Kwa Muungano huu mabadiliko ni lazima

Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu maoni juu ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba(kulia) akizungumza na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wakati Rais alipomtembelea ofisi kwake jana.Wengine katika picha ni Makamu mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mkuu Mstaafu Mhe. Agostino Ramadhani(Watatu kushoto),Waziri wa Katiba na SheriaMhe. Mathias Chikawe(Wapili kushoto) na kushoto ni naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Angela Kairuki.

Wakati tukielekea katika mchakato muhimu wa kutoa maoni yetu juu ya uundwaji wa Katiba mpya ya Tanzania, ni wazi kuwa jambo litalokuwa na mjadala mkubwa , hasa kwa upande wa Zanzibar , ni suala la Muungano. Hii ni kutokana na sababu kuu tatu.

Kwanza , kwa vile Wazanzibari kama ilivyo kwa Watanzania Bara, hawajahi kupata fursa ya kuutolea maoni na ridhaa Muungano huu kwa ujumla wake, muundo wake na uendeshaji wake – na kwa vile umedumu hivyo ukielekea kutimiza nusu karne, hii ni fursa muhimu ya kuufanyia tathmini yakinifu kwa kuzingatia wakati mpya tulionao , mahitaji tuliyonayo na mazingira ya kisiasa na kiuchumi yanayotuzunguka wakati huu.

Pili ni kutokana na ukweli kuwa Wazanzibari , kwa mujibu wa muundo wa Muungano huu wao wana mfumo wao kamili unaoongoza mambo yao yote yasio ya Muungano – wana Katiba yao, Serikali yao , Mahkama zao, Bunge lao (Baraza la Wawakilishi),

Vikosi vyao vya Ulinzi, Serikali zao za Mitaa nk – hivyo kwa upande wa Zanzibar mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwao utajikita zaidi kwenye suala la Muungano tu, nje ya Muungano wao wana yao, na nje ya Muungano yanayobaki katika Katiba hiyo ni ya Tanzania Bara tu.

Tatu ni kutokana na ukweli kuwa Wazanzibari walio wengi wanaamini kuwa Muungano katika muundo wake huu umejengeka katika udhaifu wa kimaumbile na hivyo umepelekea kudumaza maendeleo na mustakbali wa Zanzibar katika nyanja takriban zote- malalamiko yao ni mengi mno.

Watakwambia Zanzibar imepoteza hadhi yake, Raisi wake aliyepokelewa kwa heshima kubwa Umoja wa Mataifa na kuwa na kiti chake sambamba na mataifa yote ya ulimwengu huu kabla ya Muungano ,na wakati wa Muungano akathaminiwa kwa kufanywa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano , leo kafanywa Waziri asie na hadhi yoyote ndani ya Baraza la Mawaziri la Tanzania.

Watakwambia Zanzibar haina hadhi ya kujiunga hata na Taasisi tu za Kimataifa na hapa watakukumbusha mkasa wa OIC, jumuiya ya Kiislamu yenye kujikita katika kutoa misaada ya kiuchumi na kijamii na iliyo na wanachama nchi ambazo idadi ya waislamu nchini humo ni chini ya asilimia kumi kama Uganda na Msumbiji. Zanzibar ina waislamu zaidi ya asilimia 97 hivyo haiwezi kuwa na haja ya kujiunga na taasisi za kiislamu kwa kutangaza uislamu bali ni suala la maslahi ya kiuchumi na si suala la udini. Lakini kama ni udini watakuuliza mbona Vatican ina Ubalozi Tanzania? 

Watakwambia juhudi za wanamichezo wa Zanzibar pamoja na msaada wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili waweze kujiunga na FIFA na hivyo kunufaika na maslahi ya Shirikisho hilo zilivyoshindikana , kisa muundo wa Muungano!

Watakwambia wanavyotozwa kodi mara mbili na Taasisi hiyo hiyo kwa bidhaa hizo hizo pale wanapopeleka bidhaa hizo Tanzania Bara. Watakwambia kuwa ukweli ni kuwa mfumo wa Muungano ndio umeifanya Zanzibar leo kuwa tegemezi kwa soko la Bara vinginevyo kama ingekuwa na uhuru wa kimaamuzi katika mambo ya kodi na sera za kifedha Zanzibar ingeweza kuwa kituo kikuu cha kibiashara na kamwe wasingefungika na soko finyu la Tanzania Bara tu. Watakusimulia kuwa hata hivi punde miaka ya karibuni ilipotokea msukosuko wa kiuchumi duniani na Benki Kuu ya Tanzania kutoa fedha kuokoa uchumi usiporomoke , Zanzibar haikuambulia kitu ingawaje hio ni Benki ambayo mbali na kuwa ni ya Muungano lakini katika kuanzishwa kwake Zanzibar ilitoa mtaji wa asilimia 11.

Watakwambia benki hiyo huwa mstari wa mbele kiuwezeshaji kilimo kwa kunyanyua mazao ya korosho, pamba nk lakini haifanyi hivyo kwa karafuu.

Watakusimulia mengi juu ya kero katika usimamizi wa uchumi na rasilimali, masuala ya kodi na fedha , misaada kutoka nje, mapato na matumizi yanayohusiana na Serikali ya Muungano, na mengi mengineyo. Kwa ufupi watakupa msururu wa KERO mpaka utajisikia KERO.


Hivyo kwa vigezo kadhaa wa kadhaa mjadala juu ya Muungano ndilo kiini cha mjadala wa Katiba kwa upande wa Zanzibar ; na kwa msingi huu hapana budi Wazanzibari waitumie fursa hii kwa ujasiri mkubwa , umakini na zaidi ya yote kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na sio maslahi binafsi , ya makundi au kivyama.

Ni wazi wapo wataosukuma ajenda zao katika mjadala huu kwa maslahi yao binafsi hasa ya kisiasa hata kuweza kupotosha mambo , waiangamize nchi na hata itoweke kabisa ili wao wafaidike na maslahi yao binafsi tena ya muda mfupi bila kujali mustakbali wa vizazi vijavyo.


Majuzi nilisikitishwa na maoni ya Bw. Ali Karume niliyoyasikia yakirushwa na Kituo kimoja cha TV hapa nchini na pia maoni yake katika baadhi ya mitandao ya Kijamii.

Kilichonisikitisha si maoni yake kwani hio ni haki yake kama walivyo raia wengine wote wa nchi hii bali ni ule upotoshaji uliomo katika maoni hayo.

Alipojilabu kuwa anaongea kwa uhakika kwa vile yeye ameishi sana Marekani na Ulaya akiwa mtumishi wa Tanzania katika nafasi za ubalozi na hata kuwa balozi mwanzo niliona ni hulka ya kawaida ya baadhi yetu lakini mwisho wa maelezo yake nikagundua kuwa ule ulikuwa ni mkakati mahsusi wa kuhalalisha lile atalolizungumza ili lionekane limetoka kwa mtu muelewa na mzoefu wa analolizungumzia; bila shaka akielewa kuwa bila mkakati huo watu wangemstaajabia.

Alitetea mno haja ya kuendelea na Muungano huu , bila shaka kama ulivyo, kwa vile Muungano ndio silaha ya maendeleo na akatolea mfano mataifa makubwa ya Marekani na Ulaya kuwa yanatamba duniani kwa sababu yameungana.

Hivi tujiulize ni kweli mataifa haya yameendelea kwa sababu ya Muungano tu? Amesahau kuwa mataifa ya Ulaya na Marekani yana historia refu ya kiuchumi duniani tokea enzi za biashara ya utumwa na ukoloni, yana rasilimali kedekede, yameweza kusimamia ipasavyo chumi zao, yamekuwa na ubunifu wa hali ya juu katika kila fani ya kimaisha, yameweza kunufaika hata na chumi za nchi nyengine kwa mifumo ya kifedha na kibiashara ya kinyonyaji ya kiulimwengu waliyoitandaza , amesahau uwezo wao mkubwa wa sayansi na teknolojia , amesahau ubabe wao wa kijeshi wanaoutumia kwa lengo la maslahi ya kiuchumi , amesahau walivyowekeza katika elimu ya mataifa yao na jinsi walivyoendesha nchi zao kwa misingi ya kidemokrasi .

Ametaka kutuaminisha kuwa muarobaini wa matatizo yao na muujiza wa maendeleo yao ni Muungano wao. Haya ni mawazo mpumbazo yasiyo na mashiko ya kiuchambuzi wala ukweli wowote wa kitalaam, ni muendelezo wa porojo za kisiasa za wasaka madaraka na wanaolinda mfumo ( status quo) kwa maslahi yao binafsi kwa vile ni wanufaika wa mfumo huu.

Kwa wasaka madaraka tatizo kubwa kwao katika Muungano huu watakwambia kuwe na kupokezana Urais ili mara ijayo iwe ni zamu ya Mzanzibari ili ndoto zao zitimie lakini hawawezi kuwa na msaada wowote wa kiuchambuzi yakinifu ambao utaleta maslahi kwa wananchi .

Lakini hata tukikubaliana kuwa muarobaini wa matatizo yao ni huo Muungano wao tujiulize jee muungano wao unafanana kimuundo au kwa namna yoyote na huu wetu? Wanasheria mahiri wote wanakubaliana kuwa hakuna muungano wowote duniani wenye muundo kama huu na huishia kuuita muungano wa kipekee.

Kwa kawaida Muungano hutegemewa uongeze nguvu kwa walioungana na sio kupototoa nguvu zote za upande mmoja na upande huo ukabaki bufuru tupu ( kwa maneno ya Professor Shivji). Katika muundo huu Zanzibar imepoteza nguvu, uwezo na madaraka yake yote kama nchi na yametumbukizwa katika himaya ya Tanganyika lakini Tanganyika ilipoteza jina tu lakini nguvu , uwezo na mamlaka viliongezeka.

Lakini kuufananisha muungano wa Zanzibar na Tanganyika na ule wa Jumuiya ya Ulaya au ule wa Marekani ni kufananisha tembo na chura. Sawa wote ni wanyama. Lakini fanya uchambuzi wa hali zao uone tofauti zao!


Zaidi ya yote , tukubaliane tena na Mheshimiwa wetu kuwa muungano ndio silaha ya maendeleo . Ni kwa nini basi sisi tuko hali hii wakati tuna silaha hii kwa takriban miaka 50 sasa . Tatizo letu na nini na kwa nini alishindwa kulitaja ?

Awe mkweli atupe uchambuzi Zanzibar ilivyokuwa kabla ya muungano ndipo ilipo leo ukitilia maanani kipindi cha muungano huu kuwa ni cha takriban miaka 50 sasa . Tuichukue Zanzibar ilivyokuwa katika nyanja zote- kiuchumi , kielimu , kibiashara nk halafu pima kiwango cha maendeleo ( PACE OF DEVELOPMENT GROWTH) kwa mwaka kilivyokuwa halafu zidisha kwa miaka 50 halafu utapata jibu na utaamua kama kweli Muungano umeiendeleza au umeidumaza Zanzibar.

Kama huo ni uchambuzi wa shida waulize wazee watakwambia ilivyokuwa nadra na aibu kwa Mzanzibari kuomba, leo iangalie hali ya umaskini ilivyoshamiri.


Tumedumu kuwa watumwa wa siasa porojo zenye lengo la kulinda maslahi binafsi na sio siasa yakinifu za manufaa zenye kulinda maslahi mapana ya jamii yote. Kama hoja ni maendeleo basi muungano unapokuwa kikwazo cha maendeleo tukiondoe na tuweke mfumo ambao utatuwezesha kufikia hayo maendeleo , tuache siasa ng’an’ganizi za mwaka 47.


Kama Muungano ndio suluhisho la kufikia maendeleo mbona ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Rwanda pekee ambayo inaaminiwa kuonesha miujiza katika maendeleo , wengine ni kusuasua tu, ingawaje Rwanda haina rasilimali zozote za maana na ni miaka 15 tu sasa tokea waanze kurudi tena kwenye mfumo wa kiuendeshaji ( GOVERNANCE) tokea watoke katika mauaji mabaya ya kimbari katika historia ya binaabamu.


Nilitegemea Mheshimiwa angetumia mfano wa Singapore na Malaysia ambao unafanana takriban kwa kila namna na hali ya Muungano wetu. Pengine hakuuona kwa vile hajafanya kazi huko katika utumishi wake wa kibalozi au haumpendezi kwa kusukuma mbele ajenda yake iliyotaabanika . Singapore ikiwa ni kisiwa kidogo kama Zanzibar iliungana na Malaysia September 1963 wakiamini Muungano huo ungeleta neema na maslahi makubwa kwao kwa vile walikuwa katika hali ngumu ajabu ya kiuchumi.

Hata hivyo baada ya kugundua tofauti kadhaa za kimsingi za kiutawala na kisera na kuona uchu wa Malaysia wa kuifanya Singapore mkoa mwengine wa Malaysia kama mkoa wa Malacca na Penang , Muungano wao ulidumu miaka miwili tu na Singapore ikajitoa katika Muungano huo.

Wakati huo Singapore ilikuwa katika dimbwi la ufukara usioweza kufananishika na vigezo vya umaskini vya ulimwengu wa tatu katika kipindi chochote cha historia ya sasa (modern history) Ilikuwa na kila aina ya changamoto utazozifikiria kuanzia ukame , miundombinu,huduma za jamii, ulinzi na usalama,uchumi,jamii mchanganyiko (multilingual,multicultural,multi-religious) n.k.

Hutoamini kusikia kuwa wakati wanajitoa katika muungano hata nyumba ya Waziri Mkuu wao ilibidi igongelewe mabati katika madirisha yake ili iwe ndio hifadhj ya kiulinzi. Walikuwa hoi bin taabani hata upatikanaji wa maji ilikuwa ni dhiki ajabu.

Kwa kiwango cha muda mfupi kwa umri wa taifa, Singapore ,ikiwa nje ya Muungano, ilipiga hatua za ajabu katika maendeleo katika kila sekta mpaka ikatinga katika kundi la ulimwengu wa kwanza ( First World) tena ulimwengu wa kwanza kwa kuwapita wengi (First World by far) Ilitumia vyema maumbile yake ya ukisiwa kilicho karibu na mabara na hivyo kujipanga vyema kunufaika na hilo na wakatumia vyema majaaliwa ya watu wake waliojaaliwa vipaji vya ubunifu na biashara, uchapakazi, uaminifu na uzalendo.


Hivyo basi kama muungano umewapeleka wengine kwenye maendeleo, utengano pia emewapeleka wengine kwenye maendeleo.

Hoja ni kuwa tusidanganyane kuwa muungano ndio msingi wa maendeleo. Misingi ya maendeleo ni mambo mengine kabisa ; ingawaje muungano unapojengwa kwa nia safi , kwa muundo wa usawa, unaojali maslahi ya pande zote, unaotoa fursa ya kujirekebisha, unaozidisha nguvu za pande zote zinazohusika na sio kudhoofishana basi huweza kuwa na msaada katika kusukuma mbele maendeleo na ustawi wa jamii husika.

Upande wowote katika muungano unapoona unadhoofika kwa kisingizio cha muungano hauna budi kujiangalia upya juu ya umuhimu na haja ya kuendelea na muungano huo.


Hili linakuwa na uzito hasa inapotokezea yalioungana ni mataifa yasio sawa kwa kila hali.Inapotokezea nchi kubwa yenye idadi kubwa sana ya watu ikaungana na nchi ndogo , tena kisiwa, ikiwa na idadi ndogo ya watu ni lazima mazingira maalum yaandaliwe ambayo yatahakikisha kutunza ustawi wa upande uliokuwa ‘dhaifu’ Na hii sio kwa miungano tu. Hata nchi moja inapokuwa na maeneo yenye mahitaji maalum ya kutunzwa ( hasa visiwa- kutokana na udogo wake) nchi hizo huweka sera na sheria maalum zitazotoa hifadhi kwa maeneo hayo.

Kwa mfano Hong Kong na Macau ni visiwa vya China; huko miaka ya nyuma Hong Kong illikodishwa kwa Uingereza kwa muda wa miaka 100 na Macau ilikodishwa kwa Ureno kwa muda wa miaka 100. Inasemekana China ilifanya hivyo kwa maslahi yake ya kuweza kuzifikia na kugida chumi za kibepari kupitia maeneo hayo. Baada ya kumalizika mikataba ya ukodishwaji visiwa hivi vimerudi kwao kama zamani.

Sasa angalia sera na sheria za China zilivyosukwa ili kuweka mustakbali mwema na endelevu kwa visiwa hivi. Pamoja na kuwa China ni moja , mchina kutoka bara haingii kiholela Hong Kong au Macau bila udhibiti na utaratibu maalum, vivyo hivyo kwa ajira, umiliki wa ardhi, uendeshaji biashara na mengineyo.

China hivyo ni visiwa vyake ila imeweka mikakati maalum ya kuvienzi, kuvihifadhi na kuviendeleza. Kwa upande wa Tanzania, huu ni Muungano tu , sasa tujiulize ipo mikakati iliyowekwa ambayo inalenga kuihifadhi, kuitunza na kuiendeleza Zanzibar. Kila hatua ya kuihifadhi Zanzibar inakuwa nongwa kwa upande wa Bara.

Suala la uingiaji Zanzibar kwa utaratibu unaoeleweka lililokuwepo kabla ya Muungano na hata baada ya Muungano kwa muda mrefu lilifanywa nongwa la kisiasa mpaka likaondolewa .

Leo hii Zanzibar ni nchi pekee duniani isiyoweza kudhibiti uingiaji wa watu. Unaweza kutoka popote duniani ukishaingia Tanzania Bara basi utaingia Zanzibar bila udhibiti wowote.

Zanzibar ina jukumu la kupanga mipango yake ya uchumi , huduma za jamii, miundombinu nk – haya yote si mambo ya Muungano lakini huwezi kupanga hayo bila kujijua kitwakimu idadi ya watu wako na makisio ya wageni wako . Zanzibar haina uwezo wa kudhibiti lolote.

Unaweza kutoka Kongo , utapitia taratibu za udhibiti kuingia tuseme Dar (wao Dar wako makini na hilo) lakini ukishaingia Dar , Zanzibar unashuka tu – shamba la bibi.

Leo Zanzibar imekithiri matukio ya wizi wa kutumia silaha wakati inajulikana wazi Zanzibar raia haruhusiwi kumiliki silaha .

Na kwa hivyo wanawakuta raia wasio silaha na hivyo inakuwa kazi nyepesi tofauti na Bara ambako kwa vile raia wanaruhusiwa kuwa na silaha basi wanakuwa angalau na khofu.


Hivi majuzi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipopendekeza kutoa kipaumbele kwa Wazanzibari katika suala la ajira katika sekta ya utalii nongwa ziliibuka tena eti ni ubaguzi na hivyo iachwe huria kwa Watanzania wote.

Hivi tunajua maana ya neno ubaguzi? Ubaguzi maana yake ni pale watu wa aina moja wanapotendewa tofauti. Katika muktadha huu Wazanzibari kwa udogo wa soko lao la ajira hawako sawa na ndugu zao wa Tanzania Bara ambao wana soko pana sana la ajira hata ukiwashusha huko Wazanzibari wote halitetereki!

Kuwajengea mazingira ya hifadhi kuna ubaya gani ? Hata Tanzania ,ikiwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunaiona ilivyo makini katika kulinda haki za Watanzania katika maeneo mbali mbali kama ardhi,ajira,uraia n.k ! Nongwa ni kwa Zanzibar tu.


Hakuna ubishi kuwa mataifa mengi yanaingia katika mkondo wa kuungana lakini tusiishie hapo twende mbele zaidi tuone huo muundo wa muungano jee unatoa fursa sawa au ni muungano wa kumezana na kudhoofishana.

Tujiulize kama muungano wetu ni tunu ya kuenziwa mbona umedumu miaka 50 hakuna aliyetamani kujiunga na hata wazo la kuunda EAC lilipoibuka mbona hakuna aliyetaka kuuendeleza huu uliopo na badala yake waliunda mpya tena wa Mkataba tu wenye kurekebishika unaotoa fursa sawa na wenye matumaini na ndio maana walianza watatu leo wameongezeka wawili na wengine wanalilia kujiunga.

Huo Umoja wa Ulaya ulianza na wanachama sita leo ni takriban 30 na wengine wanaomba kujiunga. Kulikoni na huu wetu?

Mwisho tujiulize kama tuliungana kwa lengo la mashirikiano mapana na wenzetu jee kwa nini hatuoni haja ya kujiunga na Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama mataifa mawili kamili tukasukuma mbele zaidi dhana ya Pan –Africanism badala ya kun’gan’gania miungano midogo midogo huku tukiwa na kero kibao na ikiwa tunajenga utata mtupu wa kuingia katika muungano wakati tumo katika muungano? 


Advertisements

6 responses to “Kwa Muungano huu mabadiliko ni lazima

 1. Pingback: Kwa Muungano huu mabadiliko ni lazima·

 2. Labda Bwana Ali Karume alidhani pekee ndio aliewahi kufanya kazi ulaya na kuishi huko.Wazanzibari ni wengi tuu washafika ulaya na wanafanya kazi humo, na wengine wamehajir na kuwa hata raia wa nchi hizo nyingi ikiwamo hio Marekani.

  Barani ulaya, hakuna muungano wa kikatiba.Kila nchi inaendelea na shughuli zake kama ilivyokuwa awali.Kila nchi inachagua viongozi wake, bila ya kuingiliwa na nchi nyengine kama ilivyo Zanzibar kila siku tunachaguliwa viongozi kutoka Dodoma.

  Nachelea kusema kulinganisha umoja wa ulaya na Zanzibar ni ujinga wa hali ya juu.Sina lengo la kusema Bwana Ali ni mjinga, lakini mawazo yake ndio ya kijinga.

  Wasalaam,

 3. aseme anayetake chochote , sisi hatusikii wala hatuoni tunataka nchi yetu za znz iachwe huru , tukiona hakuna faida kuwe peke yetu tutatafakari kama tuungane tena , lakini kwa sasa tuacheni watanganyika na nyinyi muendeleze nchi yenu na sisi tuendeleze nchi yetu tuwe marafiki na kushirikiana kwenye mambo tutayokubaliana hapo baadae, Ikiwa hamtaki kwa amani basi ngojeeni litalotokea , kikwete hata uongeze majeshi hayasaidii kitu , alikuwepo firauni na wengineo kabla yako , lazima utambue kile chenye mwanzo huwa na mwisho na hii ni kawaida , lazima tukubali mabadiliko na asiyekubali ni chizi

 4. Kikwete ni muislamu lakini ni uncivilized, moga na hapo hapo dictator, mfuata mawazo ya wachache hii ni kwa sababu mawazo ya wengi ndio haya kuwa muungano lazima ujadiliwe kuwepo au kutokuwepo kwake na kama uwepo kwa Muundo gani?

  Sasa unaposema usijadiliwe unamsikiliza nani? Aibu kubwa hii Kikwete, utadhalilika mpaka lini mjomba?

  Au Mkeo kasema usijadiliwe?
  Maana yeye mawazo yake ni muhimu kuliko yetu sisi wavuvi, wakwezi na wakulima ambao ni ngazi zenu za kupandia kwenda madarakani.

  Pia Kikwete hutupendi Wazanzibari, tunaumia wewe ndio kwanza unashirikiana na Waziri Dr. Ally Moh’d Shein kutuumiza na kutuumiza zaidi tena kwa ubabe. Eti “Muungano ubaki kama ulivyo ili kudumisha amani”. Je! Amani idumu halafu sisi tule mawe?. Kuna amani pasipo na haki? Kama amani mnaipenda sana basi mara hii mtaikosa labda mjirekebishe Muungano, asiyesikia la Mkuu huvunjika guu na mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi.

  Mbona wewe kwenu Bagamoyo umemuweka mwanao Ridhuwani Kikwete na team yake wazuwie uuzwaji wa ardhi kwa wageni kutoka nje ya Bagamoyo?

  Au mkuki kwa nguruwe kwa binadamu unauma?

  Kikwete basi ndugu yangu hebu mshauri huyu Waziri wako Shein, anatutha aibu mno, aache kukuogopa wewe na awe anatusikiliza na sisi washamba wa Kizanzibari ambao anatuona hatujasoma na wala hatumuoni Yesu kama ni Mungu, na kwa kosa letu hili adhabu yake ndio hii yaani hatusikilizwi!

  Kikwete usipowapenda Wanzibari leo utawapenda kesho utakapoondoka kwenye mzinga wa asali na kuanza kuhudhuria Mashindano ya Qur-an na maulidi kama Baba yako Mwinyi leo anavyopita akiambulia vibao vya mashavuni. Aibu iliyoje! Na yeye alijifanya kama wewe ingawa wewe sasa tunaona umeazidi na kufurutu aah! “MUUNGANO USIJADILIWE”? Kenge weee! Shut up.

  MUUNGANO HATUUTAKI.

  “When peace fails apply force”

  Busara ikishindwa tumia nguvu.

  Nawasilisha.

  SERELLY.

 5. HAIWEZEKANI KAMWE KUZUNGUMZIA KATIBA YA TANZANIA BILA YA KUJADILI MUUNGANO. HIVI KIKWETE UMEFIKIRI KATIKA HILI? KUZUIA MUUNGANO USIJADILIWE MAANA YAKE NI SAWA NA KUSEMA WAZANZIBARI AMBAO HAWARIDHIKI NA MUUNGANO HUU ULIOPO SASA HAWANA HAKI YA KUSEMA ILA WENYE HAKI NI WATANGANYIKA TU. MZEE KARUME ALIBURUZWA NA NYERERE NA WEWE SASA UNATAKA KUWABURUZA WAZANZIBARI NA TAYARI UMESHAAMUA HIVYO. HII INATHIBITISHA KUA MUUNGANO HUU NI WA VIONGOZI TENA WA CCM PEKE YAO NA HAUWAHUSU WANANCHI WA PANDE ZOTE MBILI. WATANGANYIKA WAO KWA KUA WANAFAIDI CHINI YA MFUMO WA MUUNGANO ULIOPO HAWASEMI KITU LAKINI SISI WAZANZIBARI TUNAOPATA HASARA HATUNA HAKI YA KUSEMA. KWA HILI JITAYARISHE KUMWAGA DAMU KAMA ALIVYOFANYA ALIEKUTANGULIA MKAPA MWAKA 2001. AMEONDOKA MIKONO YAKE IKIWA IMEJAA DAMU YA WAZANZIBARI. SISI WAZANZIBARI KWA HILI TUNAPENDA KUEKA WAZI KUA MUUNGANO NI LAZIMA UJADILIWE NA KAMA HILI HULITAKI HAKUNA HAJA YA KUWAULIZA WAZANZIBARI KUHUSU KATIBA MPYA KWANI MAONI YAO INAONEKANA HAYATAKIWI KATIKA MCHAKATO HUU WA KATIBA MPYA. TUNAJUA FIKA KUA MSIMAMO UMESHATOLEWA NA KAMATI KUU YA CCM KUA NI WA SERIKALI MBILI LAKINI SISI WAZANZIBARI TUNASEMA MUUNGANO HUU ULIOPO SASA AMBAO KILA DALILI ZINAONYESHA KUA SIO WA HALALI, NI WA GHILBA, UTAPELI, KULAZIMISHANA, NA UNA HARUFU YA UVAMIZI WA NGUVU WA DOLA MOJA HURU DHIDI YA NYENGINE AMBAO KWA LUGHA NYEPESI TUNAWEZA KUSEMA NI SAWA NA UKOLONI WA WATU WEUSI HAUFAI NA KAMA ALIVYOWAHI KUSEMA MZEE KARUME KUA SASA UNATUTIA JOTO NA LAZIMA KOTI TULIVUE.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s