Watumishi hewa wasakwa serikalini

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala bora, Haji Omar Kheri akifanya majumuisho katika kikao cha baraza la wawakilishi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeahidi kuwatafuta wafanyakazi hewa ‘Gost Workers’ katika taasisi zake  na mashirika ya umma na kuwachukulia hatua za kisheria watakaobainika na vitendo hivyo. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala bora, Haji Omar Kheri amewaambie wajumbe wa baraza la wawakilishi jana wakati akifanya majumuisho ya ripoti ya kamati ya kuchunguza na kudhibiti hesabu za serikali na mashirika ya (P.A.C) ya mwaka wa 2011/2012 kuhusu ufuatiliaji hoja za ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu wa ya mwaka 2008.2009.

Alisema zoezi la kuwatafuta wafanyakazi hewa wa serikali ilianza mwezi uliopita kwa watumishi wote kuhakikiwa upya na kutakiwa kuleta vieleelzo vyao ikiwemo kupokea mishahara yao wizarani kupitia kwa wahasibu.

“Mheshimiwa Spika kazi ya kuwahakiki watumishi wa serikali imeanza na tunataka kujuwa idadi yao kamili na kutafuta watumishi hewa, pia tunawatafuta wale watumishi wanaopokea fedha mara mbili pamoja na wale ambao wamefariki lakini wameingizwa katika mtandao wa mishahara na wanalipwa licha ya kuwa wapo makaburini” alisema.

Aidha Kheri alisema kazi hiyo ilianza kwa wizara ya miundombinu na mawasiliano, wizara ya elimu na mafunzo ya amali na wizara ya kazi na uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuendelea katika wizara nyengine za serikali.

Aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba kazi hiyo inaendelea hadi hapo serikali itakapojiridhisha na kuahidi kwamba zoezi hilo litakuwa endelevu kwa lengo la kuweka mipango mizuri ya maendeleo ya nchi na uwajibikaji.

Kheri alisema kwa sasa zoezi la kuhakiki watumishi wa Serikali lipo katika vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vya JKU, Vyuo vya Mafunzo, kikosi cha Zimamoto, KMKM na Valantia.

Waziri huyo alisema lengo la serikali kuamua kufanya uhakikia huo kwa wafanyakazi ni kuona kwamba hakuna mtumishi anayepokea fedha kinyume na utaratibu wa sheria za utumishi serikalini.

Aaliwaahidi wajumbe hao wa baraza kwamba uchunguzi zaidi wa kuweza kuwatambuwa watumishi hewa wanaochukuwa mishahara kinyume na sheria unaendelea na taarifa kamili zitatolewa mara zoezi hilo litakapomalizika.

Alisema mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali kuchukuwa juhudi za makusudi kuijengea uwezo taasisi hiyo ambayo ni moja ya eneo la utawala bora katika kuendesha shunguli za Serikali.

Mshimba aliomba radhi baraza la wawakilishi.

HATIMAE Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM) Makame Mbarouk Mshimba jana ameliomba radhi Baraza la Wawakilishi hatua ambayo ni utekelezaji wa agizo alilopewa na Spika wa baraza hilo Pandu Ameir Kificho wiki iliyopita.

Mbali ya kuliomba radhi baraza Mshimba pia amewaomba radhi wananchi wa Zanzibar na kumuomba radhi Spika wa baraza hilo kwa kushindwa kuwasilisha ripoti yake ya Mawasiliano na Ujenzi ya baraza la wawakilishi ambapo wakati akitajwa Mwenyekiti wa kamati hiyo kuja kuwasilisha ripoti yake hakuwepo barazani.

Awali Spika Kificho mbele ya wajumbe wa baraza lake aliisoma barua iliyoandikwa na Mshimba akisema anawaomba radhi sana baraza na wananchi kutokana na kitendo hicho kilichotokea cha kushidnwa kuwasilisha ripoti yake kutokana na kudharurika siku hiyo.

Mshimba alisema sababu kubwa iliyomkwamisha kufika katika kikao hicho ni kupata matatizo ya kiafya kutokaa na kuwa alikuwa akiumwa na tumbo lakini alichokosea ni kule kushindwa kuliarifu baraza na kumuarifu Spika juu ya tukio hilo.

“Mheshimiwa Spika nilidharurika siku ile ambayo nilitakiwa kuwasilisha ripoti ya kamati yangu, kwa kweli nilikuwa nikiumwa na hivyo kushindwa kuhudhuria katika kikao nilikuwa nikiumwa na tumbo na kwa bahati mbaya nilishindwa kukuarifu na pia nilighafilika kwani sikuweza kumpa taarifa hiyo mjumbe mwengine yeyote” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyowasilishwa kwa Spika.

Katika barua yake Mwakilishi huyo aliahidi kwamba kitendo kilichotokea kitakuwa ni cha mwisho na hakitojirudia tena katika uhai wa Baraza la Wawakilishi.

Spika Kificho aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kiwamba barua ya Mwakilishi huyo imempa matumiaoni hasa pale alipoahidi kwamba atahakikisha kitendo hicho hakitajirudia tena katika uhai wake.

Katika kuhakikisha suala hilo halitokezei tena Spika aliwakumbusha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na mawaziri kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuzingatia wajibu wao wa kuwawakilisha wananchi.

Spika aliwataka wajumbe hao kuweka utaratibu mzuri na kufuata kanuni zilizowekwa na baraza hilo kwani wananchi wengi wanafuatilia vikao hivyo lakini pia umakini wa chombo hicho muhimu cha kutunga sheria kinategemea na uwajibikaji wa wajumbe wake ambao ni wawakilishi na mawaziri.

Hivi karibuni Spika wa Baraza la Wawakilishi alikasirishwa na kitendo cha Mwenyekiti wa kamati ya Mawasiliano na Ujenzi, Makame Mshimba Mbarouk ambaye alishindwa kuwasilisha ripoti ya kamati hiyo kutokuwepo katika kikao hicho bila ya kutoa dharura kwa Spika.

Spika alimtaka Mwakilishi huyo aliombe radhi baraza la wawakilishi na wananchi kutokana na kuwa wananchi wanafuatilia vikao hivyo na wanataka kuona uwajibikaji na umakini wa chombo hicho.

“Waheshimwia wajumbe wa baraza la wawakilishi tunatakiwa tuwe makini sana wakati tukiendesha shunguli za baraza la wawakilishi zaidi katika kipindi hichi ambapo mijadala hii imekuwa ikirushwa hewani moja kwa moja na vyombo vya habari, wananchi wanataka kujua kila kinachoendelea hapa barazani” alisema Spika.

Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na Zanzibar Cable zimekuwa zikirusha moja kwa moja matangazo ya vikao vya baraza la wawakilishi ambapo wananchi wengi wamekuwa wakifuatilia kwa umakini vikao hivyo.

Udanganyifu wakosesha wafanyakazi fedha za likizo

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyakazi umechangia kuvuruga utaratibu wa kuwalipa wafanyakazi fedha za likizo.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji alisema hayo jana wakati akijibu maswali katika kikao kinachoendelea Chukwani Mjini hapa.

Alisema kuwa hali hiyo ilisababisha serikali kuwa na utaratibu wa kuwalipa fedha hizo baada ya kutoka katika likizo zao.

Duni alikuwa anajibu swali la Panya Ali Abdalla Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake (CCM)  aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kulipa deni la fedha za likizo kwa wafanyakazi wa wizara ya afya.

Mwakilishi huyo alisema kutolipa deni hilo kwa wafanyakazi kutapunguza moyo na ari kwa wafanyakazi kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Akijibu hilo la kutokuwepo ufanisi wa kazi Duni alisema “Wizara yangu inalielewa hilo na inaweza ikawa ni sababu moja wapo ya kupunguza ufanisi wa kazi”.

Waziri Duni alisema chanzo ni udanganyifu miongoni mwa baadhi yao pamoja na ukosefu wa fedha kwa upande wa serikali.

Alisema sababu za kutolipwa fedha za wafanyakazi kabla ya kwenda likizo ni huo udanganyifu unaofanywa na watumishi hao wa umma ambao wanaidanganya serikali.

“Mheshimiwa Spika ni kweli wafanyakazi wengi hawajapata fedha za likizo,  hii imetokana na kutokuwa na mpango endelevu wa malipo hayo, kubwa zaidi kuliko yote ni kulikuwa na udanganyifu wa kupindukia na ufinyu wa fedha kutoka serikalini” alisema Waziri huyo.

Alisema upungufu huo ulisababisha utekelezaji wa haki hiyo kwa wafanyakazi kutolewa kwa misingi ya upendeleo na wengine kutolipwa kabisa.

Katika hatua wanazozichukua kukabiliana na tatizo hilo, Waziri Duni alisema wizara yake inandaa utaratibu utakaowezesha kurugenzi ya fedha kutenga fungu kwa ajili ya malipo ya likizo badala ya kazi hiyo kupewa idara ya utumishi ya wizara hiyo.

Akijibu suala la malipo ya sa za baada ya kazi (Overtime) Duni alisema utaratibu wa kulipa posho wafanyakazi wa afya kwa kufidia upungufu wa wafanyakazi haupo.

Alisema posho huwa zinalipwa kwa wafanyakazi wa afya wale ambao hawaingii ‘shif’ na wanapoitwa kutoa huduma baada ya saa za kazi ndio wanaostahiki kupewa posho ‘overtime’.

Aidha alisema katika kukabiliana na tatizo la uchache wa wafanyakazi wizara iliajiri wafanyakazi 162 mwaka 2010 amabo wamemaliza chuo cha sanyansi za afya Mbweni na asilimia 61 ya waajiriwa hao walipelekwa Pemba.

Fedha za serikali na matumizi mabaya

Wajumbe wa baraza la wawakilishi wameambiwa kuwa bado kumekuwepo na matumizi mabaya ya fedha za umma bila ya kuwa na vielelezo ambayo hufanywa na watu wenye mamlaka serikali.

Akisoma muhrasari wa ripoti ya kamati ya kuchunguza na kudhibiti hesabu za serikali na mashirika (P.A.C) ya mwaka 2011/2012 Mwenyekiti wa Kamti hiyo Omar Ali Shehe alisema ripoti ya mwaka 2008/2009 imeonesha kuwa wakati wa ukaguzi wa mahesabu kwa taasisi mbali mbali, Jumla ya Tsh 5,170,000/ ambazo zilitumika kama malipo ya masurufu (Imprest) vielelezo vyake havikupatikana kuthibitisha uhalali wa malipo hayo.

Akitaja ubadhirifu huo uliofanyika alisema Jumla ya Shilingi 29,251,380 zilitumika kununulia vifaa ambavyo havikuingizwa katika madaftari ya kuhifadhia (Store Ledger) ili kuthibitisha uhalali wa manunuzi hayo na Jumla ya Tsh 138,053,207 pamoja na Dola 94,209 zilitumika kama malipo ambayo hayakuwa na vielelezo ambapo jumla ya 103,294,571 zilitumika kama malipo ambayo hayakuwa na stakabadhi za malipo na Jumla ya shilingi 413,648,097 zilitumika katika malipo yasiyokuwa na Mikataba.

“Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, wa Hesabu za Serikali ukaguzi unaonesha kuwa jumla ya fedha zote ambazo matumizi yake hayakuthibitika wakati wa ukaguzi ni Tsh 689,417,255” alisema Shehe.

Akizungumzia suala la kukosekana vielelezo, Mwenyekiti huyo alisema ripoti imeonesha namna mali za Serikali zinavyokuwa hazikuwekewa kumbukumbu, kutofahamika thamani yake pamoja na kukosekana kwa hati miliki ya mali hizo. Kutokuwepo kwa mambo hayo kwa mali za umma zinazomilikiwa na Serikali, sio tu kunatoa fursa kwa wajanja wachache kujimilikisha, lakini pia tatizo hili linapelekea kuathiri sana mfumo mzima  wa kimahesabu katika uchumi, pamoja na uhai wa taasisi hizo hususan taasisi za umma zinazojitegemea, kama vile Mashirika ya Umma.

Aidha katika suala hilo kamati hiyo imependekeza serikali iandae muongozo wa utayarishaji wa daftari la kuwekea kumbukumbu za mali za Serikali kwa kila taasisi ya Umma pamoja na Serikali Kuu (Consolidated Asset Register), iaandae utaratibu wa kutathmini mali zote za Serikali hasa majengo,iandae utaratibu wa kuandaa Sera ya Ushukaji na Upandaji wa Thamani (Depreciation and Apreciation Policy), na iandae utaratibu wa kuzitoa (Disposal) mali ambazo ziko katika thamani inayokubalika kutolewa katika milki ya SerikaIi.

“Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu imeripoti kasoro hii inayofanywa na baadhi ya Maafisa Wahasibu wa Taasisi zetu, kasoro ambayo huchangiwa zaidi na suala la kutokuwajibika na uzembe wa watendaji” alisema Mwenyeketi huyo.

Mwenyekiti huyo aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, imeainisha mrundikano mkubwa wa madeni yanayotokana na Idara ya Nyumba kwa wananchi mbali mbali wanaoishi katika Nyumba za Maendeleo na zile zinazomilikiwa na Serikali.

Alisema ripoti imeonyesha pia mrundikano wa madeni yanayo daiwa na Mamlaka ya Maji – ZAWA, Kama ni huduma ya maji kwa wananchi na taasisi mbali mbali za Umma na taasisi binafsi.

“Kwa upande wa deni la Idara linalotokana na kodi za wateja wa majumbani ni shilingi 678,744,000,  taasisi binafsi zinadaiwa shilingi 5,205,000 na taasisi za Serikali  ni Shilingi   9,000,000 jumla ya deni lote kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti, ni shilingi 692,949,000 (Madeni haya ya Maji ni kwa upande wa Mamlaka ya Maji Pemba tu ambayo ndio Kamati iliyoifanyia kazi” alisema Mwenyekiti huyo.

Wakati fedha za serikali zikiwa zimekosa vielelezo vinavyotakiwa pia ukosefu wa kutopatikana kwa tarifa juu ya fedha na vifaa vinavyotokana na wafadhili imeelezwa kuwa ni tatizo jengine linaloikabili serikali.

“Katika mafunzo yaliyofanyika hivi karibuni, ambayo yaliandaliwa na Jumuiya ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola- CPA yaliyofanyika Nchini Uingereza, ambayo yalihusu Kamati za PAC, suala hili liliibuka katika mjadala. Rai iliyotolewa katika mjumuiko wa wajumbe katika kutafakari namna ya kupata  suluhisho la tatizo hilo linatokea baina ya wafadhili na wafadhiliwa ni kwamba, ilipendekezwa kuwa ili ionekane kuwa mikopo ama misaada hiyo inatumika vyema na inaleta faida kwa wananchi, moja kati ya masharti ya kuridhia  misaada ama mikopo, iwe ni kwa kuwahusisha wakaguzi  wa mahesabu wa pande zote zinazohusika kwa lengo la kupeana taarifa muhimu zinazohusiana na matumizi na ukaguzi wa fedha zilizotolewa na misaada mengine yote ya kifedha” alisema Mwenyekiti huyo.

Familia ya Karume matatani tena

KAMATI Teule ya Baraza la Wawakilishi imegundua ufisadi wa kutisha katika maeneo tofauti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), huku familia ya Rais mstaafu wa visiwa hivyo, Aman Abeid Karume ikitajwa kukiuka sheria kwenye umiliki wa ardhi.

Wakati familia hiyo ya Rais mstaafu Karume ikituhumiwa kukiuka sheria za ardhi, mfanyabiashara maarufu nchini Said Salim Bakharessa ambaye naye ametajwa kujipatia kiwanja cha Serikali kwa bei ndogo, alijitetea mbele ya kamati na kumlipua waziri aliyekuwa na dhamana ya ardhi akisema, “Mimi nilipigiwa simu na waziri akiniambia kuna kiwanja kinauzwa.”

Akisoma ripoti hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Omar Ali Shehe, alitaja maeneo ambayo yalibainika kuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria ambayo mbali na sekta ya ardhi ni ajira katika utumishi Serikali, mikataba katika maeneo nyeti na ukiukaji wa sheria za ununuzi.

Akizungumzia uhalali wa mikataba ya nyumba ya Serikali iliyopo Kiponda inayodaiwa kwamba alipewa mwananchi na baadae kuiuza kwa mtu mwingine, Shehe alisema Kamati imebaini kwamba, mikataba yote ya mauziano iliyofungwa baina ya Serikali na Juma Ali Kidawa na baina yake na Amina Aman Abeid Karume, ni batili na ya udanganyifu.

Shehe alisema kumekuwapo uvamizi wa fukwe na uharibifu wa mazingira kwenye hoteli inayopakana na Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Maruhubi, kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani-Zanzibar na Hoteli ya Misali iliyopo Wesha, Chake Chake-Pemba.

Aliongeza kwamba Kamati imejiridhisha kwamba Ramadhan Abdallah Songa na Mama Fatma Karume walishiriki katika udanganyifu wa mkataba wa mauziano uliofungwa baina ya Serikali na Kidawa.
“Aidha, hati ya matumizi ya ardhi aliyopewa Karume na Mansour Yussuf Himid, (Akiwa Waziri wa Ujenzi, Nishati na Ardhi), imekiuka taratibu za kisheria na kiutawala), ” alisema mwenyekiti huyo.

Shehe alisema Kamati inapendekeza nyumba hiyo ambayo sasa imeshajengwa Hoteli ya Amina Aman Karume, hati zote za umiliki wake, zifutwe na apatiwe tena hati ya umiliki wa ardhi husika na baadae atakiwe kumsaidia Kidawa kwa kiwango cha fedha kisichopungua Sh20 milioni, kujinasua na maisha.

“Hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wananchi wote waliohusika katika udanganyifu uliojitokeza katika upatikanaji wa mikataba ya mauziano kutoka katika mamlaka ya Serikali na kumuuzia Kidawa na mauziano baina ya Kidawa na Amina Aman Abeid Karume,”alisema Shehe.

Shehe alisema pia kwamba imegundulika Machano Othman Said akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Miundombinu na Mawasiliano) katika Serikali ya awamu hiyo ya sita, anamiliki asilimia 10 ya hisa katika mradi wa Hoteli ya Misali Sunset Beach, iliyopo Wesha Pemba.

Alisema kwa nafasi yake wakati huo akiwa waziri, Machano (ambaye kwa sasa ni Waziri asiye na Wizara Maalumu), alitumia nafasi yake kuisaidia kuendeshwa hoteli hiyo bila kibali cha mazingira wala leseni ya utalii kutoka Pemba, ambako ndiko kwenye mradi huo hivyo awajibishwe.

Katika ripoti hiyo, Shehe alibainisha kuwa uchunguzi uliofanyika kuhusu uhaulishwaji wa kiwanja cha Wizara ya Miundombinu na Mawasililiano ambacho kipo kwenye eneo ilipokuwepo Karakana na wizara hiyo, eneo la Mtoni, Mjini, Zanzibar, umeonyesha kuna ukiukwaji mkubwa sheria na taratibu za uuzaji wa mali za Serikali.

Shehe, alisema wamejiridhisha kwamba wizara hiyo ya Miundombinu na Mawasiliano haikufuata taratibu za uuzaji wa kiwanja hicho ilichokuwa inakimiliki na kuamua kukiuza kwa kampuni binafsi bila ya kufuata taratibu za kiutawala na taratibu za kisheria.

“Hali hiyo imepelekea wasi wasi mkubwa wa kuwepo kwa harufu ya ubinafsi na harufu ya rushwa, zaidi ukizingatia thamani ya kiwanja hicho kuwa ni sawa na Sh200 milioni bei ambayo ni ndogo kwa mujibu wa bei ya soko na kwa kuzingatia ukubwa wa kiwanja chenyewe na eneo kilipo,”alisema Shehe.

Alisema kulikuwa na matumizi mabaya ya madaraka ya Ofisi ya Rais kwani walipokuwa wakiangalia namna gani ulitolewa uamuzi mzito wa kuuza kiwanja hicho cha Serikali, ilibainika iliruhusiwa na Ofisi ya Rais.

“Katika utafiti wetu, tuligundua kuwa, maombi ya ruhusa ya kuuzwa kwa kiwanja hicho, yametoka kwa Katibu wa Rais, Haroub S. Mussa, ambaye aliandika barua, tuliyoifanya kielelezo Namba. 9 cha Ripoti yetu,” alifafanua.

Shehe alisema Haroub hana mamlaka ya kuruhusu uuzwaji wa kiwanja, wala kusimama katika nafasi ya kupeleka uamuzi wa Rais kwa mtu mwengine yeyote kwani kazi hiyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kifungu cha 49(1), inafanywa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Kutokana na hali hiyo, kamati imependekeza aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mawasiliano na Uchukuzi (2008-2010, Machano) na watendaji wote waliohusika katika kuingia mikataba na Kampuni ya Coastal Fast Ferries Ltd, wawajibishwe kwa misingi ya sheria.

Kuhusu kuchunguza suala zima la Uwanja wa Ndege wa Zanzibar, alisema ulipaji wa fidia kwa watu ambao mali zao zimeathirika kutokana na ujenzi wa uzio wa uwanja huo umegubikwa na utata.

“Matatizo ya ununuzi wa jenereta, mikataba ya ukodishwaji wa sehemu za biashara kwenye eneo la uwanja na utaratibu wa ajira na utoaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo ya uwanja na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa ujumla, haukuzingatia sheria,” alisema Shehe.

Alisema kamati imegundua na kujiridhisha kwamba, kumefanyika uzembe wa makusudi na Wizara zote mbili zimehusika katika uzembe huo yaani Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na matokeo yake zaidi ya Sh300 milioni, zinaelekea kupotea huku jenereta lililonunuliwa kwa fedha zote hizo, limeshindwa kujaribiwa kwa kipindi chote cha muda wake wa majaribio (warrant period).

“Aidha, kitendo cha jenereta kukaa bila ya matumizi ya muda mrefu pia ni sehemu ya uharibifu wake. Kwa mantiki hiyo, Kamati inafahamu kwamba, jenereta hilo limetelekezwa,” alisema.

Alisema kamati inapendekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika na uzembe wa ununuzi wa jenereta hilo, huku msisitizo ukiwekwa kwa makatibu wakuu wa Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano; Mkurugenzi na Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege.

“Kuhusu mikataba, kamati inapendekeza mikataba yote inayohusiana na ukodishwaji wa biashara mbali mbali katika eneo la uwanja wa ndege ipitiwe upya ili iendane na mabadiliko ya biashara na msisitizo ukiwekwa katika gharama za kodi husika,”alisema.

Katika utoaji ajira kwa upendeleo, Shehe alieleza kuwa Waziri wa Wizara Miundombinu na Mawasiliano, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, wamekuwa wakiwaajiri watoto, ndugu ama jamaa zao, huku wakiwapa fursa nyingi za upendeleo kinyume na utaratibu.

“Spika, naomba kwa makusudi wajumbe wako wapate taarifa hizi katika mfanyakazi, Aisha Msanif Haji, mtoto wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ambaye ameajiriwa na bado akiwa katika kipindi cha majaribio, tayari amepewa ruhusa ya kusoma, huku akiwa anaendelea kupokea mshahara kama kawaida.”

Alisema imethibitika kwamba, kuna mfanyakazi analipwa mshahara wa ngazi ya mtaalamu (msomi wa shahada) wakati bado hajafikia elimu hiyo.

“Huyu si mwengine isipokuwa mtoto wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano,”alisema. Shehe alisema kutokana na hali hiyo, Kamati imependekeza viongozi na watendaji wakuu wa wizara zote mbili (Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora) waliohusika na kadhia hiyo wawajibishwe kisheria.

Pia uajiri wa wafanyakazi wote ambao kamati imeona hawana sifa za kuajiriwa, ufanyike upya kwa kufuata muongozo wa sheria zilizopo.

 

 

Advertisements

5 responses to “Watumishi hewa wasakwa serikalini

  1. Hivi fedha zote hizi zinazoibiwa na maafisa wa Serikali bila ya hata kua na khofu zinachukuliwaje? Hii serikali ipo au iko likizo au ndo sera yake kila mtu awahi chake mapema? Mimi nahisi bado wezi serikali inawalea kwa faida yake ya kisiasa. Hivi inakuaje mtumishi wa serikali ambae mshahara wake hauzidi shilingi laki 8 mpaka milioni 1 amiliki mali za mabilioni? Jee serikali haiwaoni watu wa namna hii? Jibu inawaona lakini hawa wakati wa uchaguzi ndio wachangiaji wakubwa wa kampeni za uchaguzi hivyo wanaachiwa makusudi warejeshe fedha zao. Kama serikali iko makini ni kutaka waonyeshe ni vipi wamezipata mali hizo wakati mishahara yao hairuhusu. Asilimia 90 ya majumba ya mbweni upatikanaji wake unapaswa kuhojiwa kwani mtumishi wa kawaida na hata Waziri hawezi kujenga majumba yale kwa kutegemea mshahara tu na kama wana biashara waonyeshe risiti zao wanazolipia ZRB.

  2. Pingback: Watumishi hewa wasakwa serikalini·

  3. HATA MKAUNDA KAMATI MIA MOJA WIZI HAUTAKISHWA KWANI NI SERA YA CCM. WIZI UTAMALIZIKA PALE TU CCM ITAKAPOINGIA KABURINI. KAMA KWELI TUNATAKA WIZI WA MALI ZA SERIKALI UISHE NA MLALAHOI APATE NAFUU DAWA NI MOJA TU NAYO NI KUHAKIKISHA KUA CCM INANG’OKA MADARAKANI MWAKA 2015. HII NDIO DAWA YA MATATIZO YOTE YA ZANZIBAR IKIWEMO KERO ZISIZOKWISHA ZA MUUNGANO. MZANZIBARI POPOTE PALE ULIPO HAKIKISHA KUA UNAFANYA KILA LIWEZEKANALO KUONA KUA CCM HAICHUKUI UONGOZI WA NCHI 2015.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s