Zanzibar ingekuwa nyingine wangepatanishwa Abeid Karume na Ali Muhsin

Marehemu Sheikh Ali Muhsin Barwany aliyekuwa Kiongozi wa Chama Cha Hizbu

Ahmed Rajab

HALI za maisha Zanzibar ni ngumu. Watu wanaishi lakini wengi wao wanaishi maisha ya taabu. Imekuwa kana kwamba Wazanzibari wa leo ni mahuluki taabu. Asilimia kubwa ya vijana hawana ajira, wenye ajira wanalipwa mishahara ya chini kabisa kulinganishwa na wanavyolipwa wafanya kazi wenzao katika nchi jirani za Afrika ya Mashariki.

Wazanzibari wanayapata maji kwa taabu. Umeme vivyo hivyo. Ukija upande wa huduma nyingine zinazotolewa na Serikali ya Zanzibar mambo ni hayohayo.

Matatizo huzidi kuzuka pale serikali inapolazimika kutumia fedha nyingi isizoweza kuzimudu. Serikali hulazimika kufanya hivyo ama kutokana na shinikizo za kisiasa au uendeshaji na usimamizi mbovu wa wakuu wa idara.

Kati ya matatizo ya Zanzibar ni kwamba serikalini hakuna udhibiti wa kutosha wa madeni ya serikali na dhamana au rahani za madeni hayo.

Wizara ya Fedha ina mfumo maalumu wa matumizi ya kipindi cha wastani. Lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kwamba fedha zinagawanywa kwa kipindi cha miaka mitatu kwa mujibu wa vipaumbele vya kitaifa na vya sekta maalumu.

Hadi sasa lakini utaratibu huo haufanyi kazi sawasawa. Bado masuala ya matumizi ya fedha za serikali yanapangwa kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja na hakuna mahusiano baina ya makadirio ya matumizi ya mwaka mmoja na viwango vya juu vya bajeti vya mwaka unaofuatia.

Japokuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita kumepatikana maendeleo katika utoaji wa huduma za kimsingi za afya na elimu, kiwango cha vifo vya watoto wachanga ni 61 kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa hai. Na inakisiwa kwamba utapiamlo unawaathiri kama thuluthi moja ya wakaazi wa Zanzibar.

Inakisiwa pia kwamba sasa Visiwa vya Zanzibar vina wakaazi wapatao milioni moja na robo — ikiwa asilimia 2.7 ya wakaazi wote wa Tanzania. Na idadi ya wakaazi wa Zanzibar inaongezeka kwa kima cha takriban asilimia 3.1.

Kama nusu ya idadi ya wakaazi wa Zanzibar wanaishi chini ya mstari wa umasikini. Hivyo, uwezo wao wa kuyakidhi mahitaji yao ya kimsingi ya maisha ya kila leo ni mdogo mno.

Tukiziangalia hali za maisha ya Wazanzibari kwa kile kipimo ambacho wataalamu wa kiuchumi wanakiita kizigeu wiano cha Gini cha tofauti kati ya tajiri na maskini (the Gini coefficient of inequality) tutaona kwamba kuna usawa zaidi wa hali za maisha huko Zanzibar kuliko ilivyo Tanzania Bara au hata katika nchi nyingine za Afrika ya Mashariki. Bahati mbaya huo ni usawa wa ufukara. Hali za wengi wao ni za umasikini.

Moja ya athari za umasikini huo uliozagaa katika jamii ni kuongezeka kwa ufisadi pamoja na vitendo vingine vya ulaji rushwa na vya matumizi mabaya ya mali za umma. Ufisadi huo unazidi kwenda arijojo kwa vile mashirika au taasisi zinazowajibika kuuzuia hazina uwezo wa kuuchukulia hatua madhubuti.

Taasisi hizo pia huvunjwa nguvu kwa tashwishi za kisiasa za viongozi waliopanda vichwa na kujiona kuwa wao ndio wao, wenye nchi na vyote vilivyomo nchini.

Huo uroho wao wa mali na matumizi mabaya ya madaraka yao ya kiserikali ndio unaowafanya wakawa watovu wa nidhamu na wakathubutu kukiuka sheria na kujichukulia mali za umma, toka ardhi, majumba au kuzikodisha, tena kwa ujeuri, rasilimali za umma kwa bei za kutupwa ilimradi wao binafsi wanufaike. Potelea mbali ikiwa nchi inaingia hasara.

Hata hivyo, na juu ya shida zao zote hizo za kiuchumi, Wazanzibari wako makini na wanaonyesha kuwa wana subira na uvumilivu mkubwa. Wanaendelea kuwa na matumaini, pengine yaliyo makubwa kuliko pale yalipopatikana maridhiano na suluhu kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi — Civic United Front (CUF) — na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Ilipoundwa serikali hiyo, Novemba 2010, Wazanzibari wengi waliamini kwamba yale matatizo ya kiuchumi na ya kijamii waliokuwa wakiyakabili kwa muda mrefu yatatoweka.

Miongoni mwa matatizo hayo ni kuruka kwa haraka kwa bei za vyakula na za bidhaa nyingine zilizo muhimu kwa maisha, ufisadi na uzorotaji wa kazi serikalini, huduma zisizoaminika au kutabirika za umeme na maji na uchumi ambao kwa jumla umekuwa ukirudi nyuma ijapokuwa takwimu za serikali zinaonyesha vingine.

Ukweli wa mambo ulivyo hii leo Zanzibar ni kwamba jambo linalowashughulisha wengi ni namna ya kujipatia ajira ya halali itayowawezesha kupata pato. Hivyo changamoto yao kubwa ni namna ya kujipatia rizki na kujilisha wao na walio wao. Wengi wao wameshindwa.

Hata hivyo, bado wangali wakiamini kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa itachukuwa hatua za haraka za kuiondosha hiyo njaa iliyozagaa nchini.

Hapana shaka yoyote kwamba juu ya shida na mashakil ya kimaisha yaliyopo Zanzibar, maridhiano yamefanikiwa kuuzika ule uhasama wa kisiasa ulioibuka tangu mwaka 1957 pale wakoloni Wakiingereza walipoanzisha mfumo wa uchaguzi Visiwani humo.

Mfumo huo haukutumika toka 1964 hadi 1995 wakati ambapo kulikuwa na mfumo mbadala wa utawala wa chama kimoja, mfumo ambao tumeona jinsi ulivyowawezesha watawala kutumia vibaya madaraka yao.

Inatupasa tushukuru kwamba hii leo watu hawaonekani kuwa ni maadui wa taifa au makhaini wanapochukua msimamo wa kijasiri wa kuikosoa serikali yao, kama kwa mfano kuhusu suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Msimamo huo, niliokuwa nikiuashiria kwa muda mrefu katika makala mbalimbali, sasa umedhihirika bayana katika vikao na mihadhara inayofanywa Visiwani kuhusu Katiba mpya ya Tanzania.

Kikichojitokeza wazi ni jinsi Wazanzibari wanavyoupinga Muungano wa miaka 48 kati ya nchi yao na Tanganyika. Kwa kawaida, Wazanzibari ni watu walio wavumilivu, walio wataratibu na wa pole na wanajivunia ukarimu wao wa kuwapokea wageni wanaozuru Visiwa vyao. Hata hivyo, wana sifa ya kuwa wakali wanapohisi kuwa wanaingiliwa na wageni katika mambo yao ya ndani.

Historia imetuonyesha athari mbaya za wageni kuingilia siasa za Zanzibar kama kwa mfano pale Tanganyika ilipokiunga mkono chama cha Afro-Shirazi Party na Misri ilipokiunga mkono chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu).

Labda mambo yasingeliharibika lau nchi jirani zingewapatanisha Sheikh Abeid Karume na Sheikh Ali Muhsin waliokuwa viongozi wa vyama hivyo viwili vya huko Zanzibar. Uhasama kati ya vyama hivyo ndio uliopelekea Mapinduzi ya Zanzibar, kuundwa kwa Muungano na kutoweka kwa Zanzibar katika ramani ya dunia.

Wazanzibari wameshuhudia jinsi hali zao za kiuchumi, za kijamii na za kimazingira zilivyodidimia katika kipindi ambacho serikali yao ilipoteza mamlaka yake makuu ya kuendesha nchi. Mamlaka hayo yakaingizwa katika ‘mambo ya Muungano’ na kwa bahati mbaya hakuna ushahidi wenye kuonyesha kwamba Serikali ya Muungano ilifanya chochote cha kuisaidia Zanzibar ipate maendeleo.

Ndiyo maana Wazanzibari, hasa wa kizazi cha baada ya Mapinduzi, wanashikilia kwamba mfumo wa Muungano ubadilishwe na uwe juu ya msingi wa Mkataba na si Katiba.

Matokeo yake yataifanya kila moja ya nchi hizo mbili za kindugu — yaani Tanganyika na Zanzibar — iwe sawa na mwenzake bila ya mmojawao kujifanya kaka wa mwenzake. Wanachodai ni kila moja ya nchi hizo mbili iwe na uhuru wake na isiwe na haja ya kutaka ridhaa ya mwenzake inapochukuwa hatua kuhusu mustakbali wake.

Bila ya shaka nchi hizo zinaweza zikashauriana lakini ziwe zinashauriana zikiwa nchi sawa ndani ya Muungano unaotambua haki ya kila nchi kuwa na kura ya turufu na haki ya kujitoa katika jambo lolote kati ya mambo yatayokubaliwa kuwa ni mambo ya kushirikiana kati ya nchi hizo mbili.

Mchakato huu wa sasa wa Katiba umezipa nchi zote mbili za Tanganyika na Zanzibar fursa nzuri ya kujiandalia mwanzo mpya wa kujenga mahusiano ya karibu zaidi, yaliyo mema zaidi na yenye manufaa kwao. Nchi hizo zimekwishaamuliwa na historia pamoja na jiografia kwamba lazima ziwe zinafuata sera za ujirani mwema na zisiwe na uhasama wa nchi moja kutaka kuyachimba maslahi ya nchi nyingine.

Hizi ni nchi zenye historia moja na mustakbali mmoja na lazima zishirikiane kunyanyua hali za maisha ya Watanganyika na ya Wazanzibari — na hasa za Wazanzibari kwa sababu ingawa Tanganyika imepata maendeleo kwa kiasi fulani Zanzibar imerudi nyuma.

Viwango vyake vya maendeleo vinaaibisha na yote hayo yanatokana na miongo minne ya utawala mbovu huko Visiwani pamoja na sera ya ubaguzi iliyokuwa ikifuatwa kujaza nafasi za kazi serikalini.

CHANZO: RAIA MWEMA

Advertisements

One response to “Zanzibar ingekuwa nyingine wangepatanishwa Abeid Karume na Ali Muhsin

  1. Mada imeandikika vizuri, inafurahisha kuisoma licha yakuwa sources za references ya takwim zilizowekwa haziko wazi. Aidha tittle ya makala hii na contents iliyomo kwa mawazo yangu haikumatch. Ukweli hatujui engikuwa wapi,lakini kila Akupalo Mungu lina heri nawe

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s