Bajeti ya pili SUK na changamoto mtawalia

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha,Uchumi na Mipango ya maendeleo),katika utekelezaji wa mpango wa kazi za Ofisi hiyo huko Ikulu Mjini Zanzibar

RAFIKI zangu, wakiwemo wasomaji wa safu hii wamenijia juu. Wananisema. Wanadai namsakama Dk. Ali Mohamed Shein bila ya kuangalia mazonge yanayomsibu. Mmoja anasema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ana hali ngumu. Kwamba kama ni mshambuliaji hodari katika timu ya mchezo wowote ule, inasihi kusema amebanwa kulia, kushoto, mbele, nyuma na katikati pia.
Kwa lugha rahisi kueleweka, wanasema Rais Dk. Shein hafurukuti. Wanataja mambo mawili kuwa ndiyo yanayomsumbua akili kwa sasa.
Kwanza, shinikizo kutoka kwa Baraza la Wawakilishi likitaka awatie adabu mawaziri na watendaji wa serikali ambao wameguswa na tuhuma za ufisadi.
Pili, wanasema Rais anasongwa na harakati za asasi za kiraia chini ya mwamvuli wa UAMSHO, zinazohamasisha wananchi kuukataa muungano. Shinikizo ni kubwa. Uamsho wamesambaza fomu maalum wanazohimiza Wazanzibari wazijaze kuibana serikali iitishe kura ya maoni itakayoamua wabaki nao au waondokane nao. Wakati hayo wanayaita mambo magumu kwa sasa kuyatafakari na kujua hatima yake, inajulikana bado Rais Dk. Shein hajatoa majibu ya matatizo kemkem yanayokabili serikali katika kutimiza ahadi zake kwa wananchi.
“Sasa huoni wewe haya ni mazonge makubwa kwa mheshimiwa rais wetu? Si ungemuacha atulie ili atafakari matatizo haya badala ya kumletea mara hili mara lile kila unapoandika?” Niliwaachia waseme nikijua wataishiwa na kusita. Zamu imefika kuwajibu. Waliposita nikavuta pumzi kujiweka sawa. Nikatabasamu. Nikaanza, “Kwa hivyo mnadhani mambo yamemzidi rais. Tumpe muda apumue siyo?”
Alas! Rais wetu ana nguvu nyingi, hajatumia hata robo yake. Angalieni staili yake. Anakaa wiki mbili-tatu Unguja, anapanga safari ya Pemba kufuatilia kampeni ya kulinda karafuu. Anazilinda hasa.
Si mnaona, akimaliza ziara ya Pemba, ikiwemo kuzindua matawi ya chama chao – CCM – anarudi makaoni Unguja na kusubiri vikao vya chama hicho Dar es Salaam au mji mkuu wa ndoto, Dodoma? Ngojeni niwaambie: Mheshimiwa Rais akimaliza vikao mwezi huu, ataruka pipia kwa ziara za nchi za nje. Mtamuona tu huyooooooo ametua labda Ulaya au Uarabuni.
Siku hiyohiyo mtaona picha zake akishikana mikono na kiongozi mwenyeji wake kule alikoenda. Mtaona anaangalia mradi unaoongeza ajira kwa wenzetu. Tena, lazima pembeni yake mtamkuta waziri mmoja au mawili wa serikali ya umoja wa kitaifa. Safari ile alitokeza labda Mohamed Aboud Mohamed, safari ijayo aweza kuwa waziri kutoka Chama cha Wananchi (CUF). Wanashuhudia maendeleo ya wenzetu huko.
Hebu fikirieni tangu alipoapishwa Novemba 2010 ametembelea nchi ngapi. Nashindwa kujua idadi kamili. Ni nyingi.
Uzuri kila aendako, angalau huambatana na mpigapicha wa picha za gazeti maarufu la Zanzibar Leo. Anatupigia picha za rais wetu mpendwa na tunaziona katika magazeti machache ya Dar es Salaam.
Mnaona rafiki zangu, akirudi atakutana na waandishi wawili-watatu pale uwanja wa kimataifa wa ndege wa AA Karume, pale Kisauni, na kujilazimisha kujibu maswali yao. Labda nyinyi hampati nafasi ya kuangalia stesheni yetu ya siku nyingi, TvZ, ambayo sasa imepewa jina zuri zaidi la ZBC – Zanzibar Broadcasting Corporation.
Kupitia stesheni hii, ndio utajua rais wetu mpendwa alipo; amefuatana na nani, utajua tu. Nikaendelea: akitoka Ughaibuni, rais atatulia kidogo Ikulu. Punde, ataitisha kikao cha mawaziri wake – Baraza la Mawaziri. Hapo utakuta picha ya gazeti na TvZ, nadhani wanataka lazima iitwe ZBC bila ya kujali viwango vya utangazaji, habari na vipindi vyake.
Utajua tu rais anafanya nini na wapi. Kati na kati, huchoki kubaini rais wetu mpendwa anakutana na wageni wanaomtembelea Ikulu ya Zanzibar, ileile inayogombaniwa kwa udi na uvumba ufikapo uchaguzi mkuu. Mara mtendaji wa taasisi fulani ya Umoja wa Mataifa au Ulaya; mara mtendaji wa taasisi kubwakubwa za mas’ala ya uchumi na jamii au balozi mwakilishi wa nchi ya kigeni. Kumbe, kwa kupokea wageni tu, si haba angalau watatu kwa mwezi huwapata.
Ninawathibitishia rafiki zangu rais wetu mpendwa alivyo na nguvu nyingi. Kila Rais Jakaya Kikwete anapofanya kikao cha mawaziri wake, rais wetu mpendwa hujongea karibu – mmesahau? Yeye ni mjumbe pale! Nasita, nisikilize kama wamebakisha lolote waseme. Wanasema kwa mpigo “Lakini wewe bwana bora ungepunguza kumkaba ili apate utulivu wa kufanya kazi. Mwenyewe si unazidi kuziorodhesha, ujue ni nyingi na zote zinamuwajibikia azitekeleze.
Naona nguvu za rafiki zangu kumlinda rais asiandikwe zimepooza. Kama nimewazidi vile. Basi naanza polepole kubabua: Mnajua, haya mambo mengine rais anajiingiza tu hayamjengei mlahaka mzuri na wananchi. Ni bora hata angeamua kushinda mashambani wakati wao wakilima, wakifuga au kuangalia wakirudi kuvua, ingekuwa na maana.
Au angebaki kwenye mashamba ya mpunga Cheju, Mtwango, Bumbwini Makoba kule; angekagua mashamba ya kuotesha majani ya malisho ya mifugo, ingekuwa na maana. Si tunataka kuongeza uzalishaji wa maziwa ili kufikia kila mtu kunywa angalau lita 150 kwa mwaka? Basi rais akikagua mashamba ya kuzalisha ndama bora wa maziwa au vituo vituo vya vetenari, ingemsaidia.
Pia, rais angekuwa kila baada ya wiki tatu anafika katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazimmoja kukagua wagonjwa na kuangalia mazingira ambamo madaktari, wauguzi, wakunga na wafanyakazi wa kada nyingine za afya, ingemletea tija. Rais anayebaki nchini akajishughulisha na shughuli wanazofanya wananchi, anajijenga. Kwa namna nyingine, inamkurubisha sana na watu wa kawaida.
Basi atapendwa hata kama utendaji serikalini si mzuri hivyo. Ni foramu kama hizi humpatia kiongozi hupata hili na lile yanayopita serikalini.
Hii pitapita yake kila pembe ya nchi, itamuondolea msongo wa mawazo, na itamzidishia kujiamini mbele ya vyombo vya habari ambavyo hajavitambua vilivyo. Na ni bahati mbaya maana alipozindua Baraza la Wawakilishi Novemba 2010, aliahidi kukutana na waandishi kila baada ya miezi mitatu ili kuwaeleza shughuli za serikali zinavyokwenda.
Mmeona leo, amekutana mara moja tu nao. Wana mengi ya kumuuliza maana mawaziri aliowaagiza wawe na vikao vya aina hii mara kwa mara, wamembeza. Usimamizi mzuri wa shughuli za serikali ungemsaidia kufanya maamuzi magumu kwa wakati muafaka kunapotokea jambo la ziada kama haya mawili – shinikizo za kuadabisha mawaziri na watendaji waovu na harakati za Uamsho.
Kwa sababu muda mwingi anazunguka nje na kwenye vikao vya chama, anakosa muda wa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
Matokeo yake, wananchi wanazidi kulalamikia gharama za maisha: chakula, umeme usafiri bei zinaruka. Kwenye chakula, vingi vinavyoingizwa kutoka nje, ukiwemo mchele, chakula kikuu kwa Zanzibar, ni vibovu.
Mdudu ufisadi serikalini anazidi kustawi na watendaji wanazidi ulafi; huku mazingira yakizidi kuchafuliwa na wakata misitu na wachimba mchanga kwenye fukwe na mabondeni. Labda bajeti yake ya pili itayosomwa mwezi ujao, itayajibu haya.

4 responses to “Bajeti ya pili SUK na changamoto mtawalia

  1. Sisi tuko imara kura ya maoni kwanza mambo mengine baadae. Viongozi mukinuna mukitaka musitake sisi muungano hatuutaki. Tumechoka kupangiwa viongozi Dodoma

  2. HAYA NDIO MATATIZO YA VIONGOZI WASIOCHAGULIWA KWA KURA ZA WANANCHI. KIONGOZI ALIECHAGULIWA NA WANANCHI HUWAJALI NA KUWASIKILIZA WANANCHI WAKE NA KUTENDA VILE WANAVYOTAKA WAO. DR SHENI NI RAISI WA WAZANZIBARI NA WAZANZIBARI WAMEMTUMA KUWAAMBIA TANGANYIKA KUA MUUNGANO HAWAUTAKI ANASHINDWA KUWASEMEA NA BAYA ZAIDI ANAWAKARIPIA KWA KUWAMBIA ASIETAKA AHAME. ALA INA MAANA WAZANZIBARI SOTE TUHAME MAANA SOTE HATUUTAKI MUUNGANO? TWENDE WAPI NA HAPA NDIO KWETU? NADHANI WA KUHAMA NI YEYE KWA KUA AMESHINDWA KUTUTUMIKIA AHAME NA AENDE KWA HAO ANAOWATUMIKIA.

  3. na si wazanzibari wote wasiotaka muungano kama alivosema msemaji hapo juu wapo wanaoutaka uwepo japo kwa masharti usiwasemee wazanzibari wote kama hawautaki

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s