Tofauti ya Muungano wa Katiba na wa Mkataba

Ahmed Rajab

Mwenyekiti wa tume ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba na tume yake walipokuja kuitambulisha tume kwa wazanzibari

ULE mjadala mkubwa — na mkali— unaovuma na kuchaga Visiwani Zanzibar kuhusu mustakbali wa Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar umefichua jambo moja lenye kuwagusa na kuwaunganisha Wazanzibari wengi.  Nalo ni dai la kutaka pafanywe mageuzi ya kimsingi katika mahusiano baina ya hizo nchi mbili zilizo katika Muungano wa Tanzania.

Wanapoulizwa kwa nini wanasisitiza mahusiano hayo yageuzwe wanatoa kila aina ya sababu.  Baadhi yao wanazieleza sababu hizo kwa makini wakizijenga juu ya misingi ya hoja za kimantiki.  Wengine  wanajibu kwa jazba.

Shutuma wanazozitoa ni nzito.  Kuna wanaosema kuwa miaka 48 ya Muungano haikuinufaisha kitu Zanzibar.  Kuna wanaosema kuwa Muungano umeifanya Zanzibar itoweke kwenye ramani ya dunia.  Kuna wasemao kuwa Muungano umeifanya Zanzibar idhurike kisiasa, kiuchumi na kijamii ikilinganishwa na visiwa vingine kama vile Mauritius na Seychelles.

Kuna wanaoutupia Muungano lawama zote za dhiki za kiuchumi na shida za kijamii zilizoisibu Zanzibar kwa muda wa takriban nusu karne.  Wanasahau kwamba katika kipindi chote hicho pamekuwako na utawala mbovu Visiwani na kwamba matatizo mengine ni ya kujitakia wenyewe.

Kadhalika, kwa vile Zanzibar imepoteza mamlaka muhimu ya kidola kwa kuungana na Tanganyika kuna wanaokereka na utata uliopo kuhusu hadhi ya Zanzibar: iwapo ni nchi ama si nchi ndani ya Muungano.  Wanalalama kwamba Zanzibar haina uwezo wala uhuru wa kujiamulia yenyewe njia gani ya kiuchumi na kijamii ya kuifuata ili iweze kujigomboa kutokana na shida ilizo nazo.  Wananung’unika kwamba kwa muda wa miaka 48 serikali ya Muungano haikuyatumia vyema madaraka iliyoyatwaa kutoka Zanzibar kupigana na umasikini, magonjwa na ujinga.

Bara pia kuna watu wenye mtizamo sawa na ule wa Wazanzibari wenye kutaka mageuzi ya kimsingi yafanywe katika mahusiano ya Tanganyika na Zanzibar.  Baadhi yao nao pia wana jazba na wanasema kwamba Zanzibar imekuwa mzigo wa Bara na kwamba potelea mbali iachwe itokomee.  Wanasema kwamba Wazanzibari hawana kheri na waachiwe wajionee wenyewe kitachowafika watapouua Muungano.

Visiwani Zanzibar hakuna mgogoro kuhusu nini uwe mustakbali wa visiwa hivyo.  Inavyoelekea ni kwamba wengi wa wananchi wa huko wanaiunga mkono ile wanayoiita Ajenda ya Zanzibar yenye lengo la kuirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili ya kidola na kubadili mfumo wa mahusiano kati ya Zanzibar na Tanganyika.

Huenda ikawa Wazanzibari wanatofautiana juu ya mbinu za kulifikia lengo hilo lakini si juu ya mkakati wenyewe kwani hata wale wasio na imani na mchakato wa sasa wa kuiandika upya katiba ya Tanzania nao pia wanakubali kwamba mustakbali wa Zanzibar unapaswa uwe wa uhuru na utaoirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili ya kujitawala.

Huo muundo mpya wa ushirikiano wa baadaye wanaoutaka baina ya Zanzibar na Tanganyika ni tofauti kabisa kinadharia na kiutendaji na ile dhana ya kuuimarisha Muungano ambayo huenda ikawa na maana ya kuwa na serikali moja katika taifa moja.

Dhana hiyo si ngeni.   Viongozi kadhaa wa Tanzania wamekwishawahi kuipigia debe.   Mmojawao ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye mnamo mwaka 1995 katika hafla yake ya kuyaacha madaraka alisema wakati umefika wa kuwa na Muungano wa serikali moja.   Miaka kadhaa baadaye alipoulizwa iwapo Zanzibar ni nchi au si nchi alisema hajui.

Hamna shaka yoyote kwamba ukiibuka Muungano wa aina hiyo anaoutaka Mwinyi wa kuwa na serikali moja nchini Tanzania basi itabidi pasiwepo Serikali ya Zanzibar na pingine visiwa vya Unguja na Pemba vitakuwa mikoa au tarafa za Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.  Nakumbuka Dk Mohamed Gharib Bilal alipokuwa waziri kiongozi wa Zanzibar aliwahi kusema kwamba hilo halitotokea hata miaka 100.

Kwa upande mwingine,  kuna watu Bara wanaoamini ya kuwa muundo bora wa Muungano ni wa kuwa na ‘Dola moja, serikali mbili.’  Katika muundo huo Zanzibar itakuwa huru kuyashughulikia mambo yake yote yasiyo ya Muungano.  Hivyo, kwa kiwango kikubwa Muungano utabaki kama ulivyo isipokuwa tu utafanyiwa marekebisho ya hapa na pale ya kuzibaziba viraka na kuondosha zile zinazoitwa ‘kero’ za Muungano.

Halafu kuna wanasiasa na wasomi wa Bara wanaohisi kwamba lazima pawepo na ‘nipe, nikupe’ na hivyo pande mbili za Muungano zisikilizane na zikubaliane kuwa na Muungano wenye muundo wa shirikisho wenye serikali tatu.  Muundo huo utahakikisha kwamba Muungano unaendelea kuwapo.  Wenye kutoa rai hiyo wanashikilia kwamba muundo huo wa shirikisho uwe miongoni mwa mapendekezo yatayozingatiwa na Tume ya Katiba.

Mapendekezo yote hayo ya kikatiba yana ila moja: yanazinyima Zanzibar na Tanganyika na hivyo watu wa nchi mbili hizo za kindugu haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe na kuwa na uhuru wa kujipangia mambo yao bila ya kuingiliwa na wageni; yaani bila ya Watanganyika kuyaingilia mambo ya ndani ya Zanzibar na bila ya Wazanzibari kuyaingilia mambo ya ndani ya Tanganyika.

Kwa hivi sasa Zanzibar na Tanganyika haziwezi kuwa na hata vyama  vyao vya kisiasa visivyo na sifa au sura ya kimuungano.  Wazanzibari kadhalika wanapinga nguvu za walio wengi kuwaamulia wasio wengi na wanaiona hali hii kuwa ndilo tatizo kubwa ambalo lazima litafutiwe ufumbuzi ili maslahi na mahusiano ya baadaye ya nchi hizo mbili yasihasirike.

Hadi sasa nimekuwa nikiuzungumzia muundo wa Muungano uliojengwa juu ya mfumo wa kikatiba.  Lakini mfumo huo una madosari mengi na haufai kwa mahusiano ya nchi mbili zilizo huru na zilizo na usawa machoni mwa sheria ya kimataifa na mwenendo wake ambao hauruhusu kuwako kwa ile dhana ya ‘ukaka’ kwani nchi zote, ziwe kubwa au ndogo, zinaangaliwa sawasawa kisheria na jumuiya ya kimataifa ilimradi ziwe huru na ziwe na mamlaka kamili ya kidola.

Ndiyo maana  kuna Wazanzibari wengi wa itikadi zote za kisiasa, wa vyama tofauti vya kisiasa na hata wasio wanachama wa chama chochote wanaopinga kabisa aina yoyote ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Wanachotaka wao ni kurejeshwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar baada ya kura ya maoni itayowauliza Wazanzibari iwapo wanautaka au hawautaki Muungano. Watu wenye fikra hiyo wanahisi kwamba huu mchakato wa sasa wa katiba unastahiki ufanywe baada ya hiyo kura ya maoni.

Kinyume nao ninavyohisi ni kuwa wengi wa Wazanzibari hawauoni mchakato huo wa katiba kuwa hauna maana.  Wanavyoona wao ni kuwa mchakato huo ni fursa nzuri waliyoipata ya kulitanzua tatizo liliopo.

Wanakumbusha kwamba kinyume na mambo yalivyokuwa zamani safari hii wananchi wenyewe wanashiriki katika mchakato wa katiba utaomalizika kwa kupigwa kura mbili za maoni — moja Bara na nyingine itapigwa Zanzibar. Wanaamini kwamba matokeo yake yatakuwa kupatikana mfumo mpya wa mahusiano baina ya nchi hizo mbili zilizoungana kikatiba tangu Aprili 1964.

Baada ya kuukataa muundo wa Muungano wa Katiba, wanatoa hii dhana ya mfumo ulio tofauti kabisa yaani mfumo wa Muungano wa Mkataba.  Wengi Visiwani hivi sasa wanaiunga mkono dhana hii ambayo pengine ndio yenye suluhisho bora na mujarab kwa Muungano.

Mahusiano yatayojengwa kwa Mkataba yatairejeshea Tanganyika na pia Zanzibar mamlaka yao kamili ya kidola na yatawezesha kuwapo na utaratibu wa ushirikiano kati ya nchi mbili zilizo sawa na zilizo huru na zenye mamlaka kamili ya kidola.

Mkataba utaoongoza mahusiano hayo utaweka wazi ni mambo gani nchi hizo zitashirikiana na namna ushirikiano wao wa baadaye utavyokuwa.

Pale nchi iliyo na mamlaka yake kamili inapoandikiana mkataba wa kuwa na ushirikiano au muungano na nchi nyingine inakuwa haiyapotezi mamlaka yake au uhuru wake.  Hali hiyo ni kinyume na Muungano wa kikatiba uliopo sasa ambao umeifanya Zanzibar iyahaulishe kwenye Serikali ya Muungano mamlaka na madaraka yake ya kimsingi.

Zanzibar imezitoa mhanga nguvu zake za kidola wakati mwenzake Tanganyika haikulazimika kujitosa na kutoa mhanga kama huo kwa vile utawala wa Tanganyika unaendeshwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Jambo jingine lenye kuvutia panapokuwako ushirikiano au muungano wa Mkataba ni kwamba kila nchi iliyotia saini mkataba wa muungano inakuwa na nguvu ya ‘turufu’.

Hivyo hata katika mambo yaliyokubaliwa kuingizwa katika ushirikiano nchi inayohusika inaweza kuitumia nguvu yake ya turufu na ikaomba hifadhi ya watu wake endapo inahisi kwamba inahatarishwa na sera za huo muungano katika utekelezaji wa mahusiano na ushirikiano wa nchi hizo.

Muungano wa aina hiyo, yaani wa Mkataba, utairejeshea Serikali ya Umoja wa Kitaifa mamlaka na  madaraka muhimu ambayo Zanzibar haikuwa nayo kwa muda wa miaka 48.  Yakitumiwa vyema madaraka hayo yataiwezesha Zanzibar kutekeleza sera zitazoirejeshea Zanzibar adhama na fahari iliyokuwa nayo zamani na kuifanya ishiriki kikamilifu katika shughuli za kanda ya Afrika ya Mashariki na ya Kati na hata kupindukia mipaka ya kanda hii.

Gazeti la Raia Mwema

Advertisements

13 responses to “Tofauti ya Muungano wa Katiba na wa Mkataba

 1. Sisi wazanzibar hatutaki muungano. Kama ninayosema uwongo 2leteeni KURA YA MAONI. Hakuna m2 asiyetaka kuishi kw raha. Ila nashkuru hata wale MAWAZIRI we2 baadhi tayari wameamka. Allah awape uimara kw hali na mali waikomboe nchi hii.

 2. ewe ahmedi kuna siku utarudi kwa mungu ndugu yangu , haya mafanikio madogo ya kidunia yasikupoteze , kulipwa vipesa kidogo na hao watu wanaokuambia kuandika makala feki , hawatokusaidia chochote, wazanzibari hawataki MUUNGANOOOOOOOOOOOOOOOO

 3. nimesikia maoni ya katiba yanaweza kuwasilishwa kutumia barua pepe , tunaomba hio tume ikishaanza kazi tupate email kwa wale au website yao , tuweze kuwasilisha oni letu moja kuwa muungano hatuutaki ,

  • Ni kweli. Hakuna haja ya kuumishwa vichwa saaaana. Kitu easy & simple ni kua “TUACHIWE TUPUMUE” Hatutaki Muungano jamaniiii. Jamani nyi mna akili gani hasa, hadi ikawa mnazidi kuongelea kile kile tunachokipinga kila siku, nyi mmetushika kutupeleka kwengine. Sisi bwana hatutaki Muunganooo. MnatuFORCE kujadili katiba kama kwamba tumewaomba huo Muungano. Tuulizeni kwanza tunautaka? Mkishapata jibu kua tunautaka hapo ndo mtafanya Ihsani ya kutushirikisha kwenye hayo maoni ya katiba. Msijifanye wajanja kujifanya wakarimu eti kwa kutushirikisha katika hili la Katiba……….Jamani kama mna Ihsani kweli tupeni Kura Ya Maoni Kwanza……..Hatutaki Muunganooooooooooooooooo..!! Mnypsxxssy.
   By: Sule Al’Rumhy.

 4. Af mi naomba ndugu zangu walio nje ya Zanzibar na nje ya Afrika nao tunatamani japo siku moja tuskie wamefanya maandamano ya amani na halali huko huko waliko, kama sheria za nchi walizoko zitawaruhusu, ili kuonyesha kihali kua wako nasi, pia kuona Uzito wa UZALENDO wao, na kuonyesha athari ya hisia zao juu ya Dhulma dhidi ya Zanzibar yetu TUIPENDAYO, kwa kuona hasa machozi yao yenye ishara ya mapenzi yakiwatoka kwa kuihurumia Zanzibar kwa vile na wao walishaiona ZANZIBAR ikizidi kuzamishwa siku siku hadi kubakia kichwa, kichwa ambacho amekabidhiwa WARIOBA na tume yake kushirikiana kuizamisha yote, jambo ambalo ndani yake mna ndugu zetu wa damu, ila nao wako tayari kushirikiana na WARIOBA kulitimiza hilo, badala ya kushirikiana na JOPO LA WAZALENDO la akina SH. MSELLEM na SH. FARID.
  Tunasema HATUTAKI MUUUNGANOOOOOOOOOOOOOOO….!
  Nawakilisha Al’Rumhy.

 5. ahsante kaka Ahmed kwa somo hilo Allah akupe umri na uzima uendeleze uzalendo wako kwa zanzibar, inshallah tutaipata zanzibar yetu,

  • Nikweli ndugu yangu hakuna kisichochosha nasi Wazanzibar tuachizwe ten maana mtoto akisha timia miaka miwili anaachizwa kisheria, ili umuangalie kama ataweza kujimudu na maisha.

 6. muungano wa mkataba ndo suluhu pekee na hio ndo itatupa ahueni wa kujitutumua na kufanya mambo yetu ya kiuchumi na kujiunga na kuwa na mahusiano na mataifa na mashirika ya kimataifa kama fao,ifad,fifa nk zanzibar yenye mamalaak kamili iwe ndo slogan yenu wazanzibar wote wapenda maendeleo ya kweli isiwe kila siku vikao vya kero ya muungano na waheshimiwa kuvaa suti na kukaa katika viyoyozi vya baridi na kupeana bahasha na kuwacha kila jambo ju ya meza hilo basi tumechoka

 7. Leo Bwana Ahmed Rajab umenifurahisha kwa kusema kweli kuwa mawazo haya ni yako wewe na sio ya Wazanzibari.

  Mimi kwa muda mrefu nimekuwa nikipiginia KUVUNJIKA kwa Muungano na wala sijabadilika. Lakini ndugu zangu hii makala ya Ahmed Rajab tunaweza tusiione maana yake.

  Naomba mnifuatilie vizuri hapa chini:-

  Zanzibar matatizo ya Muungano wetu ni sawa na yale ya Ireland ya Kaskazini na Scotland kama sijakosea ambao na wao wanadai nchi yao kwa kupitia kura ya maoni kama tunavyopendelea sisi, zifuatazo ni tafauti za kimsingi baina yetu na Ireland ya Kaskazini ambazo lazima tuzijue:-

  1. Kwao wanaopambana dhidi ya Muungano wao ni Serikali sambamba na wananchi wake.

  Lakini Zanzibar wanaopambana dhidi ya Muungano ni Raia na asasi zao wakati Serikali inapambana kuunga mkono Muungano na baadhi kutaka kurekebisha muundo tu. HUU NI UDHAIFU SUGU.

  2. Wenzetu Kura ya maoni imepangwa kupigwa mwaka 2014.
  Je! Nini maana yake?
  Hawa wenzetu hawa ni wajanja na hii mbinu mkakati ya kisomi, kwa sababu wamegundua kuwa wanapinga Muungano huo wengi wao ni wasomi na vijana mpaka chini ya miaka 18 halafu ndio wengine wanafuatia. Kwa hivyo wameiweka 2014 ili hata wale vijana wenye miaka 16 na 17 wafikie umri wa kupiga kura ili kuongeza idadi ya wapinga muungano-wapiga kura sambamba na kuitisha uandikishaji mpya wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura.

  Bila shaka mpango wa Tanzania ni kupata katiba mpya ifikapo 2014. Na sirahisi serikali zetu hizi mbili kukubali kurefusha muda hadi angalau mwaka 2014 ili kuwapa fursa ya kupiga kura vijana ambao kwa sasa hawajatimia umri wa kupiga kura, hii ni kwa sababu mbali na kuwepo mpango wa kupata katiba mpya 2014 Serikali mbili hizi za CCM zinaendeshwa chini ya athari, matakwa, maslahi na miongozo ya Kanisa kwa kupitia wakala wa kanisa waliomo ndani ya chama na serikali zinapenda na zinapapatua muungano huu tushindwe kuuvunja wala kuurekebisha bali uzidi kutubana, hivyo sirahisi kuruhusu muda uende mbele eti “wapinga muungano wafike umri wa kupiga kura”.
  Kura hii wakitupa sasa wametuua, kunavijana na Wazanzibar ambao waliipuuza michakato ya upigaji kura katika chaguzi zilizopita hawamo kwenye daftari la kudumu la wa wapiga kura. Hii ni hasara kubwa kwenye kura maoni.

  3. Kwao Ireland Kaskazi Tume ya Uchaguzi ni huru, na hata kama ingekuwa sio huru ikawa inafuata matakwa ya watala wa Ireland basi watala hawa ndio wapinga muungano wakubwa wanataka uvunjwe basi.

  Lakini ZNZ Tume ya uchaguzi kwa muda wa miaka 20 sasa imekuwa ikalalamikiwa kwa madai yasiopingika ya kufanya udanganyifu na wizi wa kura katika chaguzi takriban zote. Wachilia mbali katika ngazi ya kitaifa (URAISI) hata katika majimbo mfano Jimbo la Mji Mkongwe ambapo wakaazi wengi wanajuana kuwa CCM ni kidogo mno wengi wao ni CUF, lakini wachambuzi wa mambo walikuwa wakipigwa na butwaa jinsi Jimbo hilo lilivyokuwa likibebwa na CCM mpaka hapo wanamji wenyewe Mkongwe walipolivalia njuga jambo hili. Mifano ni mingi mno.

  Je! Tunauhakika gani wa Tume kama hii kuweza kutenda haki katika kura ya maoni ukizingatia ukweli kuwa Tume hii daima hufuata matakwa ya CCM vyovyote yawavyo? Na hali CCM wameapa kuulinda Muungano kwa gharama yoyote!
  Bila shaka kumbe yawezekana sana tena sana kwa asilimia 98% kura ya maoni ikawa ndio njia pekee kwa CCM kutuhalalishia DUDE hili kwa miaka teeele ijayo kwa kisingizio cha eti ridhaa ya Wazanziri kupitia kura ya maoni.

  WAZANZIBAR TUSIKURUPUKE HAPA NI WAKATI MUHIMU.

  4. Hili ni la ZNZ pekee bila kuiangalia Ireland.

  Zanzibar ina wakaazi millioni 1 na laki 2 yaani 1.2ml. Lakini daftari la kudumu la ZNZ linawapiga kura laki sita na kidogo tu. Katika hao inasemekana si chini ya wakaazi laaki tatu wapo Tanganyika kwa ajili ya kazi, biashara, masomo, maisha n.k Je! Hawa tena kama watakuja kwenye hiyo kura wanaweza kutuunga mkono katika kuuvunja Muungano ukilinganisha na kasumba za eti Muungano ukivunjika watu watarudishwa makwao na uchungu wa watu juu ya mali, wake au waume zao wa Kitanganyika?
  Sasa hivyo kama ndivyo ilivyo basi zinaweza kuingia katika mgawanyi tusioutarajia.

  Taasisi za kiraia na Serikali wenye uchungu na nchi kuna haja kubwa na kukaa pamoja haraka iwezekanavyo lengo ni moja tu la kupata msimamo wa pamoja.

  Allah Allah jamani tusije tukakosa kaa na nganda lake. Muungano wa mkataba ni muwafaka kutokana na mgawanyiko uliopo pale tutakaposhindwa kukubaliana kuwa sote kwa kauli moja tuuvunje.

  MUUNGANO HUU HATUUTAKI.

  JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR KWANZA.

  “When peace fails apply force”

  SERELLY.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s