Nilisema, nikasihi, serikali haikusikiliza

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,alipokuwa akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari Ikulu Zanzibar

Jabir Idrissa

HALI mbaya ya usalama iliyoanza Jumamosi usiku, imesadifu nilichokieleza wiki mbili zilizopita. Nilimsihi Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kupitia safu hii, kuwa asikubali maneno ya fitna anayolishwa na wasaidizi wake. Nikasema akikubali fitna, atajishawishi kukasirika; na matokeo ya mtu kukasirika, ni kuchukua hatua yenye madhara makubwa.
Ilikuwa katika makala iliyojadili uhuru wa watu kusema na kujadili mambo ya nchi yao – ilitoka na kichwa cha habari kisemacho, “Hasira zako Dk. Shein, ni hasara kwako.”
Kweli, hasira zilizowajaa viongozi wa serikali na vyombo vyao, zimezaa hasara. Sasa nchi, iliyokuwa imetulia kabisa, watu wakienda na kurudi kwenye shughuli za kutafuta maisha, imerudi kwenye hofu kubwa.
Rais hakuongoza vizuri au walioelekezwa kuongoza hawakutenda vizuri. Hapa, hapakutumika hekima na busara kwa kiwango. Hapa, kuna hali ya serikali kutoonyesha uvumilivu kwa raia.
Kwa kuwa Rais Dk. Shein ndiye kiongozi mkuu Zanzibar, analazimika kubeba lawama kwa madhara yaliyotokea. Yeye atatafuta wengine wa kuchangia lawama hizo.
Kosa kubwa lililofanywa katika kadhia hii, ni uongozi kuruhusu Jeshi la Polisi kukamata kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho, Sheikh Mussa Juma.
Hapana. Kumkamata mtu si kosa, ila mazingira yaliyotumika. Ya Sheikh Mussa yalikuwa ya kigaidi na kijambazi. Yaliwashtua walioshuhudia. Wakajenga chuki dhidi ya serikali.
Hebu nitangulize hali ilivyokuwa Jumapili kabla ya kurudi kueleza kilichotokea Jumamosi usiku.
Soko la Darajani (maarufu la Mkunazini), lilifungwa kutwa nzima. Ndio tegemeo kwa wakazi wote wa maeneo ya katikati ya mji na nje kidogo (ng’ambo).
Stendi kuu ya magari (daladala) inayohudumia wananchi (daladala) ilifungwa. Stendi hii pia inahudumia wasafiri watokao vijiji vya mkoa wa Mjini Magharibi, na mkoa wa Kusini Unguja (Wilaya ya Kati na ya Kusini).
Usafiri wa umma na binafsi ulikwama kwa kuwa eneo la mkabala na lilipo soko hilo lilizuiwa kuingia magari.
Mji mzima na vitongoji vyake ulienea sauti/milio ya risasi za mipira na mabomu ya machozi zilizofyatuliwa na polisi.
Watalii walifadhaika sana kila waliposikia milio ya risasi.
Vijana wenye hasira walienea mitaani kuleta tafrani.
Mali nyingi ziliharibiwa, yakiwemo makanisa mawili.
Inafaa sasa kueleza kwanini hayo yalitokea. Najadili yaliyojiri Jumamosi. Ilianza kwa utulivu kama kawaida, mpaka jioni. Nilikuwa mjini katika moja ya hoteli tukijadiliana masuala ya kitaifa na wenzangu.
Tulipotoka saa 11, nilikimbilia waandishi wa habari kupata hili na lile – mambo yanayohusiana na habari. Utulivu mtupu.
Nikasimuliwa Jumuiya ya Uamsho iliendesha mhadhara mpaka mchana kwenye uwanja wa Lumumba katika mfululizo wa ratiba inayoendelea kwa miezi sita sasa.
Mihadhara ya asasi hii ya kidini, imekuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi, hasa vijana ambao huwa wengi na kuifuata mpaka maeneo ya mikoani. Uamsho wameshaendesha zaidi ya mihadhara 50 Unguja na Pemba.
Mhadhara ulihusisha matembezi yaliyoongozwa na Amir wa Uamsho, Sheikh Farid Hadi, msafara ukipitia Gulioni, Msikiti Mabuluu, Mlandege, Michenzani, Rahaleo, Kwa Biziredi na kurudia uwanjani Lumumba.
Ilipofika saa 7 mchana, ulikuwa umekwisha; watu wametawanyika kwa amani na hakukuripotiwa tukio lolote la vurugu pamoja na askari polisi kuingilia msafara eneo la Kombawapya, wenyewe ukiwa umeshaingia uwanjani. Shwari ikaendelea mjini.
Ilipokaribia saa 2 usiku, alitokea kijana mtanashati kufika msikiti wa Kwa Bizireni anaposali na kusomesha Sheikh Mussa, mmoja wa viongozi waliohudhuria. Hakuna aliyemfahamu kijana huyu.
Alitoa salamu na kuitikiwa na wote waliokuwepo. Yule kijana aliyeonekana akishuka kwenye gari aina ya Noah, iliyopaki pembeni, alimvuta kiungwana Sheikh Mussa akimuomba wazungumze pembeni kidogo.
Sheikh Mussa alimfuata kijana ambaye akiifuata gari. Alipofika akiwa nje ya gari, huku mlango wa nyuma ya dereva ukiwa wazi, Sheikh Mussa alisalimiana na mtu aliyekuwa ndani. Lakini, ghafla akavutwa ndani ya gari, mlango ukafungwa kwa nguvu, na dereva akaondoa gari kwa kasi.
Ile ikashtua watu waliokuwa msikitini. Wakabaini Sheikh Mussa amechukuliwa na gari imeelekea Kariakoo.
Walibaini baadaye iliishia kituo kikuu cha Polisi Mkoa kilichopo Mwembemadema. Wakapata uthibitisho kuwa Sheikh Mussa amekamatwa na kushikiliwa Madema.
Waumini waliokuwa Kwa Biziredi walifadhaishwa. Hawakulala. Viongozi wa msikiti wakateua ujumbe kwenda kufuatilia Madema.
Hakukuwa na kiongozi wa polisi kuthibitisha. Taarifa zilivuja kutoka ndani ya kituo kwamba Sheikh Mussa kweli anashikiliwa pale kituoni.
Jitihada za viongozi wa msikiti kusihi Polisi wamuachie na kama kuna tuhuma apewe dhamana, hasa kwa kuwa familia yake haijui, zilishindikana. Taarifa za kukamatwa kwake zikaanza kuenea taratibu mjini.
Haikuchukua muda, makundi ya watu wakakimbilia Madema kutaka kujua hatima ya Sheikh Mussa. Kwa kuwa Polisi hawakutaka kujadiliana, walijiandaa kulinda kituo chao na kulinda “mtuhumiwa” wao.
Mwanzo wa matatizo ukawa umewadia. Polisi hawataki kusema wamemshika kiongozi wa Uamsho kwa tuhuma gani; wala hawapo tayari kujadiliana na yeyote ili kumpa dhamana. Huku watu waliokuwa wanajazana kituoni wakitaka kujua hatima ya kiongozi huyo.
Ilipotimu saa 3 usiku, eneo la Michenzani, mita chache kufika Madema likawa limejaa watu wanaofuatilia hatima ya Sheikh Mussa. Ndipo polisi walipoanza kulinda hadhi yao baada ya kuamini wanachezewa.
Risasi za mipira na mabomu ya kutoa machozi zikaanza kufyatuliwa moja baada ya nyingine. Kwenye saa 5 usiku, eneo hilo likawa limeenea harufu ya kemikali na moshi mzito. Sasa hata waliokuwa wapita njia na waliolala wakalewa sumu.
Nilishindwa kupita kwa gari Kariakoo. Palikuwa na kundi kubwa la vijana; barabara imezibwa kwa mawe na mapande makubwa ya zege huku matairi yakiwaka moto.
Niliposogea kwa kutembea nikijaribu kufika Michenzani, niliishia kwenye mkunazi, mita 100 hivi kufika. Nikaona magari ya polisi waliosheheni silaha mbele ya ofisi kuu za Idara ya Majenzi.
Kila baada ya muda fulani, nikasikia milio ya risasi na mabomu ya machozi zikielekezwa walipo vijana Kariakoo. Moshi na kemikali ziliponichosha, nikarudi eneo la Posta tulipoegesha gari.
Pale Kariakoo, nikabaini vijana wamekata tamaa; hawakuwa na ujasiri wa kusonga mbele kwenda kufuatilia kiongozi wao Madema. Wafanyeje? Wakaanza kuondoka katika vikundi vidogovidogo wakielekea maeneo ya ng’ambo.
Wakati wakitembea huku wengi wakiwa na mawe, marungu na mapande ya nondo, nilisikia baadhi yao wakisema, “Sasa kwa kuwa wametuzuia kumpata kiongozi wetu, tunasaka makanisa na baa tutayateketeza.”
Wamekasirishwa na maudhi ya dola. Nikajua kazi itakayofanywa kutoka hapo, ni kazi chafu.
Ndivyo ulivyokuwa usiku wa Jumamosi. Mpaka nilipolala, nikiwa hoteli ya Grand Palace, Malindi, nilikuwa nikisikia milio ya risasi ya hapa na pale.
Hata nilipokuja juu yapata saa 9.30, nilisikia milio ya risasi, hali iliyoendelea hadi nilipoondoka mjini Zanzibar saa 7 mchana Jumapili.
Sishangai kusikia Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amesema walikamata watu saba baada ya vurugu. Hakusema kamwe kama walimchukua kihuni kiongozi wa watu na hatimaye kuvutia umati kufika kituoni Madema kufuatilia.
Taarifa yake ilikuja saa kadhaa baada ya uongozi wa Uamsho kutoa tamko wakisema hawahusiki na vurugu wala uharibifu wa mali uliofanywa. Uislamu unakataza vurugu, wamesema.

Advertisements

6 responses to “Nilisema, nikasihi, serikali haikusikiliza

 1. Pingback: Nilisema, nikasihi, serikali haikusikiliza·

 2. Kwa mtaji huu, watanganyika hawatuachi ng’o
  Wameweza kutumia makachero wao kubadilisha agenda na wamefuzu kwa hilo. Sasa kinachozungumzwa na kuchomwa makanisa tu. Leo kwenye sala ya Ijumaa sheikh Suraga alitumia hotuba zote mbili kuzungumzia tafshani liotokea mwisho wa wiki. Waislamu wenyewe wamegawika kivyama. Niliyaona haya baada ya sala watu wakapokezana mawazo na wengi wanashtumu ima Wapemba au CUF bila kutaja jina. Wanatumia “hawa ndugu zetu wa kisiwa chaPili”

  Sijui lakini nina wasiwasi kama Watanganyika hawa kwa mbinu hii kama watatuachia

 3. Hii ni kanuni ya kimaumbile ya kupata uhuru popote pale jitihada zaidi inahitajika tusiondoke kwenye ajenda yetu. Mambo yashakaa ndipo tukaze uzi miezi na hata miaka Allah (s.w) atashusha nusra. Amin
  Hapatatawalika mpaka kieleweke.

  MUUNGANO HATUUTAKI.

  JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR KWANZA.

  “When peace fails apply force”

  Nawasilisha.

  SERELLY.

 4. Kaka uchambuzi wako kwa kweli ni mzuri na ni wa kina kabisa.Mimi mawazo yng yanafanana na yako kwani bado uchomaji moto wa makanisa naamini ni mchezo mchafu hata kama tupo katika kupambana na Wakoloni watanganyika.ZANZIBAR kwanza!

 5. Aslaam Aleykum jamiiya. Baada ya yote haya tunayojadiliana, FUNGA KAZI inakuja karibuni tu hapa – pale uongozi wa UAMSHO utakapotaja majina ya watu wanaotuhumu kuwa ndio waliohusika kuchoma makanisa. Hapa ndipo ninarudi kule tulipokuwa tukishuhudia mijeledi kwa wananchi; vinyesi visimani na madarasani. Siku wananchi wa Shumba mjini walipoamua kupiga gadi (guard), lahaulaaaaa, waliokutwa kwenye landrover ya serikali ni makachero wa polisi na Intelligence. Na kweli ndio waliokuwa wakifanya USHENZI, uthibitisho ni kushindwa kwa kikosi cha Kamishna Robert Manumba, sasa ni DCI, kutoa ripoti ya uchunguzi uliofanywa kubaini nani hasa waliokuwa wakihusika na milipuko ile, niliyoiita ya KISHETANI wakati ule kupitia gazeti la RAI.
  Wallah serikali za kidhalim zina mambo kwelikweli. Haya TUSUBIRI, muda utaamua!!!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s