Mazingile mwanambiji yanayomkabili Warioba

Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba

Ahmed Rajab

TUME ya Katiba, chini ya uwenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, imekwishaanza kujipanga na kujipangia namna itavyokuwa inafanya kazi. Kwa mujibu wa sheria ya kuundwa kwa Tume hiyo kazi yake kubwa itakuwa ni kupita kila pembe ya Tanzania kwa madhumuni ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya ya taifa, kuyachambua maoni hayo na kuyaratibu.

Hadi sasa hatujui ni mwongozo gani utakaofuatwa na Tume hiyo katika kuendesha shughuli zake. Nielewavyo ni kwamba kwa sasa wajumbe wa Tume wanaipima hali ya mambo ilivyo nchini kuhusu mchakato mzima wa Katiba mpya.

Mengi bado hayajulikani kuhusu namna Tume hiyo itakavyofanya kazi zake lakini nafikiri kwamba kufikia mwisho wa wiki au mwanzoni mwa wiki ijayo Warioba ataweza kutueleza jinsi Tume yake itakavyoanza kuendesha shughuli zake.

Jambo la kwanza la kutiwa maanani ni kwamba itakuwa muhali kwa wajumbe wote wa Tume kufuatana pamoja kwenda kila mahala. Watabidi wagawane sehemu watazokwenda; hawa wende huku na wengine wende kwengine. Vikundi vya Tume vitakuwa vya mchanganyiko wa watu kutoka Bara na wale wa kutoka Visiwani.

Kwa ufupi, Tume ya Katiba ina kazi mbili: mosi, kushauriana na wananchi na kujua wanasema nini kuhusu Katiba na pili, kuyatathmini maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo.

Juu juu kazi hiyo inaonyesha kuwa ni rahisi na isiyokuwa na utata. Si jambo gumu kutega masikio na kuyasikiliza maoni ya watu ila labda pale wenye kutega masikio wanapokuwa na masikio ya kufa. Na sidhani kwamba wajumbe wa Tume ya Katiba ni watu wa sampuli hiyo.

Tatizo litazuka katika kuyachambua na kuyaratibu hayo maoni ya wananchi ambayo lazima yatakuwa ni yenye kutofautiana na kukinzana. Tatizo kubwa zaidi litazuka pale wajumbe wa Tume watapokaa kitako wakawaza na kuwazua na kuyatathmini maoni watayoyapata na kutoa mapendekezo.

Hapo patahitajika uadilifu wa hali ya juu kabisa katika kuyapambanua maoni hayo na kuyapanga. Uadilifu huo utahitajika kwa sababu lazima patatolewa maoni ambayo hayatowapendeza wale wenye kujiona kwamba wao ndio wenye uamuzi wa mwisho juu ya mustakabali wa taifa.
Hayo yako bayana zaidi huko Zanzibar ambako tayari tunasikia sauti kubwa zikipazwa kuupinga mfumo wa sasa wa Muungano, sauti ambazo baadhi ya wakubwa wanataka zizimwe. Bado haijulikani lini Tume itafunga safari yake ya kwanza kwenda Zanzibar kusikiliza maoni ya wananchi.

Warioba aliwakuna wengi alipotamka kwamba Tume yake haitofanya kazi kwa shinikizo za mtu yeyote au za kikundi chochote. Ijapokuwa hadi sasa hatujui ni mwongozo gani Tume hiyo itaufuata ni jambo la kutia moyo kuona kwamba Warioba ametoa hakikisho hilo. Ni jambo la kutia moyo kwa sababu endapo atajiachia ashinikizwe basi naye anaweza akawapotosha wajumbe wa Tume yake kwa kuwapitisha kwenye mazingile mwanambiji ya kichaka cha huo mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya.

Nikizungumzia yanayojiri Zanzibar wananchi wengi wa huko wanaisubiri kwa hamu kubwa Tume ya Katiba kwani itawapa fursa ya kutoa maoni yao juu ya aina ya Katiba waitakayo na hususan juu ya mfumo wa Muungano wanaoutaka. Wanaipata fursa hiyo kutokana na ile sheria iliyouanzisha huu mchakato wa Katiba mpya.

Sheria hiyo hiyo inatambua kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Muungano wa nchi mbili tofauti, yaani Tanganyika (au Tanzania-Bara) na Zanzibar. Utambuzi huo ndio msingi wa Tume ya Katiba yenye wajumbe 32 (tukimjumlisha mwenyekiti na kaimu wake), iwe na wajumbe 16 kutoka Bara (Tanganyika) na 16 wengine kutoka Zanzibar.

Hii ni hatua muhimu sana kwa sababu labda hii ni mara ya mwanzo Zanzibar inawakilishwa inavyostahili katika taasisi za Muungano tangu Muungano wenyewe uundwe miaka 48 iliyopita. Ni matarajio ya wengi kwamba kwa vile Zanzibar inawakilishwa vilivyo kwenye Tume hiyo basi maslahi yake yatalindwa na wajumbe wa Tume watokao Visiwani.

Hayo bila ya shaka yatategemea juu ya msimamo utaochukuliwa na wajumbe wa Katiba – ama wa kila mmoja wao binafsi au wa pamoja kama kundi la Wazanzibari walioteuliwa na Rais wa Tanzania baada ya kupendekezwa na Rais wa Zanzibar na kwa ridhaa yake. Wajumbe hao wataiwakilisha Zanzibar mpaka utapopatikana mfumo mpya wa uhusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar, mfumo ambao utapatikana kwa makubaliano ya pande hizo mbili ama juu ya msingi wa Katiba au, kama Wazanzibari wengi wanavyotaka, juu ya msingi wa mikataba baina ya nchi mbili, kila moja ya nchi hizo ikiwa na uhuru na mamlaka kamili ya kuendesha shughuli zake za ndani na ya nje ya nchi.

Wajumbe wa Tume kutoka Zanzibar wana fursa isiyo na kifani ya kuhakikisha kwamba Wazanzibari wanaupata mradi wao na hivyo kujenga msingi madhubuti wa uhusiano wa karibu na wa kindugu baina ya Tanganyika na Zanzibar. Wazanzibari wanataraji kwamba uhusiano huo mpya utaziwezesha nchi hizo mbili ziheshimiane na zitambue kwamba kila mojawao ni sawa na mwenziwe. Kwa lugha ya mitaani wanachotaraji Wazanzibari wengi ni kwamba hakuna nchi itayojaribu ‘kuionea’ nyingine kwa misingi ya ukubwa wa eneo la nchi au nguvu za kijeshi.

Inavyoonyesha ni kwamba wengi wa Wazanzibari wamekwishaamua wanataka nini kitokee utapomalizika mchakato huu wa Katiba. Wanachotaka ni kuiona serikali yao inarejeshewa mamlaka yake kamili yatayoiwezesha kuyatanzua matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyoikumba nchi yao kwa muda wote huu wa miaka 48 tangu ulipoundwa Muungano.

Kwa sasa serikali hiyo imelemaa kwa sababu haina uwezo wa kuyalinda ipasavyo maslahi ya Zanzibar kwa vile wanaamini ya kwamba shughuli zote za utawala zilizo muhimu na za kimsingi zimehaulishwa kwenye Serikali ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano.

Tatizo ni kwamba Katiba hiyo yenyewe haikutungwa kihalali na wananchi hawakuwa na usemi wowote katika utungwaji wake. Matokeo yake, na huu ndio ukweli unaowachoma Wazanzibari, Serikali ya Zanzibar imegeuka kuwa sawa na ‘serikali ya mkoa’ au serikali ya manispaa. Ndio maana hakuna ushahidi kwamba Serikali ya Tanzania inashiriki katika maendeleo ya Zanzibar au kwamba inatenga fungu la fedha za Serikali ya Muungano kwa maendeleo ya Zanzibar. Kwa hakika, tunaweza kusema kwamba hiyo ndiyo sababu moja kubwa inayowafanya Wazanzibari wawe wanaupinga vikali Muungano na wanasubiri tu fursa itayowawezesha kuyamwaga rasmi na hadharani malalamiko yao.

Wajumbe wa Zanzibar katika Tume ya Katiba wameteuliwa kuiwakilisha Zanzibar kama wenzao walivyoteuliwa kuiwakilisha Tanzania-Bara. Uteuzi huo unaainisha kwamba wakuu wa Tanzania wanaelewa wazi kwamba ile iliyokuwa Tanganyika ina maslahi yaliyo tofauti na yale ya Zanzibar. Hivyo, wajumbe wa Bara katika Tume watautetea msimamo wa Tanganyika na haitostaajabisha endapo watataka mfumo wa Muungano uliopo sasa uendelee vivi hivi ulivyo baada ya kutiwa viraka vya hapa na pale.

Wenzao kutoka Zanzibari watakuwa na jukumu gumu zaidi la kuhakikisha kwamba maoni ya Wazanzibari wengi yanaheshimiwa na kuwasilishwa kwa njia itayowaridhisha. Maoni hayo ni yenye kutaka pawepo mageuzi makubwa zaidi na ya kimsingi katika mfumo wa Muungano.

Kadhalika ni wazi kwamba umma wa Zanzibar unaofuatilia mchakato huu kwa shauku kubwa utakuwa unawaangalia kwa macho mawili wajumbe Wakizanzibari walio katika Tume ya Katiba.

Ili waweze kuyatetea maslahi ya Zanzibar, wajumbe Wakizanzibari watawajibika wafanye kazi kwa pamoja na itakuwa jambo zuri iwapo wataongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. Serikali hiyo nayo inawajibika iwe na msimamo ulio sawa na ule wa Wazanzibari wengi juu ya Muungano, hasa kwa vile Zanzibar inajigamba kuwa ni yenye utawala wa kidemokrasia wenye kuongozwa na matakwa ya Wazanzibari.

Advertisements

9 responses to “Mazingile mwanambiji yanayomkabili Warioba

 1. Bwana Ahmed Rajab tunaona ushaanza kutumika au kama ni mawazo yako kweli basi naomba ufanye utafiti kwanza unapotaka kuyazungumzia mambo yalivyo huku visiwani kuhusu Muungano huu. Unasema “watu wengi wanataka mabadiliko kuhusu mfumo wa Muungano wa sasa na uwe wa mkataba”, Je! unauhakika kuwa watu wa aina hiyo ni wengi hapa Unguja na Pemba ? Je! kama unauhakika kuwa ni wengi umetumia data au takwimu kutoka chanzo gani ? Na Je! chanzo hicho kiliifanya kazi hiyo lini? Na kilianzia wapi? Na kumalizia wapi ? Na chanzo hicho kiliagizwa na nani kwa malengo gani na kwa manufaa ya nani ?
  Mimi naamini Wazanzibari waliowengi wamechoka na kitiu hichi kiitwacho Muungano wa kiwizi wizi tu.
  Pia kwa mimi sijui kwa wenzangu imenikera na kuniumiza moyo sana makala hii kwani imeandikwa na Mzee ninaemheshimu na kumtegemea lakini naona kaboronga sana na ameniudhi sana. Kwa taarifa yako Mzee Ahmed Rajab Muungano wa aina yoyote unayoijua wewe na watu hawa walaghai hatuutaki, na kama nyinyi watu wazima wahafidhina wa Muungano mnaoamini kuwa eti bila ya Muungano maisha Zanzibar hayawezi kuwepo na kiayama kitasimama mara moja basi tunasema umri wenu alhamdulillah mmeumaliza kwenye Muungano wenuhuu umri wetu sisi hatutaki wala hatutakubali umalizikie kwenye ginyingi hili na wallah thumma wallah kama mnatulamizimisha mtajuta si muda mrefu sisi hasa.
  Ahmed Rajab tunakujua kama unauchukia Muungano huu, pia unawajua Watanganyika kwa wizi na ulaghai hata kama utaweka Muungano wa aina gani wao kwa kadiri siku zitakavyokwenda watavilaghai vizazi vijavyo vya Waislamu Wakizanzibari na kuvidhalilisha tena kama uonavyo leo watoto wa Nyerere wanasimama mabungeni na kusema “ZANZIBAR SI NCHI” bila ya hata kumalizia kuwa Je! ni chupi ya mama yake au nini? au usinga wa mganga wake ? Baya zaidi wakati haya wanayasema na kuyasimamia kidete wabunge wetu na viongozi wetu wakuu wa nchi hapa Zanzibar wakenua meno tu na wengi hata kujitia kujustify kauli chafu kama ile kuwa ni sahihi ila wazanzibari wakuielewa. Sasa Bwana Ahmed Rajab unafikiri sisi wazanzibari tunatarajia kutetewa na viwete hawa wa kufikiri wanaojali matumbo yao kuliko jamii yao kuwa eti watuletee Muungano fair hali ya kuwa tushawasikia mara kwa mara wakiusifu Muungano huu kwa kuwa na faida za mapolo ya mbatata kutoka TANGANYIKA na kusisitiza kuwa ubaki kama ulivyo?.
  SAMAHANI sana Bwana Ahmed Rajab tunakustahi kwa utetezi wako mkubwa wa jamii ya kizanzibari lakini kwa sasa zingatia tunapita katika kipindi muhimu na nyeti sana katika historia ya Zanzibar, unapotaka kuandika lolote kwanza tizama vizuri ndugu zako wanashida gani sio tunataka barafu unatulea chumvi utatukera na tutaondoa Imani kwako, huwezi nyamaza kimya.

 2. Bwana Ahmed Rajab inaonesha kama ushaanza kutumiwa sasa unasema “Wazanzibari waliowengi wanataka mabadiliko katika Muundo wa Muungano wa sasa na uwe Muungano wa Mkataba” Je! unauhakika kuwa kundi la watu wa aina hiyo ni wengi huku Ungaja na Pemba? Na kama unauhakika umetumia data au takwimu kutoka chanzo gani? Na Je! Chanzo hicho ni cha uhakika kwa kiasi gani? Na Je! chanzo hicho kimefanya utafiti (research) hiyo lini? Na Je! kilifanya utafiti huo lini? Na Je! kilianzia kutafiti wapi na kimalizia wapi na kwa mbinu gani? Na Je! chanzo hicho kilitumwa au kuagizwa na nani? Na Je! ni kwa malengo gani na kwa manufaa ya nani?
  Nijuavyo mimi wazanzibari kweli wanataka mabadiliko katika Muungano huu uwe wa Serikali mbili kila mtu na yake kwake na raha zake na karaha zake, ambapo utabaki ujirani mwema wakutembeleana kwa ruhusa maalumu ya maandishi maalumu ya muda maalumu, na ninasema hivyo kwa sababu ni watu wa aina hiyo tu wanaofanya harakati ya kutaka azma hii itimie na halijapatapo kuchomoza kundi kubwa kama hili lenye hiyo misimamo iliyobakia, na mimi binafsi nimepata kuhudhuria na kujionea mambo yanavyokwenda zaidi ya mara moja katika nyumati kubwa kubwa, Je! Bwana Ahmed Rajab ndio tuseme na wewe umeamua leo kuungana na ZBC waanzilishi wa hoja hii kuwa eti “kuna kikundi kidogo tu kinachotaka Muungano uvunjike na kinahatarisha amani”.
  Bwana Ahmed Rajab sisi tunakujua msimamo wako juu ya Muungano huu kuwa huukubali na unauchukia, sasa unaogopa nini kusema uvunjike? wakati Watanganyika unawajua vyema kwa ulaghai wao na wizi uliojaa khiyana, kiasi kwamba hata kama tutaweka Muungano wa Barua kwa kadiri siku na miaka itavyopita na kwenda wataubadilisha na kupata njia ya kuvidhalilisha vizazi vijavyo vya Wazanzibari, watu ambao kwa muda wa miaka 48 wamekuwa Duniani hawapo na Akhera hajafika, kisa eti Muungano, Nasema hivi kwa sababu nia yao katika Muungano huu haikuwa njema na hurithishana nia yao hiyo dhidi yetu, mfano huoni leo watoto wa Nyerere (Pinda) wanasimama katika mabunge na kutamka wazi wazi tena dhaahiri shaahiri kuwa “ZANZIBAR SI NCHI” bila hata ya kumalizia ni nini, je! ni Chupi ya mama yake au ni usinga wa kupungia wa mganga wake? inauma sana. Baya zaidi, wakati wanayasema haya wabunge wetu na baadhi yia viongozi wakuu wa nch yetu ZNZ ndio kwanza wanakenua meno na kuthubutu hata kuwatetea wakatoliki hawa “Eti mheshimiwa Waziri mkuua alikuwa na nia njema bahati mbaya Wazanzibari waliowengi hawakumuelewa” unajua nini alichokisema Mshenzi huyu? alisema “I didn’t sleep my tongue I know what I was saying ZANZIBAR SI NCHI” yaani (Sikuteleza ulimi nakijua sana nilichokuwa nakisema “ZANZIBAR SI NCHI”. Unafikiri sisi tunatarajia kutetewa na viwete hawa wa kufikiri watetea matumbo yao hawa ambao hata hawana uchungu na Imani yao wala Jamii yao? unafikiri hawa nyumbu wanaweza kusimama mbele ya Wafalme wao watanganyika na kutuletea angalau huo unaouita wewe ni Muungano wa mkataba? Hawa tayari tumewasikia mara kwa mara wa kibweka na kuusifu Muungano huu kuwa unafaida ya mapolo kwa mapolo ya mbatata kutoka mjini Tanganyika yakiletwa hapa shamba (ZNZ) na kwa hinyo eti ni muhimu na uendelee kama ulivyo. Shabbash upuuzi! gani huu!.
  Sisi tunasema hivi Muungano nyinyi mnaupenda na mnaamini kuwa bila ya Muungano Zanzibar maisha yatasita na Qiayama kisimama haraka haraka, sadakta sasa alhamdulillah kama mliupenda sana maisha yenu ndio yamemalizikia kwenye GINYINGI hili la Muungano na muda huo mlikuwa mkivuna mlichokipanda sasa wakati umefika na sisi tuachiwe tupande tunachokitaka ili tusiendelee kuvuna mlichokipanda, maisha yetu hatutakubali nayo yamalizikie kwenye huu Mlumbano kama hayo yenu kwani hakuna mlicho tuandalia zaidi ya udhalilifu, kudharaulika na dhiki kali za kila aina pamoja na kuiharibu Dini ya Allah ambayo hamkuita kama mnavyotuachia sisi, Bwana Ahmed Rajab na kama nyinyi wahafidhina wa Muungano mnatulazimisha mnajuta si mrefu.

  MUUNGANO HATUUTAKIIII! JAMANI HEEH VISIWI AU DHARAU?
  JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR KWANZA
  Nawasilisha

  SERELLY

 3. Ndugu zangu shida ya Zanzibar toka zamani si nani atawale ni vipi itawaliwe. Tusiendelee kuzozana kama vile Mmaknode alivyo mwacha mkewe kwa kutokubaliana kuhusu mtoto wangu atakaezaliwa pasi na hata koo kupandwa. Fursa ya Mchakato wa katiba ni muhmu kwa sisi ili tupate kwa nguvu kuingiza mawazo ya kukubalika kikatiba wagomea huru. Hii ikipatikana hatua itayofata ni kwa zAnzibar kujitawala kwa kuwa haya wanayoyataka kina Rashid Addiy yatokee Barazani yatawezekana. Hii pia inaweza kuwapa watu kama kutoka UAMSHO kuingia katiba vyombo vya kutunga sheria na hivyo ukombozi kamili kupatikana

  • Wazo lako ni zuri kakini linamaana kuwa kwa sasa kwanza tubaki ndani ya Muunganooo mpaka tena baadae Sheikh Msellem atakapo kuwa mwakilishi kupitia tiketi ya mgombea binafsi ndio apeleke mswada barazani au vipi? Halafu ndio ukipita tupate nchi au siyo?. Au atakapokuwa Raisi wa ZNZ kwa teketi hiyo. Wazo hili ni gumu kutekelezeka na ni ubahatishaji wa hali ya juu, dhamana ya nchi yetu na Imani yetu itakuwa tumeiweka mikononi mwa Mkatoliki Jaji Joseph Warioba ambaye pamoja na kuwa na wajumbe kutoka Zanzibar ndani ya tume yake yeye ndie mwenye maamuzi ya mwisho katika majadiliano yoyote yale na ninaamini Maaskofu wako karibu nayeye sana kwa sasa ili kuyalinda maslahi ya Kanisa, na hakuna asiyejua namna ya viongozi wa kisiasa na kiserikali miongoni mwa wakristo wanavyowasikiliza Mapadri na Maaskofu kwa lolote lile hata kama ni kinyume na sheria za nchi.

   Pia wazo hili ni gumu kukubalika kwa sababu CCM Tanganyika na CCM Zanzibar wanamsimamo mkali kinyume na wazo hili kuhusu mgombea binafsi sababu kubwa ni kuwa wanaogopa madaraka kujakuangukia mikononi mwa watu wenye “social influence” yaani (ushawishi katika jamii) kama hawa Viongozi wetu watukufu wa Uislamu Zanzibar. Maana hawa CCM hujiona wao ndio wenye nchi hii na wengine ni wapangaji tu ambao wamezaliwa ili waongozwe na wao CCM ni “unique classic people” yaani (watu wateule) waliozaliwa wajekuongoza hapa duniani, hata kama maana ya uongozi hawaijui wala hawana uchungu wa dhati kwa nchi na wananchi wao.

   Kiufupi tusirudi nyuma uzi mmoja tu Muungano hatuutaki kabisa uvunjike right from now.

   MUUNGANO HATUUTAKI.

   JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR KWANZA
   Keep it up.

   SERELLY.

  • Baba kama jina lako lilivo sikulaumu, ivi kweli una imani naTume hili mpaka unafikia kusema tuingie kwenye mchakato huu wa kuhuni ??? I can’t believe ndugu yangu !!!

   Kiukweli hatuna imani na wala hatutokuwa imani na Tume kama hizi huku Znzbar maana tushdanganywa sana, na mara hii hatukubali tena, ikiwa wewe una imani hujakatazwa nenda, LAKINI SISI LA MUHIMU NI KURA YA MAONI NA SIO KATIBA, YA TANGANYIKA, Zanzibar tunayo katiba na wala hatuhitaji katiba ila UHURU ndio la msingi.

   EREVUKA BABA USIWE NA MAWAZO MGANDO YA AKINA SEFU IDDI & ABUDI & SHAMHUNA.

 4. Pingback: Mazingile mwanambiji yanayomkabili Warioba·

 5. Muungano ni batili. Tunataka kura ya maoni ili kuhakikishia ulimwengu kwamba huwo muungano haukubaliwi na wazanzibar. Hu mchakachuo wa katiba mpya ni hila tu za viongozi walioko madarakani kutaka kutukandamiza. Kwa tume hii hatutoi maoni yetu ni kupoteza muda tu. Hayo maoni ya wananchi hayasikilizwi. Kama yanasikilizwa sisi wananchi tunataka kura ya maoni mbona hamutusikilizi? Sisi wananchi tulio na uchungu wa Zanzibar hatuutaki muungano wala musitulazimishe. Tushachoka na muungano unatunukia uvundo. Sasa tumeshaamuwa kwa hilo. Enyi viongozi mulioko madarakani musijidanganye mukasema eti ni kikundi kidogo tu. Mimi nawahakishia kuwa UMA WA KIZANZIBARI HATUUTAKI MUUNGANO HATA MUKATISHA VIPI SISI TUMESHAAMUWA HATA MUKATUUWA BASI LAKINI MUUNGANO HATUUTAKI. Tunaamini tuatashinda tu kwa nguvu za Mwenyenzi Mungu. Ishallah.

 6. nakubaliana na wachangiaji huyu Ahmed Rajab ana lake, lakini akumbuke adui/ rafiki mkubwa wa binadamu ni kifo ambacho kinamwandama muda wote , asijisahau kifo hicho kinaweza kumpeleka kwenye urafiki au uadui kutegemea na nini amepeleka mbele ye Mola. Hawa ni pamoja wale waliochaguliwa kwenye tume wamurikwe. HATUUTAKI MUUNGANO BW.AHMED RAJAB , KAWAAMBIE WALIOKUTUMA kabla ya kukutana na muumba siku nzito ambayo hawatoweza hao mabwana wako kukusaidia chochote.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s