Mwaka 1 sasa, Dk. Shein arudi kutafakari

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Dk Ali Mohamed Shein,akisamiana viongozi wa Chama hicho huko Kijiji cha Jambiani Kibigija Wilaya ya Kusini Unguja jana, alipokuwa katika ziara ya Uimarishaji wa Chama cha Mapinduzi katika wilaya hiyo

NILIJUA tangu siku ile Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar, amekosea. Aliposema kuwa serikali haipaswi kuhojiwa kwa kuuza au kukodisha mali yake, hakika niliamini alijikwaa. Nikajua itafika siku atalazimika kufikiria upya kauli yake hiyo aliyoitoa kwa sauti ya kutisha huku mbele yake akizongwa na kamera na vinasa sauti. Dk. Shein, mtaalamu bingwa wa tiba ya binadamu, alikuwa ndio kwanza ametua Uwanja wa Ndege wa Zanzibar akitoka ziarani nchini Uturuki.
Kauli yake hiyo ilitokana na swali aliloulizwa na mmoja wa waandishi wa habari wa serikali kuhusu wananchi kuhoji hatua ya serikali  kuuza majengo ya kihistoria yaliyopo eneo la Mji Mkongwe.
“Serikali haifanyi makosa, serikali ina uamuzi wake hasa kwa kuuza mali zake na hakuna anayeweza kuihoji. Ikiamua kuuza jengo itauza tu. Mambo Msiige ni jengo la serikali hatujauza mali ya mtu.
“… Wengine wanasema hatujatangaza tenda kuuza majengo haya, kwani lazima kutangaza tenda? mbona hayo mengine tuliyoyauza hatukutangaza tenda.
Anaongeza kusema ni khiyari yetu… kama kuna wananchi wanaopinga uamuzi huu wa serikali, serikali ninayoiongoza haiwezi kuwazuia kwenda katika vyombo vya sheria maana huko ndiko kwenye haki kwa yeyote anayehisi imevunjwa. Lakaini nawahakikishia tutawashinda.”
Ndivyo alivyosema rais. Sasa nami nasema labda Dk. Shein ameanza kutafakari upya matamshi yake.
Sasa imethibitika kuwa sheria, taratibu na kanuni za serikali kuuza au kukodisha majengo inayoyaita “mali yake” zilikiukwa.
Kwamba walioandaa mikataba na kuidhinisha kuyatoa majengo adhimu yale yanayolindwa kwa taratibu za kimataifa za urithi wa utamaduni, walivunja sheria.
Pengine kuvunja sheria kungekuwa na maana nyepesi kama waliohusika wangekuwa maofisa wa kati na ikaonekana ilitokana tu na njaa zao.
Imegundulika kuwa wao walitekeleza tu maagizo ya viongozi walio juu yao kivyeo na kimamlaka.
Kumbe Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi iliyochunguza namna majengo hayo yalivyotolewa kwa kampuni ya makabaila kwa kivuli cha “mwekezaji” imebaini yote hayo yalitokana na mpango “ulioagizwa” na rais.
Wakati ule, rais alikuwa mtu aitwaye Amani Abeid Amani Karume, mtoto mkubwa wa rais wa kwanza wa Zanzibar baada ya mapinduzi ya 12 Januari 1964 – Abeid Amani Karume.
Mzee Karume, aliyeuawa kwa kupigwa risasi 7 Aprili 1972 akiwa makao makuu ya ASP Kisiwandui, mjini Zanzibar, kwa kutambua umuhimu wa majengo ya Mji Mkongwe, mengi yakiwa yaliyojengwa tokea karne ya 18, aliyataifisha na kuwa ni mali ya serikali.
Kamati Teule imethibitisha kuwa majengo hayo yaliyokuwa yanatumiwa kama ofisi za taasisi mbalimbali za serikali, yalikodishwa katika utaratibu ambao “haukuzingatia maslahi ya taifa.”
Ripoti ya tume inasema ukodishaji huo umefanywa kupitia mkataba wa miaka 99 kwa makabaila wenye fedha za kumwaga lakini kwa malipo ya dola milioni 1.5.
Ugunduzi huu unakuja mwaka mmoja baada ya kauli ya Rais Dk. Shein kwamba “serikali haikufanya makosa yoyote kuuza mali yake… isihojiwe kitu.”
Na uchunguzi ulifanywa na kamati teule ya baraza baada ya suala hilo kuzusha majadiliano marefu ndani ya Baraza la Wawakilishi yaliyoandamana na maneno makali wakati wa mkutano wa bajeti, Juni mwaka jana.
Wajumbe wawakilishi walilalamika sana kuhusu uamuzi wa serikali kuyatoa majengo muhimu kwa njia ya ovyo hasa kwa kuwa hakukufuatwa utaratibu wa tangazo la zabuni na hakukuwa na uwazi.
Walimbana Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame na kumtaka aeleze ni utaratibu gani ulitumika, wapi fedha zimewekwa na kama kulikuwa na zabuni.
Wajumbe walitaka kuelezwa sababu za serikali kuacha majadiliano na watu waliojitokeza awali kuomba kupewa majengo hayo wakati makubaliano yalishafikiwa.
Majengo ya Mambo Msiige yaliopo kwenye uso wa bahari na Bandari ya Malindi, yanapakana na majengo ya zamani ya mitambo ya simu za upepo (Extellecoms) – za kwanza kwa Afrika Mashariki, ambayo sasa ni hoteli ya Serena Inn.
Taarifa za awali kabisa, zilisema kampuni inayoendesha hoteli ya Serena Inn, ndiyo iliyotangulia kuomba majengo hayo kwa ajili ya kupanua hoteli yake; na kutoa ofa kubwa lakini bado wakatelekezwa na serikali.
Siri inafichuka leo kuwa maofisa wa Serena waliotoka Geneva, Uswisi, waliachwa solemba katika siku ambayo wenyeji wao, taasisi ya Agha Khan waliahidiwa na serikali kuwa itakuwa ni hafla ya kusaini mkataba.
Ahadi hiyo ilitokana na kukamilika kwa majadiliano ya ukodishwaji wa majengo hayo Julai 2004.
Kamati Teule inaeleza katika ripoti yake iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi mwezi uliopita, kwamba “Mradi huo una utata mkubwa kutokana na Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan Development Network (AKDN) mnamo Julai 26 mwaka 2004 ilikubaliana na SMZ kukodishwa eneo hilo na majengo ya Mambo Msiige na kutayarisha mkataba wa makubaliano (MoU) ambayo maofisa watatu wa Aga Khan kutoka Geneva walitumwa kuja kushuhudia utiaji wa saini mkataba huo.
“… Ulipangwa kufanyika tarehe 26 Julai 2004 mnamo saa 4:00 asubuhi wakati wajumbe kutoka Aga Khan (Geneva) wakiwa wanasubiri lakini hawakuelezwa kitu chochote cha msingi mpaka majira ya saa 7:00 mchana. Baadaye wakajulishwa kuwa sherehe ya utiaji saini imeahirishwa mpaka itakapotolewa taarifa nyingine.”

Maelezo hayo yamekaririwa mdomoni mwa Mohammed Bhaloo, mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar ambaye Kamati Teule imemtambulisha kama ndiye msemaji wa AKDN. Kamati ilimhoji Bhaloo.

Ajabu, Bhaloo aliieleza kamati hiyo kuwa baada ya kimya cha muda mrefu tangu tukio hilo, walipokea taarifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa majengo hayo sasa yamekodishwa.

Ilielezwa kuwa yamekodishwa kwa kampuni ya ASB Holdings Ltd kwa kiasi kilekile cha dola milioni 1.5 na wamiliki wa Zamani Zanzibar Kempinsky kwa lengo la kujenga hoteli ya kisasa ya daraja la nyota tano.

Kampuni hiyo Zamani Zanzibar Kempinsky tayari ilikuwa inaendesha hoteli mbili nchini Tanzania – moja yenye jina hilo iliyoko Mkoa wa Kaskazini Unguja, na iliyokuwa Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.
UNESCO ndio shirika linaloratibu masuala ya utamaduni ikiwemo kuidhinisha hadhi ya majengo au aina nyingine ya raslimali za taifa kote duniani, kuwa ni ya urithi wa kidunia.
Sasa katika hali kama hiyo ya mkanganyiko uliosababishwa na utendaji wa kilaghai wenye harufu ya rushwa, ni nini kilichotendeka kama si madudu matupu yaliyoifedhehesha serikali?
Na je, sasa serikali inasemaje? Itaendelea kujivuna iliuza chake na isihojiwe? Wale wasaidizi wa “mheshimiwa sana” rais watamshauri arudi kwa umma kuungama kuwa anajuta?
Tena itaje kwa ufasaha ni nani wahusika kubuni na kufanikisha mpango huo; kama ni kweli, ni nani huyo anatajwa kimbinu kuwa aliamrisha au kuagiza; ni hatua gani watachukuliwa na lini zitachukuliwa.
Ends.

Advertisements

2 responses to “Mwaka 1 sasa, Dk. Shein arudi kutafakari

 1. Mjomba Amani katuibia na huyu ashaonesha mwelekeo wakutuibia huku mbele twendako lakini atachina, iko siku ngojea tuushughulikie huu Muungano halafu tuanze kuweka misinga ya uadilifu ambapo Raisi atashitakiwa hata kama yuko madarakani na ataweza kuachia ngazi ikibidi kafanya makosa.

  MUUNGANO HATUUTAKI.

  ZANZIBAR KWANZA

 2. Toka mapema ilionekana kuwa Serikali hii ingekuwa mbaya kuliko zote zilizotangulia. Hii ni kwa sababu zifatazo:
  1. Viogozi wake wamo katika honeymoon ya MUAFAKA na hivyo kila kitu hakiwezekani kwa katika honeymoon ugomvi wa wapenzi hautakikiwi.
  2. Ni Serikali pekee amayo hakuna mpaka wa Serikali inayotawala na Upinzani. Keleleza Back benchers ni swa na kelele za Mlango hazimzuiliii mwenye nyumba kulala. Ivi sasa tayari wameanza kuitoa kasoro ripoti ya TUME ya Omar Ali Shehe wakidai kuwa ina kasoro nyingi.
  3. Serikali hii inaongozwa na viongozi wanaogopa wanawaongoza. Ivi sasa kaulli ya Rais si chochote mbele ya baadhi ya Makatibu wakuu. Baya zaidi ni kuwa Serikali iliyomo mmadarakani ni masikini kuliko watumishi wake. Baadhi watumishi wake wanaendesha miradi mikubwa kuliko Serikali yenyewe.
  4. Serikali hii imeundwa na Katiba ambayo ili kubali kukompromise ili MUAFAKA upatikane. Vyama vyote vilivyounda Serikali viliiingia tuu kichwa kichwa huko Serikali yao ikiachwa bila nguvu za Kikatiba kusema nane aongoze. Mkuu wa Mkoa ashindwapo kuwatumikia watu ni mfano mzuri.
  5. Serikali inakasoro nyingi za kupita kiasi na haya ya kiongozi kusema hili na wafuasdi kusema lengine ni reflection ya kasoro hizo!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s