BURIANI: Dk Yussuf daktari aliyepigania haki na demokrasia

Wa Lillahi Inna Ilayhi Rajiun, Kwa mujibu wa taarifa nilizozipata alfajiri ya leo kutoka France kwa Bw. Mohammed Saleh ni kuwa Dk Yussuf Salim Saleh amefariki dunia katika hospitali ya Copenhagen huko Denmark, Tutakumbuka kwamba Dk Yussuf ni miongoni mwa wazanzibari mwenye kuumwa na kuitetea Zanzibar kwa hali na mali umri wake wote amekuwa aikitumikia nchi yake.Yarrabi upokee mwili huu . Insha'Allah Allah amlaze mahali pema peponi Ameen.

 Ahmed Rajab

 WATETEA haki, hususan wale Wakizanzibari, wana kilio. Hiki ni kilio cha msiba uliowagusa wengi wa Wazanzibari walio nje na ndani ya nchi.  Ni kilio cha kuondokewa na mmoja wa majasiri wao, Dakta Yussuf Saleh, aliyefariki dunia mjini Copenhagen, Denmark, alfajiri ya Jumamosi iliyopita.

Moja ya alama za ujasiri wake ni ushujaa aliouonyesha kwa namna alivyokuwa akiishi na ugonjwa wa saratani aliougua kwa muda wa miaka kadhaa na uliokuwa sababu ya kifo chake. Mauti yake yamewapokonya Wazanzibari mtu aliyejitolea mhanga kupigania maslahi yao. Mchango alioutoa katika mapambano hayo hausemeki; ulikuwa mkubwa mno. 

Ulikuwa ni mchango wa fikra, wa mbinu na mikakati, wa hali na mali.  Atakumbukwa hata na vizazi vijavyo kuwa ni mpiganiaji asiyeteteleka wa haki za Wazanzibari.

Yussuf alizifuata nyayo za akina Agostinho Neto wa Angola, George Habash wa chama cha ukombozi wa Wapalastina cha PFLP na Mzanzibari mwenzake Dakta Said Himidi, nikiwataja matabibu wachache tu wanaonijia kichwani waliokuwa pia wanaharakati wa kupigania haki na kuondosha dhulma.

Ukarimu wake na moyo wake wa kujitolea ulikuwa wa kupigiwa mfano. Kwangu alikuwa rafiki tuliyeheshimiana, ndugu na komredi mwenzangu kwa vile alikuwa mfuasi wa chama cha zamani cha Umma Party cha Zanzibar. Kwa muda wa miaka chungu nzima tulikuwa tukishirikiana, pamoja na wenzetu wengine walio ughaibuni na nyumbani, katika harakati mbalimbali zinazohusu majaaliwa ya Zanzibar. Zanzibar ndiyo iliyotuleta pamoja na Yussuf alikuwa na uchungu na nchi yake.

Saa nyingine Yussuf alikuwa mkaidi, akipenda kushindana na kubishana tangu utotoni mwake. Akishikilia msimamo ilikuwa huwezi kumyumbisha. Akitumia mizaha kukupiga vijembe lakini daima moyo wake ulikuwa safi.

Niliongea naye mara ya mwisho siku chache tu kabla hajafariki, nikipata taabu kumsikia kwa vile sauti yake ilikuwa inafifia. 

Nilimuona mara ya mwisho Juni 2009, akiwa na umbo lililokuwa tayari limedhoofishwa na maradhi yaliyokuwa yamemsibu. Tulikutana katika tawala ya kifalme ya Sharjah wakati nilipokuwa nikiutumikia Umoja wa Mataifa huko Dubai na yeye alipokuwa ziarani. Nilifunga safari kwenda Sharjah alikoalikwa chakula cha usiku.  Ingawa sikualikwa niliuchuna uso nikapandia kwenye karamu aliyoandaliwa ili nimuone na kusikiliza fikra zake.

Siku hizo chumi za nchi za Magharibi zilikuwa zimepata mshtuko wa ghafla ambao uliutikisa pia uchumi wa Dubai, Iraq ilikuwa hamkani, mapigano Afghanistan yakiendelea, Palestina kukizidi kuwaka moto na mengi yakitokea barani Afrika. Yussuf lakini hakuyaweka hayo mbele. Takriban yote aliyoyazungumza yalihusu Zanzibar na kama ilivyokuwa kawaida yake alikuwa na fikra na rai mbalimbali za namna ya kuisaida nchi yake.

Alikuwa ni mtu niliyekuwa nikimfahamu tangu utotoni mwetu.  Mama zetu walikuwa walimu. Wangu akisomesha shule ya wasichana iliyokuwa Forodhani na mama yake akisomesha shule ya Kikwajuni Mixed School ambayo ilikuwa marufu kwa jina la ‘Kwa Msellem’.  Ilikuwa ni shule ya mwanzo ya serikali visiwani Zanzibar kuwa na wanafunzi mabanati na wavulana waliokuwa wakisoma pamoja.

Ingawa Yussuf alinizidi umri kidogo tulijikuta sote tumeingizwa darasa moja katika skuli ya Kwa Msellem.  Waalimu wetu wote walikuwa wanawake wakiwa chini ya Mwalimu Mkuu Bi Zainab Himidi, mmoja wa wataalamu wakuu wa mambo ya elimu nchini na mshairi mahiri.

Mwanafunzi mwenzetu mwingine tuliyekuwa naye darasa moja na aliyeondokea pia kuwa na itikadi ya mrengo wa kushoto ni Salim Msoma, katibu mkuu mstaafu katika wizara ya mawasiliano na uchukuzi katika kipindi chote cha utawala wa rais Benjamin Mkapa.

Mbele yetu walikuwako wengine wawili waliokuja kuzikumbatia siasa za mrengo wa kushoto.  Mmoja alikuwa  Ali Mohamed Said, ambaye ukubwani mwake alikuwa China kwa muda wa miaka kadhaa, na Salim Himidi, nduguye mwalimu wetu mkuu na aliyekuja kuwa waziri katika serikali mbalimbali za Comoro.

Hatukudumu wa muda mrefu kwenye skuli hiyo kwani mara ilifungwa na wanafunzi wake tukagawanywa na kupelekwa katika shule nyingine mbalimbali huko huko Unguja kwa masomo ya msingi.

Yussuf lakini alimfuata mamake na kwenda Pemba alikoingia shule ya msingi ya Michakaini huko Chake Chake. Baada ya hapo akarudi Unguja na akaingia shule ya msingi ya Kizimkazi, kwenye ncha ya kusini ya Unguja na halafu akasoma shule ya Gulioni, Unguja mjini.

Alipomaliza darasa la nane huko Gulioni aliingia shule ya Aga Khan, iliyokuwa Saateni hapo hapo Unguja. Wakati huo Yussuf alikuwa amekwishaanza kuvutiwa na siasa za mrengo wa kushoto zilizokuwa zikihubiriwa na Abdulrahman Babu aliyekuja baadaye kuwa mwenyekiti wa Umma Party.

Itikadi ya chama hicho ilijengeka juu ya msingi wa nadharia za Karl Marx hasa zile zilizokuwa zikiemelea mafundisho na fikra za Mwenyekiti Mao wa China.

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 12 Januari mwaka 1964, Yussuf alipelekwa Budapest, Hungary, kusomea udaktari. Hakumaliza masomo yake kwani aliyakatiza mwaka 1967 na akarudi Tanzania. Baada ya muda alipata kazi kwenye Ubalozi wa Cuba, mjini Dar es Salaam.

Alifanya kazi katika ubalozi huo hadi 1972 alipokamatwa na kuwekwa kizuizini pamoja na kaka yake Meja (Mstaafu) Salim Saleh kwa kuhusishwa na mauaji ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Sheikh Abeid Amani Karume.

Aliachiwa kwa muda halafu akakamatwa tena na akaselelea jela ya Ukonga, mjini Dar es Salaam, mpaka alipofunguliwa mwaka 1974.

Kama wenzake wengine waliokuwa kizuizini kwa kuhusishwa na mauaji ya Karume, Yussuf alikuwa akipiganiwa na shirika la haki za binadamu la Amnesty International lililokuwa likifanya kampeni kubwa ya kimataifa kutaka wafungwa hao waachiwe huru.

Alipofunguliwa alikwenda Denmark alikoomba hifadhi ya kisiasa na akapewa bila ya bughdha yoyote. Tangu wakati huo akawa mkimbizi akiishi uhamishoni alikovuta pumzi yake ya mwisho.

Kadhalika Denmark ilimpa Yussuf fursa nyingine ya kuerejea chuoni kwa masomo ya udaktari.  Kwanza alisoma lugha ya Kideni na halafu akaanza upya kusomea udaktari. Hatimaye alibobea katika tanzu ya magonjwa ya moyo. Alipohitimu masomo yake ya udaktari alifanya kazi nchini Denmark na pia katika nchi za Norway na Sweden.

Aliwapandisha vichwa Waafrika, hasa Watanzania, walipomuona akihojiwa kwenye televisheni ya taifa ya Denmark kuhusu uchunguzi wake wa maradhi ya ukimwi.

Wakati wote huo hadi kufariki kwake, toka anasoma mpaka akiwa anafanya kazi na kuiangalia familia yake na kuwalea wanawe, Yussuf daima alikuwa mbioni. Alikuwa hapumui kujitumbukiza katika harakati mbalimbali za kisiasa.

Miongoni mwa harakati hizo ni uwanachama wake wa Dantan (Umoja wa Kirafiki Baina ya Denmark na Tanzania.) Ingawa lilipoanzishwa vuguvugu la Harakati za Kuleta Maendeleo ya Kidemokrasi (HAMAKI), chini ya uwenyekiti wa Babu huko Malmo, Sweden, Desemba 1989 Yussuf hajakuwako mkutanoni, baadaye alikuwa mwanaharakati wake thabiti na hatimaye kuliongoza vuguvugu hilo.

Baadaye akachaguliwa kuwa katibu mkuu wake lakini mwishowe alilipa mgongo vuguvugu la HAMAKI, hasa tangu pale vuguvugu hilo lilipoanza kufifia kutokana na harakati mpya zilizoanza Zanzibar ambapo HAMAKI ikishirikiana sana na chama cha CUF.

Yussuf pia ni mmoja wa waanzilishi wa Umoja wa Wazanzibari Skandinavia na ndiye aliyeandika muswada wa mwanzo wa katiba ya umoja huo. Alichaguliwa kuwa katibu wake wadhifa alioushika kwa muda wa miaka mingi mpaka alipobadilishwa na pahala pake kuchukuliwa na Hamed Hilal.

Harakati za umoja huu za kupigania haki za Wazanzibari zilikuwa zikiwanyima usingizi viongozi wa serikali na wa chama cha CCM hata baadhi yao kukwepa kwenda Denmark na kama ikibidi basi wakenda kwa kificho.

Yussuf hakuwa mshiriki katika siasa tu bali hata katika vyama vya mipira vya Wazanzibari vilivyokuwepo Denmark pia alikuwa akishiriki kikamilifu kwa kuamini kwamba kila njia ifanyike ili kuwaleta pamoja Wazanzibari.  Utotoni mwake alikuwa mshabiki mkubwa wa mpira akichezea timu ya Raha Leo pamoja na akina Enzi Talib na Shaaban Salim.  Katika mwisho wa uhai wake akizungumza sana na Shaaban Salim kuhusu haja ya kuifufua tena timu yao.

Kwa muda wa miaka mingi Yussuf alikuwa akisaidia kutafuta madawa na vifaa mbalimbali vya hospitali na kupeleka Zanzibar, hata hali yake ya kiafya ilipokua mbaya sana bado akenda mahospitalini kutafuta vifaa ili apeleke Zanzibar.

Kadhalika alikuwa mwenyekiti wa vuguvugu la Mustakbali wa Wazanzibari (MUWAZA) jumuiya ambayo moja ya malengo yake ni kulirudisha  suala la Muungano kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho.

Alikuwa wa mwanzo miongoni mwa Wazanzibari walioko nje walioliunga mkono na kulisaidia vuguvugu la KAMAHURU lililoizaa CUF. Alifanya juhudi kubwa ya kuifanya HAMAKI ikishirikiana na CUF iwe mwanachama wa Jumuiya ya Nchi na Watu Wasio na Uwakilishi (UNPO) yenye makao yake makuu mjini Hague, Uholanzi.

Kwa muda baada ya Zanzibar kuingizwa kwenye Jumuiya hiyo, uwenyekiti wake ulishikwa na Maalim Seif Sharif Hamadi ambaye sasa ni makamu wa kwanza wa Rais katika serikali ya umoja wa kitaifa huko Zanzibar.

Yussuf akiongoza kwa kuonyesha mifano mema. Moja ya hiyo ni mkono wake usiokuwa ukibania. Hakuwa akitaka sifa na mara kadha wa kadha akitoa fedha kusaidia Zanzibar bila ya kutujulisha wenzake. Nadhani lau angeweza kuifanya nafsi yake isijuwe kwamba ametoa mchango fulani au amemsaidia mtu fulani basi angalifanya hivyo.

Mawazo yake kuhusu Zanzibar yamo kwenye kitabu alichokiandika  ZANZIBAR DOLA, TAIFA NA NCHI HURU

Dakta Yussuf alioa mara mbili.  Mara ya kwanza alimuoa bibi mmoja mwananchi wa Hungary aliyezaa naye watoto watatu.  Chuo chake cha pili kilikuwa na Bi Nadra Nassor aliyezaa naye watoto wanne.

Chanzo: Gazeti la Raia Mwema 

.

 

Advertisements

9 responses to “BURIANI: Dk Yussuf daktari aliyepigania haki na demokrasia

 1. kila kilicho umbwa kitaocha umauti,NIMEPOKEA KWA MASIKITIKO MAKUBWA MNOO KIFO CHA MKOMBOZI HUYU MUNGU MUNGU AMJAALIE FIRDAUS NUZULAA, MUNGU AMJAALIE ULEZI MZURI NA USIMAMIZI NA KHIFADHI NZURI YA KIZAZI CHAKEE MUNGU AKISIMAMIE ULIZI KIZAZI CHEKE, NIKIMPENDA SANA KIONGOZI HUYU HASA PALE TULIPOKUWA TUKICHATI KWENYE MTANDAO WA KIJAMII WA FACEBOOK EWE MUNGU MUJAALIE FIRDAUS NUZULAA

 2. Inna lillah wa inna illayhi raj uun Insha allah Mwenyezi Mungu atamjaalia awe ni mtu wa peponi pamoja na masahaba. Alikua mstari wa mbele katika ukombozi wa Zanzibar. Kazi ya M.Mungu haina makosa.

 3. Leo tumeondokewa na mmoja katika wanaharakati wakubwa waliosimamia na kupigania Uzanzibari na kupigania maslah ya Zanzibar. Mola amsamehe makosa yake na amlaza pema peponi. Amin. Inna Lillahi wa Inna Illahi Rajiuun.
  Kutoka Copenhagen.
  Said Juma Mohamed

 4. this is a very sad news of doctor yusuf may god rest his soul in peace…he was a good person & my condonlence to his wife & children & family.. …….may allah rest his soul in peace….brown veve shirazi & family

 5. Ya RABBI ipokee roho yake kwa mapenzi makubwa na ihifadhi. Naikumbuka sana makala yake ya barua ya wazi kwa baraza la wawakilishi ya trh 5apr ni barua iliyojaa uzalendo mkubwa. Dk umekwenda tutaendela kukuunga mkono hadi tone letu la damu ya mwisho. Zanzibar yetu kwanza.

 6. Innalilah wainnailaih raju’un. YAA RAB MUEKE MAHALIPEMA PEPONI MZALENDO WA ZANZIBAR HUYU. Ninatoa mkono wa pole kwa ndugu jamaa na marafiki wa marehemu huyu. TUPO PAMOJA KATIKA KIPINDI HICHI KIGUMU CHA MAOMBOLEZO. Marehemu alikuwa mstari wa mbele katika harakati za kudai UHURU WA ZANZIBAR kutoka mikononi mwa MAKAFIRI WEUSI WA TANGANYIKA.

 7. Ya Rabbi Mola wa kila kitu usie na mfano msamehe mja wako huyu hakika yeye ametangulia na sisi tutayaonja mauti kwa rehema zako mlaze pahala pema na wako wema… Amina hakika alikuwa mfano kwetu na daima sisi vijana wa kizanzibari tutafata nyayo zake hatutopuuza kamwe mawazo yake na bila ya shaka kwa uwezo wa Allah nchi yetu ya Zanzibar itakapopatikana kwenye mikono ya watanganyika.

 8. Isikitisha kuwa Dr. Yussuf amefia ugenini kwa kuwa hapa kwao ajira zinatolewa kwa kadi za Chama au Uzawa au ukereketwa au uzawa. Mungu mlaze mahali pema shujaa huyu. Yeye hafananani na Mafisadi 100 walio Unguja ambao pamoja na kuiba kupita kiasi wanaonekana wakifatana na Rais wetu bila yeye mwenyewe kujua kuwa watu wachafu kufatana nao kunamchafulia heshima yake naye!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s