Viongozi hawalindi muungano, bali maslahi yao

Na Jabir Idrissa

WAKATI tuliopo, hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuzuia watu kusema. Ni muhimu na haki kwa binadamu kusema anavyojisikia. Zama za “serikali” kuchagulia watu cha kusema zimekwisha. Katika hali yoyote ile, na hata kama Rais Jakaya Kikwete amesema Watanzania wasijadili kuwepo au kutokuwepo kwa muungano, hakuna kinachosimamisha wananchi kuujadili muungano na hatima yake.

Kwa sababu hiyo, kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar , Mohamed Aboud Mohamed kwamba wanaotaka kuelimisha umma kuhusu maoni ya katiba mpya, waombe Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni kutisha watu. Hata kama waziri na serikali nzima watasema kauli hiyo imetolewa kwa nia njema, kwa desturi ya viongozi wa Zanzibar, unaposikia kauli kama hiyo basi huwa imelenga kuminya haki.


Desturi kama hii imezoeleka sana . Viongozi hujifanya wanajua kila kitu na kujitia wao ndio wanaona mbele zaidi ya wananchi wanaowaongoza. Ninaitazama desturi hii kama ishara ya viongozi kujipendekeza kwa Serikali ya Muungano, na hasahasa kwa chama chao – Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Nataja CCM kwa sababu waziri Aboud anamfuata Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, mwana-CCM, kutoa kauli inayoashiria kutisha watu wanaojadili muungano. Siku zote, viongozi wa Zanzibar hujikweza panapotokea jambo linalogusa uhusiano na Tanzania . Nia ya kufanya hivyo, huwa ni kuonyesha kuwa wanajitahidi “ sana ” kulinda uhusiano.


Ukweli, wanapofanya hivyo hawalindi muungano, bali wanalinda maslahi yao; wanazidi kupalilia vyeo walivyonavyo. Ndani ya nafsi zao wanajua kuwa misimamo yao hiyo ya kujitia kulinda muungano kimabavu, inatofautiana na maoni ya wananchi. Sasa unapokuta msimamo wa wananchi katika jambo hili unatofautiana na ule wa viongozi wao, ujue tunalo tatizo.

Lakini, katika hali hii, aghlabu, wenye tatizo huwa ni viongozi. Kwanini?
Asili ya uongozi, ni kuongoza kulingana na matakwa ya wananchi ambao ndio wenye dhamana na uongozi wa nchi yao , ila kwa sababu wao hawawezi kuongoza wote, huitoa dhamana hiyo kwa viongozi wachache. Kwa hivyo, viongozi wanapaswa kuongoza kwa mujibu wa dhamana waliyopewa na wananchi ambao kikatiba ndio wenye mamlaka ya nchi yao.


Waziri Aboud pamoja na viongozi wenzake wanajua kuwa muungano wa Tanzania ulioasisiwa tarehe 26 Aprili 1964, ndio msingi hasa wa uhusiano uliopo kidola, kati ya Zanzibar na Tanganyika. Lakini pia, wanajua muungano huu umekuwa ukilaumiwa kuwepo kwake kumeipora Zanzibar mamlaka kwa hata yale mambo ambayo kwa asili ya muungano huu, hayakuwa ya muungano.

Viongozi hao wanajua pia kwamba kwa muda wote wa muungano, miaka 48 sasa, wananchi hawajawahi kupewa nafasi ya haki kusema kama unawafaa au wangependa mabadiliko. Viongozi wanajua hakika kuwa wananchi wa Unguja na Pemba wamekuwa wakiuchukulia muungano kama kitu kibaya kilichowafunika katika siasa za kimataifa na za ndani ya nchi. Badala yake, wanaamini muungano huo umetumika kuwaonyesha wao kama ni watu wasiojua siasa njema – wamegombanishwa.


Viongozi wanajua pia kwamba chini ya muungano huo Zanzibar haijanufaika kiuchumi kwa kuwa uchumi si katika eneo linalotazamwa pamoja kimfumo wa muungano. Hata zile fursa za uchumi wa Zanzibar kukua zimekuwa zikifujwa na upande wa pili kwa sababu msimamizi wa sera na sheria za fedha – Benki Kuu – hawajibiki kwa viongozi wa Zanzibar bali wa Serikali ya Muungano. Je, wenzetu Ulaya muungano wao unatenga watu wa taifa moja dhidi ya jengine? Asilani abadani, kwa hakika unawaunganisha chini ya Eurozone.


Kwa ufupi, viongozi wa serikali Zanzibar pamoja na wale wa CCM, wanajua kuwa mara kadhaa katika nyakati tofauti mwaka hadi mwaka, Wazanzibari wamekuwa wakiupa muungano majina mabaya.


Muungano kwao ni kama dude linalowanyonya kiuchumi na kiutambulisho mbele ya medani ya kimataifa. Na hili ni kinyume kabisa na Zanzibar ilivyotokana kihistoria. Ikitambulikana hasa. Hiyo ndiyo hali halisi. Hivi ndivyo namna Wazanzibari walio wengi wanavyouchukulia muungano. Haya siyatungi.


Mjadala ulioanza tangu mapema mwaka uliopita Rais Kikwete alipokuja na wazo la kuanzisha utaratibu wa kuandikwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , ni ushahidi mzuri. Nilidhani viongozi wetu wameelewa maoni ya wananchi kuhusu muungano na nafasi yake katika kuwasaidia waondokane na mkwamo.


Na hapa napata hofu kwamba ina maana ile mijadala iliyofanyika kupitia asasi mbalimbali za kiraia ni kelele za mlango kwa viongozi wetu? Kwamba hawaoni kuwa wananchi wanatumia haki yao kueleza wanachokiona na kuhimiza wanachokitaka? Haiwezekani.


Hebu niwakumbushe. Wamesahau, Wazanzibari wakiongozwa na Rashid Hadi walifungua kesi Mahakama Kuu ya Zanzibar kutaka serikali iwasilishe “Hati Halisi” ya Muungano kama ilivyosainiwa muungano ulipoasisiwa?


Kwa kumbukumbu zao, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati ule, Iddi Pandu Hassan, aliieleza nini mahakamani? Alishindwa kuwasilisha. Alisema yeye hajawahi kuiona na hajui ilipo labda kama wao (walalamikaji) watamsaidia kujua. Jibu lake linamaana ya kutilia shaka uhalali wa muungano.

Mimi ningependa watu waseme. Watasemaje kama wanakwazwa? Kwa kupenda hivyo, maana yake watu waachiwe haki yao na wapewe uhuru wa kusema wanafikiri nini.

Lililo muhimu ni kuwapa wananchi fursa ya kueleza wanachokitaka.
Kwani viongozi wanaogopa kitu gani kuona muungano unajadiliwa kama muungano huo unawahusu watu si viongozi peke yao ?
Kama viongozi hawataki watu wajadili muungano na kuamua hatima yake, waakuwa tu wanathibitisha kile kinachosemwa miaka yote, “Wetu ni muungano wa viongozi tu.”


Ni sawa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoendeshwa kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) imekwepa madai ya kutakiwa iitishe kura ya maoni ili kuwauliza wananchi kama wanautaka muungano na kama wanautaka, uwe wa mfumo gani. Lakini, viongozi hao wajue kuwa kukwepa huko ni sawa na mtindo wa mbuni kujificha kwenye minjugu akidhani haonekani. Kumbe, shingo yote iko nje.


Na wenyewe wanaahirisha tu tatizo, bali maung’uniko hayatafutika hata baada ya katiba mpya kupatikana. Wananchi watatoa hisia zao tume itapowafikia, na watabaki na maoni yao hata wakipuuzwa.

 

Advertisements

6 responses to “Viongozi hawalindi muungano, bali maslahi yao

 1. Pingback: Viongozi hawalindi muungano, bali maslahi yao·

 2. Jabir

  Ahsante kwa uchambuzi. Wewe unafahamu hasa mahitaji ya wakati na jinsi ilivyolazima kwa watu kukubaliana na mahitaji yake. Wale ambao wanaongoza Serikali yenye scandals nyingi ni bora wawaachie akina Sheiks wahuburi habari za Muungano kwa kuwa kuwakatalia kutatoa nafasi kwa Masheikh kubadilisha ajenda na hii intawaathiri sana akina RCs waliuza Ardhi Makangale Pemba, Akina Rcs ambao kwa mujibu wa Ripoti ya Omar Ali Shehe walilazimisha ajira za watoto wao katika taasisi za Serikali na viongozi wengine ambao yakitajwa madhambi yao watatamani ardhi ifunuke waingie. Jabir ndugu akina Plato walipozungumzia siasa waliihusisha na kuleta faida kwa watu ” brings good to the people.”. Hawa wakatzao mazungumzo juu ya Muungano hawalijui hili kwa Shule zao ni za kuunga. ” Walisoma hawakujua, Wakajifunza Wakatambua”. Wanaona kila kila kwa kutumia nadharia hii ni sawa- kumbe sivyo.

  Mimi siamini kuwa Muungano ambao ni zao la ubongo wa binadamu ambaye ni falliable unaweza kukosa kasoro. Hata kama hauna kwa unahusu maisha ya watu basi ni lazima uzungumzwe kwa kuwa ni kwa kupitia watu ndio legitimacy yake inapatikana. Muungano wa hayati Karume na Nyerere haukubalika lakni watu kwa woga waliunyamazia. Ile ya TRA kutoza kodi mara mbili kwa watu wa Zanzibar ni ishara ya kutokubalika kwa Muungano hata huko Bara ambako kuna sauti za kulaumu kuhusu kukataliwa Muungano Unguja.

  Muungano utakaokuja baada ya Katiba mpya utakuwa na misukosuko zaidi ya huu wa sasa. Wako watu wengi bara ambao leo wanahoji uwepo wake na faida zinazopatikana. Na hawa ni watu wa kutoka Wala nchi hadi wananchi. Viongozi wetu ingekuwa bora waruhusu watu wazungumze kuhusu Muungano kwa kwa kufanya hiivyo kutawawezesha kuona kasoro ambazo wao wakikaa katika kamati za Chama hawazioni. Vile vile mazungumzo juu ya Muungano yataisafia Tume ya Warioba kupata mawazo mengine ambayo hawatayapata katika vikao rasmi vitakavyoitishwa. Ningekuwa mimi ningeruhusu watu waseme watakavyo kwa mwisho kura maoni ndio itaamua na baada ya kura uhalali wa Muungano utakuwa wa kweli. Vile vile ikumbukwe kuwa watu leo wanafahamu mambo kwa upeo mpana zaidi. Wakati wa kutafuta Serikali ya Umoja wa Kitaifa wako waliopinga. Hatahivyo, ilibidi wakubali kuunga mkono kwa waliokubali walikuwa wengi.

  Leo hii wamo Serikalini hata walipiga kura ya Hapana kwa zaidi 90%. Ndio “democracy hii”. Wasichokijua hawa viongozi ni kuwa “Democrats not only respect verdict by majority but also appreciate varied opinions.” Ukiheshimu uchaguzi ni lazima uheshimu uhuru wa mtu kuchagua anachokitaka. Mfumo wa kijamii ni lazima uendeshwe kijamii. Mwanafalsafa moja alisema “A sample taken from any part of human body is enough to lead the reasecher to come to a conclusion. This is not possible when studying people whose thinking is very dependednt on the environment within which they live”. Akina hawa RCs wanadhani mtu ni sawa biologically and socially. Wangealia watoto wao wanavyochukuwa sura zao na wakatofuatiana mitizamo yao kisha wakauliza kwa nini basi ingekuwa Shule nzuri kwao.

  Jabiri endelea tuu kwa kuwa hawa hawalindi tuu maslahi yao lakini wanaogopa mabadiliko kwa kuwa hawataweza kuhimili ” Survival for the fittest”

 3. HATUUTAKI MUUNGANO UNATUNYONYA NA UNATUPOTEZEA MILA DESTURI NA UCHUMI Viongozi walioko madarakani ndio wanaofaidika na huo muungano na wapo hapo kuulinda huwo muungano kwa kufarahisha mabwana zao lakini uma wa Wazanzibari walio wengi tunasema hatuutaki muungano. Tushachoka kupangiwa viongozi wetu Dodoma. Tunataka Zanzibar yenye mamlaka kamili. Wacheni kutukandamiza. Tunaka kura ya maoni ifanyike. Tumechoka na udhalim wa Muungano. Inshallah tutashinda kwa uwezo wa ALLAH. HATUUTAKI MUUNGANO WACHENI UMBUMBUMBU. SISI HATUNA JESHI WALA SILAHA TEGEMEO LETU NI ALLAH NA INSHALLAH TUTASHINDA. Amin.

 4. Assalaam alaikum wazanzibari wenzangu hapa la muhimu ni kufanya juhudi za kuuvunja muungano na sio fikra za kuweka aina nyengine yeyote ya muungano sisemi wenye fikra hizo hayafai mawaz yao la kini na penda kuwafahamisha wenzangu wenye mawazo hayo wenzetu wa tanganyika wa kikubali aina yeyote ya mungano bac lengo lao ni dhulma kwe tu hata tuwe na uamuzi gani ila kubwa kabisa ni kutubebesha msalaba kama walivyo ubeba wao kwa hiyo wanataka tupotee kama walivyo potea wao kama alivyo tuambia Allah subhanahu wataala kwaba hawatokuwa radhi mayahudi na wakristo mpaka mfuate mila zao .
  Kwa hivyo na wachi wale wote wanaotaka muungano uendele ni kuendeleza kanisa ndani ya zanzibar.
  Na msihi makamo wa kwanza wa raisi maalim seif Sharif Hamad haya yote unayaelewa na husemi ukasikika kuonyesha kwamba unauchukia muungano kama wanavyosema viongozi wenzako kuutetea muungano bila ya kuona aibu hali ya kuwa wanajua kufanya hivyo ni kuendeleza kanisa ndani ya zanzibar.
  Maalim nakukumbusha kauli yako ulipo sema uwanja wa taifa ya kuwa muislam asione haya kujitangaaza kama yeye muislam kwa ni uislam ndio dini ya haki.
  Kwa hiyo na wewe usione haya kupinga kubebeshwa kanisa ndani ya zanzibar kwahiyo ili kuoyesha chuki dhidi ya kanisa basi ukatae muungano waziwazi kama wanavyoukubali viongozi wenzako.
  Kwani wao wanatete ukristo kwa njia ya muungano na wewe chukia ukristo kwa njia hiyo2 kwa kuukata.
  Muhimu hapa ni kura ya maoni kwanza kuliko mchakato wa katiba.
  Kama kweli wanasema wanaokataa mungano ni kidogo kwa nini muwe wazito kuleta kura ya maoni laki mnajua kama wanaoukataa muungano ni wengi ndio maana munakataa kura ya maoni kwa kisikingizio kuwa kufanya hivyo ni kuchochea fujo.

 5. INABIDI TUWE TUNACHUNGA HISIA ZETU KATIKA KUELEZEA CHUKI ZETU KUHUSU MUUNGANO NA HASA TUNAPOONGELEA UISLAMU NA UKIRISTO KWANI HATA HUKO BARA KUNA WAISLAMU KWA HIYO TUSITUMIE KAULI KAMA ALIZOTUMIA BWANA ALIYETANGULIA HAPOO JUU

 6. apende asipende nd kikwete na wale wanaomshauri upotofu , muungano hautakiwi na wazanzibari , wako wapi hawa CHADEMA na Kina CUF wanaojidai wakipata nchi wataweka serikali tatu , mbona mmekaa kimya madudu? hatutaki MUUNGANO ND KIKWETE waeleze na wale wanaokupeleka mchomo , usije kuitia nchi ktk umwagaji damu , utambue damu haitomwagika znz pekee itaikumba na tanganyika vile vile. Na hawa vifaranga vya nyerere kina salimu amedi salimu karibu kuingia kwenye makaburi lakini bado wanang’ang’ania ukubwa na utukufu wa dunia , ole wenu mtapokutana na mola , mtapigwa virungu kama vile Nyerere anavyopata joto ya jiwe huko aliko ,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s