Hali bado ni tete Zanzibar

Kikosi cha Kuzuwia Fujo FFU kikizunguka kikiwa kimejihami katika maeneo ya Michenzani ambapo tayari jeshi la polisi limepiga marufuku mikusanyiko yoyote Mjini hapa

WASIWASI mkubwa umetanda kwa siku ya pili mfululizo katika mitaa ya miji ya Zanzibar baada ya askari wa jeshi la polisi kupiga mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya wafuasi wa taasisi za kidini zinaozongozwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).

Wafuasi hao ambao walikusanyika katika makao makuu ya polisi mkoa wa mjini magharibi Madema jumamosi jioni, kushindikiza kutolewa kwa viongozi wao wanaoshikiliwa kituoni hapo.

Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari kuwa wafuasi hao wamefanya uharibifu mkubwa ikiwa pamoja na kuchoma moto makanisa mawili na kwamba watu saba wanaotuhumiwa saba wamekamatwa na jeshi hilo.

Akizungumzia kuhusu hali hiyo ofisini kwake Ziwani Mjini Unguja Kamishna Mussa alisema kwamba jeshi lake litaendelea kuwasaka na kuwatia mikononi wote waliopanga fujo hizo pamoja na viongozi wote wa jumuiya ya Uamsho.

Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar ndio iliyohusika na kuwachochea vijana kukusanyika na kufanya uharibifu ikiwemo kuchoma moto gari, kupanga mawe barabarani na kufanya hujuma mbali mbali kinyume cha sheria. Tutaendelea kuwasaka kwa gharama zote” alisema Mussa.

Kamishna alisema kwa sasa mikusanyiko yote ya mihadhara ya kidini na vyama vya siasa lazima ipate kibali cha polisi vyenginevyo jeshi lake litatumia nguvu za ziada kutawanya mikusanyiko hiyo ili kulinda sheria za nchi, amani na utulivu.

Maeneo kadhaa na mji wa Zanzibar hasa Darajani na Michenzani ambapo muda wote ni sehemu ambazo zenye harakati nyingi za biashara jana zilikuwa zimebakia tupu kutokana na askari waliojihami kufanya doria katika mitaa yote na kuripua mabomu kila penye kikundi cha watu waliokusanyika wakinywa kahawa.

Mitaa hiyo ilikuwa imechaguliwa na mawe, matufali na magogo yaliowekwa barabarani kuziba njia kuzuwia magari yasipite huku mipira ya magari ikiwashwa moto na vijana hao.

Hata hivyo Kamishna wa Polisi alijizuwia kuhusisha harakati za Uamsho na chama cha siasa pamoja na kukataa kutaja majina ya viongozi ambao tayari wanashikiliwa na jeshi lake.

Mpaka sasa hivi sina majina yao kwa jumla lakini tumewakamata viongozi wa Uamsho na tunatendelea kuwasaka lakini jina moja tu ndio ninalo ambalo ni Mussa Abdallah Juma” alisema Kamishna huyo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Bishop Dickoson Maganga alisema watu wasiojulikana walivamia kanisa lao eneo la Kariakoo Mjini Zanzibar majira ya saa 4.30 usiku na kuvunja ukuta, kuchoma viti vya plasitiki pamoja na gari yake.

Nasikitika na tukio hili ambalo tayari tumeiarifu polisi ambao jana usiku walifika hapa wakishirikiana na kikosi cha kuzima moto na kufanikiwa kuuzima moto huo ambayo kwa habati nzuri haujaathiri paa la kanisa letu” alisema kiongozi huyo.

Alisema kundi la watu ambalo lilikuwa likitoa maneno ya kashfa na kutishia maisha ya waumini waliokuwa wakifanya ibada usiku huo kukatisha ibada hiyo pamoja na kusababisha uharibifu wa mali ya kanisa hilo yenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni mia moja.

Kutokana na hali hiyo jumuiya ya Uamsho imetoa taarifa yake kwa vyombo vya habari kwa kukanusha kuhusika na kuchochea watu kuchoma kanisa pamoja na kuharibu mali za watu.

Hata hivyo Katibu wa Jumuiya hiyo, Abdallah Said alisema katika taarifa hiyo kwamba jeshi la polisi linapaswa kubeba lawama kwa yote yaliotokea kutokana na kuvunja sheria na kuwakamata viongozi bila ya utaratibu wa busara.

Uislamu ni dini ya amani na inahimiza mashirikiano na utulivu na hatuwezi kuwatuma watu kwenda kuvunja makanisa na kuharibu mali kwa sababu ndani ya imani zetu tunajua hilo ni kosa na jambo ambalo halifai katika maarisho ya dini yetu” alisema Sheikh Abdallah.

Taarifa hiyo ilisema pia kwamba Uamsho imekuwa wazi katika kudai maslahi ya Zanzibar na sio vyenginevyo na kuahidi kufanya hivyo kwa njia za amani na iwapo watakuwa wamekosea basi wapo tayari kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Ni lazima polisi wajue kwamba tupo tayari kufanya kazi kwa misingi ya kisheria na hata kwa kujisalimisha tupo tayari lakini ukamataji busara na sheria haukubaliki na ni vigumu kwa wafuasi wetu kuwadhibiti wasilalamike, tunachokitaka ni kura ya maoni haraka na hilo tutaendelea kulidai” alisisitiza Katibu wa Jumuiya hiyo katika taarifa yake.

Wakati viongozi wa Uamsho wakiendelea kutafutwa na jeshi la polisi nyumba ya kiongozi aliyeongoza maandamano juzi Sheikh Farid Hadi Ahmed inadaiwa kuvunjwa milango usiku wa manane alipokuwa akitafutwa na jeshi la polisi.

Hata hivyo taarifa hizo zimeshindwa kuthibitishwa na jeshi la polisi iwapo ni kweli polisi ndio waliofanya kitendo hicho au laa lakini wanafamilia wanasema waligongewa milango na kutakiwa wafungue baada ya kutofungua walisikia kishindo kikubwa cha kusukumwa milango hiyo, nyumba iliyopo eneo la Mbuyuni Mjini Unguja.

Vijana katika mitaa ya Zanzibar jana walionekana wakiwa na hamasa kubwa wakidai kuendelea kuungana na viongozi wao kudai haki ya Zanzibar pamoja na kutaka Zanzibar huru kutoka ndani ya mikono ya Muungano.

Sisi tunachokitaka Zanzibar yetu watupige mabomu, watuuwe, watukamate lakini tunataka Zanzibar yetu na hatusikii lolote” Vijana walisema katika nyakati tofauti.

Advertisements

11 responses to “Hali bado ni tete Zanzibar

 1. Wazanzibari wazalendo ni lazima tuwe makini na kutambua kuwa maadui zetu wanapanga kila hila kutupotezea malengo yetu ya kudai nchi kutoka kwa mkoloni mweusi. nashauri kuwa tunapaswa kuwasikiliza viongozi wa harakati yetu hii ya kudai nchi vyenginevyo tutajikuta tumenasa katika mtego. yaonekana wazi kuwa siku nyingi polisi walitafuta njia ya kuzuia mihadhara ambayo kwao ilikuwa ni tishio, ndio maana wamecreate hiyo fujo ya tokea jana ili wapate kusema viongozi na wafuasi wa UAMSHO wanafanya fujo.

 2. Naomba jeshi la wananchi watumie busara na serikali iwe sikivu kwa wananchi wake.kwani ndio waliowaweka.

 3. HAIJAWAHI HATA SIKU MOJA KWA SERIKALI NA VYOMBO VYAKE KUKUBALI MAKOSA. MWAKA 2001 SERIKALI YA TANZANIA BILA YA SABABU ZA MSINGI CHINI YA UTAWALA WA MKAPA ILIWAUA WAZANZIBARI ZAIDI YA 70 BILA YA KUA NA HATIA AU SABABU ZA MSINGI. SERIKALI ILIKUA NA JUKUMU LAKINI TUME YA MBITA IKASEMA NI MATATIZO YA KIHISTORIA TU. TUKIO HILI LA JANA NAAMINI LIMEPANGWA KWA MAKUSUDI NA VYOMBO VYA USALAMA WA TAIFA NA WALE VIONGOZI WA SMZ VIBARAKA WA TANGANYIKA KUWAKAMATA VIONGOZI WA UAMSHO KATIKA KIPINDI HIKI WAKIJUA FIKA KUA KITENDO HICHO KITASABABISHA UVUNJIFU WA AMANI KAMA ILIVYOKUA ILI WAPATE SABABU YA KUWAKAMATA VIONGOZI WA UAMSHO NA KUPIGA MARUFUKU MIHADHARA. UAMSHO KAMA TAASISI YA KIISLAMU HAINA UGOMVI WOWOTE ULE NA DINI NYENGINE SISI TATIZO LETU NI MUUNGANO AMBAO HAUNA UHUSIANO NA UKRISTO. HILI TUNALIEKA WAZI KUA HATUTAKI MUUNGANO NA TUNAOMBA WANANCHI WAULIZWE HILI KWA KURA YA MAONI. HII INAONEKANA WAZI KATIKA KAULI YA KAMISHNA MUSA. HIVI POLISI WANA MAMLAKA GANI YA KUZUIA HAKI YA KIKATIBA YA WAZANZIBARI MPAKA WATOE WAO KIBALI? KAZI YA POLISI NI KUSIMAMIA AMANI KATIKA MIKUTANO YA UAMSHO NA JUMUIA AU VYAMA VYENGINE VINAPOFANYA MIKUTANO NA SIO KUTOA VIBALI. TUNATAMKA WAZI KUA HATUTOOMBA VIBALI KWA KITU AMBACHO NI HAKI YETU. HIYO MISHAHARA MIKUBWA TUNAYOKULIPENI MNADHANI NI KWA KAZI GANI? MUSA HUNA HAKI WALA MAMLAKA YA KUINGILIA UHURU WETU WA KIKATIBA KWA VISINGIZIO VYA KUPANGA. TUNAJUA KUA UMETUMWA NA NANI UNAMTUMIKIA. HII PICHA YOTE INAONYESHA KUA NI YA KUPANGWA ILI MMPATE SABABU YA KUZIMA HARAKATI ZA UAMSHO. MUSA TUNAKWAMBIA UWE MAKINI SANA WEWE NI MZANZIBARI NA USIKUBALI KUTUMILIWA KWA KUA UNAPATA MASLAHI BINAFSI. ANGALIA KABLA YA KUKAA WEWE HAPO WANGAPI WAMEPITA NA LEO WAKO WAPI? WENGINE WAMESHAFUNGWA MFANO WA PIPI, WENGINE HAWAJIJUI WALA KUJITAMBUA. MAISHA NI MAFUPI TU HAYA. HAKIKA MWENYEZI MUNGU NI MWENYE KUJUA KILA KITU.

  • ni kweli kabisa kua jeshi la polisi kazi yake sio kutoa kibali kazi yake ni kulinda usala wa raia ambae yeye ndie aliemuweka alipo . JAMANI TUKUMBUKE USALA WA WA ZANZIBAR NI WA KILA MZANZIBAR SIO MWENGINE YOYOTE .

  • yaani kuvunjiwa mlango sheikh Farid imekuuma sana lakini kuchomewa gari mchungaji na kuchomwa kanisa haijakuuma kabisa?Kuwa na roho ya kibinadamu hivi mlango na gari ipi ina bei kubwa?

 4. Kamishna wa polisi elewa kwamba wewe ni muislam na binadamu kumbuka kwamb iko siku utaondoka ktk mgongo wa ardh utamjibuje mungu usihadaliwe na punz na kipato vyote vko ktk transion

 5. Ni dhahiri hili tunalodai limewasakama na kuwauma, hao wanaopiga mabomu bila shaka wakirudi nyumbani wanakaa kwenye vipembee na kulia kimnyakimnya, mishahara haitoshi, mazingira mabaya ya kazi, wanapiga ndugu zao, lakini ndugu zetu tuungane tupate Zanzibar yetu acheni ushambenga mukija kwetu tutawapokea na tija ni kubwa huko mbele kwetu sote.
  haki naitendeke haturudi nyumba tunasema kila pahala mimi mwana wa Kizimkazi

 6. Acheni kuhusisha dini ya Mwenyezi Mungu na mambo ya kisiasa; hakuna dini yoyote hapa duniani ambayo inachochea vurugu. Mmesahau “Lakum dinukum waliyadin”? Kama mnaamini kuwa mwenyezi Mungu atahukumu kwanini mnataka kuwahukumu watu? Chuki za nini manake mnawachukukia waislamu wenzenu pia kisa ni wa bara. Laanakum! Ndo maana matatizo hayaishi nyie mnadhani kuwa mmebarikiwa hakuna lolote.

 7. Ni muhimu Viongozi wote wakatafakali kwa makini Tatizo ni nini na kuweza kupata Ufumbuzi wa suala hilo na Jeshi la polisi lifanye kazi yake Ipasavyo. Amani haiwezi kuwepo kama watu wataendelea kufa, Hakuna mtu ambaye anaweza kusahau nini kilitokea mwaka 2001.
  Hivyo Kutonesha kidonda ambacho hakijapona KITALETA madhara makubwa kama hatua za haraka haziwezi Kuchukuliwa

  Tunaomba Serikali ICHUKUE Tahadhali kabla ya Hatari, Hali hii INATISHA, ni ngumu kumaliza hili kwa MABAVU inahitajika BUSARA zaidi.
  Mwenye makosa achukuliwe Kisheria sio kwa kupigwa. Wakati umefika wa Kila MTANZANIA kusikilizwa kwa shida yake wakati muafaka sio mpaka KUMWAGIKE DAMU NDIO ANASIKILIZWA.

  Maisha mema katika Ujenzi wa Taifa letu

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s