mwezi. Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe (CUF) Salim Abdallah Hamad walitaka kujua sababu za uchafu kuzagaa katika mji ambao ni wa kitalii.

Akijibu suali hilo pamoja na masuala mengine ya nyongeza, Waziri wan chi ofisi ya rais anayehusika na seikali za mitaa Dk Mwinyihaji Makame Mwadini alisema uchafu unatokana na upungufu mkubwa wa vitendea kazi.

“Baraza la manispaa linatoza ada ya huduma za ufasi kwa wafanyabiashara na wakaazi wa mji kwa mujibu wa kanuni ya manispaa. Na wafanyakazi wanajitahidi kufanya usafi tatizo ni upungufu wa vitendea kazi” alisema waziri.

Alisema kila siku wafanyakazi wa baraza la manispaa wanafanya usafi na kuweka katika mji katika hali nzuri na kwamba mashirika mengine binafsi yana fursa ya kusaidia. “Kwa kuwa usafi wa mji unaweza kufanikiwa kwa mashirikiano ya pamoja baina ya wananchi na manispaa, manispaa iko tayari na imeshajihisha vikundi vya mazingira zaidi ya 17 kwa lengo la kushirikiana katika kutoa huduma za usafi katika shehia zote za mjini” alieleza waziri huyo.

Waziri Makame alisema baraza la manispaa limeanzishwa kitaratibu kwa kufunga mikataba na vikundi mbali mbali ili kuwa mawakala katika kukusanya ada na kuimarisha takwimu za huduma za usafi.
Wajumbe hao wa baraza la wawakilishi walitakiwa kusaidia kuhamasisha wananchi katika suala la kudumisha usafi ikiwemo kutotupa taka ovyo.

MWISHO

UDANGANYIFU WA MISHAHARA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Haji Omar Kheri amesema hivi karibuni baadhi ya watumishi wa serikali walifanya udanganyifu katika elimu zao na kulazimisha serikali kupunguza mishahara yao.

Akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Mjini Zanzibar, Waziri alisema kwamba hivi sasa serikali ipo makini katika kufuatilia viwango vya elimu kwa watumishi wake.

“Wapo baadhi ya watumishi waliwasilisha wizarani vyeti vinavyoonesha viwango vya juu ya elimu kinyume na hali halisi na baada ya uchunguzi wa kina tumewapunguzia mishahara yao” alisema Kheri. Na kuwaonya watumishi kuepukana na udanganyifu.

Jaku pamoja na baadhi ya wajumbe wengine walitaka kujua sababu zilizopelekea serikali kupunguza viwango vya mishahara vya baadhi ya watumishi wake wakati ambapo serikali imefanya marekebisho viwango vya mishahara.

Aidha wajumbe wa baraza la wawakilishi walitaka kujua kwa nini kuna tofauti za viwango vya mishahara katika baadhi ya taasisi za serikali na mashirika. Waziri Kheri akijibu suali hilo nyongeza alisema kwamba sheria za utumishi zinaruhusu mashirika kuwalipa wafanyakazi wake mshahara mzuri kulingana na uwezo wa shirika hilo.

“Kima cha chini cha mishahara cha serikali ni 125,000 fedha za Tanzania mfano shirika la bandari wanalipa kiwango cha chini 144,000 na mashirika mengine yanaruhusiwa kufanya hivyo kulingana na kipato cha mashirika hayo” alisema waziri huyo.

Waziri aliwaambia wajumbe wa barza hilo kwamba tangu kupandishwa kwa viwango vipya vya mshahara mwaka jana serikali imekuwa ikifanyia marekebisho hayo kwa wafanyakazi wote na kukanusha kuwa wapo wafanyakazi ambao hawajaanza kufaidika na mabadiliko hayo.

Hata hivyo waziri alisema kama wapo watumishi wenye malalamiko wawasilishe kwa mamlaka zinazohusika ili malalamiko yao yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.

MWISHO

UHARIBIFU WA MAZINGIRA

WIZARA ya Mawasiliano na Miundombinu imelaumiwa kwa kuchangia katika uharibifu wa mazingira katika Kisiwa cha Pemba. Lawama hizo zimetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma ambaye alisema kwamba katika baadhi ya maeneo ambayo kumechimbwa mchanga, mashimo makubwa yanahatarisha usalama wa wananchi wa maeneo hayo.

Akitoa mfano wa uharibifu huo Mwakilishi huyo alitaja kijiji cha Makaani Vitongoji Pemba na baadhi ya vijiji vya Kibokoni, Udusini na Vumba sehemu ambazo zimeharibika kabisa kwa uchimbaji wa mchanga.

“Mheshimiwa Spika wizara inachangia kwa kuharibu mazingira kwa uchumbaji wa mawe na mchanga na uchimbaji huo umekuwa mkubwa kiasi cha kusababisha kuzuka kwa maji ya chumvi katika mashimo ambapo ni uharibifu mkubwa wa mazingira” alisema Mwakilishi huyo wa Wawi.

Akijibu lawama hizo, Naibu Waziri wa wizara hiyo Issa Haji Ussi alisema wizara yake imekuwa ikichukua hatadhari zote wakati wa uchimbaji wa mawe na mchanga kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
“Mheshimiwa Spika wizara yangu inaendelea kufata taratibu na maelekezo yote yanayotolewa na idara ya mazingira na hadi hivi sasa hakuna eneo amablo limechimbwa na kutoa maji ya chumvi katika mashimo” alikanusha.

Naibu waziri huyo alisema uchimbaji wa mchanga na mawe katika maeneo ya Micheweni, Kangagani, Mwambe na maeneo yaliotajwa, wizara yake kwa kushirikiana na wananchi kwa kutafukia mashimo hayo  na kuwashajiisha kupanda miti kuhifadhi mazingira.

Katika kuonesha kutokuridhika na majibu ya naibu waziri huyo, Mwakilishi huyo alimtaka naibu waziri huyo wende pamoja kisiwani Pemba akamuoneshe uharibifu wa mazingira ambao pia yanachangia kuwatia njaa wananchi wanaotegemea matumizi ya ardhi ya kilimo amabyo sasa imejaa maji ya chumvi.

MWISHO

UDANGANYIFU WA MITIHANI


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imethibitisha kuwa wanafunzi walifanya udanganyifu katika mitihani iliyopita na kuahidi hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya walimu na maafisa waliohusika.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Zahra Ali Hamad alipokuwa akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliyehoji iwapo Zanzibar ilijiridhisha na sababu za kufutwa kwa matokeo ya mitihani ya kidatu cha nne mwaka jana.

“Mbali na baraza la mitihani la taifa NECTA wizara yangu kwa kutumia wataalamu wa Zanzibar walifanya utafiti na kuthibitisha kuwa wanafunzi walifanya udanganyifu na hivyo kukubaliana na NECTA” alisema Zahra.

Alisema kwamba matokeo ya watahiniwa 3030 walifutiwa mitihani yao lakini baada ya kilio cha wanafunzi hao na wazazi watahiniwa hao wataruhusika kurudia mitihani mwakani 2013. Zahra aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba hatua zaidi zimekuwa zikichukuliwa ili kuzuwia vitendo vya udanganyifu visijitokeze tena ikiwa ni pamoja na kuwataka maafisa na waalimu waliosimamia mitihani mwaka jana kujieleza.

“Tumewaandikia barua na baadhi yao wameshajibu, tunafanya uchunguzi na wote watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria” alisema Naibu waziri huyo.

Aidha aliwataka wajumbe wa baraza hilo pamoja na walimu kushirikiana kupiga vita udanganyifu katika mitihani ili kuwa na wanafunzi bora watakaosaidia maendeleo ya taifa siku za baadae.

MWISHO

MSONGAMANO WA WAGONJWA

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema wingi wa wakaazi wa vijiji vya Mwera na vijiji vya jirani vimechangia kuwa na msongamano katika kituo cha afya cha Mwera na kusababisha wizara kulazimika kupandisha kituo hicho daraja.

Naibu Wzairi wa wizara hiyo, Dk Sira Ubwa Mwamboya aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kuwa hivi sasa wizara yake kupitia ufadhili wa benki ya maendeleo ya afrika ADB ina mpango wa kukifanyia utanuzi na ukarabati mkubwa kituo hicho.

“Kukifanyia utanuzi na ukarabati mkubwa kituo cha Mwera ikiwemo kuongeza wafanyakazi wa kutosha na wenye sifa tutatoa huduma za ziada” alisema naibu waziri.

Dk Sira aliwajulisha wajumbe wa baraza hilo kwamba  miongoni mwa juhudi za haraka ambazo zinachukuliwa katika kuimarisha kituo cha Mwera ni bodi ya afya ya kituo hicho imeshajenga jengo pembeni mwa kituo kwa ajili ya utawala, famasia na ofisi ya bodi.

Alisema kukamilika kwa kituo cha afya Mwera Pongwe na pia utakapomalizika ujenzi wa kituo cha afya Kinuni, idadi kubwa ya wananchi itapungua kwa kupata huduma katika vituo hivyo.

Dk Sira alisema Zanzibar hivi sasa inajivunia kwa kuwa na vituo vingi vya afya kwa wastani wa kilomita tano katika maeneo yote ya Zanzibar. Akielezea changamoto katika utoaji wa huduma za afya, Dk Sira alitaja upungufu wa vitendea kazi na wataalamu na kwamba serikali imeelekea kuimarisha vituo vya afya badala kujenga vipya.

MWISHO

UNYANYASAJI WA KIJINSIA NA UBAKAJI

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi jana waliendelea kulalamika kuendelea kuongezeka kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia Unguja na Pemba. Wakizungumza katika kikao cha baraza la wawakilishi wakati wa masuala na majibu, wajumbe hao waliitaka serikali kuchukua hatua ili kupunguza unyanyasaji ikiwemo ubakaji na kulawiti watoto.

Akijibu malalamiko hayo, Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Watoto na Wanawake Zainab Mohammed Omar alikiri kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji hususan kwa watoto wadogo wakiume.

“Lakini ukubwa wa tatizo hilo la unyanyasaji wa kiume linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina ili kujua hali ya ukubwa wa tatizo lenyewe” alisema Waziri huyo.

Alisema kwamba wizara yake tayari inaandaa utafiti wa kina wa tatizo hilo kwa nchi nzima pamoja na kuelimisha wazazi na watoto juu ya athari ya jambo hilo kupitia wadau mbali mbali, mikutano na vyombo vya habari kama radio na televisheni.

Waziri huyo alisema alisema suali la kupiga vita unyanyasaji Zanzibar linahitaji mashirikiano ya dhati na kwamba juhudi hizo ni lazima ziwe endelevu.

Wajumbe wa baraza la wawakilishi akiwemo Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Mwajuma Faki Mdachi alieleza masikitiko ya kuendelea kwa unyanyasaji licha ya juhudi zinazoendelea za kutoa elimu.

Nyanyasaji wa kijinsia umekuwa ukilalamikiwa mara kwa mara katika visiwa vya Unguja na Pemba ambapo baadhi ya wananchi wanapendekeza wanaopatikana na hatia wahasiwe au kufugwa kabisa.

Advertisements

5 responses to “Wananchi watakiwa kuwa makini

  1. akina wawakilishi hivi hamwasikii wananchi au nyie mmezaliwa viziwi? watu hawataki katiba yoyote ile , wanachotaka ni muungano kuvunjwa tu ! kama mshakula rushwa kama kawaida yenu ili muendelee kuwa vibaraka wa tanganyika hilo si geni , mtasababisha mtafaruku visiwani , muungano hautakiwi na hii ni haki ya wananchi kutaka ua kutotaka muungano , msiwe kama njia ya haja kubwa ambayo haiwezi kutengana na mavi,

  2. Mie nashngaaaa kabisa nini wanachofanya na sjui nini wanachokiogopaa wakati wananchi ndio wenye nchi na hawati huu muungano wa mkolono mweusi tunataka znz yetuu kwanini mnashindwa kufanya kazi zenu kama wawakilishi wa nchii hii jamani hapa kikitifuka ujuwe hakieleweki mpaka tupate nchi yetu…

  3. musiwazonge wananchi bureeeeee, wazanzibari wameshasema hawautaki muungano , unawaambia wasome katiba watikati mtu kula yake ya siku haitimii.msijitie upofu MUTUACHEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEE TUPUMUEEEEEEEEEEEEEEEE.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s