Wasanii waaswa kutopotosha jamii

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja ya wasanii wa filamu ya Touba na badhi ya wasanii maarufu wa filamu Tanzania, katika uzinduzi wa filamu hiyo uliofanyika hoteli ya Bwawani Zanzibar jana usiku tarehe 18/05/2012.

Mabadiliko ya Kiulimwengu ambayo yaligusa kila pembe ya kimaisha kuanzia miaka ya 1980s, yalileta Mapinduzi makubwa katika nyanja hii ya mawasiliano na sanaa kwa ujumla. Tumeshuhudia faida zake, lakini pia na madhara makubwa. Kati ya madhara makubwa kubwa zaidi ni kuporomoa kwa mila na tamaduni za nchi kama hizi zetu. Maendeleo hayo yalituathiri zaidi nchi masikini kwa sababu tumekuwa ni wapokeaji tu wa mambo tunayotayarishiwa na mataifa yenye nguvu. Watu wetu hasa vijana wamekuwa wakikumbatia tamaduni na mila za kigeni na hasa za nchi za Kimagharibi. Mabadiliko hayo ambayo yamepewa jina la Utandawazi yamesabisha utaratibu wa mawasilinao kuwa tafauti na ule wa zamani. Vituo vya Senema tulivyotangulia kuvitaja hapo awali ni kwa nadra sana sasa kuviona. Kwa mfano Zanzibar vituo hivyo vingi hivi sasa vimegeuzwa ‘Super Markets’ ofisi na zimekuwa sehemu za biashara, lakini hazioneshi tena filamu. Filamu zilizokuwa zikioneshwa kwenye televisheni hivi sasa zinauzwa mikononi kama njugu kupitia CD na DVDs, huku kukiwa na urahisi mkubwa kwa mtu kuangalia picha anazotaka, hata kupitia simu yake ya mkononi au kompyuta.

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA HAFLA YA UZINDUZI WA FILAMU YA TOUBA TAREHE 18 MEI, 2012 UKUMBI WA SALAMA HOTELI YA BWAWANI MJINI ZANZIBAR

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi
Waheshimiwa Mabalozi
Waheshimiwa Watendaji wa Serikali
Waheshimiwa Viongozi wa Dini
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa
Waheshimiwa Wafanyabiashara
Waheshimiwa Wasanii mbali mbali
Waheshimiwa Waalikwa nyote Mabibi na Bwana
Assalam Alaykum
Awali ya yote sina dudi kuchukua fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwenye wingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na wenye afya njema, na kutuwezesha kufika hapa leo hii kujumuika kwa pamoja katika hafla muhimu ambayo malengo yake makuu ni kudumisha na kuendeleza mila, silka na desturi njema za Wazanzibari kupitia fani ya sanaa.
Vile vile, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa uongozi wa Kampuni ya CY & CL kwa kubuni wazo hili zuri la kutumia ujuzi na utaalamu wao katika nyanja ya sanaa ya filamu, kudumisha na kulinda hadhi na heshima ya Utamaduni wa Wazanzibari. Aidha, sina budi tena kukushukuruni Kampuni ya CY & CL kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuja kujumuika nanyi pamoja na wote mulioalikwa, katika hafla hii muhimu.
Tukio hili la uzinduzi wa filamu ni la kisanaa zaidi, na najua katika jamii yetu kuna Magwiji waliobobea katika ulingo huu. Bila shaka yoyote mungeweza kuwapa hadhi ya kuwa wageni rasmi hapa. Lakini hao wote mmewaacha na kuamua kunialika mimi kuja kujumuika nanyi. Nasema kwangu mimi binafsi heshima mliyonipa ni kubwa na nina inathimini sana. Ahsanteni.
Waheshimiwa viongozi na Waalikwa wenzangu
Sanaa yoyote ile iwayo ni kielelezo muhimu cha utamaduni wa watu na jamii maalum, kwa maana hiyo sanaa haina budi kulindwa, kuenziwa na kuendelezwa, lakini vile vile jamii inayohusika ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha sanaa hiyo ndiyo halisi, na wala haiharibiwi na kusababisha utamaduni, silka na mila zao kupotoshwa.
Kwa maoni yangu sanaa inayowasilishwa kwa njia ya filamu ina umuhimu wa kipekee. Sababu ya kusema hivyo ni kwamba sanaa hiyo huhusisha matumizi ya moja kwa moja ya vyombo vya habari, ambavyo nafasi yake katika jamii ni kubwa sana. Vyombo vya habari kama televisheni na intanet, ambapo sanaa hii ya filamu hupitishiwa kwa ajili ya kuwasilishwa kwa hadhira kwa urahisi zaidi vina nguvu kubwa ya kuibadilisha jamii.
Mabadiliko hayo yanaweza kuwa ni kwa faida ya jamii yenyewe au kwa kuisababishia madhara au hata maafa makubwa, ikiwemo hayo ya kupoteza uasili, hadhi na heshima ya jamii yenyewe.
Nyanjaya Filamu Zanzibar, kama ilivyo katika fani nyingi ni kongwe na tunaelezwa kuwa nchi yetu Zanzibar ni ya kwanza kuwa na Senema katika eneo la Afrika Mshariki mnamo miaka ya 1920s. Katika miaka hiyo Bwana John Sinclair alijenga Majestic Cinema, eneo ambalo sasa kuna chuo kikuu cha Taifa SUZA, Sinema ambayo kwa muda mrefu ilitoa mchango mkubwa wa kuonyesha filamu zenye ujumbe na maudhui tafauti, ambazo zilipendwa kwa mujibu wa wakati huo.
Mbali na Majestic Cinema vituo vyengine vya kuoneshea filamu vilifunguliwa baadaye, kati ya hivyo wengi mnavikumbuka ni Empire Cinema na Cine Afrique, ukiachilia mbali sinema ambazo zilianzishwa na kuendelea kudumu kwa muda mrefu zaidi katika miji ya Wete na Chacke Chake kwa upande wa Pemba.
Kuwepo kwa historia kubwa na ya kipekee katika nyanja hii ya filamu na kwa kuzingatia Zanzibar ni kati ya nchi za mwanzo kuwa na televisheni ya rangi Barani Afrika, ni dhahiri jamii ya Wazanzibari inauelewa mpana na uzoefu mkubwa wa kupata burudani, lakini pia kupokea elimu pamoja na ujumbe unaowasilishwa kwa njia hii.

Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa wenzangu
Mabadiliko ya Kiulimwengu ambayo yaligusa kila pembe ya kimaisha kuanzia miaka ya 1980s, yalileta Mapinduzi makubwa katika nyanja hii ya mawasiliano na sanaa kwa ujumla.
Tumeshuhudia faida zake, lakini pia na madhara makubwa. Kati ya madhara makubwa kubwa zaidi ni kuporomoa kwa mila na tamaduni za nchi kama hizi zetu. Maendeleo hayo yalituathiri zaidi nchi masikini kwa sababu tumekuwa ni wapokeaji tu wa mambo tunayotayarishiwa na mataifa yenye nguvu. Watu wetu hasa vijana wamekuwa wakikumbatia tamaduni na mila za kigeni na hasa za nchi za Kimagharibi.
Mabadiliko hayo ambayo yamepewa jina la Utandawazi yamesabisha utaratibu wa mawasilinao kuwa tafauti na ule wa zamani. Vituo vya Senema tulivyotangulia kuvitaja hapo awali ni kwa nadra sana sasa kuviona. Kwa mfano Zanzibar vituo hivyo vingi hivi sasa vimegeuzwa ‘Super Markets’ ofisi na zimekuwa sehemu za biashara, lakini hazioneshi tena filamu.
Filamu zilizokuwa zikioneshwa kwenye televisheni hivi sasa zinauzwa mikononi kama njugu kupitia CD na DVDs, huku kukiwa na urahisi mkubwa kwa mtu kuangalia picha anazotaka, hata kupitia simu yake ya mkononi au kompyuta.
Hali hiyo kwa upande mwengine imeleta athari kubwa sana katika jamii zetu. Utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2000, ulionesha watoto wadogo walio katika umri wa kwenda skuli ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa njia hizi za kisasa za mawasiliano.
Katika baadhi ya nchi zilizohusika na utafiti huo zipatazo 23, ilibainika watoto hao katika maeneo ya mijini asilimia 93, hutumia zaidi ya asilimia 50 ya muda wao kuangalia filamu, kama njia zao za burudani. Suala muhimu la kujiuliza hapa ni je watoto hao wanaagalia filamu kama hii ya Touba, au wanaangalia filamu za aina gani?
Athari na matokeo ya mambo hayo kwa jamii ni kuongezeka kwa vitendo vya kuiga vivazi visivyo kuwa vya heshima, kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wanawake na watoto, vijana kujiingiza katika vitendo vya ujambazi na wizi wa kutumia nguvu, kwa sababu ya kuiga yale wanayoyaona kwenye filamu hizo.
Hapa Zanzibar pia athari hizo zinajitokeza na filamu nyingi zinazoangaliwa ni za kigeni. Katika filamu hizo hatuna uhakika na kile kilichomo na mafundisho yanayopatikana ndani yake. Miongoni mwa filamu zinazoangaliwa zaidi ni zile zinazoitwa ‘Bongo Movies’, yaani zinazotoka Tanzania Bara, ambazo ukifuatilia nyingi kati ya hizo zimetawaliwa na mapenzi, udhalilishwaji wanawake, ikiwemo kimavazi na hata baadhi ya wakati filamu hizo kuhamasisha uhalifu.
Kwa maana hiyo napenda kuishauri jamii pamoja na Serikali yetu tuwe na mikakati ya makusudi ya kuandaa na kuhamasisha matumizi ya filamu na sanaa za aina zote zinazozingatia mila, silka na utamaduni wetu Wazanzibari.
Hapa naomba niwakumbushe kuwa hapa Zanzibar tumewahi kuwa na michezo mizuri yenye mafunzo na pia kulinda utamaduni, mila na silka za Mzanzibari. Wengi mnakumbuka mchezo wa Dk. Ayoub ulioandaliwa, kuongozwa na kuchezwa na Wasanii Wazanzibari. Mchezo huo ulichukuliwa TVZ na ukawa unaoneshwa na TVZ ambayo sasa ni Shirika la Utangazaji Zanzibar. Siku za kuoneshwa mchezo huo karibu kila mtu alikuwa kwenye TV yake. Hivyo uwezo upo na sababu tunazo. Sasa tutie nia.
Katika kufikia lengo hilo hatuna budi kuwaunga mkono wale wote wanaoamua kuanzisha kampuni au vikundi vya kutengeneza filamu kama hii ya CY &CL ambazo zitauokoa utamaduni, silka na mila adhimu za Wazanzibari, utamaduni ambao hivi sasa umeanza kuvamiwa na kuharibiwa.
Lakini vile vile katika nyanja hii ya filamu au sanaa kuna fursa nyingi za ajira kwa vijana wetu. Katika kuandaa filamu wanahitajika vijana waliofunzwa kuchukua picha, wahariri, waigizaji na wasimamizi wa programu zenyewe. Bila shaka tukiwa na kampuni nyingi za aina hiyo tutakuwa tumepiga ndege wengi kwa jiwe moja. Kwa sababu tutakuwa tunalinda hadhi na heshima zetu, lakini pia kuwasaidia vijana na wananchi wetu kupunguza ukali wa maisha.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaelewa athari na hatari iliyopo ya kupotea mila na desturi nzuri za Wazanzibari. Inajua kuwa iwapo hakutakuwa na juhudi za makusudi kukabiliana na kitisho hicho utambulisho wa Wazanzibari upo hatarini. Na ndio maana Sera pamoja na Mipango madhubuti imewekwa na itaendelea kuwekwa na kutekelezwa kudhibiti athari za jambo hilo.
Mimi mwenyewe binafsi nimekuwa nikisisitiza sana jambo la kulindwa Utamaduni wetu. Nakumbuka ni wiki chache tu ziliopita nilipata bahati ya kufanya ziara katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, ambayo kwa hakika tumeibebesha jukumu zito la kusimamia na kuhakikisha utamaduni wa Mzanzibari unaendelezwa, badala ya kuteketezwa.
Nilipokutana na watendaji wa vyombo vya habari niliwakumbusha kwamba vyombo hivyo hasa televisheni havipaswi kuwa chanzo cha kuharibu au kupotosha utamaduni, bali visaidie kuulinda. Na hili lizingatiwe na vyombo vya habari vyote, viwe vya serikali au vya makampuni na watu binafsi.
Kwa upande wa Kamisheni ya Utamaduni na Michezo, mambo muhimu niliyoyasisitiza na napenda kuyakumbusha tena hapa leo kwa sababu yanatugusa sote ni;
Tujiandae kukabiliana na changamoto za Utandawazi ili kulinda Utamaduni wa Wazanzibari.
Tuwe na mikakati ya kuendeleza mafunzo ya sanaa kwa vijana ili kukuza ajira na kuimarisha utamaduni wetu hasa kwa watalii.
Katika hili nasisitiza sana tujikite zaidi na kutengeneza sanaa zenye asili ya Kizanzibari, ili wageni na watafiti wanaokuja wasipotoshwe juu ya sanaa zetu.
Tuwe na mkakati wa kudhibiti filamu ambazo hazilingani na maadili ya watu wa Zanzibar.
Baada ya kusema hayo naona nisiwachoshe. Naamini sote kila mmoja wetu akiazimia kuuhifadhi na kuulinda Utamaduni wetu, Wazanzibari heshima yetu itaendelea kuwepo na itadumu kwa vizazi vilivyopo na vile vitakavyokuja.
Nawashukuru nyote kwa utulivu mkubwa na kunisilikiza kwa makini kabisa katika muda wote nipokuwa nikizungumza.

Ahsanteni.

Advertisements

5 responses to “Wasanii waaswa kutopotosha jamii

  1. Sadakta haya maneno ni mazima sana. Bongo film zinavuruga utamaduni wa Mtanzania kwani nyingi kati yao zinakosa maadili na kwa kua hakuna usimamizi tunashuhudia filamu ambazo zinapelekea kuiga tamaduni nyengine. Wazee akina Mashaka na wenzake filamu zao zilikua zinaendana na maadili ya Mzanzibari kuna haja ya kuzifufua na ikiwezekana kuwekwa kwenye CDs. TVZ nayo lazima iji controll na vipindi na filamu zisizo na maadili. Inaonekana kama TVZ sasa ni kituo cha Wahuni tu kikijionyeshea filamu ambazo hata hazina maadili. Lazima kue na udhibiti. Wakati mwengine hata hao watangazaji wa TVZwanavyoonekana na mavazi yao kwa kweli wanatoa picha mbaya sana kwa Zanzibar.

  2. tusipotoshane hapa, suala muhimu ni kuvunja muungano , hailekei kwa nd hamadi kujishighulisha na masuala yasio muhimu katika muda huu

    • Hili ni muhimu pia,kwani ukiwa huna khulka za asili yako ushakua mtumwa uliyebeba utamaduni wa watu .

  3. Haya ndio anayotaweza Maalim Seif.
    Tuache sisi tugombanie Zanzibar yetu kutoka kwa masahibu wako wa Tanganyika.
    Kwa mtaji huu watanganyika hawatuachii ng’o

  4. Uchunguzi na ufatiliaji wa bongo movies lazima uwe mkubwa, nyingi ya filamu zake hazistahiki kuangaliwa na vijana waliochini ya miaka 18, Pia wazee wanahaki kubwa yaidi ya kuliangalia hili.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s