Yasemwayo kuhusu Muungano yasikilizwe

Rais Jakaya Kikwete, akisalimiana na Makamu wake Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati akiwasili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam leo Aprili 26, 2012 katika sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Ahmed Rajab

LEO tarehe 26 Aprili Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, yaani Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utatimiza miaka 48, ukikaribia nusu karne.  Huo si umri mdogo. Bara siku hiyo itasherehekewa rasmi.  Zanzibar itapita tu huku wengi wa wananchi wake wakiwa wanaguna na kujiuliza kwa muda gani Muungano huo utaendelea kuwako kama hivi ulivyo katika muundo wake wa sasa.

Kwa namna tunavyoiona hali ya mambo ilivyo hivi sasa Visiwani wananchi wa moto na hakuna suala kubwa la kisiasa linalowashughulisha zaidi ya hili la Muungano.  Haya yanaonekana bayana unaposikiliza maoni ya wananchi katika majukwaa ya kuhamasisha watu katika mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri hiyo na pia katika majukwaa ya mawasiliano ya kijamii.

Serikali inaweza kuyapuuza maoni hayo na inaweza pia ikatumia mkono wa chuma katika jaribio la kuyazima maoni hayo.  Ikifanya hivyo itafanya kosa kubwa sana.  Si tu kwamba itakuwa inakwenda kinyume na maadili ya utawala bora na kwamba itakuwa inawanyima wananchi haki na uhuru wao wa kutoa mawazo wayatakayo lakini pia itahatarisha amani.  Mrindimo na mngurumo uliopo sasa Visiwani kuhusu Muungano hauwezi kuzuiwa kwa matumizi ya nguvu.

Lakini wenye maoni ya kuupinga muundo wa Muungano kama ulivyo hivi sasa nao pia wana jukumu la kuendesha kampeni zao kwa njia ambazo hazitotishia amani.  Wakifanya vitendo vyenye kukiuka sheria au hata wakianza kutumia matusi katika hoja zao huenda wakahatarisha mengi zaidi ya amani na hali ya utulivu.

Mwenye macho haambiwi tazama na mwenye masikio hawezi kuepuka kuyasikia maoni ya Wazanzibari dhidi ya muundo wa sasa wa Muungano na mengine dhidi ya kuwako kwa Muungano wenyewe.  Maoni haya yanasikika kutoka kwa wanachama wa vyama vyote vya kisiasa nchini humo na pia hata kutoka kwa wale wasio wanachama wa vyama vya kisiasa au hata wasiopendelea kwa kawaida kuzijadili siasa.

Wapo bila ya shaka Wazanzibari wanaopendelea Muungano uliopo uendelee vivi hivi ulivyo na wasioona kuwa kuna dosari kubwa yoyote katika mahusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar isipokuwa ‘kero’ za hapa na pale zinazoweza kuondoshwa kwa mashauriano kati ya pande mbili za Muungano.  Watu wenye fikra kama hizi wapo lakini ni wachache Visiwani.

Ukiwadadisi Wazanzibari utang’amua haraka kwamba wengi wao wanahisi ya kuwa kuwapo kwa Muungano kumezidi kuyaathiri vibaya maisha ya Wazanzibari wa kawaida.  Ukiwauliza kwa nini watakupa hoja aina kwa aina — pamoja na zile ambazo pengine haziingii akilini.  Wanavyofikiri wao ni kwamba matatizo yao ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii yamezidi kuwa mawi kwa nchi yao kuungana na Tanganyika.  Kwa upande wa pili, kuna Watanganyika wasemao kwamba nao wamechoka ‘kuibeba’ Zanzibar na ikiwa Wazanzibari wanataka kujitoa kwenye Muungano basi nawatoke watokomee mbali.

Kwa ufupi, hoja kubwa inayotumiwa na Wazanzibari ni kwamba wanahisi ya kuwa nchi yake imemezwa na Tanganyika. Na ilipomezwa ikapokonywa madaraka yake kamili ya kuendesha shughuli zake za kiuchumi, kijamii na za kisiasa.  Zanzibar haiwezi kuchukua hatua yoyote ya maana kuhusu mustakbali wake bila ya kupata idhini ya Bara.  Hivyo ndivyo wanavyohisi.

Pili, wanatambua kwamba yale yaitwayo ‘Mambo ya Muungano’ ndiyo yanayotumiwa na serikali ya Tanzania (kwa maana ya Bara au Tanganyika) kuikalia kichwani Zanzibar.  Kinachozidi kuwaudhi ni kuona kwamba hayo ‘Mambo ya Muungano’ yameongezwa kutoka 11 na kufikia idadi ya 22.

Sasa Wazanzibari wamemaizi kwamba  kwa vile wana umoja wa kisiasa na kuna utulivu nchini mwao wana kila haki ya kudai warejeshewe mamlaka yaliyoporwa na serikali ya Muungano.  Wanachotaka ni kurejeshwa tena Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyotoweka mwezi Aprili mwaka 1964 baada ya Muungano kuundwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.  Hiyo hatua iliyochukuliwa tarehe 26 Aprili mwaka 1964 na marais hao wa Tanganyika na Zanzibar hii leo inakosolewa sana Zanzibar kwani inaonekana kuwa ni hatua iliyokwenda kinyume na maslahi ya kitaifa ya Zanzibar.

Hizi si hisia za leo na jana. Ni hisia zilizokuwepo tangu siku ya mwanzo ya kuundwa kwa Muungano.  Hata akina sisi twenye kupigania nchi za Kiafrika ziungane na ziwe na umoja, tukitetea itikadi ya ujumuiya wa Afrika (pan-Africanism), pia tulikuwa na shaka kubwa.  Tukiamini kwamba Muungano uliundwa kwa papara na si kwa muundo ambao ungezishajiisha nchi nyingine barani Afrika ziwe na hamu ya kujiunga nao.

Ingawa juujuu uliweza kutumiwa kuwa ni mfano wa nchi zilizoungana kwa nia ya kuleta umoja wa Afrika, kwa hakika undani wake ulidhihirisha mapema kwamba utakuwa kikwazo cha kuleta umoja uliokuwa ukitetewa na watu kama kina Kwame Nkrumah wa Ghana.

Kwa jumla, wengi wa Wazanzibari wamekuwa wakiupinga Muungano kwa sababu wanahisi ya kuwa haujawaletea manufaa yoyote ya maana kwa upande wa kisiasa, kiuchumi au kijamii.  Kadhalika, hata wale wachache wenye kuutetea Muungano wanasema kwamba wanaupinga muundo wake wa sasa.

Hiyo ndiyo halisi ilivyo leo Visiwani.  Hali hiyo itazidi kujidhihirisha wakati wananchi watapowasilisha maoni yao kwa Tume ya Katiba katika mchakato wa kutafuta katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.  Ndiyo maana hivi sasa  Wazanzibari wanaliona zoezi la kuiandika upya Katiba ya Muungano kuwa ni lenye kuwapa fursa ya kuzidai haki zao za kurejeshewa madaraka yao.

Wanavyotaraji ni kwamba patatokea mageuzi makubwa ya kimsingi kuhusu hadhi ya Zanzibar na nafasi yake katika Muungano au nje ya Muungano.  Kikubwa wanachodai ni kwamba kama Muungano uwepo basi uwe ni Muungano wa Mkataba na si wa Katiba.

Ingawa ni vigumu kwa sasa kuweza kutabiri jinsi mchakato huo utavyoendelea na nini matokeo yake yatavyokuwa, lakini tukiyakumbuka yaliyojiri kwenye mikutano mbalimbali, kongamano na mihadhara iliyohudhuriwa na umati wa watu tunaona kwamba Wazanzibari wote hao wamekuwa na kauli moja wakiifuata ajenda moja.

Wanachosema ni kwamba wanataka muundo wa sasa wa  Muungano ubadilishwe na kwamba Zanzibar na Tanganyika ziungane kwa  kutumia mkataba baada ya Zanzibar kuyatwaa tena mamlaka yake ya kuiwezesha kujiamulia mambo yake.

Ni muhali kuweza kuendelea na mchakato wa sasa wa kuijadili na kuichambua Katiba ya Muungano bila ya kuwa na majadiliano ya maana na ya kijituuzima kuhusu muundo wa Muungano.  Majadiliano hayo hayaepukiki hasa miongoni mwa Wazanzibari. Hayaepukiki kwa sababu Wazanzibari wamekwishaanza kuuliza swali la kimsingi: mchakato huu utakuwa na maana gani iwapo wananchi watazuiliwa kuujadili Muungano?

Kwanza, tayari suala hilo limo midomoni mwa wananchi kufika hadi ya kuwapandisha jazba. Pili, vijana wa leo, wakike na kiume, wengi wao waliozaliwa baada ya kuundwa Muungano wanasema wanataka kuona mageuzi makubwa yanatokea nchini mwao yatayowawezesha Wazanzibari wajiamulie mambo yao yenyewe.

Wapo pia Wazanzibari wenye msimamo mkali wenye kushikilia kwamba kabla ya mchakato huu wa katiba kuendelea kwanza pangepigwa kura ya maoni Visiwani Zanzibari kuhusu Muungano wenyewe. Wanachotaka ni kwamba Wazanzibari wangeulizwa iwapo wanautaka au hawautaki Muungano na kama wanautaka ni Muungano wa aina gani wautakao.

Kwa maoni ya wengi endapo kura ya maamuzi ya aina hiyo itatayarishwa leo Visiwani na Wazanzibari watakuwa na uhuru kamili wa kuamua basi wengi wao wataukataa Muungano kama ulivyo sasa.
Huu ni mtihani mkubwa kwa serikali zote mbili za Tanzania — ile ya umoja wa kitaifa huko Zanzibar na ya Muungano jijini Dar es Salaam.  Panahitajika hekima na si mabavu kuyatathmini maoni ya walio wengi na kutafuta njia za kuwaridhisha.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

7 responses to “Yasemwayo kuhusu Muungano yasikilizwe

  1. Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia rehma mtume wetu MuhammadS.A.W Napenda kutoa pole kwa wazanzibar kwa hudhuni zilizotujaa nyoyoni mwetu cku ya leo. Pia nakupongeza kaka yetu sheikh ahmed rajab kwa kuweza kuakisi fikra za wazanzibar juu ya hii dhulma ya muungano kwa ustadi mkubwa bila ya kutia chumvi. Huu ndio ukweli na hauwezi kupingika. Wazanzibari tunayo fursa ya kujikwamua na balaa hili pasi na umwagaji wa damu, wala utumiaji jazba na nguvu zisizoelekezi. Busara, elimu , ujuzi, umoja, ari na kutokata tamaa vitatuvusha! Mifarakano, vijembe, fujo, shitizai na kukosa uzalendo vitatuangusha.! Zanzibar ni moja! Kwa moyo mmoja! Tuweni pamoja! Allah atatuwezesha . Amin!

  2. Wazanzibar tuwe macho mno na hawa tunao ambiwa ni ndugu zetu wa damu! Nakumbuka kipindi fulani nilikuwa huko tanganyika kuna jamaa mmoja akaniuliza hivi wazanzibar munaweza kujiendesha kama nchi. Ni kamjibu ndio tena bila ya wasiwasi wowote! Akacheka sana na akajibu hivi sisi watanzania tutawaichia nyinyi mujitawale ikiwa sisi tuko macho huku akiendelea kucheka! Uchungu uliopata moyo ulipiga! Lakini habar ndio hiyo usipuuze mzanzibari!

  3. Kila mzanzibari halisi siku ya leo ni siku ya kua na HUZUNI kubwa kwani ndio siku ambayo nchi yetu ilinakamizwa katika hili jinamizi ambalo mpaka leo linaitafuna. Wenzetu tulioungana nao wamefanikiwa kueka watawala mapandikizi akina Dr Shein, Balozi Iddi, Mohd Aboud na wengineo kama hao ambao njaa zao zinawafanya wawe ni wasaliti wa wazanzibar wenzao. Muungano huu kila mmoja anajua kua haufai. Hata Kiwete anajua hivyo lakini kwa kua wanafuata wosia wa BABA inabidi waulazimishe. Napenda kutoa angalizo kua kwa hapa tulipofikia hata mkatumia mbinu gani Wazanzibari hatutaki tena muungano huu kwani tumeshaona madhila yake. Muungano huu ndio sababu ya matatizo yote ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayoikumba Zanzibar leo. Kama kweli mmungano huu ni mzuri kama wanavyodai inakuaje leo miaka 48 mpaka leo hakuna hata nchi moja angalau iliyooomba kujiunga? Kijografia muungano baina ya nchi yenye watu milioni 1.5 na yenye milioni 45 hauna uwiano nadhani ni vyema Tanganyika ikaungana na Congo, au Uganda au hata Kenya na ikaiacha Zanzibar ikawa huru.

  4. Pingback: Yasemwayo kuhusu Muungano yasikilizwe·

  5. jambo lolote lile, kama halikuwa na msingi mzuri na nia safi ,basi huu ndio mwisho wake!! watazuwia , lakini mpaka lini? Allahu yaalaam !!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s