Matumizi ya fedha za serikali yachunguzwe

Mwakilishi wa Jimbo la Chakechake (CUF) Omar Ali Shehe akiwa pamoja na Mwakilishi wa kuteuliwa Panya Othman (CCM) wakiingia katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi huko Mbweni nje ya Mji wa Zanzibar.

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wamesema Zanzibar inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi pamoja na changamoto za fedha kutokana na usimamizi mbaya wa fedha za serikali kutokana na kutodai haki kutoka serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Wakichangia bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/2013 wajumbe walisema upo udhaifu mkubwa katika usimamizi wa fedha za serikali katika wizara mbali mbali pamoja na muungano kutotendea haki Zanzibar.

Mwakilishi wa Jimbo la Chakechake (CUF) Omar Ali Shehe alisema uchunguzi unaonesha kuwa fedha nyingi zinapotea kwa kuchukuliwa na watendaji wasiokuwa waaminifu huku serikali ikitafuta fedha kwa njia za kuongeza kodi.

“Hakuna sababu kuongezea wananchi mzigo wa maisha kutokana na kupandisha kodi ambazo serikali ingeweza kuepuka. Kupandisha kodi ya mafuta maana yake ni kuleta mabadiliko ya mfumko wa bei nchini” alisema Shehe.

Alisema serikali haiwatendei haki wazanzibari wanyonge kwa kupandisha kodi na kutowachukulia hatua watendaji wabadhirifu wa mali za serikali. Mwakilishi huyo pia alisema ukimya wa serikali ya Zanzibar katika kudai mapato kutoka serikali ya muungano umesababisha wazanzibari waishi katika maisha magumu na serikali kupandisha kodi bila kuangalia athari zake kwa maisha ya wananchi.

Mwakilishi wa mjimkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu alisema mkanganyiko wa mahesabu katika vitabu vya bajeti na mipango ni ushahidi tosha wa kukosekana kwa umakini katika idara za serikali na matumizi mabaya ya fedha.

“Namuomba waziri wa fedha achukuwe hatua dhidi ya watendaji ambao wanashindwa kutekeleza wajibu wao. Inakuaje katika vitabu vinavyoletwa kwa wajumbe vinakuwa na hesabu zisizoelewa wakati ni muda mrefu wa kuandaa vitabu hivi,” mwakilishi jussa alilalamika.

Aidha Jussa alimtaka rais wa Zanzibar Dr Ali Mohamed Shein, makamo wa rais Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Iddi, pamoja na mawaziri kusimama kidete katika kudai maslahi ya Zanzibar kutoka serikali ya muungano.

Alisema kuwa muungano bado unaonekana kutokuwa na maslahi kwa Zanzibar kutokana na serikali ya muungano kushindwa kutoa gawio la zaidi ya  bilioni 18 za faidaa katika benki kuu ya Tanzania (BoT).

Jussa, “Muungano huu umekuwa haina tija kwa Zanzibar tuna pessa zetu nyingi katika BoT, na pesa zinazotokana na kodi kwa watumishi wa serikali ya muungano wanaofanya kazi Zanzibar. Hi haikubaliki na lazima tudai.”

Mwakilishi huyo pia alisema kuwa uchumi na bei za bidhaa zimekuwa zikipanda kutokana na sarafu ya Tanzania kushuka thamani kwa Dola za kimarikani, na kwamba Zanzibar haistahiki kupata shida kutokana na hilo.

Alisema waziri wa fedha wa Zanzibar ni waziri pekee asiye kuwa na umiliki wa sera na fedha zake duniani, “nashauri bora Zanzibar tume na benki yetu kuu na pesa yetu kwa sababu inawezekana katika muungano.”

Alisema si haki Zanzibar kuendelea kupata shida katika kupanga mipango yake kutokana na kutokuwa na sera kuhusu fedha yake, “mfano mdogo ni nchi ya Seychelles ambao ina watu 85,000 tu lakini lakini pesa yake ni imara dhidi ya dola ya Marekani.”

mwisho

    Kamati hairidhishwi na upandishwaji bei

Kamati ya kudumu ya baraza la wawakilishi Zanzibar imesema hairidhishwi na uamuzi wa serikali ya Zanzibar katika kupandisha bei ya umeme, pamoja kodi katika mafuta.

Kauli hiyo imo katika hotuba ya kamati hiyo iliyosomwa ndani ya baraza na mwenyekiti wa kamati Hamza Hassan Juma, mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura ambapo alisema sababu za mabadiliko ya viwango vya kodi haziridhishwi.

“Tusiwaongezee wananchi mzigo wa kodi, na kwamba mapato kutoka serikalini yanatosheleza kupanga maendeleo bila ya kuathiri wananchi” alisema Juma. Akitoa mfano wa shirika la umeme Zanzibar (ZECO) ambalo hivi karibuni lilipandisha bei ya umeme, alisema hakuna sababu za msingi za kufnaya hivyo kama mapato yanayopatikana yanatumika kwa njia zinazokubalika kisheria.

“Kuna ubadhirifu katika shirika la umeme na pia katika idara nyengine za serikali hakuna uwazi wa matumizi ya fedha za serikali, ni muhimu serikali kupanga na kufanya uchunguzi kabla ya kupandisha kodi ili wananchi waondokane na hali ngumu” alisema mwenyekiti wa kamati hiyo.

Katika taarifa ya kamati hiyo serikali imetakiwa kufanya uchunguzi wa kina juu ya pesa zaidi ya billion 8 zilizotolewa na wizara ya elimu ya Zanzibar kwa wanafunzi hewa. “inashangaza kuwa pesa zimetolewa kwa watu ambao hawajulikani, haiukubaliki lazima uchunguzi ufanye wabainike hao waliochukua fedha hizo ili fedha hizo ziwasaidie wengine kwa sababu wapo wanafunzi wengi ambao wanataka kusoma na wazee wao hawana uwezo wa kuwalipia” alisema mwakilishi huyo.

Akizungumzia kuhusu faida zinzopatikana katiak benki kuu (BoT) alitaka serikali ya Zanzibar kuhakikisha kuwa fedha zaidi ya billioni 8 zinapatikana ili ziwafae wazanzibari. Alisema kuna maeneo mengi yakiwemo kodi zinazotozwa kutoka kwa watumishi wa serikali ya muungano wanaofanya kazi Zanzibar na visa kwamba mapato yanayopatikana hayaingii katika mfuko wa Zanzibar na badala yake huingia katika mfuko wa serikali ya muungano.

  MWISHO

   Mafuta hayatachimbwa hadi…..

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza kwamba haitaruhusu uchimbaji na utafutaji wa mafuta katika eneo lake kabla ya kufikiwa makubaliano na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliyetaka kujua kwa nini kumekuwepo na ucheleweshaji wa kupatikana ufumbuzi juu ya suala hilo.

“Nataka serikali itoe kauli juu ya ucheleweshaji huu unaofanywa kusudi na serikali ya muungano na tayari kampuni moja hivi karibuni imeruhusiwa na serikali ya muungano kufanya utafutaji wa mafuta katika kitalu 18 ambayo ni eneo la Zanzibar” aliuliza Jussa.

Akijibu suali hilo pamoja na suali kutoka kwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni (CCM) Salmin Awadh Salmin, Waziri Aboud alisema hakuna kampuni itakayothubutu kuingia eneo la Zanzibar.

“Tayari tumeiandikia serikali ya muungano barua juu ya msimamo huo na nategemea hakuna kampuni itakayoingia katika eneo la Zanzibar, tunaahidi kusimamia hilo” alisema Aboud.

Pia alisema kwamba serikali ya Zanzibar imo katika mazungumzo na serikali ya muungano juu ya matakwa ya Zanzibar kuyaondoa mafuta na gesi asilia kutoka orodha ya mambo ya muungano na kwamba muelekeo ni mzuri baada ya kauli nyingi za Rais Kikwete kuonesha kuridhia.

Alisema ufumbuzi utapatikana hivi karibuni na kuwataka wajumbe wa baraz ala wawakilishi pamoja na wanasiasa kuwa na subra na kwamba kamwe viongozi hawatokwenda kinyume na matarajio ya wazanzibari.

Mapema Mwakilishi Jussa na Salmin walisema kuwa licha ya serikali ya muungano kuahidi kulishughulikia suala hilo ndani ya miezi mine hivi sasa ni miezi mitano imepita bila ya kupatikana ufumbuzi wa suala hilo.

Suala la mafuta limekuwa likichukua nafasi kubwa katika mjadala wa baraza la wawakilishi kilichoanza juzi huku wajumbe wakikosa ustahamilivu na kutaka suala la mafuta lipatiwe ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amekuwa akiahidi kuwa suala la mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa ajenda zilizopewa kipaumbele katika vikao vya kujadili kero za muungano na kwa mara ya mwisho mwaka huu aliahidi kuwa suala hilo lingeweza kupatiwa ufumbuzi ndani ya miezi minne.

Mwisho

   Vikao vya rais vina tija kubwa

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa baraza la wawakilishi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini amesema vikao vya mara kwa mara vya rais na wizara vinaleta tija katika utendaji serikalini.

Alisema hayo katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Mjini Zanzibar kuwa rais alianzisha utaratibu wa kukutana na wizara moja moja kila baada ya miezi mitatu ili kuleta ufanisi serikalini.

Kauli ya Dk Makame ilikuwa katiak kujibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani (CCM) Ali Salum Haji aliyetaka kujua kwa nini serikali isiunde chombo maalumu cha kufuatilia watendaji serikalini badala ya rais kufanya vikao vya mara kwa mara.

“Rais Dk Shein amejiwekea utaratibu wa kutathimini utekelezaji wa shughuli za serikali kwa kuzingatia malengo na vipaumbele vya bajeti vya kila wizara, utaratibu huu tayari unaonesha kuleta matunda” alisema Dk Makame.

Akitetea zaidi utaratibu huo wa rais, waziri alisema manufaa makubwa yamepatikana katika zoezi hilo hasa katika kupima kiwango cha utekelezaji wa shughuli za serikali, matumizi, na upatikanaji wa fedha.

“Waziri pamoja na watendaji kupata fursa ya kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao kubaini matokeo na jitihada zao pamoja na changamoto zinazowakabili” alisema waziri huyo.

Dk Makame alisema utaratibu huo ulioanza mwaka jana pia umewahamasisha watendaji kufanya kazi kwa pamoja na kuongeza kazi ya uwajibikaji na ufanisi.

Waziri huyo alipinga suala la kuanzishwa chombo maalumu cha kufuatilia utendaji serikalini kwa kusema kwamba tayari vipo vyombo vyengine vilivyowekwa kisheria kufuatilia utendaji na shughuli za serikali.

MWISHO.

   Kupata risiti baada ya malipo ni tatizo

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wamelalamika juu ya risiti za malipo kutotolewa katika hospitali kuu ya mnazi mmoja na kutaka wizara kuondoa kasoro hiyo.

Mwakilishi wa Jimbo la Koani (CCM) Mussa Ali Hassan alisema katika kikao cha baraza la wawakilishi kwamba katika baadhi ya vitendo vya hospitali ya mnazi mmoja sehemu za cliniki za waja wazito risiti hazitolewi baada ya malipo.

Aidha mwakilishi huyo alisema sehemu ya masikio, pua na koo kadhalika ukishalipa risiti hazipatikani na kuhoji pesa zinapopelekwa.

Akijibu suali hilo, Naibu Waziri wa Afya Dk Sira Ubwa Mamboya alisema huduma zote ambazo huchangiwa zikiwemo pua, koo, masikio, macho pamoja na clikini za wanawazito hutolewa risiti na kama kuna kitengo ambacho hupokea fedha bila ya kutoa risiti wizara haina taarifa hizo na wala haijapokea malalamiko yoyote.

“Wizara ya afya kwa kushirikiana na wizara ya fedha tumekubaliana kuwe na utaratibu maalumu wa ukusanyaji wa fedha utaowezesha kuwa na sehemu kuu moja ya malipo (centralized collection point) alisema.

Naibu waziri alisema hata hivyo wizara yake inatoa wito kwa wafanyakazi wa afya kutoa risiti kwa malipo yoyote ambayo mgonjwa huwa anachangia ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wagonjwa.

Aidha Dk Sira alisema kuna upungufu wa wahasibu katika hospitali hiyo na kwamba kati ya wahasibu wanane wanaohitajika kufanya kazi saa 24 ni wahasibu watatu tu wanaojituma na ambao wamewekwa kwenye sehemu nyeti.

Advertisements

6 responses to “Matumizi ya fedha za serikali yachunguzwe

 1. NAOMBA KUTUPA UJUMBE WANGU HUU KWENU

  Assalamu alaikum
  Maana huo ndio uislamu na ndivyo tulivyoagizwa na Mtume wetu Muhammada (SAW) kua pale wasiolamu mnapokutana basi tuleaneni salam. Maana hiyo ndio tofauti kubwa ya wale wasilamu na wale wasiokuwa waisilama.

  Sasa naanza nakile nilichokikusudia kukizungumza, tunajua kua sasa wazanzibar tumekumbwa na tatizo kubwa la Muunguno kama vile wanavyouita ndungu zetu wadamu (Watanganyika) japo kua ukweli wake ni myang’anyano. Wakati umefika kwa Wazanzibar kua kitu kimoja na sio kuangalia siasa kama baadhi ya watu walivyo ndani ya Zanzibar. Nasema hivi kwa ushahidi mkubwa juzi siku ya Jumapili 17/06/2012 Jumuiaya ya UAMSHO iliandaa muhadhara wa Kiislamu huko Donge, lakin kuna wapumbavu wacheche ambao sioni shida kuwataja Pembe, Panya na Dubwana jengine sijui linaitwa Haji Omar Kheir. Yalitoka yalikotoka yakenda mpk kituo cha Polisi mkokotoni kwenda kupinga muhadhara huo kwa kuwasingizia Wadonge kua wamekata “Inallilahi waina illaihi rajiun” huu ni msiba mkubwa.

  Ila hawa wakae wakijua kua pindi ingalitokea mtu akapigwa risasi na kupoteza maisha basi wakae wakijua sisi tunakaa nao wao, watoto wao na hao polisi (mbwa wa usasi) wasijewakazania tutamuachia mungu. M/mungu alishatufundisha kua “tusidhulumu wala tusizulumiwe” tutakuja onana wabaya. Kama wao ndio wanatumiwa na Watanganyika bila ya kujijua kuwahujuma wananchi wao basi wasome alama za nyakati. Maana waangalie Tangayika juzi wamefanya maanandama yaliopigwa marufuku na jeshi la polisi lakini hakuna hata mtu mmoja alikamatwa wale askari aliekwenda kupiga mabomu iweje sisi Wazanzibar mihadhara pia tunapigwa mabomu sasa wakati umefika tuweni macho.

  Tunasema na tunasema …..MUUNGANO SISI HATUUTAKI….TUACHIWE TUPUMUE

 2. Si vyema wazanzibari kuvunja mungano chamsing tuangalie ni mungano wa aina gani utakao utakaorudisha jamuhur ya watu wa zanzibar kwn kuna nchi zimeungana lakn zna mamlaka kamili na istoshe ktk rasimu ya katiba mpya tukumbuke kwamba kunakipengele kinachozungumzia ni kosa kuvunja mungano{kutoa maon yanayoashiria kuuvunja mungano} cha msingi tujitokeze kutoa maoni juu ya aina ya mungano utakaoifanya zanzibar huru na inawezekana hofu yangu kwa madai ya sasa kwamba kuitishwa kura ya maoni kwa wazanzibar ni kujiparia mkaa kwan wazamzibar mtakubaliana nami kwamba tume inaweza kuchakachua kama tulivyozoea ktk uchaguz zilizopita mi naona muna umefika kwa wazanzibari kutumia fursa ya ukusanyaji maoni kuelezea aina ya mungano. Maswali magumu najiuliza endapo mungano tunataka kuvunja je tumeshajipanga ktk masuala ya nishati? Ulinzi? Na chuki itakayotanda juu ya watu wa pande mbili za mungano istoshe tumeshea damu na imani? Mikakati zaid inahitajika kukomboa zenji na wala sio jazba. NI MIMI MZALENDO NA MWENYEUCHUNGU WA ZANZIBAR DHID YA WANAOIDHULUMU uhuru wa zanzibar inawezekana.

 3. Waheshimiwa kusemea matumizi mabaya ya fedha za Serikali pasi na hatua zozote kuchukuliwa imekuwa nyimbo ya SMZ. Waheshimiwa walitakiwa pamoja na mambo mengine wamuulize Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni kwani alishindwa kuwachukulia hatua Makatibu Wakuu ambao Katika Budget ya 2011/2012 aliwataja kuwa miongoni mwa Wabadhirifu wakubwa wa fedha za Serikali. Kwa kuwa katika budget ya 2012/2013 Waziri wa Fedha hakusema lolote kuhusu hawa ni dhahiri kuwa hatafanya lolote hata kama wawakilshi watesema kwa sauti ya juu kupita kiasi. Hali hii ya ubadhirifu wa fedha za Serikali tuliyonayo Zanzibar inachangiwa na mambo.

  Kwanza, Serikali yote inawajibika kwa mtu moja tuu. Ikitokea hali kama hii na muajibishaji kuwa kimya tuu na ikitokea kusema hainekani kuwa mkali mambo lazima yaharibike.

  Pili. imekuwa utamaduni wa watu wa Zanzibar kutocukia waovu. Watu wanaoiba wanajulikana, lakini haijwahi kutokea watu kumtenga hata mwizi moja na hivyo kujihisi kuwa watu wanachukia matendo yake. Wakati Zanzibar ina upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi eti watoto wengi leo wanakimbilia kusemea uhasibu kwa kuwa yaonekana ni kada yenye kutajirisha mtu hara ivewezekanavyo.

  Tatu, legislative body we have is weak kuiweka Serikali kitimoto na kuiwajibisha. Wawakilishi waliowengi ni school dropouts ambao uoni wao wa mambo ni mfupi kama mkia wa mbui. Utasikia Barazani kwa mfano, Waziri anatoa jibu na dakika 3 baadae anasimama mwakilishi mwengine na kumuuliza suali lile. Mheshmiwa Naibu Waziri wa Afya Jumatano June 20, 2012 alieleza kuwa “Zanzibar imefanikiwa kupunguza maradhi ya kichocho kutoka 60% hadi 15% kwa Pemba na 50% hadi 08% kwa Unguja. Kisha Mheshmiwa moja bila kujua kuwa majibu ya suali lake yametolewa akamuuliza Naibu Waziri suali lile. Mwengine akaeleza kuhusu Wachina walivyo wamaliza makonokono kwenye mto huko China na kisha akechekesha kwa suali ambalo Waziri alishalijibu. Hali hii yaonesha jinsi baraza lilivyofanywa na watu wengi wanahitaji kwenda kwenye kisomo cha watu wazima katika level ile ile ya miaka ya mwanzo wa Uhuru. Legislative body we have is also made of people coming from the destitute backgrounds. Watu kama hawa ambao wanajua 2015 hawatarudi tena Barazni kwa mtindo wa kupasiana vijti walionao si rahisi kuwa na msimamo Wengi wao wanajifunza kazi huku wakiwa na pressure za haja ya kukimbia majimbo yao ili wasiombwe au wakijaribu kuua warithi wao ambao wamekaa midomo wazi huko majimboni. Watu hawa si dhani wanaupeo mkubwa zaidi ya mahitaji haya 2.

  Tatizo lengine tulilonalo latokana na kuwa executives, particularly ministers wanadannganywa na watendaji wao na kwa kuwa watendaji wao wananguvu kutokana na utukufu wao kwa vyama Mawaziri wajikuta wakiwa dhaifu kama ndifu. Naibu Waziri asemapo kuwa hana habari kuwa watu hulipia huduma pasi risiti katika hospital ya Mnazi Moja inakuwa kichekesho. Kuna Idara ya Ex-Ray, Maabara, Kitengo cha Mapinduzi Kongwe cha Occupational Health Unit ambavyo matendo yao yanakaribia na Firauni. Mheshimiwa Naibu Waziri atoe e-mail yake ili tumtumie documents za huduma za hapo ambazo zilitolewa pasi na risiti.

  Mambo hayo na mengine mengi ambayo si rahisi yote kuyataja hapa ndio kikwazo kikukbwa kwa Zanzibar kupiga hatua. Kusonga mbele kwa Zanzibar kunatemea kiasi gani tutakuwa tayari kufanya haya:

  (a) Zanzibar kutawaliwa kwa mfumo wa kimajimbo na hivyo, Mamlaka makubwa kuweka kwa Serikali za mitaa ambazo sasa haziwashi wala hazizimi. Hili litahitaji mabadiliko au uindikaji upya wa Katiba.

  (b) Kila mtu katika nafasi aliyonayo atangulize maslahi ya wwote mbele na awe tayari kujinyima leo kwa faida ya watu wanaokuja.

  (c) Baraza letu Waakilishi lifanywe na wakereketwa wa vyama lakini wenye sifa.

  (d) Mawaziri wawe executives in the true sense of the word. Sasa nafasi zao ni ceremonial – huku Wahasibu na makatibu wakuu wakikaaa juu ya vichwa vyao. Angali Wizara ya Mawasilano na Scandal ya Watoto wa Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Si Wizara ya Elimu – miaka ya nyuma ghost workers sas student loan scam. Bado watu hawa wapo tuu utafikiri Mungu aliwaumbia kwa kazi hii.

  (e) Serikali iwe ijisimamie – watu waingie kwa sifa na si nasaba. Ukiajiri kwa nasaba usitarajie jipya zaidi ya uhamishwaji wa matarajio ya koo hizo kutoka majumbani kuja maofisini. Mifano ya sasa inatosha kujibu hali hii.

  Wakala huu hautoshi kuleza kila kitu!

 4. Unapomnyima mtu haki yake ya msingi na ikawa unajua kama mtu huyu ninamuonea tu lakini kweli hii ni haki yake , basi hakuna suluhu isipokuwa kwanza urejeshe haki yake halafu ndio mkae kwa mazungumzo.

  Zanzibar imedhulumiwa haki zake zote za msingi na Serikali ya Muungano,
  Muungano umejifanya ni Mrithi halali wa Mali za Wazanzibar .
  Muungano umehodhi Uhuru ,Utu na heshima za Watu wa Zanzibarbila kujali .
  Sasa tunapoukataa huu Muungano wao hawana sababu za kutulazimisha,
  Ikiwa Bank Kuu ni mtaji wa Nchi mbili Zanzibar naTanganyika zilizotowa mtaji sawa vipi leo muuzaji mhasibu mpokeaji na mtumiaji awe Tanganyika tu na huyu Zanzibar asipewe hata kipande cha mkate halafu akubali,
  Huu ni Ujambazi wa makusudi na wa muda mrefu tunaukataa
  Unapomkataa mke au mke kumkataa mume huwa kuna sababu za kukataana ,
  Mke akiwa mdokozi na Mume akiwa mwizi basi hakuna makubalianotena . Sisi kwa vile tumemuona mke huyu ni mdokozi wa ndani tumeamua kuachana nae mpaka arejeshe alivyoiba kwa mume
  Sisi ndio waume kwa sababu ndio tunaoacha na Muungano hatuutaki tunauwacha kwa ila zake hizo.
  Mkitulazimisha mnachukuwa sheria mikononi mwenu na sisi tutawaita DUNIA waje kushuhudia Dhulma zenu.
  Hamuwezi kuwaburura wazee wetu watoto wetu na sasa vijukuu vyetu mnaviibia sisi tuwatazame tu , haiwezekane , hata Dini hakubali kuonewa ukakaa kimya. NO NO NO ENEOUGH IS ENEOUGH .

 5. Pingback: Matumizi ya fedha za serikali yachunguzwe·

 6. GOOD POINTS I LIKE THIS. I THINK PEOPLE WITH GOOD IDEAS LIKE THESE ONES ARE STILL NEEDED IN ZANZIBAR. WITH GOOD IDEAS LIKE THIS AND INDEPENDENCE FROM THE CURRENT GHOST MUUNGANO WE CAN MAKE IT. CHEERS AND KEEP IT UP.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s