Hata tuyazime, maswali yale yale kuhusu Muungano yanaturejea

Mzee Aboud Jumbe akipewa pole na Dk Mohammed Gharib Bilal siku ya msiba wa mtoto wake Dk Suleiman Aboud Jumbe aliyefariki Decemba 2010

Jenerali Ulimwengu

HUKO nyuma nimeeleza kwamba haiwezekani kuijadili Tanzania pasipo kuujadili Muungano, na kwamba dalili za makundi ya watu kuhoji Muungano wetu kama ulivyo leo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Fursa tuliyo nayo hivi sasa ya kujadili na kuandika katiba mpya ni fursa adhimu tunayoipata kuujadili Muungano kwa kina na kuupatia ufumbuzi utakaotupeleka masafa marefu kidogo.

Ye yote anayetaka kujua jinsi masuala ya Muungano yalivyotusumbua katika historia yetu ya takriban nusu karne atakumbuka mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na tume na kamati mbalimbali zilizoundwa katika jitihada za kujaribu kurekebisha baadhi ya masuala yaliyoonekana kukera makundi ndani ya nchi, na jinsi ambavyo jitihada hizo zote na kamati na tume hizo hazikufanikiwa kuondoa malalamiko kuhusu Muungano.

Sasa itakuwa ni jambo la ajabu iwapo, wakati tunasema tunataka kuandika katiba mpya, tutajinyima wasaa wa kuujadili Muungano kwa kuwauliza wananchi wa pande mbili (Tanganyika na Zanzibar) ni nini wanachotaka, iwapo wanataka Muungano au hawautaki.

Swali hilo la msingi likiiisha kupatikana, na jibu likawa kwamba wanautaka Muungano, ndipo sasa itawezekana kuangalia kwa undani ni mambo gani ndani ya mfumo na taratibu za Muungano yafanyiwe marekebisho ili kuyaweka sawa na kukidhi matarajio ya pande mbili zilizoungana.

Binafsi nakataa dhana ya kuwaambia watu kwamba kuujadili Muungano ni sharti tujadili namna ya kuuboresha. Mtu huboresha jambo analotaka kuendelea nalo, na kama hataki kundelea nalo ni upuuzi kuanza kuliboresha. Haina maana hata kidogo. Na si kweli kwamba hatujasikia sauti za watu wanosema kwamba hawautaki Muungano, na wala pia si kweli kwamba hawana haki ya kuwa na mawazo kama hayo.

Njia pekee kwa wale wanaopenda Muungano uendelee kuwapo (pamoja na marekebisho yatakayokubaliwa) ni kuwaacha wana-Muungano wenyewe waseme kwamba wanataka kuuendeleza kwa kuuboresha. Iwapo watasema kwamba hawautaki, na tujue kwamba hiyo ndiyo kauli yao, huo ndio utashi wao. Kujidai kwamba tutauendeleza Muungano bila ridhaa ya Watanganyika na Wazanzibari ni ndoto za Alinacha.

Katika historia yetu tumekuwa na matukio kadhaa yaliyoutikisha Muungano lakini ikawezekana kuyazima kwa njia moja au nyingine. Tutakumbuka sakata la “kuchafuka kwa hali ya hewa” Visiwani mwaka 1983-84, iliyosababisha kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi.

Kimsingi alichokuwa akisema Jumbe ni kwamba Muungano ulihitaji marekebisho katika muundo wake ili uweze kukidhi mahitaji ya Wazanzibari.

Tukumbuke pia kwamba wakati Jumbe akichukua hatua za kufanya mapendekezo ya kuuboresha Muungano kadri alivyoona inafaa, alikuwa ni kipenzi cha Mwalimu Nyerere, ambaye alijiona raha kufanya kazi na ‘msomi’ mwenzake baada ya kusumbuana sana na Abeid Karume, muasisi mwenzake wa Muungano, Karume akiwa ni mtu asiyetabirika, na mwenye maamuzi yaliyotatanisha.

Inawezekana kwamba usiri wa hatua alizokuwa akitaka kuzichukua Jumbe ndio uliomuudhi Nyerere hata akaamua kumwadhibu Jumbe. Hata hivyo, haijulikani msimmao wa Mwalimu ungekuwa upi iwapo Jumbe angepeleka mapendekezo yake mbele ya kikao rasmi cha CCM au serikali na kuomba ridhaa juu ya mawazo yake ya kuboresha Muungano.

Tofauti na hii leo, ambapo majadiliano ndani ya NEC ya chama-tawala yanajulikana Kariakoo na Manzese kabla kikao hakijafungwa, wakati ule wa sakata la Jumbe kikao cha siri maana yake ilikuwa ni kikao cha siri. Kikao hicho hakina hata ‘hansard’. Ndiyo maana itakuwa vigumu kujadili kwa undani maudhui ya mjadala uliofanyika ndani ya kikao kilichohitimishwa kwa kumvua Jumbe nyadhifa zake zote na kumpeleka ‘uhamishoni’ Mji Mwema.

Muongo mmoja baadaye kundi la wabunge wa CCM lililojulikana kama G-55 (jina lilinuniwa na Issa Shivji) likaibuka na kudai marekebisho katika muundo wa Muungano kwa kuasisi serikali ya Tangayika na kuwa na muundo wa Shirikisho.

Hoja iliyopelekwa bungeni na kundi hili iliungwa mkono kwa nguvu kubwa na watu wengi na hatimaye serikai ikaridhia hoja hiyo na kukubali marekebisho hayo yafanyike.

Kwa mara nyingine tena ilikuwa ni Mwalimu Nyerere aliyesimama na kuipinga hoja hiyo, ikiwa tayari imekwisha kupitishwa na Bunge, na hatimaye juhudi zake zikafanikiwa kuitengua hoja hiyo.

Ikumbukwe kwamba Mwalimu wakati huo hakuwa rais wala mwenyekiti wa chama chake, lakini kwa ushawishi aliokuwa nao aliweza kufanya alivyofanya.

Nakumbuka, nikiwa mmoja wa kundi la G-55, tulikuwa na mabishano mengi na Mwalimu nyumbani kwake Msasani katika kipindi hicho, na nakumbuka kwamba Mwalimu alishikilia msimamo wake bila kutetereka, ingawaje baadhi yetu hatukuona mantiki ya kile alichokuwa akikitetea.

Kimsingi, msimamo wake ulikuwa kwamba muundo wa serikali tatu ungevunja Muungano. Sisi tulikuwa na mawazo tofauti, kimsingi, kwa sababu tulikuwa hatuoni matiki ya kuwa na serikali mbili, moja ikiwa ni ya Zanzibar na ya pili ikiwa ni ya Zanzibar na Tanganyika.

Hiyo ni historia. Lakini sasa zimejitokeza sauti zinazotoa mwangwi wa haya ninayoyasimulia, kwa mara nyingine zikidai muundo wa serikali tatu. Hizi ziko pande mbili za Muungano, nazo zinadhihirisha ukweli kwamba jambo hili halijaondoka; lipo na linahitaji mjadala wa kina ndipo lipatiwe ufumbuzi. Kulizimazima hakutasaidia sana.

Nimekuwa nikikagua kumbukumbu ili kujua kama Mwalimu Nyerere aliwahi kupiga marufuku mjadala kuhusu Muungano. Sikumbuki. Alimtoa Jumbe madarakani. Aliizima hoja ya G-55. Lakini sikumbuki hata mara moja akisema kwamba ni marufuku kuujadili Muunagno. Aliwaachia waliomzunguka waelewe kwamba kwake Muungano ulikuwa kitu azizi kwake na hapendi kichezewe, lakini hakusema kinagaubaga kwamba ni marufuku kuujadili.

Ninaweza kwenda mbali zaidi na kusema kwamba, hata kama Mwalimu angekuwa amesema waziwazi kwamba ni marufuku kuujadili Muungano, bado tungeweza, katika mazingira ya leo, tukasema kwamba pamoja na heshima yetu kubwa kwake, lakini Muungano unajadilika. Mambo yamebadilika, na dunia inasonga mbele, na alichokiamini baba yako sicho unachotakiwa lazima ukiamini leo.

Kama hivyo ndivyo, hakuna sababu yo yote ya kuweka makatazo katika majadala kuhusu Muungano. Acheni ujadiliwe kwa uwazi mkubwa kiasi kinachowezekana, mawazo yanayokinzana yashindanishwe na mumo tupate elimu ya kuuboresha Muungano.

Mimi binafsi ni muumini mkubwa wa mamlaka ya watu ndani ya sehemu wanamoishi, kwa sababu mamlaka hayo ndicho kielelezo thabiti cha dhana ya kujitawala.

Hatua yo yote inayopunguza uwezo wa wananchi wa sehemu fulani kujiendeshea shughuli zao kwa uhuru mpana kiasi kinachowezekana ndani ya umoja wa jumla, ni kitendo kinachokinzana na maendeleo.

Wako Wazanzibari wanaosema uhuru wao wa kuendesha mambo yao umebinywa mno; wako Watanganyika wanaodhani kwamba katika Muunago huu Wazanzibari wanapewa nafasi ambazo si zao, na kwa hiyo wanawanyima nafasi Watanganyika. Hususan, dhana ya u-Zanzibari imekuzwa mno hadi inaamsha jawabu la u-Tanganyika.

Shetani naye amejiingiza. Waziri wa zamani wa mafuta nchini Venezuela aliwahi kusema kwamba mafuta ya peteroli ni kinyesi cha Shetani nasi sote tunaogelea ndani yake.

Inaelekea Shetani ametutembelea hivi karibuni, na tunasikia kelele za “Yangu! Yangu!” Baadhi ya Wazanzibari wameanza kuogelea mumo kabla hata Shetani hajaenda msalani.

Bila shaka viyu kama hivyo (mafuta, gesi asilia, ardhi, misitu, rasilimali-bahari na kadhalika) vitakuja kutusumbua huko tuendako. Na tutakumbana na ile dhana ya mzandiki anayesema, “Chako chetu, changu changu.” Njia pekee ya kuondokana na uzandiki huo ni kuwa na mjadala mpana, wa wazi, na wa kituo.

CHANZO: RAIA MWEMA

Advertisements

8 responses to “Hata tuyazime, maswali yale yale kuhusu Muungano yanaturejea

 1. Jenarali

  Wewe hamia Unguja uwape somo kina RCs wanaofanya kujadili Muungano ni haramu. Napenda uliposema ni ujinga kujadili kitu usicho kitaka.

 2. huyo mwl nyerere keshatangualia mbele ya haki , atajuana na mola wake kwa makosa aliyofanya , muungano hautakiwi tena hapa na waznz na watanganyika halisi , kwa hio tunaomba mtuachie kwa amani kabla hamjasababisha mtafaruku na kumwaga damu. watu waliopo sasa sio wale wa miaka ishirini iliyopita mbumbumbu ambao wakiambiwa na nyerere walikuwa hewala akiwadanganya kwa kuvaa kofia za kiznz , MUUNGANO BASIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIII

 3. kwanini iwe kosa kujadili au kutamka kitu nisicho kitaka hee sasa ndio democrasia gani hii mimi ninachopenda kusema serekali ya tanzania bara au tanganyika inalo jambo limekusudia sio bure maana imekua kama kulazimishana kitu ambacho mtu hakitaki na kumlazimisha akitake
  wazanzibari sasa hivi washaamka na hawatalala tena wanacho dai ni kimoja tuu zanzibar yao bila ya muungano hili linajulikana wazi kabisa

 4. @ Jeneral Ulimwengu

  Moh’d Aboud na Balozi Ally Iddi mwalimu ndio huyu mfuateni akakusomesheni maana ya Uongozi na Democracy. Viziwi njaa.

  Hii ni aibu kubwa, kuwa wanaodhulumiwa ni Wazanzibari lakini viongozi wao ndio eti hawaoni bali kazi kusifu Muungano tuuu! Mpaka Watanganyika wasamaria wema sasa wanawatetea Wanzibari kama hivi, aah ama kwelii hii ni aibu tena aibu. Lakini SMZ Kazi kutisha watu kuhusu uvunjifu wa amani na utulivu. Sasa amani bila haki umeona wapi? Na je! Amani idumu katika hali kama hii halafu sisi tule mawe?

  Jenerali Ulimwengu endelea kumsaidia kazi iliyomshinda Waziri wa Muungano bila wizara maalum Dr. Ally Moh’d Shein.

  Huyu Waziri Dr. Shein ni yatima wa kisiasa hapa Zanzibar maana anauongozi lakini hana wafuasi-wapenzi ndani ya CCM wala CUF sasa anatapa tapa tu, hajui afanye nini, na yeye analijua hili hivyo yuko njia panda, ukweli ni kuwa akiwaunga mkono Wazanzibari kuikomboa Zanzibar atawakera Watanganyika waliompa rushwa ya Uongozi, na akiwaunga mkono Watanganyika yeye anaamini ataendelea kukaa Ikulu maana anajua iliyomuingiza Ikulu sio Kisiwa ndui bali ni Dodoma. Chadema chukueni nchi tuwaone mabichwa wapuuzi wasiojitambua.

  Lakini Waziri Dr. Shein sikiliza nguo ya kuazima haisitiri matako, fimbo ya mbali haiui nyoka, mcheza kwao hutunzwa na mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi.

  Usipobadilika utatukoma.

  MUUNGANO HATUUTAKI.

  JAMHUSI YA WATU WA ZANZIBAR KWANZA.

  “When peace fails apply force”

  Nawasilisha.

  SERELLY.

 5. sheni jitayarishe na safari ya kukimbiliya mafichoni kwani wazanzibar hawadanganyiki tena na upuuzi wenu wa uccm na ucuf

 6. Bora uwaelimishe hao mana sisi tushachoka viongozi mjifunze kupitia wananchi wenu yawekana wananchi wanajua zaidi ya nyinyi msijione mko kwenye viti mkajiona ndo nyie

 7. Kujadili Muungano na kuuliza maswali kuhusu nchi yako ni haki ya kila raia, akiwa bara au visiwani

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s